Home Makala JANUARI NA HISTORIA MBAYA KWA AFRIKA

JANUARI NA HISTORIA MBAYA KWA AFRIKA

1156
0
SHARE

NA JOSEPH MIHANGWA


KWA Afrika, Januari ni mwezi wenye kubeba historia na kumbukumbu nzito katika uhusiano wa Kimataifa, kwa bara hili kugeuzwa uwanja wa majaribio ya kupiga shabaha miaka ya 1960, kati ya nchi za Ubepari wa Magharibi kwa upande mmoja, na nchi za Usoshalisti za Mashariki, kwa upande wa pili, katika ugomvi wao kipindi hicho cha “vita baridi”.

Kilikuwa kipindi hatari kwa Viongozi wanaharakati barani Afrika, kujipambanua na upande mmoja katika mpambano huo bila kuhatarisha maisha.

Kwa Afrika huru, wahanga wa kwanza wa vita hivyo ilikuwa nchi ya Congo Leopoldville [sasa DRC], ambapo Waziri Mkuu wake wa kwanza mzalendo, Patrice Emery Lumumba, aliuawa kikatili na mabeberu, Januari 17, 1961.  Mhanga wa pili alikuwa nchi ya Zanzibar ambayo kwake, mpambano wa kambi hizo ulizaa Muungano ambao haukutarajiwa, kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na baadaye kuitwa “Tanzania”.

Wakati mpambano nchini Congo ulisababisha mapinduzi ya kibeberu dhidi ya Serikali ya Kisoshalisti ya Waziri Mkuu Patrice Lumumba; nchini Zanzibar, mpambano kama huo ulisababisha Mapinduzi ya kisoshalisti dhidi ya Serikali mpya ya kibaraka wa Sultani wa Zanzibar na Uingereza, Mohamed Shamte, Januari 12, 1964, iliyoingia madarakani Desemba 10, 1963.

Mwaka huu Wazanzibari  wameadhimisha kumbukumbu ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Kisoshalisti hapo Januari 12; lakini Januari 17, mwaka huu, Wakongo wameomboleza kumbukumbu ya kupinduliwa na kuuawa kwa kiongozi wa kwanza msoshalisti na mzalendo wa nchi yao, Patrice Lumumba.

Matukio yote mawili ni ya kipekee na ya aina yake kwa siasa za Afrika huru na kielelezo pia cha nguvu ya ubeberu na dhana nzima ya ukoloni mamboleo unaotishia uhuru wa nchi za Kiafrika hadi leo.

Tangu 1961 hadi hivi karibuni, kuuawa kwa Lumumba kumebaki  kitendawili bila mteguzi. Mwanzoni baada ya tukio, serikali ya Congo ilitoa sababu za kujikanganya; mara eti Lumumba alijiua akiwa mahabusu; mara yeye na mahabusu wenza walitoroka kutoka Gereza la Thysville, na katika harakati hizo, walipita kwenye kijiji cha Kabila adui, wakauawa.  Hata hivyo, hakuna hadi leo aliyewahi kuonesha au kuona kaburi la Lumumba ambaye alizaliwa mwaka 1925, katika Jimbo la Kasai,  kabila la Batatela.

Harakati za uhuru wa Kongo zilianza mwaka 1957 kwa Chama cha Kikabila cha “Abakongo [ABAKO] cha Joseph Kasavubu, kwa lengo la kuwaunganisha Wakongo wa kabila la Abakongo ndani na nje ya Congo, kwa sababu kuu mbili—kuimarisha  matumizi ya lugha ya Kikongo, na kudai uhuru. Kasabuvu, ambaye kabla ya hapo alipata mafunzo ya uhubiri wa dini, alipania kuwaunganisha Abakongo wa Kongo Leopoldville, Congo Brazaville na Angola, ili kufufua Ufalme wa Kongo ya karne ya 16.

Mwaka 1958  kilianzishwa chama cha The Movement National Congolais [MNC], cha Patrice Lumumba. Na Chama cha tatu cha kikabila cha “Confederation des Association Tribales du Katanga” [CONAKAT] cha Moise Tshombe, azma yake ikiwa ni jimbo la Katanga kujitawala, lakini kuwa na uhusiano wa karibu na vikundi vya Wakoloni wa Kibelgiji. Hadi kufikia Novemba 1959, jumla ya Vyama vya siasa 53 vilikuwa vimesajiliwa, na kuongezeka kufikia 120 mwaka 1960, vingi vikiwa vya kikabila na kimajimbo.

Kati ya mwaka 1958 na 1959, serikali ya Leopoldville ilikabiliwa na maasi ya hapa na pale yaliyochochewa na Chama cha Lumumba dhidi ya utawala wa kikoloni—ambao  hatimaye ulichukua hatua za kumfunga jela kwa miezi sita kwa kosa  la  uchochezi.

Hatua hiyo ilizidisha maasi nchi nzima kiasi kwamba, Januari 1960, serikali ililazimika kuvialika Vyama 13, vikiwamo ABAKO, CONAKAT na MNC, kujadili ratiba na masharti ya Uhuru. Lumumba alihudhuria kikao hicho akitokea gerezani. Katika kikao hicho, Ubelgiji ilishinikiza kuwe na hatua nne kuelekea Uhuru, ambazo zingechukua miaka minane kufikiwa, jambo ambalo lilikataliwa na Wazalendo. Na kwa sababu hiyo, serikali ikasalimu amri na kukubali kutoa uhuru Juni 30, 1960 ili kuepusha ghasia zaidi.

Haya yakiendelea, Kongo ilikuwa na upungufu mkubwa wa wataalamu wazawa ambapo, kati ya watumishi 1,400 wa serikali, ni watatu tu walikuwa wazawa.  Hapakuwa na daktari mzawa, walimu wa sekondari wala maafisa wa jeshi wa ngazi za juu. Lakini cha kushangaza ni kwamba, nchi hiyo ilikuwa na idadi kubwa ya Wahubiri wa dini wazawa zaidi ya 6,000 walioshibisha umma kwa nadharia ya “heri” sita za ubeberu wa kiroho, ikiwamo ile ya “watawala wote huwekwa madarakani na Mungu”, na kwamba ashindanaye na watawala “ashindana na Mungu”.

Uchaguzi Mkuu ulipofanyika mwaka 1960, Chama cha Lumumba cha MNC kilishinda viti 41 vya Bunge kati ya viti 137, na viti 96 vilivyobaki vilichukuliwa na vyama 12.

Lumumba andamwa

Pamoja na ushindi huo mkubwa, Serikali ya Ubelgiji haikumruhusu Lumumba kuunda serikali, badala yake ikamtaka Kasavubu kuunda Serikali; lakini uamuzi huo ulipowasilishwa Bungeni na kupigiwa kura, mambo yalikuwa tofauti. Lumumba aliungwa mkono na Wabunge 74 kati ya 137.

Hivyo kwa shingo upande, serikali iliruhusu Lumumba kuunda serikali, yeye akiwa Waziri Mkuu Mtendaji, na Kasavubu kama Rais asiye na mamlaka.

Kuthibitisha hasira yake dhidi ya wakoloni kwa maovu waliyomtendea yeye na nchi yake, Lumumba, alimbwatukia Mfalme Boudouin wa Ubelgiji aliyehudhuria sherehe za uhuru kwa kumwambia, “Sisi si nyani wako tena”. Mfalme Bouduin akafura kwa hasira.

Mkasa wa kwanza kwa utawala wa Lumumba ulikuwa ni kuasi kwa Jeshi la nchi – “Force Publique” [FP] lenye wapiganaji 2,500, wakati huo lingali chini ya Maafisa wa Kibelgiji 1,100, likidai nyongeza za mishahara na madaraka kwa Askari Wazawa.

Kichocheo kingine kilikuwa kuibuka ghafla kwa matajiri miongoni mwa watumishi wa serikali, wanasiasa—matumizi makubwa ya fedha na anasa; kuwa na magari ya kifahari, wakati wanajeshi wakipewa mshahara kiduchu.

Tukio hili linaweza kufananishwa na hapa kwetu na tabia kama hiyo miaka ya 1960 baada ya uhuru, ambapo vigogo wa serikali walipewa jina la “Wabenzi”. Hii ilikuwa moja ya sababu za mgomo wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1966. Sababu kubwa walikuwa wakipingta mpango wa lazima wa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa [JKT].

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akawafukuza wanafunzi na kuwarejesha baada ya mwaka mmoja. Inawezekana ilikuwa sababu ya kuandika Azimio la Arusha—ili  kukata mzizi wa ulimbukeni wa viongozi na kuwanyonya wanyonge.

Kamanda wa Jeshi la Kongo, Jenerali Emile Janssens, alitupilia mbali madai yote mawili.  Kama vile kuchochea hasira za wapiganaji, aliandika ubaoni Makao Makuu ya Jeshi, maneno yenye kashfa kwa kila Askari kusoma: “Kabla ya Uhuru, baada ya Uhuru”, kumaanisha kwamba uhuru wa Kongo haukubadili hali wala kumwongezea chochote Mkongo.

Na hivyo ndivyo ilivyokuwa—kwamba, pamoja na serikali kuongozwa na Baraza la Mawaziri wazawa, lakini shughuli zote za serikali, jeshi, utumishi na uchumi viliendelea kubakia mikononi mwa Wabelgiji. Wanajeshi wakamtaka Lumumba kumfukuza kazi Jenerali Janssens, naye akafanya hivyo na kumteua Sajini Victor Lundula kuwa Mkuu wa FP; na akamteua pia rafiki, mshirika na Msaidizi wake mwaminifu, Sajini Meja, Joseph Desire Mobutu, wakati huo akiwa na umri wa miaka 29, kuwa Mkuu wa Utawala Jeshini [CoS].

Kabla ya hapo, Sajini Mobutu alitumikia Jeshi la Kibelgiji hadi mwaka 1956 alipomaliza mkataba wake, kisha akawa Mwandishi wa Habari wa kujitegemea na Jasusi wa kulipwa wa Ubelgiji.

Mabadiliko hayo hayakuweza kutuliza maasi; unyanyasaji kwa wageni, watawa wa kike na wahubiri wa dini, uliendelea kwa kasi kubwa; maelfu wakaikimbia Kongo.

Kwa madhumuni ya kutuliza hali, serikali ya Ubelgiji ilimuomba Lumumba aruhusu vikosi vya Jeshi la Ubelgiji vitumike kurejesha amani, lakini alikataa.  Ubelgiji ikaamrisha vikosi vyake kuingia kwenye mapambano, na kupeleka askari zaidi kutoka nje ya nchi hiyo.

Kadri vikosi vya Ubelgiji vilivyozidi kuteka mji mmoja baada ya mwingine, Lumumba alishawishika kwamba nchi hiyo ilikuwa imetangaza vita dhidi ya nchi yake kwa lengo la kutawala kwa mara ya pili;  naye akatangaza kuingia vitani na taifa hilo la kigeni lenye nguvu kijeshi.

Katika mtafaruku huo, Moise Tshombe, kiongozi wa KONAKAT wa Jimbo la Katanga, kwa msaada wa Ubelgiji na Makampuni ya madini ya Kibelgiji ya jimboni humo, alipata mwanya wa kujitangazia serikali huru ya Katanga. Na kufuatia hatua hiyo, majeshi ya Ubelgiji yalianza kuwanyang’anya silaha askari wa Lumumba na kuwafukuza kutoka Katanga, huku yakiwapa mafunzo Askari wa Tshombe na misaada lukuki kumwezesha Tshombe kudhibiti hali na madaraka.

Lumumba aliomba msaada wa majeshi kutoka Umoja wa Mataifa [UNO] kuyafukuza majeshi ya Ubelgiji; na ulipochelewa, kwa hasira ya mlipuko, Julai17, 1960, akatoa tishio kwamba, kama Umoja huo usingetuma vikosi Kongo kabla au ifikapo Julai 19, angeitaka Urusi kuingilia kati kwa kuleta majeshi Kongo kupambana na majeshi ya Wabelgiji.

Hatua hii ya Lumumba iliamsha hisia na hofu ya Marekani juu ya vita kati ya mtaifa haya makubwa kuhamia Afrika na kuigeuza Kongo kuwa “Cuba ya Afrika”, kwa hofu ya kutokea Mapinduzi ya Kikomunisti kama yale yaliyofanywa nchini Cuba mwaka 1959 na Fidel Castro, dhidi ya serikali ya kibaraka wao Fulgencio Batista.

Baraza la Usalama la Marekani lilipoketi, Julai 22, 1960, chini ya Rais Eisenhower, hofu ya Marekani ilikuwa dhahiri—huku Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Marekani [CIA], Allen Dulles, akimwelezea Lumumba kuwa “sawa na Castro au mbaya zaidi ya huyo”; na kuongeza kwamba, “Ni vyema kumhesabu Lumumba kuwa amenunuliwa na Wakomunisti”.

Hatimaye majeshi ya Ubelgiji yaliondolewa Kongo; lakini pamoja na hilo, Lumumba alitoa sharti jipya; kwamba Vikosi vya Umoja wa Mataifa vitumike pia kukomesha harakati za kujitenga kwa jimbo la Katanga. Umoja wa Mataifa ulipokataa sharti hilo kwa madai ya kutokuwa na mamlaka ya kuingilia mambo ya ndani ya Kongo, Lumumba, alilaani kitendo hicho, na kuituhumu UN kula njama na Ubelgiji kuivamia Kongo, tuhuma ambayo ilimtia hofu Katibu Mkuu wa UN, Dag Hammarskjold, kwamba haikulenga kuiangamiza Kongo pekee, bali kuchafua pia sifa na heshima ya UN.

Agosti 15, 1960, kwa kujawa matumaini ya kushinda kijeshi Katanga na Kasai Kusini—eneo  lenye utajiri mkubwa wa madini ya almasi; Lumumba alichukua uamuzi wa kimaangamizi kwake, wa kuwaita Warusi nchini Kongo kuja kumpa msaada wa kijeshi, ili kwa kuanzia, kuikomboa Kasai Kusini kabla ya kuelekea Elizabethville na Katanga kumpindua Tshombe.

Mipango ya kumuua

Katika kikao kingine cha Baraza la Usalama la Marekani, Agosti 18, 1960, Rais Eisenhower aliambiwa wazi na washauri wake juu ya uwezekano wa Lumumba kuitimua UN nchini Kongo; naye papo hapo, akaidhinisha kuuawa kwa Lumumba akimfananisha na mbwa kichaa. Ndipo Agosti 26, Mkurugenzi wa CIA, Allen Dulles, alituma simu ya maandishi kwa Mkuu wa kituo cha CIA mjini Leopoldville, akiagiza: “Kuuawa kwa Lumumba liwe jambo la haraka sana na muhimu”.

Haya yakiendelea, majeshi ya Lumumba yalikuwa yakisonga mbele kuelekea Kasai, yakiua watu wa kabila la Baluba kwa mamia, na wengine kuikimbia nchi.

Lakini Kanali Joseph Mobutu hakufurahishwa na mpango huo; akaamua kumsaliti Lumumba kwa kuungana na mahasimu wake.

Septemba 5, 1960, Rais Kasavubu [mteule wa Lumumba], akatangaza kupitia redioni, akimshutumu Lumumba kwa kuendesha utawala wa kimabavu na hivyo kuiingiza nchi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe; kisha akafuta uteuzi wa Lumumba kama Waziri Mkuu na badala yake akamteua Joseph Ileo, mtu wa siasa poa, kuchukua nafasi ya Lumumba. Siku hiyo, Lumumba, baada ya kusikia tangazo hilo, naye akatangaza kumfukuza kazi Rais Kasavubu; mtafaruku wa kisiasa ukazidi kushika kasi nchini Kongo.

Nani alikuwa na mamlaka na uhalali wa kumfukuza mwenzake—Kasavubu na Lumumba?.  Nini kilitokea?.

………… Itaendelea.