Home Makala Jenerali Waitara: Viongozi hamasisheni utalii wa ndani

Jenerali Waitara: Viongozi hamasisheni utalii wa ndani

889
0
SHARE

Na ELIYA MBONEA

JENERALI Mstaafu, George Waitara kwa miaka kadhaa ameongoza timu ya watumishi wa idara mbalimbali za Serikali na sekta binafsi kupanda Mlima Kilimanjaro Desemba 9 kila mwaka.

Matembezi hayo yamepewa jina la Uhuru Expedition ambayo yamelenga kuhamasisha Watanzania kujenga utamaduni wa kupanda mlima huo kama sehemu ya kutangaza kivutio hicho cha kipekee barani Afrika.

Mbali ya umri alionao na majukumu ya Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Jenerali Mstaafu Waitara amekuwa kinara mwongozaji wapanda mlima wanaowasili Uhuru Peak wakiwa timu moja.

Kwa miaka yote anayopanda mbali ya kusisitiza mambo ya utendaji, kuboresha malazi, miundombonu, kutunza mazingira ya mlima bado hakuacha kuhamasisha Watanzania kujenga utamaduni wa kupanda mlima.

Kama ilivyo kwa Luteni Jenerali Mstaafu James Mwakibolwa aliyekabidhiwa dhamana ya kuongoza timu ya Uhuru Expedition 2018 hadi kileleni hakuacha kutembea juu ya nyayo za Jenerali Mstaafu Waitara.

Mpiganaji huyo asiyeishiwa vichekesho kwa watu waliomzunguka akiwa Uhuru Peak katika mahojiano na wanahabari alisema, Mlima Kilimanjaro ni zawadi ya kipekee kwa Watanzania iliyotolewa na Mungu.

Ni muhimu Watanzania wakajenga utamaduni wa kupanda mlima huu hasa wanaosoma na wanaokwenda kwenye mikutano nje ya nchi kwani kutachagiza kuendelea kutangaza kivutio hicho.

Luteni Jenerali Mstaafu Mwakibolwa alikwenda mbali katika hoja yake akitolewa mfano kwamba si jambo jema kwa Mtanzania anayekwenda nje ya nchi bila kuwa amepanda Mlima Kilimanjaro.

“Jambo hili linaweza kuonekana la kawaida lakini kwa wenzetu wanaotumia fedha nyingi kusafiri na kuja kupanda Mlima Kilimanjaro wanaweza kukushangaa wewe unayetoka Tanzania.

“Mfano, mtu anatoka Buswokelo akikutana na mzungu Ulaya analizwa umewahi kupanda Mlima Kilimanjaro, Mtanzania huyu atatafuta visingizio ikiwamo eti kuna umbali kutoka Buswokelo hadi Moshi-Kilimanjaro.

“Bila kukumbuka kwamba wapo watu wanaosafiri kutoka nchi mbalimbali duniani kuja Tanzania kupanda Mlima Kilimanjaro na kurudi makwao,” anasema Luteni Jenerali Mstaafu Mwakibolwa.

Kupitia hamasa ambayo amekuwa akiitoa Jenerali Mstaafu Waitara, Luteni Jenerali Mstaafu Mwakibolwa anakwenda mbali na kuyataka makundi mbalimbali ya Watanzania kuanza kujenga utamaduni wa kupanda.

Anasema, makundi ya wanafunzi wa vyuo, wanavijiji, makundi ya Watanzania ya wafanyabiashara, wafanyakazi idara na mashirika ya serikali au binafsi wanaweza kupanga ratiba ya kupanda angalau mara moja.

Anasema mfumo huo ukijengwa miongoni mwa jamii ya Watanzania unaweza kuibua kundi kubwa la watalii wa ndani kupanda mlima na kuchangia pato la taifa badala ya kutegemea watalii kutoka nje ya nchi.

Licha ya kuandika sauti ya Jenerali Mstaafu Waitara na Luteni Jenerali Mstaafu Mwakibolwa kuhusu kuhamasisha Watanzania kupanda mlima natambua wazi kuwapo pia viongozi wengine wanaofanya hivyo.

“Nimewatumia wapiganaji hawa wawili kama sehemu ya wasilisho la sauti za viongozi na wadau wengine wanaohamasisha watu wafanye utalii wa ndani kwenye Hifadhi za Taifa au maeneo yenye vivutio vya utalii yaliyo karibu.

“Nikirejea kwenye Mlima Kilimanjaro niwazi sauti ya Jenerali Mstaafu Waitara imesikika kwani licha ya Geita Gold Mine kupanda kila mwaka sasa tunashuhudia makundi kadhaa yakipishana njiani kuelekea Uhuru Peak,”anasema.

Kwa mfano mbali ya Uhuru Expedition, lipo pia kundi la askari magereza ambao hupanda mlima kila Desemba kama sehemu ya kuonyesha ukakamavu na kukitangaza kivutio hicho.

Kundi jingine linaloshika kasi ni linaloongozwa na Kamishna wa Jeshi la Zimamoto Thobias Andengeye ambaye amekuwa kinara mwongozaji hadi kufika kileleni akiongozana na wapiganaji wake.

Kamishna Andengenye alipanda Septemba 2019 akiwa njiani Kibo Hut kukitafuta kilele cha Uhuru Peak, alipishana na kundi kubwa la wasanii, askari, wafanyabiashara, wanahabari, viongozi wa serikali likishuka.

Kundi hili nalo lilikuwa na kiongozi wake ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangala ambaye kwa mara ya kwanza amepanda Mlima Kilimanjaro na kufika kileleni.

Waziri Dk. Kigwangala akiongozwa na kauli mbiu ya #HKKiliChallenge Twenzetu Kileleni alitimiza azma yake kujionea rasilimali hiyo muhimu kwa taifa akiwa Waziri aliyepewa dhamana na Rais Dk. John Magufuli.

Kingine ni kukagua na kujionea utendaji kazi wafanyakazi walio chini yake, vijana wanaoongoza watalii na kubeba mizigo kwani amewaona kwa macho yake namna wanavyofanya kazi ngumu na kwa nidhamu ya kuulinda utalii.

Kama alivyoeleza Luteni Jenerali Mstaafu Mwakibola kwamba wafanyabiashara bado wana jukumu la kuwajengea utamaduni wafanyakazi wao kutembelea hifadhi zilizopo kama sehemu ya motisha ya kazi.

Wito huo sasa umekwenda kwa kampuni ya Marenga Investiment ya Kiborloni mjini Moshi, ambayo kipekee kabisa imeonyesha mfano wa kuigwa kwa kupandisha Mlima Kilimanjaro wafanyakazi wake kila mwaka.

Kundi hili likiwa na bendera yao lilipishana siku moja na kundi la Waziri Dk. Kigwangala, kwamba wakati kundi la #HKKiliChallenge likishuka, kundi la wafanyakazi wa Marenga lilikuwa linapanda mdogomdogo.

Baada ya kundi la Waziri Dk. Kiwangala kushuka hamasa nyingine ikawa kwa kundi la wabunge na watu wenye ulemavu nalo likapanda Mlima Kilimanjaro na kisha kuelekea hifadhi nyingine za Taifa kutalii.

Natambua wazi kuwapo kwa makundi mbalimbali ambayo sijayaorodhesha hapa, yamekuwa yakipanda Mlima Kilimanjaro kama sehemu ya kuchangia fedha kwa ajili ya shughuli za kijamii na masuala mengine.

Katika hili lazima nikiri kwa kiwango kikubwa makundi ya kupanda mlima kuchangisha fedha kwa huduma za kijamii au kufurahia kutalii yanajengwa na watalii wengi kutoka nje ya nchi na si watalii wa ndani.

Hitimisho, Jenerali Mstaafu Waitara, Luteni Jenerali Mstaafu Mwakibolwa, Kamishna Andengenye, Waziri Dk. Kigwangala pazeni sauti zaidi kuhamasisha utalii wa ndani ili Watanzania tuendelee kupishana Uhuru Peak.