Home Makala John Komba- ‘Ng’osi’ kutoka Lituhi, mwanajeshi aliyepeleka sauti nzito kwenye siasa

John Komba- ‘Ng’osi’ kutoka Lituhi, mwanajeshi aliyepeleka sauti nzito kwenye siasa

513
0
SHARE

GERALD JOHN KOMBA

KILA mwanadamu amekuja duniani kufanya shughuli yake aliyotumwa na Mwenyezi Mungu. Sote tunaamini kila mtanzania anao wajibu wake kuilinda na kuijenga Tanzania, na pia amekuja duniani kutimiza majukumu aliyokabidhiwa na Mungu.

Kwahiyo iwe kwenye siasa, uchumi, sanaa, kilimo, ufugaji, uvuvi, usafirishaji, uhunzi, ujenzi, na nyingine zozote halali ni sehemu ya wajibu waliokabidhiwa wanadamu kutekeleza hapa duniani.

Hivi ndivyo ilikuwa kwa John Komba na wengineo. Hivi ndivyo ilivyo kwangu na watu wengine. Kila mmoja ameandikiwa kazi yake hapa duniani na muda wake ukitimia ataondoka kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Katika hilo ndipo nawiwa kusema machache katika wasifu wa marehemu John Komba ambaye ana jina kubwa kwenye siasa za nchi hii pamoja na upande wa burudani.

Jkina lake kamili ni John Damiano Komba Chintetema. Ingawa wakazi wa mji wa Lituhi uliopo wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma walipendelea kumwita kwa jina la utani la ‘Ng’osi’. Neno ‘Ng’osi’ linatokana na lugha ya jamii ya Wamanda ambao ni wenyeji wa mji wa Lituhi, lina maana ya mwanaume, lakini wengi wanaoitwa jina hilo wanalengwa kuoneshwa kama ‘watu shupavu’ yaani mahiri katika kutenda na kutekeleza jambo fulani pamoja na imani ya watu kwa mhusika.

KUZALIWA NA ELIMU; KUKUTANA NA KAWAWA

John Komba alizaliwa Machi 18 mwaka 1954. Alisoma Shule ya Msingi Lituhi mjini Lituhi wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma. Baadae alikwenda kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea (Songea Boys) iliyopo Songea, mkoa wa Ruvuma.

Akiwa Songea Boys ndiko alikutana na Mzee Rashid Mfaume Kawawa ambaye alifurahishwa sana na umahiri wake kuongoza bendi ya shule hiyo. Walipokuwa Songea Boys, Mzee Kawawa alimshawishi John Komba kujiunga na Jeshi, ambapo mwaka 1978 alipelekwa katika kambi ya Kreluu iliyopo mkoani Iringa.

KIFUNGUA MIMBA

Katika familia ya Mzee Damiano Komba, walizaliwa jumla ya watoto watatu. John Komba alikuwa wa kwanza kuzaliwa katika familia hiyo, ambapo mtoto wa kwanza huitwa kifungua mimba. Baadaye alifuatiwa na ndugu zake wengine wawili; Emilian Komba na  Elias Komba (ambaye alifariki baadae).

NDOA NA WATOTO

John Komba alifunga ndoa na Salome Mwakangale mwaka 1979. John Komba alifanikiwa kupata watoto watoto 11. Mtoto mmoja alifariki dunia ikiwa ni miaka miwili tu na mwezi mmoja tangu kufariki baba yake (Claudia Komba).

Watoto waliobakia ni Andrew John Komba,Serafina John Komba, George John Komba, Julius John Komba, Gerald John Komba, Julieta John Komba, Juliet John Komba, Lilian John Komba, Herman John Komba na Elias John Komba.

JESHI NA MUZIKI

Alikaa Jeshini kwa muda fulani, lakini mwaka 1992 aliamua kuacha baada ya siasa ya vyama vingi kuingia ambapo Mzee Ally Hassan Mwinyi kumshawishi aingie katika siasa na kuasisi bendi ya Tanzania One Theatre (TOT) akiwa Mkurugenzi mtendaji. Aliacha Jeshi akiwa katika nafasi ya Kapteni.

Katika harakati za muziki, bendi ya TOT ilipitia vipindi mbalimbali chini ya uongozi wa marehemu Kapteni John Komba. Awali ilikuwa ikiitwa Tanzania One Theatre (TOT) kabla ya baadaye kuitwa TOT Plus Band.

Baada ya mabadiliko ya bendi hiyo yalimleta mwanamuziki mahiri Banzastone, ambapo kipindi hicho iliitwa TOT PLUS kama bendi ya burudani, ikiwa inafanya maonyesho mbalimbali kote nchini ilipiga hatua kubwa zaidi sokoni. Wakati huo Banzastone alitamba na wimbo wa ‘Elimu ya Mjinga’ ambao uliwika mno kwenye tasnia ya sanaa.

MBIO ZA UBUNGE

Katika harakati za kisiasa, Kapteni John Komba amewahi kujaribu kugombea ubunge katika jimbo la Songea Mjini lakini hakufanikiwa. Miaka michache baadaye alishawishiwa agombee jimbo la Jimbo la Nyasa ambapo mwaka 2005 alishinda nafasi hiyo na kuwa mbunge rasmi hadi mwisho wa uhai wake mwaka 2015.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2005 Komba alikuwa kwenye ile kambi iliyojulikana kama ‘Mtandao’ ikiwajumuisha wanasiasa wakubwa kama vile Jakaya Kikwete, Bernad Membe, Edward Lowassa, Dkt. Emmanuel Nchimbi ba wengineo.

HELKOPTA KWENDA LITUHI

Simulizi mojawapo ya kufurahisha katika maisha ya John Komba ni wakati wa ziara ya Benjamin Mkapa akiwa Rais, barabara ya kutoka Kitai kwenda Lituhi ilikuwa ikipitika kwa tabu sana, kiasi kwamba viongozi wa serikali walitaka kumleta Rais Mkapa kwa helicopter,mkapa akashangaa inakuwaje Tanzania kuna barabara mbovu kama ile ndipo juhudi za kuitengeneza zilianza hadi leo ipo kama inavyoonekana.

NYIMBO ZA NYERERE

Miongoni mwa sifa kubwa aliyokuwa nayo Kapteni Komba ni uwezo wake wa kutunga nyimbo zenye hisia kali. Mojawapo ya nyimbo hizo ni zile zinazozungumzia kifo cha Mwalimu Nyerere kilichotokea Oktoba 14 mwaka 1999. Wimbo wa “Kwaheri Mwalimu” ulipokelewa kwa heshima kubwa na kuwa kumbukumbu kila maadhimisho ya kifo cha Nyerere yanapofanyika.

URITHI

John Komba ameacha mtoto ambaye ni mwanasiana na mwanamuziki kama Baba yake, Gerald John Komba. Mtoto wake Gerald John Komba, amekuwa katika mapambano ya dhidi ya dawa za kulenya nchini Tanzania. Kijana huyo aliyezaliwa mwaka 1986 jijini Dar es salaam, ameonyesha nia ya kufuata nyayo za baba yake kwa kutoa wimbo wenye maudhi ya kwaya, ikiwa ya kupiga vifa dawa za kulevya.

KIFO

John Komba alifariki dunia Februari 28 mwaka 2015. Hadi kifo chake kilipotokea, alikuwa Mbunge wa Jimbo la Nyasa.