Home Habari JESHI LA POLISI LIKO KWENYE MIKONO SALAMA

JESHI LA POLISI LIKO KWENYE MIKONO SALAMA

4932
0
SHARE
Na Victor Makinda

Jeshi la Polisi ni muhimu mno kwa usalama wetu. Polisi ndio tegemeo la wananchi katika kutulinda sisi na mali zetu. Kwa jicho la kawaida unaweza usiuone umuhimu wa jeshi la Polisi. Lakini Ukweli utabaki kuwa jeshi la Polisi usalama wa raia ni moyo wa ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Huko nyuma kuna wakati jeshi la polisi lilikuwa likilalamikiwa kwa baadhi ya askari wake kukiuka usimamizi wa sheria na mwenendo wenye kutia shaka. Baadhi ya askari polisi wasio waaminifu waliichafua sura ya jeshi hili kwa kuenenda kinyume na maadili ya kazi za kipolisi.

Wananchi walikuwa wakilalamika kuwa baadhi ya askari walikuwa wakiwabambikia kesi, na kuwanyanyasa raia pasipo kufuata misingi ya sheria. Hali hii ililetea uhasama kati ya raia na polisi. Vyovyote iwavyo, Ukweli Ulivyo hakutakiwi kuwa na uhasama kati ya raia na jeshi la polisi.

Dhana ya Polisi jamii ni miongoni mwa dhana zilizobuniwa minajiri ya kuwafanya raia wawaone polisi kuwa ni walinzi wa wao na mali zao. Dhana hii ilikuwa ni miongozi mwa dhana ambazo kwa kiasi fulani zilibadilisha sura ya jeshi la polisi na kulileta jeshi karibu zaidi na raia. Japo kuna wachache waliitumia dhana hii sivyo ndivyo.

Izingatiwe kuwa mahusiano mazuri kati ya raia na jeshi la polisi hufanikisha shughuli za ulinzi na usalama kwa kiwango cha ufanisi,kwani wahalifu sio wanyama, wahalifu ni binadamu wenzatu, majirani zetu, watoto wetu, marafiki zetu na ni watu tunaoishi nao katika jamii zetu. Raia asipofichua uhalifu na kutoa taarifa za uharifu kwa polisi, Polisi itawawia vigumu kuzuia na kudhibiti uhalifu. Hivyo tunaona kuwa ili Polisi afanikiwe lazima raia awe kiungo.

Raia anapokosa imani na polisi na kuona kuwa polisi ni adui hatokuwa huru kutoa na kufichua taarifa za uhalifu polisi. Kuna wakati raia pia waliwahi kuwalalamikia baadhi ya askari polisi wasio waaminifu kuwa wanataja majina ya raia pindi wanapokwenda kutoa taarifa za siri juu ya uharifu.

Polisi anapaswa kuwa msiri kumlinda rais mfichua na mtoa taarifa za uharifu. Polisi kwa ujumla wao hawapaswi kushirikiana na wahalifu kwa nmna yoyote ile iwayo. Ikiwa polisi atashirikiana na mhalifu basi polisi huyo hawezi kufanikisha shughuli za ulinzi na usalama. Izingatiwe kuwa ukaribu na urafiki wa polisi na watu wasio na mwenendo mzuri katika jamii huondoa imani ya raia kwa jeshi la Polisi.

Ukweli Ulivyo polisi wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika mienendo yao ya kila siku maishani mwao na namna wanavyotii na kufuata sheria katika jamii wanamoishi. Ni hatari sana polisi anapokuwa na tabia ambazo raia watazishuku.

Nimelazimika kuanza na nukuu hizo chache nikilenga kukumbusha na kutoa taswira namna polisi anavyotakiwa kuwa. Sisemi kuwa Polisi wetu wako hivyo, hapana, bali natoa hadhari kwa jeshi letu la polisi, kutotumbukia kinyume na maelekezo na miiko ya jeshi ili kuhakisha kuwa linabaki katika mwenendo huo dhabiti kwa usalama wa nchi yetu Tanzania

Hivi karibu Inspeta Generali wa Polisi ( IGP) Simoni Siro alikuja mkoani Morogoro. Maelezo ni kwamba Kamanda Siro alikuja kwa ziara ya kawaida ya kukagua utimilifu(Fitness) ya Jeshi la Polisi mkoni hapa. Kama ilivyo desturi yake Kamanda Siro alikagua Gwaride Maalumu na baadae kufuatiwa na maonesho mbali mbali ya Polisi kikosi cha kutuliza ghasia (FFU)yaliyolenga kuonesha mbinu mbali mbali za kimedani za jinsi ya kukabilina na uhalifu.

Nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari waliohudhuria katika maonesho hayo. Baadae IGP Siro alitupa nafasi wanahabari kuzungumza nae.

Kabla ya kujielekeza kwenye maswali ambayo binafsi nilimuuliza IGP Siro na majibu yake, nianze tu kwa kusema Kamanda Siro aliistahili nafasi aliyokuwa nayo.

Tofauti na kuwa Kamanda wa Polisi, lakini anaonesha ukaribu mno kati yake na jeshi hilo, huku akibaki kuwa kamanda mkakamavu kwa jeshi analoliongoza na jeshi hilo linatii mno mbele yake.

Kwenye maonesho hayo nilipokaa nilikuwa nimekaa na askari wengine ambao hawakuwa kwenye sehemu ya maonesho. Niliwasikia wakisema kuwa sasa Jeshi letu limepata Kamanda wa kweli anayelijua jeshi haswa na aliye karibu na askari wake. Tunamshukuru sana Rais John Magufuli kutuletea Kamanda Siro, shupavu, kakamavu, mpole, mkali, jasiri, mpambanaji, mwenye kujali, na anayesimamia weledi na miiko ya jeshi la Polisi.

Maneno hayo yalidhirishwa na namna Kamanda Siro alivyozungumza na askari wake, alivyokuwa akitoa maelekezo na amri kwa askari wake na namna alivyoonekana kuchangamana nao huku akizungumza nao kwa nmna inayovutia.

Kana kwamba hiyo haitoshi, Kamanda Siro baada ya kukagua maonesho ya ukakamavu na utayari wa Jeshi lake mkoani hapa, alifanya kitendo ambacho kilidhihirisha namna alivyo na utu na kuwajali askari wake.

Kamanda Siro, alikwenda katika moja ya nyumba za askari wake kambini hapo ambako kulikuwa na msiba. Kamanda Siro alikwenda kumpa pole askari aliyefiwa na alikaa kuzungumza na wafiwa kwa unyeyekevu na upole. Hatua hiyo iliwafurahisha mno askari waishio katika kambi hiyo ya FFU mkoani Morogoro, kwani Kamanda Siro licha ya kuja kwa kazi maalumu, alikitenge muda wake kwenda kuhani msiba.

Lengo la makala hii sio kumwagia sifa Kamanda Siro, bali ni kuonesha nmna viongozi wetu iwe ni wa kisiasa, kijamii au wa Ulinzi na usalama wanavyopaswa kuwa katika taasisi wanazo ziongoza. Kamanda Siro ni mfano wa kuigwa katika hayo.

Nikijielekeza kwenye maswali ambayo nilimuuliza Kamanda Siro, Swali la kwanza niulimuuliza kuhusu Jeshi la Polisi lilivyojipanga kukabilina na uharifu wa kimitandao hususani waharifu wa kimtandao walio nje ya nchi ambako sheria zao za mtandao hazifanani na za kwetu.

IGP Siro alieleza kuwa Polisi inacho Kitengo kinachoshughulikia makosa ya kimtandao. Ni namna gani jeshi limejipanga kushughulika na wahalifu wa kimtandao walio nje ya nchi hii inabaki kuwa siri ya jeshi. Aliongeza kusema kuwa hawezi kuweka hadharani mbinu za kipolisi lakini ifahamike kuwa polisi inashughulika na wahalifu hao.

Niliuliza swali hili nikizingatia kuwa kuna uchochezi mwingi unaofanywa na watumiaji wa mtandao walio nje ya nchi. Hawa kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiwalisha sumu watanzania kupitia mitandao ya kijamii.

Watanzania ama kwa kujua au kutojua wamekuwa nyuma ya wahalifu hawa na hata kusababisha hali ya sintofahamu katika nchi yetu. Hapa nina rai kwa IGP Siro. Pamoja na majibu mazuri uliyonipa, niliombe jeshi lako lifanye haraka kuwadhibiti majahiri hawa ambao wanatulisha sumu watanzania kupitia mitandao ya kijamii.

Swali jingine nililomuuliza IGP Siro ni kuhusu utayari wa Polisi kuyakabiri maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika 26 Aprili ya mwezi uliopita. Kamada Siro alinijibu kuwa hao wanaotaka kuandamana wamesha andamana tayari mitandaoni. Hakuna atakaye andamana. Kweli, ilipotimu tarehe 26 Aprili ya mwezi uliopita hakukuwa na maandamano.

Tulichoshuhudia ni jeshi la Polisi likiwa na utayari mkubwa mitaani kuthibiti endapo pangelitokea maandamano. Katika hili pongezi nyingi zimueendee IGP Siro na jeshi lake la Polisi kwa jinsi ambavyo walijipanga kuthibiti vurugu ambazo zingetokea eti kwa kigezo cha maandamano. Polisi imeonesha ushupavu na ukakamavu mkubwa kwa jinsi walivyokuwa tayari kuwakabili waandamana.

Ukweli ulivyo raia wa Tanzania kwa sasa tunatembea kifua mbele tukiamini kuwa tupo kwenye mikono salama ya Jeshi la Polisi chini ya IGP Siro, na hakuna mchochezi yoyote atakayefanikiwa kuivuruga amani yetu.

Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, IGP Siro amefanikiwa mno kwa kipindi kifupi katika uongozi wake ndani ya jeshi la Polisi. Amefanikiwa kuthibiti mno madawa ya kulevya, ujambazi, nidhamu jeshini na utii wa sheria bila shurti kwa raia.

Hivi sasa matukio ya kijambazi yamepungua mno. Hii ni jitihada kubwa ya jeshi la polisi analoliongoza. Lakini ni ukweli pia sasa sheria zinafuatwa kwa kiwango kikubwa. Mfano ni sheria za usalama barabarani. Ukweli ni kwamba madereva sasa wanawaheshimu abiria wao na hata watumiaji wengine wa barabara.

Ilikuwa ni nadra sana gari kusimama kuruhusu watembea kwa miguu kuvuka kwenye vivuko vyao. Leo hii, tunashuhudia magari yanasimama kwenye vivuko vya waenda kwa miguu. Madereva wanaendesha kwa ustaarabu, huku wakiziheshimu alama za usalama barabarani. Hii ni hatua ya kupongezwa mno.

Watanzania tumejielekeza sana katika kukosoa na kulaumu. Hatutajielekeza katika kupongeza na kusifu pindi mtu anavyofanya vizuri. Na ikiwa mtua atafanya hivyo. Utasikia katumwa huyu. Mimi nimetumwa na dhamira yangu kama raia mwema wan chi hii, nampongeza IGP Siro na jeshi lake la Polisi.

Pamoja na mapungufu madogo madogo ambayo yanajitokeza katika jeshi la polisi, lakini ukweli unabaki pale pale kuwa IGP Siro amelinyoosha jeshi la Polisi na anatuhakikishia raia usalama wetu na mali zetu.

Nikuombe tu IGP Siro, ongeza kasi kidogo katika kitengo cha upelelezi kwani yapo malalamiko machache huku mitaani kwetu kuhusu ucheleweshwaji wa upelelezi wa kesi. Mimi ninakupongeza sana, siko peke yangu wapo mamilioni ya watanzania wanaokupongeza. Endelea kutimua askari wote wanaokwenda kinyume na maadili na miiko ya jeshi. Kongole IGP Siro, Mamimilioni ya Watanzania wapema amani na usalama wapo nyuma yako.