Home Makala JK  alijitahidi kukuza demokrasia  

JK  alijitahidi kukuza demokrasia  

6368
0
SHARE

 

Rais mstaafu Jakaya Kikwete akizungumza na baadhi ya viongozi wa ChademaNA KIBONA DICKSON

DEMOKRASIA ya vyama vingi ilifutwa mwaka 1962 na kurejeshwa mwaka 1992.

Ifahamike kwamba mfumo wa vyama vingi haukurejeshwa kwa hiari ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) bali kwa mapambano ya kufa au kupona.

Wapinzani wa demokrasia ya vyama vingi walizidiwa na harakati za watetezi wa demokrasia ya vyama vingi, ndipo vyama vya upinzani vikaanzishwa mwaka 1992.

Kwa maana hiyo, demokrasia ya vyama vingi iliyorejeshwa mwaka 1992, ni matokeo ya jasho la watu kupambana.

Waliopambania demokrasia ya vyama vingi walikubali kupatwa na madhara yatokanayo na upinzani wa watawala.

 Baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatoa tangazo la nchi yenye mfumo wa vyama vingi kupitia sheria ya mwaka 1992 Na. 4 ibara  ya 5.

Kulingana na ibara ya 3 (i) Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na yqa kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Katika utangulizi wa Katiba ya JMT, baadhi ya maneno yanasomeka “ kwa hiyo Katiba hii imetungwa na Bunge kwa niaba ya wananchi- kwa ajili ya kuhakikisha Tanzania inaongozwa na serikali yenye kufuata misingi ya kidemokrasia, ujamaa na isiyokuwa na dini.

Baadhi ya misingi ya demokrasia ni uwepo wa vyama vingi vya siasa, uhuru (kutoa maoni, kukusanyika, kuandamana, kuabudu) na uvumilivu wa kisiasa.

Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992, inaeleza kufanyika shughuli za vyama vya siasa kwa uhuru nchini.

Jeshi la polisi kwa kuagizwa na watawala, limekuwa likiweka vikwazo vya shughuli za vyama vya upinzani.Vikwazo vimekuwa vikilenga mikutano na maandamano ya upinzani.

Kuandamana na kufanya mikutano ya hadhara ni haki na uhuru wa msingi kikatiba kwa watu na vyama vyao.

Linapokuja suala la haki na uhuru wa mtu au watu, dhima ya mamlaka si kuzuia bali kuhakikisha mtu au watu wapata au wanafurahia haki yako.

Haki ya msingi, haiondolewi na mamlaka au mtu yeyote. Ikitokea hivyo, ni ukiukaji wa haki ya msingi, katiba au misingi ya kidemokrasia.

 

Hali ya demokrasia 2005-2015:

Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, iliyoingia madarakani 2005, ilijitahidi kwa kiasi kikubwa kuhuisha na kukuza demokrasia nchini. Mwanzoni kabisa mwa utawala wake, Jk alionyesha dhamira ya kuhuisha demokrasia nchini.

 

JK na misingi ya demokrasia:

 Alihuisha baadhi ya misingi ya demokrasia ikiwamo

Uwazi

JK aliruhusu uwazi kwenye serikali yake. Katika kipindi chake, aliruhusu ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti mkuu Hesabu za Serikali(CAG) zisomwe bungeni.

 

Uhuru wa maoni
JK aliweka mazingira ya kashfa zote za kifisadi kufichuliwa katika majukwaa mbalimbali ikiwemo Bunge.

 

Uvumilivu wa kisiasa.

JK akiwa Rais aliteua hata wapinzani kuingia kwenye kamati au Bunge. Zitto Kabwe akiwa Chadema aliwahi kuteuliwa (2008) kuwa mjumbe wa tume ya kuangalia uwezekano wa kudurusu mikataba ya madini.

Uchaguzi wa mwaka 2010, James Mbatia(NCCR) aligombea ubunge Kawe na kugaragazwa vibaya na Halima Mdee(Chadema). Mbatia alipata bahati ya kuteuliwa na JK kuwa mbunge.

Kuelekea 2015, JK aliweka milango wazi ya kujadiliana na vyama vya upinzani kuhusu masuala yenye maslahi kwa taifa hususani suala la Katiba mpya; aliwahi kuwaita wapinzani ikulu na kuzungumza nao hatimaye kukubaliana baadhi ya mambo.

 

Kutenganisha madaraka

 Kwa kiasi fulani Bunge liliibana serikali na si serikali kulibana Bunge. Bunge lilionekana kuibana serikali katika masuala ya msingi kama bajeti, mipango ya muda mrefu na kashfa za ufisadi.

 

Uhuru wa vyombo vya habari.

JK aliruhusu vyombo vya habari kufanya kazi yake vizuri. Japokuwa kulikuwa na mapungufu yakiwamo kuvifungia baadhi ya vyombo vya habari.

Katika kila jambo jema changamoto hazikosekana. Katika utawala wa Kikwete kulikuwapo na mapungufu yakiwamo;

(i) kushindwa kuwachukulia hatua mafisadi.
(ii).Kushindwa kudumisha utawala wa sheria.
(iii) kutawala kwa matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu.
(iv) kuharibu mchakato wa katiba mpya.

 

Hali ya serikali ya sasa, awamu ya tano.

 Serikali ya sasa ya awamu ya tano iliyoingia madarakani 2015 chini ya Rais John Magufuli, ambayo bado haijatimiza hata mwaka mmoja, imegubikwa na changamoto kubwa yenye kila dalili ya kuua demokrasia nchini.

 

JPM na misingi ya demokrasia.

  1. Serikali kudhibiti mhimili wa Bunge

 Ili kufikia malengo ya kudhibiti Bunge, serikali ya Magufuli ilihakikisha anapatikana Naibu Spika Tulia Ackson ambaye ni mbunge wa kuteuliwa na rais. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanadai kwamba uteuzi huo ni wa kimkakati.

 

Kuzuia uwazi

 Ni marufuku kurusha moja kwa moja vikao vya Bunge wakati wa mijadala muhimu ikiwamo bajeti.

 

Kukandamiza uhuru wa mawazo

 Uhuru wa mawazo wenye mwelekeo wa kukosoa mwenendo wa serikali unakandamizwa, kila mtu anatakiwa kuisifu serikali ya JPM na si vinginevyo.

 

Kukandamiza upinzani

Vyama vya upinzani vinakandamizwa ndani na nje ya Bunge.

Jeshi la polisi linatekeleza maagizo wa watawala ya kuzuia mikutano, maandamano na hata vikao vya ndani kwa kisingizio cha intelijensia.

Lakini, inteligensia hiyo hiyo ya polisi, inashindwa kung’amua uhalifu unaofanyika nchini likiwamo tukio la mapango ya Amboni na mauaji ya kikatili kwa watu wasio na hatia.

 

Utawala wa sheria

 Watumishi wanachukuliwa hatua bila kufuata sheria za utumishi wa umma kwa kisingizio cha kutumbua majipu.

Kwa mfano, katika mkutano mmoja rais aliuliza tu umati wa watu “huyu tumfanye nini!!” Umati ulimjibu…atumbuliwee..rais alimsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe (marehemu)

 

Uhuru wa vyombo vya habari.

Serikali ya JPM, ilianza kazi kwa kulifungia milele gazeti la Mawio. Huu ulikuwa ujumbe kwa vyombo vingine vya habari vitakavyokuwa na tabia ya kukosoa serikali ya yake.

 

Hitimisho.

Kwa kukiuka misingi ya kidemokrasia ni sawa na kuielekeza nchi kwenye njia ya utawala wa kiimla. Haifa taifa lifuke huko.

Ujasiri wa kimapambano kama ule wa vuguvugu la kupigania vyama vingi miaka ya tisini, unatakiwa urejea tena kwa watu ili kulinda na kutetea demokrasia na kupinga ukandamizaji wa kisiasa.

 Tuwasiliane:0754575524.

Kibonadickson@ymail.com