Home Burudani Jide komando asiyechoka

Jide komando asiyechoka

4200
0
SHARE

*Sasa arejea kishujaa zaidi

Na Mwandishi Wetu

Oktoba 26 mwaka huu, mkongwe wa muziki wa kizazi kipya anayeng’ara zaidi katika staili ya Afro Pop, Judith Wambura a.k.a Jide, atafanya onyesho la kufa mtu katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam ambalo litapambwa pia na wasanii wengine mahiri kutoka Uganda, Juliana Kanyomozi na mwingine kutoka Afrika Kusini, Zahara Bulelwa Mkutukana.

Wakati wakali wengi wa kike wa enzi hizo wakiwa tayari wameinua mikono juu kukubali matokeo na hivyo kukaa pembeni kuwapisha chipukizi kukamata nafasi ya kutamba, Jide ameendelea kufanya vizuri na kuzidi kujichotea mashabiki kadiri siku zinavyokwenda.

Akiwa na albamu saba kibindoni Machozi (2000),     Binti (2003), Moto (2005), Shukrani (2007), Ya 5. The Best of Lady Jaydee (2012), Nothing But The Truth (2013) na Woman (2017), msanii huyo ambaye pia ni maarufu zaidi kama Lady Jaydee, ndiye msanii pekee wa kike mwenye tuzo nyingi, za ndani na nje kuliko mwingine yeyote.

Jide mwenye a.k.a nyingi katika sanaa ya muziki, anathibitisha moja ya majina yake ya kisanii ya Komandoo, kwani licha ya kuendelea kufanya muziki, lakini pia anafanya kwa kiwango cha juu, akiwaacha kwa mbali chipukizi wa sasa, ambao hawakuwahi kukutana na changamoto kama alizokutana nazo mkongwe huyu katika miaka yake mingi kwenye tasnia.

“Wanawake tunanyanyasika sana katika huu muziki, ninataka kuwakomboa, maana wanaume wamekamata karibu kila sehemu katika muziki, wasichana wa sasa wanalazimika kutoa rushwa ya ngono ili waweze kutoboa. Wale wanaokataa ndiyo unaona kazi zao hazisikiki redioni wala hazichezwi katika vituo vya televisheni, ninataka kuandaa jukwaa ambalo wasanii wa kike litakuwa ni lao,” anasema Jide, ambaye anabainisha kuwa Vocals Night, mahususi kwa waimbaji, litakuwa ni onyesho la kila mwaka.

“Nina ndoto ya kulifanya onyesho hili kuwa ni la kila mwaka na lango lake kubwa ni kutaka kuwakomboa wasanii wanawake ambao wengine wanalazimika kuuza utu wao ili wafanikiwe katika kazi zao, maana kama unavyojua wanaume wameishika hii sanaa karibu kila sehemu.

“Kama mtu hayuko tayari kutoa rushwa ya ngono inakuwa ni vigumu kupenya katika soko, lakini mimi nataka niwe daraja lao. Ndiyo maana nimemchukua msanii kama Grace, anafanya kazi nzuri lakini hasikiki,” alisema Jide.

Msanii huyo ambaye ameendelea kubakia katika ubora wa juu kimuziki licha ya changamoto nyingi zilizowafanya wenzake wengi alioanza nao kutoweka, alisema katika onyesho hilo, anataraji pia kutoa zawadi ya nyimbo yake mpya ambayo ataitoa hivi karibuni.

Katika kunogesha onyesho hilo ambalo kiingilio chake kitakuwa ni shilingi elfu 25 kwa mashabiki wa kawaida, 50,000 kwa watu maalum na 150,000 kwa walio maalum zaidi, mshereheshaji wa tukio hilo anatarajiwa kuwa Uti Nwachukwu, ambaye ni mmoja wa washiriki wa Big Brother 5 All Stars mwaka 2010 ambaye alidumu kwa siku 91.

“Uti pia ni muigizaji kule kwao Nigeria, na nimemleta mahsusi ili kuchanganya ladha katika tukio hilo ambalo ninategemea kupata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wangu ambao siku zote wamekuwa sambamba na mimi, kiasi cha kunipa faraja kwelikweli,” alisema Jide.

Msanii huyo ambaye miungoni mwa nyimbo zake za hivi karibuni ni Baby na I Miss You, amewahi pia kufanya kazi na wakongwe wa muziki barani Afrika, kama Oliver Mutukuzdi wa Zimbabwe na Salif Keita wa Mali.