Home Makala JINSI DAWA ZA KULEVYA ZILIVYOATHIRI VIJANA

JINSI DAWA ZA KULEVYA ZILIVYOATHIRI VIJANA

1911
0
SHARE

NA FLORENCE SANAWA, MTWARA


DAWA za kulevya zimekuwa wimbo katika vyombo mbalimbali vya habari, huku mamlaka husika zikiendelea kutoa matamko kadha wa kadha ambayo yanaonyesha wazi kuwa ni mapambano makali juu ya kutaka kukomesha uingizaji, usafirishaji na utumiaji wa dawa hizo.

Mapambano hayo ambayo yamekuwa yakifanyika mara kwa mara yamekuwa chachu kwa vijana hasa wanaotumia, hivyo kuanza kutafuta namna wanavyoweza kujiokoa ili waweze kuwa miongoni mwa raia wema ili kuuungana na wengine katika ujenzi wa taifa.

Katika mkoa wa Mtwara, hali si tofauti na maeneo mengine ya Tanzania. Huku pia waathirika wakubwa ni vijana ambao kwa namna moja ama nyingine waliijiingiza katika utumiaji wa madawa haya na sasa baadhi wameathirika. Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Wedson Sichalwe anasema matumizi ya madawa hayo yameathiri vijana wengi mkoani hapa.

Anasema kuwa mwaka 2015, waathirika wa madawa ya kulevya waliofika hospitalini katika zahanati na vituo vya afya walikuwa ni 102 huku wengi wao wakiwa ni vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa. Idadi ya watumiaji iliongezeka mwaka 2016 na kufikia 169. Hilo ni ongezeko la watumia 67, hali ambayo ilipelekea vijana wengi wakapelekwa katika hospitali ya taifa Muhimbili ili waweze kupata dawa za methadol.

Sichalwe anasema kuwa, tatizo linaweza kusababisha matatizo ya akili sambamba na kupata matatizo mbalimbali kiafya ikiwemo magonjwa ya ngozi, maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikitegemea matumizi gani mwathirika alikuwa akitumia.

“Hapa tumejitahidi tunacho kitengo maalum kinachotoa huduma kwa watumiaji wa madawa hayo pamoja na kukosa ‘soba house’ na kutokuwa na dawa ya methadol, lakini tunajitahidi kuwashauri ili waweze kuachana na matumizi hayo ili kuwa na afya njema,” anasema Sichalwe

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopinga matumizi na uuzwaji wa madawa ya kulevya. Kutokana na hali hii, waagizaji, wauzaji na watumiaji wa dawa hizi wamekuwa wakifanya hivyo kwa siri kubwa. Kutokana na usiri huo, imekuwa ni ngumu kuwakamata na hivyo kusababisha ongezeko la watumiaji kadri siku zinavyoenda.

Hali hii inasababisha vijana wengi kuingia katika dimbwi la matumizi ya madawa hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yamewafanya wawe watumwa, hivyo kupoteza ndoto za vijana wengi ambao wamekuwa wakitumia madawa hayo mithiri ya dozi.

Kijana Yusuph Uwesu anasema kuwa, miaka ya nyuma aliwahi kufanyakazi ya udereva katika kampuni moja mkoani Tanga. Akiwa huko, alikuwa na marafiki wengi vijana ambao ndio walichangia yeye kuingia katika matumizi ya madawa ya kulevya.

Anasema kuwa alipogundulika kuwa anatumia madawa hayo, alifukuzwa kazi hatua ambayo ilimuongezea muda wa kuendelea kutumia madawa hayo hali iliyopelekea kuathirika kwa kiasi kikubwa.

Anasema kuwa matumizi ya madawa ya kulevya yanapunguza hadhi ya mtu hivyo kutokuwa na sifa ya kuajiriwa hali ambayo inawafanya vijana hao kujiajiri wenyewe ili waweze kupata pesa za matumizi hasa ya kununua madawa.

“Mimi nilipoacha kazi ndio matumizi yaliongezeka kwa kuwa sikuwa na kazi nilikuwa na muda wa kutosha kutumia madawa. Inaniuma sana kwa kuwa mimi ni dereva nimesomea lakini madawa ya kulevya yamenifanya nisiweze kuendelea hadi leo,” anasema Uwesu na kuongeza:

“Unapokuwa unatumia madawa ya kulevya hakuna mtu anaeweza kukuamini wewe kwa jambo lolote maana wengi huwa wanatuhisi kuwa ni vibaka wakati sio kweli.”

Naye Rashid Abdallah, mkazi wa Ufukoni Manispaa ya Mtwara Mikindani anasema kuwa, toka mwaka 1990 alikuwa mtumiaji mzuri wa madawa ya kulevya hali ambayo ili mfanya afungwe jela mwaka 1994 katika gereza la Keko.

Anasema kuwa, pamoja na kwamba ana miaka 42, bado anaendelea kutumia madawa ya kulevya, hali ambayo inazidi kumuathiri hasa anapoona watoto wake wakiwa wanaolewa na kupata wajukuu.

 

“Hivi sasa watoto wangu wamekuwa najua huwa najifikiria hivi ninapoozesha watoto wakati natumia madawa ya kulevya italeta picha gani mjukuu akifika na kukuta maskani unavuta madawa?….

“Ndio maana nimeamua kujirekebisha ili kuacha kabisa matumizi ya madawa hayo ili kuirudisha hali yangu ambayo niliifukuza wakati nikiwa natumia madawa ya kulevya,” anasema Abdallah.

Said Mohamed mkazi wa Chikongola Manispaa ya Mtwara Mikindani yeye ni mwathirika wa madawa ya kulevya kwa miaka mingi. Anasema kuwa watumiaji wengi wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kutumia madawa hayo hivyo kuwafanya washindwe kushiriki katika harakati mbalimbali za kujenga familia zao.

Anasema kuwa kwa kiasi kikubwa wamekuwa na hofu kutokana na sehemu kubwa ya jamii kuwatenga ikiwepo familia zao hali ambayo imewalazimu wao kujitoa ili waweze kuacha matumizi madawa hayo.

Mohamed anasema kuwa, pamoja na kuwa na familia lakini amekuwa akishindwa kuimudu kutokana na kushindwa kutoa huduma kutokana na pesa nyingi kuelekezwa kwenye madawa ya kulevya.

Anasema kuwa, amekuwa katika wakati mgumu katika maisha yake baada ya familia kumtenga hivyo kumfanya ashindwe kuendelea kutumia madawa hayo hivyo kujiunga na vijana wengine ili waweze kupata mabadiliko.

“Mwenzetu mmoja alikufa baada ya kutumia madawa ya kulevya kifo chake kilikuwa funzo kwangu. Kwanza alikuwa mtoto wa kike, mimi wa kiume familia inanitegemea nikaamua kuchukua hatua ili niweze kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya ambayo kwa sehemu kubwa yamekuwa yakighalimu maisha yangu na familia yangu.

“Ilifikia wakati nilitengwa na familia yangu kwa kuwa muda mwingi nimekuwa nikitumia madawa ya kulevya mara kadhaa huwa nashindwa hata kula, jambo hilo limenifanya niwe kama vile nimetelekezwa naumia sana ndio maana niko tayari kucha kutumia haya madawa…..

“Wengine hapa tuna taaluma zetu, lakini tunashindwa kukaa kufanya kazi kwakuwa hatuwezi kuaminiwa katika kazi zetu jambo hili linatufedhehesha. Ndio maana tukawa na nia ya dhati ili kuweza kubadilika kwa kuacha matumizi ya madawa ya kulevya ili kurudi katika kazi pamoja na kuwa karibu na familia zetu,” anasema Mohamed

Naye Seleman Seif, mkazi wa Mtwara Mjini anasema kuwa, jamii inapaswa kuwaelewa vijana wanaotumia madawa ya kulevya  na wanapasawa kutoa ushirikiano ili kusaidia wao kuacha matumizi ya madawa hayo.

“Unajua tunakosa nyenzo muhimu za kuweza kutuongoza katika maisha yetu. Ndio maana tukilala tukiamka hatuna la kufanya wala hatuna watu wa kutukumbusha nini tunapaswa kufanya….

“Mimi nimeathirika na madawa lakini hata sikumbuki nilianza lini lakini nikipata nafasi ya kufanya jambo jingine naweza kubadilika maana nimeona madhara makubwa niliyopata kwa kipindi chote nilichokuwa natumia,” anasema Seif