Home Makala JITU SON:

JITU SON:

35191
0
SHARE

 

Kama hatutobadilika kifikra tutaiona Serikali chungu

  • Kinachowatafuna wapinzani ni kulaumu badala

ya  kujenga hoja zenye mashiko kwa wananchi

  • Wabunge tutaendelea kuibana Serikali maana

        wananchi wameingia mkataba na CCM

NA GABRIEL MUSHI


BABATI ni mojawapo ya wilaya za mkoa wa Manyara ambazo zinasifika kwa kilimo cha mbaazi. Zao hilo la mbaazi ambalo sasa limedoda hulimwa zaidi katika mikoa ya Manyara na Arusha ambapo inakadiriwa kuwa tani kati ya 38,000-60,000 huzalishwa kwa mwaka.

Tanzania ni moja kati ya nchi za Bara la Afrika ambazo huzalisha mbaazi huku asilimia 95 huuzwa nchini India ambako sasa soko kuu la zao hilo limeshuka kutokana na nchi hiyo kujitosheleza kwa mahitaji ya zao hilo.

Hata hivyo, mtifuano mkali uliojitokeza katika Bunge la bajeti lililomalizika Juni 29 mwaka huu, kila mbunge alionekana kutetea wananchi wake kwa kuzingatia mazao ambayo huzalishwa kwa wingi katika jimbo lake.

Vivyo hivyo kwa Mbunge wa Babati Vijijini, Virajilal Jitu Son (CCM) naye anakiri kupigania wananchi wake katika Bunge hilo hasa baada ya kudoda kwa soko la mbaazi ambalo limeiathiri wilaya hiyo pakubwa.

Aidha, katika mazungumzo yake na RAI hakusita kuipongeza serikali kwa kuondoa kodi katika bidhaa zinazozalisha chakula cha mifugo hivyo kuwa ni nafasi nyingine kwa wananchi wake kujikwamua kiuchumi.

RAI: Kwa kuwa umekuwa mbunge tangu mwaka 2010 ni yapi maoni yako kuhusu Bunge la Bajeti ambalo limekwisha hivi karibuni?

SON: Hakika lilikuwa Bunge zuri kwa sababu tulipitia bajeti za wizara zote na kutoa ushauri kwa serikali ambao kwa asilimia kubwa umezingatiwa.

Kwa mfano katika sekta ya mifugo, serikali imeondoa kodi na tozo kwenye bidhaa za mifugo kama vile mashudu ya pamba, alizeti na virutubisho ambavyo vinatoka nje. Sasa chakula cha mifugo kinatakiwa kupatikana kwa bei rahisi na uamuzi huu utachochea kukuza wazalishaji wa ndani kwa kuwa hamna kodi.

RAI: Wapo baadhi ya wabunge wa CCM ambao walisimama kidete kutetea masilahi ya wapiga kura wao hatua iliyowafanya kuonekana ni wasaliti, je, ni kweli wanastahili kupewa sifa ya usaliti?

SON:  Hapana si wasaliti, hata waliokuwa wakipinga tozo ya mazuo ya korosho nje kuwa fedha hizo zisipitie serikali sasa wameelewa kuwa serikali haikukosea. Fedha za ushuru huo ni za serikali si za wakulima. Serikali huko nyuma ilikubali kuwapa ili kukuza  zao la korosho. Hadi sasa tumepiga hatua na mikoa mingi sasa inapanda mikorosho. Cha msingi ni kwamba Serikali hijasema kuwa haitapeleka fedha kwa wakulima ila tu mfumo uliotumiwa haukuwa sahihi.

RAI: Soko la mazao ya mbaazi, alizeti na mahindi  limeshuka kwa kiwango kikubwa huku Babati ikiwa ni moja ya wilaya inayotegemea mazao hayo. Je, umejipanga vipi kuwatafutia wakulima masoko ya uhakika ili wafaidike na mazao yao?

SON: Tatizo kubwa lililosababisha haya yote ni vitu vitatu, moja ni masoko ya uhakika kwa sababu wananchi wanajitahidi sana kuzalisha ufuta, alizeti, pamba na mbaazi kwa wingi. Babati ilikuwa inasifika kwa uzalisha wa mbaazi aina ya ‘white’ ambayo ilikuwa inasikifika duniani, lakini bei imeshuka kutoka 3000 kwa kilo hadi 500.

Na sasa hata mazao ya mahindi na mtama yameshuka vilevile, kwa hiyo wananchi hawanufaiki na mazao wanayozalisha.

Tunaangalia namna ya kuongeza thamani kwenye mnyororo wa uzalishaji, kwamba badala ya kuuza alizeti tuuze mafuta na kupata mashudu. Kwenye mazao yote tunaangalia namna ya kuongeza thamani.

Halmashauri yetu imejipanga kukaribisha wawekezaji mbalimbali kuna eneo pale Magugu tumetenga zaidi ya hekta 85 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vikubwa na vidogo. Eneo hilo lina miundombinu yote ikiwamo maji, umeme na barabara. Hivyo tumejipanga kuwakaribisha wawekezaji ili kuongeza ajira na thamani ya bidhaa.

RAI: Katika kipindi chote ulichochaguliwa kuwa Mbunge kuanzia mwaka 2010 unajivunia nini jimboni kwako?

SON: Tangu nichaguliwa mwaka 2010, nimeendeleza mengi ambayo wenzangu walionitangulia walianzisha, ila kubwa ni kujenga Chuo cha Ualimu Mamire ambacho kina miundombinu yote. Ni chuo cha kwanza ambacho kinaendeshwa kwa pamoja kati ya serikali na sekta binafsi. Pia ni cha kwanza kwa Mkoa wa Manyara.  Nimeboresha vyuo vya ufundi stadi (Veta). Lakini tumelenga kila tarafa kuwe na Veta ili kupunguza tatizo la ajira.

Katika miundombinu tumejenga madaraja makubwa kama vile Bonga kuelekea Endanakshani mpaka Dareda, ni madaraja makubwa ambayo yamerahisisha ukuaji wa sekta ya utalii kwa sababu yamefungua njia nyingi.  Halmashauri sasa itanufaika na vivutio vya hifadhi ya Tarangire na Manyara.

Katika sekta ya nishati tulianza na asilimia 14 leo tupo kwenye asilimia 52. Awamu ya REA III ikikamiilika tutakuwa tumefikia asilimia 85. Umeme umeanza kusambazwa katika vijiji vingi vilivyopo pembezoni na baadae vitafuata vya katikati.  Katika sekta ya mawasiliano tulikua asilimia 10 lakini sasa tupo asilimia 90.

RAI: Ni changamoto gani ambayo bado unaona ni pasua kichwa na huuoni uwezekano wa kuitatua?

SON: Maji ndio changamoto kubwa, tuna vijiji 102, kata 25 na vitongoji zaidi ya 400. Hapo ndio penye tatizo kubwa kwa sababu mahitaji ni makubwa sana ndio maana tukasisitiza bungeni kuongeza tozo ya Sh 50 kwenye mafuta ili kuboresha huduma ya maji kwenye maeneo mbalimbali.

Ila uwezekano wa kuitatua bado upo kwa sababu tunaendelea kuboresha huduma ila hakika bado hali ni mbaya sana.

SERIKALI

RAI: Ni miaka miwili na nusu sasa tangu Serikali ya awamu ya Tano iingie madarakani, je, imefanikiwa wapi na wapi pengine unaona imekwama na inapaswa kupatilia mkazo?

SON: Hakuna tulipokwama kwa sababu kila zama na kitabu chake, Mfumo uliopo sasa katika serikali ya awamu ya tano ni kwamba kama hutabadilika kifikra na kufanya kazi kwa bidii utaona ni chungu, kama hutofanya kazi hutofanikiwa.

Ukifuatilia kwa makini hakuna sheria mpya nyingi zilizoongezwa.. ni kwamba wameamua kusimamia tu kanuni na sheria zilizokuwapo.

Jambo la muhimu tunatakiwa kumuunga mkono Rais kwani hata suala la rushwa limepungua, wale waliokuwa wakipiga fedha za miradi ya wananchi vijijini wamepungua na tunaamini watakwisha kabisa.

Serikali imefanya mengi na sasa Babati imepewa Sh milioni 400 kuboresha kituo cha afya Magugu ambacho Waziri Kigwangala na majeruhi wenzake wamepewa matibabu pale baada ya kupata ajali. Hizo zote ni jitihada ambazo kwa pamoja tumeweza kuboresha kile kituo na baadae kufanikiwa hata kutoa huduma ya kwanza kwa waziri na majeruhi wengine.

Tumelenga kuhakikisha fedha hizo zinaenda pia katika vituo vingine vya afya ili kuboresha huduma za afya.

RAI: Kumekuwapo na kauli kutoka kwa baadhi ya wanasiasa, wasomi na hata wananchi wa kawaida kuwa miradi mikubwa kama ya ujenzi wa Reli  ya kisasa na ununuzi wa ndege haina tija ya moja kwa moja kwa wananchi, hili unalizungumziaje?

SON: Kauli hii kweli imesemwa sana, kwa mfano sasa kuna uchaguzi wa marudio huku Babati wapinzani wanasema ununuzi wa ndege hauna manufaa kwa wananchi wa Babati, si kweli kwa sababu huko nyuma sisi wabunge haohao tuliibana serikali kuuliza kwanini hatuna ndege wakati nchi ndogo kama Rwanda inatushinda.

Kwanza ndege ina manufaa mengine kwa sababu inaleta watalii ambao wanakuja kwenye mbuga zetu hapa Tarangire na Manyara ambazo kwa namna moja au nyingine tunapata pesa.

Ujenzi wa mradi wa umeme wa Stigler’s gorge; hatuwezi kufungua viwanda bila umeme, hatuwezi kufungua vituo vya afya kama hatutowekeza kwenye umeme. Kuwepo kwa umeme wa kutosha ndio mbinu sahihi ya kuboresha huduma nyingine.

Ujenzi wa reli nao una manufaa kwa wananchi wa Babati kwa sababu kutoka Babati hadi Dodoma ni saa mbili, hivyo reli ikikalimilika mwananchi anaweza kusafirisha mazao yake kutoka Babati hadi Dodoma kwa lori alafu Dodoma hadi bandarini kwa reli ambayo ni bei nafuu.

Hii itasaidia kusafirisha mazao yanayopelekwa nje ya nchi kwa urahisi kwa sababu sasa kusafirisha mazao kutoka Babati hadi Dar es Salaam kwa lori ni zaidi ya Sh milioni tatu.

RAI: Kwa nyakati tofauti Rais John Magufuli amekuwa akisema hadharani kuwa kuna baadhi ya mawaziri wake hawamuelewi, au hawajui wajibu wao. Unaweza kuzungumzia vipi kauli hiyo na unatoa ushauri gani kwa mawaziri hao?

SON: Hili suala linategemea mahali ambapo Rais ameweka kipaumbele, kwa mfano suala la kodi kwenye misaada inayoelekezwa kwenye huduma za kijamii kama elimu, afya na maji.

Awali waziri hakuwa na mamlaka ya kutoa msamaha wa kodi kwenye misaada hiyo, lakini sasa amepewa mamlaka hayo.

Kwa sababu mfadhili hawezi kutoa msaada alafu umpige kodi, hili ni jambo la ajabu na sasa tumefanikiwa kupata ule mkopo wa Sh trilioni moja kutoka India ambao utanufaisha wilaya 17 kupata huduma za maji.

RAI: Agosti 12 mwaka huu, kunatarajia kufanyika uchaguzi wa marudio katika kata 72 na jimbo la Buyungu. Hata hivyo wapinzani wamekuwa wakilalamikia rafu nyingi za chaguzi ambazo zinaharibu sifa ya demokrasia iliyokuwapo nchini. Hili unalizungumziaje?

SON: Sijaona rafu iliyochezwa, maeneo ambayo wagombea wao wamejaza fomu vizuri na wana sifa, tunashindana nao vizuri. Tatizo ni kwamba baadhi maeneo kama kata ya Babati na kule Hanang’  viongozi wa kitaifa wa upinzani badala ya kuzungumzia masuala ya kata husika kuhusu changamoto za maji, afya na elimu, wao wanazungumzia reli, bandari na ndege ilihali ni mambo ambayo hayawahusu kwenye kata zao.

Mwananchi wa babati ukimweleza kuwa serikali imechukua hela za korosho  sasa atakuelewa nini? Wananchi wanaweza kuhoji mbona hela za hifadhi ya Tarangre sisi hatunufaiki nazo badala yake tunanufaika Taifa zima?.

Wapinzania badala ya kwenda na hoja za maendeleo wanabali kulaumu tu. Katika saa nzima ambayo wanaongea ni dakika mbili au tano wanamnadi mgombea na mgombea huyo kuanza kuelezea sera zake. Wanasahau kabisa kuzungumzia shida za kata husika ambalo ndio hitaji la watu hao. Ukiwa mbunge unatakiwa ukatetee jimbo lako na pili mambo ya kitaifa ambayo yanawalenga moja kwa moja wananchi wako.

Sio kwamba kila jambo lazima utetee kwa sababu sasa hivi nikianza kutetea korosho, wananchi wangu watanishangaa linawahusu vipi ilihali mbaazi zimewadodea.

Siku hizi hakuna tena mambo ya kudanganyana kwa sababu mitandaon ya kijamii inaanika kila kitu hadharani. Mambo ya kudanganya hamna tena, watu wanatakiwa kuja na hoja kuwa tumefanya moja mbili tatu, tushindane kwa sera na maendeleo mambo ya kudanganya kama zamani hamna tena.

RAI: Hata hivyo wimbi la baadhi ya wabunge na madiwani wanaohamia CCM kutoka upinzani nalo linalamikiwa kuligharimu taifa kwa kuingia kwenye chaguzi ndogo kila mara. Hili nalo unalizungumziaje?

SON: Kipindi cha Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, wagombea wengi wa upinzani walikuwa viongozi wa CCM, kwa mfano Waitara au Kalanga ambaye alisema wazi kuwa hakutarajia kuwa mpinzani. Hili ni tatizo kubwa la upinzani kwani hata wale ambao hawajahama bado hawaruhusiwi kutoa maoni yao kwa uhuru. Uhuru wa kuzungumza ni jambo muhimu sana ndio maana Katibu mkuu wa CCM amesema akina Bashe na Nape ni haki yao kuzungumza na kuikosoa  na kuibana serikali.

Hata mimi mbunge wa CCM nikiona serikali haifanyi vizuri nitaibana tu, lazima nitetee chama changu na wananchi walionituma. Sio kwamba serikali ni yetu yaani ya CCM nitanyamanza, hapana kwa sababu wananchi wameingia mkataba na chama kuunda serikali.

Yale matakwa ambayo tunataka serikali iende isimamie lazima yatekelezwe kikamilifu,  watendaji wengine waliopo serikali kila mmoja ana uhuru wa kuchagua chama chake hujui kama wanakusaliti ama lah. Hivyo sisi wana CCM tukiwa wakali dhidi ya mawaziri wetu tukiona mahali ambapo wanaenda kinyume na ilani lazima watabadilika na tutaendelea kuwabana. 0715126577