Home Makala JOKATE: CHANGAMOTO ZINANIPA ARI KUTUMIKIA JAMII

JOKATE: CHANGAMOTO ZINANIPA ARI KUTUMIKIA JAMII

667
0
SHARE

NA GRACE SHITUNDU


KUKATA tamaa ni hali ya mtu kupoteza tumaini au imani juu ya matarajio au malengo ambayo amejipangia.

Mara nyingi wanawake wanashindwa kufikia malengo au maono yao kutokana na kukata tamaa wao wenyewe au kwa kukatishwa na watu wanaowazunguka.

Hii inakuwa tofauti kwa aliyekuwa Miss Tanzania namba mbili mwaka 2006, Jokate Mwegelo, ambaye hakubali kukatishwa tamaa na mtu yeyote, hali inayomwezesha kufanya vitu vingi tofauti.

RAI ilifanya mahojiano na mrembo huyo ambaye pia ni mwigizaji, mwimbaji, mtangazaji,  mjasiriamali (akiwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kidoti) na sasa ameingia kwenye siasa, ambapo ni kiongozi wa vijana kama Kaimu Katibu Idara ya  Uhamasishaji na Chipukizi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Jokate amezaliwa miaka 30 iliyopita na kusoma Shule ya Msingi Olypio -Upanga, elimu ya sekondari ameipata katika Shule ya Mtakatifu Antony na kidato cha tano na sita katika shule ya Loyola High, kisha kujiunga na kuhitimu shahada ya sanaa katika sayansi ya kisiasa na falsafa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Aidha, baada ya kuingia kwenye siasa, baadhi ya vijana wenzake wa CCM wamekuwa wakilalamika katika mitandao ya kijamii kutokana na yeye kupewa nafasi ndani ya UVCCM ilhali bado hajapata uzoefu wa kutosha wa kukitumikia chama.

Kutokana na hali hiyo, Jokate anasema daima huwa harudishwi nyuma na maneno yanayosemwa.

“Katika maisha wanasema daima mti wenye matunda ndio hupigwa mawe, hivyo sikati tamaa na hii nawaambia na wengine wasikate tamaa katika mambo wanayodhamiria kuyafikia.

“Yalipotokea hayo nilijiangalia mimi mwenyewe na kuwalinganisha na hao waliokuwa wakisema kwenye mitandao, nilijiona kuwa nafaa tofauti na wanavyodai.”

Anaongeza: “Kwa yale yaliyosemwa nikaona ni kweli wengine wamezoea kuniona katika tasnia ya sanaa na watu wengi tunaonekana tukiwa katika sanaa ni wasanii tu, ni kama watu ambao hatuaminiki.

“Lakini mimi nina upande mwingine wa kutumikia watu, nina upande ya kusoma na si kusoma tu kwa kupita, nimesoma na nimefaulu vizuri pale UDSM na nilibakishwa kusoma Master, pengine sasa ningekuwa Dk. Jokate Mwegelo, lakini nikasema ngoja niingie tu mtaani, kwa hiyo nikiangalia mimi mwenyewe uwezo wangu binafsi najiona natosha.”

Hata hivyo, Jokate anasema watu hao waliosema maneno hayo wamempa ari ya kufanya kazi kwa bidii na haijamvunja moyo, kwa kuwa hakuna mtu hata mmoja aliyepata mafanikio bila kupata changamoto na ukiona kuna changamoto ujue mafanikio yapo karibu.

Akizungumzia mikakati katika uhamasishaji na chipukizi, Jokate anasema ipo mingi, ikizingatiwa chama hicho kina misingi ya kuwa na hazina ya viongozi.

Anasema hajawahi kuwa chipukizi, lakini anaamini anatosha kwa kuwa hajawahi kuamini kuwa amevunja maadili na amekuwa msichana anayeyasimamia kwa kiasi kikubwa.

Anasema matarajio yake katika siasa ni kutumikia watu kwa weledi waweze kupata manufaa kwa utumishi na hatarajii kugombea nafasi ya ubunge kwa sasa.

“Nimekuwa ni mtu wa kufanya mambo mengi kutokana na kulelewa na bibi yangu ambaye alikuwa ni mwasisi wa UWT Mkoa wa Ruvuma miaka ya nyuma.

“Bibi yangu alipendwa na watu kwa kuwa alikuwa anapenda watu na kujitoa, alikuwa maarufu kama bibi Danidani, hakufanikiwa kusoma, lakini alihakikisha watoto wake wote wanasoma.

“Nimekulia mazingira hayo, nimekuwa mtu wa kujitoa katika sehemu zote nilizosoma na watu wananiamini kuwaongoza, napenda kuona tunatoka pointi A kwenda B,” anasema.

Aidha, anasema mwaka huu ndio ameingia rasmi kwenye siasa na kuteuliwa kuwa kiongozi katika UVCCM  na umoja huo unatakiwa kutumika kama chombo na vijana kuwafikia viongozi walioko serikalini.

“Ni lazima tubadilike kwa kuangalia changamoto wanazokutana nazo vijana tuweze kuzisemea, pia ni jukumu letu na kuwahamasisha vijana kushiriki katika uongozi, si lazima katika siasa, lakini hata katika shughuli wanazofanya,” anasema.

Anasema kijana awe mfano kwa kutengeneza njia kwa wengine kwa kutumia ubunifu wake na kipaji na ni lazima vijana wafunguliwe akili kwa kuwa changamoto siku zote zipo.

Anasema Kidoti imekuwa ni sehemu ya vijana ambapo wengi huenda kujifunza mambo mbalimbali.

“Nilianzisha Kidoti miaka minne iliyopita na nilipoanza kufanya vitu tofauti watu walianza kunikatisha tamaa kuwa kila kitu nafanya mimi, lakini niliendelea na kwa upande wangu ilikuwa ndio sehemu ya kuanzia.

“Napata nafasi ya kupitia yale niliyopitia na kuweza kusimama, jukumu langu kuwatia moyo vijana, mazingira yetu yana changamoto nyingi, kwa hiyo ukipata mtu anayekutia moyo inasaidia, inakufanya uweze kuweka bidii,” anasema.

Pamoja na mambo mengine, anasema anapenda kuzungumza na vijana na kuwahamasisha kwa sababu anajua nguvu iliyopo katika kumuinua mtu mmoja.

“Tuna brand ya Kidoti inajihusisha na utengenezwaji na usambazaji wa nywele, bidhaa mbalimbali na bidhaa yetu kubwa kwa sasa ni nywele na tupo pale Kariakoo tuna nywele mbalimbali na hivi karibuni tuna msanii wetu mkubwa hapa Tanzania atakuwa kama balozi wetu

“Vilevile tuna mabegi, tuna aina tano ambazo tumezitambulisha mwaka huu, natumaini baadaye nitaingiza zaidi vitu vya shule, nina mpango wa kuingiza notebook, counter book, pen, pencil, nadhani itakwenda mwakani na tutaagiza aina nyingi zaidi za mabegi.

“Tulikuwa na slipper, lakini tulipata nazo changamoto, sisi tuliona kuna sehemu tunaweza kuziboresha, ingawa watu walizipenda na pia tulijaribu kutambulisha  mafuta ya kupaka –lotion, ilibidi niwe nayo makini kwa kuwa ni kitu ambacho kinagusa ngozi, hivyo kinaweza kuleta madhara endapo hautakuwa makini, kwa hiyo mchakato wake unakuwa mrefu na bado tunaifanyia kazi.”

Anasema pia anafanya mambo ya kijamii  ambapo alianzisha kampeni ‘Bekidotified’, lakini sasa yeye na washauri wake wanafikiri kubadilisha kampeni hiyo na kuwa na taasisi itakayosimama yenyewe.

“Kuwa taasisi itawafanya waweze kuaminika na  kushirikiana na taasisi kubwa, kwa mfano mwaka jana tulijenga kile kiwanja cha basketball, tulishirikiana na Mo Dewji. Foundation ile ifanikiwa kwa kuwa tu  Mohamed Dewji ni mtu ambaye amenisapoti katika biashara zangu tangu nimeanza harakati zangu”.

Katika shughuli za kijamii, Jokate anasema aliandaa bonanza la michezo lililokusanya wanafunzi mbalimbali wapatao 3,000, ambao walionyesha vipaji vyao katika Shule ya Sekondari Jangwani.

“Na niliona vipaji vingi, ulikuwa ni mwanzo mzuri, niliona natakiwa kufanya jambo kubwa zaidi, kwa utafiti wangu mdogo nikagundua kuwa shule nyingi za serikali hazina maeneo ya michezo kwa ajili ya watoto na watoto hawajifunzi tu darasani, bali wanajifunza pia nje ya darasa, kama kufanya usafi, kusafisha kiwanja, kushiriki na watoto wenzie ktika michezo inasaidia sana kumjenga mtu.”

Anasema wakajega kiwanja cha two in one ambacho ni cha mchezo wa kikapu na pete na kwa kiwanja hicho kimezaa timu ya kikapu iliyoshiriki ligi ya Junior mwaka huu.

Kuhusu kuwa mama, Jokate anasema anapenda watoto sana na anatamani kuwa na watoto mapacha ambao wakifika umri wa miaka 10 waende kijijini kujifunza zaidi.

Katika kujiepusha na skendo, Jokate anasema anapenda kukaa nyumbani na familia, si mtu wa kutoka, hata ikiwa hivyo ni majukumu ya kikazi.