Home Latest News JOHN CHILEMBWE: MCHUNGAJI ALIYEWEKWA KWENYE NOTI YA KWACHA MALAWI

JOHN CHILEMBWE: MCHUNGAJI ALIYEWEKWA KWENYE NOTI YA KWACHA MALAWI

6408
0
SHARE

 NA KIZITO MPANGALA                  |                    


Kila noti katika kila nchi haikosi picha ya mtu fulani ambaye anaaminika kwa jambo fulani. Nchini Tanzania tunaona picha za Mwalimu J.K. Nyerere, A.A. Karume na A.H. Mwinyi. Hii ni kutokana na huduma zao nchini. Jamii hupata mafundisho mbali mbali kutoka kwa watu wa namna hiyo.

Nchini Malawi, John Kaundama Chilembwe anakumbukwa katika noti mojawapo za fedha ya nchi hiyo. John Kaundama Chilembwe alizaliwa, 1871 katika Mji wa Sangano, Wilaya ya Chiradzulu, Mkoa wa Kusini, Nyasaland (sasa ni Malawi).

John Chilembwe alizaliwa katika familia iliyokuwa na muingiliano wa makabila. Baba yake, Mzee Kaundama, alikuwa Myao na mama yake, Nyangu, alikuwa Mmang’anja. John Chilembwe kabla ya kubatizwa na wazungu kutoka Scotland, mwaka 1890, alikuwa akiitwa Nkologo Kaundama Chilembwe.

Mwaka 1892, John Chilembwe aliajiriwa kama mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya Joseph Booth, mmisionari wa kujitegemea. Joseph Booth aliwasili Malawi mwaka huo huo 1892, na kuanzisha misheni yake katika eneo la Zambezi karibu na Mji wa Blantyre (sasa ni Jiji). Aliwashawishi wenyeji kujiunga na kanisa lake. Baadaye aliongeza misheni zingine saba nchini Malawi.

Akiwa katika kazi nyumbani kwa Joseph Booth, John Chilembwe alipendezwa na ukarimu wa Booth na pia alipendezwa na mafundisho ya dini aliyokuwa akiyapata kutoka kwa Booth. Mwaka 1897, Joseph Booth alirudi Ulaya na alirejea tena Malawi mwaka 1899. Na mwaka 1902 alirudi moja kwa moja Ulaya na kuwaacha John Chilembwe na Elliot Kamwana wakiwa waumini waaminifu.

Mwaka 1897, Chilembwe alisafiri pamoja na Joseph Booth hadi Marekani. Licha ya misukosuko mbali mbali ya usafiri, waliwasili Marekani na kupokelewa na mchungaji Lewis Gordon.

Baadaye, John Chilembwe alianza masomo ya Teolojia katika seminari ya Lynchburg, mjini Virginia. Seminarini hapo, Chilembwe alisoma pia historia ya Wamarekani weusi.

Mwaka 1899, John Chilembwe alitawazwa kuwa mchungaji hapo hapo seminarini, Lynchburg, Virginia. Aliendelea na masomo mengine ya kichungaji akiwa tayari mchungaji. Mwaka 1900 alimaliza kozi hiyo na alirudi nchini Malawi kwa msaada wa washirika wa kanisa la seminarini aliposoma.

Akiwa Malawi katika kanisa ;lake la P.I.M (Providence Industrial Mission), wilayani Chiradzulu, miaka 12 ya mwanzo wa kazi ya uchungaji, aliwahimiza wenyeji kuwa na nidhamu na kuchangamkia fursa za elimu, uwajibikaji katika familia na kuwa na bidii katika kazi.

Aliungwa mkono na Wakatoliki waliokuwa nchini humo, ingawa mahusiano yake na Wakatoliki yalikuwa si makubwa. Baada ya mwaka 1912, John Chilembwe alishawishi makanisa mawili ya wenyeji kujiunga naye ili kuwa kanisa moja.

Mwaka 1913, John Chilembwe alianza kujihusisha na siasa kwa nguvu. Alipinga sheria ya umiliki wa ardhi kwa wenyeji na hali mbaya ya maisha ya vibarua katika eneo ambalo alizaliwa.

Mwaka 1915, alidaiwa kuhubiri na kutoa vitisho vya kuanzisha ghasia dhidi ya Wazungu. Lakini sehemu kubwa ya mahubiri yake ilikuwa ni kuhimiza umoja na bidii ya kazi kwa wenyeji. Kisha alianza kuwabatiza waumini wapya katika kanisa lake bila kuwapa muongozo wa sababu ya kubatizwa kama yafanyavyo makanisa ya aina yake sasa.

Chilembwe alipata changamoto mbali mbali licha ya kuwa Mwafrika aliyepata elimu ya Magharibi. Alexander Livingstone alizuia Wafrika wasipate elimu kwa kuwa hawakustahili.

Hivyo, eneo ambalo Chilembwe alikuwa anaishi ambalo pia lilikuwa na watu wengi, Wazungu walimiliki sehemu kubwa ya ardhi na walizusha kodi ambayo iliwaumiza wenyeji wengi akiwemo John Chilembwe.

Makanisa yote ya Waafrika yalifungwa na walizuiwa kujihusisha na masuala ya dini. John Chilembwe aliibuka na kuwa msemaji wa watu wa Malawi (wakati huo iliitwa Nyasaland), na walipojaribu kuanzisha kanisa jingine lilichomwa moto na Alexander Livingstone ambaye aliona kwamba kupitia makanisa hayo, Wamalawi wakiongozwa na John Chilembwe, walikuwa wakitetea haki zao za msingi hasa katika umiliki wa ardhi jambo ambalo Alexander hakupenda.

Chilembwe alichukizwa na namna wenyeji walivyokuwa wakitendewa, hasa wale waliopata elimu wakati huo. Chilembwe alidai kuwa na wawakilishi wa wenyeji katika serikali ya kikoloni. Wale ambao walipata elimu zaidi yake aliwachukua na kuwa makamanda katika himaya yake.

Chilembwe alipata taabu sana kutoka kwa Wazungu ambapo walikuwa wakimpa taabu, ili aachane na wazo lake la kuzusha ghasia. Wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia, watu 19,000 walichukuliwa kuhudumu katika vita.

Zaidi ya hapo, yapata watu 200,000 walilazimishwa kushiriki katika vita hiyo ya dunia. Sepetemba 1914, Chilembwe aliliandikia barua gazeti la ‘Nyasaland Times’ liandike habari kwamba watu wake wengi wamemwaga damu katika nchi yao vitani na walilazimishwa kushiriki vita isiyo yao. Aliunda vikundi vya mapigano.

Aliwachukua zaidi wale waliopata elimu Jijini Blantyre na maeneo mengine. ili walete morali zaidi.  Serikali ya kikoloni ilizuia kuchapishwa kwa habari hiyo iliyotumwa kama barua, na mwaka huo huo, John Chilembwe alihesabiwa kuwa mchochezi kutokana na kukataliwa kuchapishwa barua yake gazetini.

Disemba 1914 na Januari 1915, John Chilembwe na kikundi chake waliazimia kuivuruga serikali ya kikoloni kwa ghasia na kuiondoa. Lakini alipata tetesi kwamba serikali ilidhamiria kumpeleka Mauritius kama adhabu ikiwa angeanzisha ghasia. Hivyo, Chilembwe alisogeza mbele muda wa kufanya ghasia ili asikamatwe.

Mpango wa kwanza wa Chilembwe na kikundi chake, ulikuwa  ni kuwavamia wakoloni katika eneo ambalo alizaliwa ambako ndiko kulikuwa na watu wengi, na mpango wa pili ni kuvamia makazi ya wakoloni. Mipango yote hii ilidhamiriwa kufanyika kwa pamoja. Wapiganaji wengi wa Chilembwe walitoka katika kanisa lake.

John Chilembwe alitumaini kwamba wenyeji walionyang’anywa ardhi yao na ndugu za askari waliokufa vitani, wangejumuika naye katika mipango yake ya kuwavamia wakoloni. Mpango aliofaulu ni mmoja tu kwa kuwa wapiganaji wengi hawskushiriki kikamilifu.

Alivamia makazi ya wazungu na kuua wanne, pia wenyeji wawili waliuawa. Sehemu kubwa ya ghasia aliyozusha haikupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wazawa.

Chilembwe alikamatwa na kuuawa akiwa katika mchakato wa kutorokea Msumbiji. Washirika wake wengi pia walikamatwa na kuuawa. Watu wengi walimlaumu John Chilembwe kwa kuchanganya siasa na masuala ya kidini.

Baada ya uhuru, serikali ya Malawi iliweka kumbukumbu ya picha yake kwenye noti mojawapo ya Kwacha ya Malawi tangu mwka 1997 hadi mwaka 2012 ambapo noti mpya zilichapishwa.

Kwa sasa noti ya Kwacha 500 inatumia picha ya John Chilembwe. Na mwaka 2016, Malawi ilichapisha noti mpya ya Kwacha 2,000 ambayo pia imetumia picha ya John Chilembwe.

Januari 15 kila mwaka ni siku ya kumbukumbu ya John Chilembwe nchini Malawi. Chilembwe anakumbukwa pia kwa kuhimiza umoja, nidhamu na bidii ya kazi. Mambo hayo ni muhimu kwetu sote na si kwa Malawi pekee.