Home Makala Jonas Savimbi alikuwa muasi au ukombozi?

Jonas Savimbi alikuwa muasi au ukombozi?

2089
0
SHARE

NA FRANCIS DAUDI

Tulipokuwa tunakua, mtoto mtundu na mkorofi, aliitwa SAVIMBI, kwa wakati huo sikujua Savimbi maana yake nini. Mara nyingine nilihisi ni jina maalumu kwa watu wakorofi. Historia ilifungua macho yangu!

Baada ya nchi nyingi za Afrika kupata uhuru bado zilitumbukia katika mapinduzi na kila aina ya ghasia. Hii ilitokana na sera za mataifa makubwa kutaka kuendelea kuyatawala mataifa hayo huru, ukabila, vita baridi na uchu wa madaraka waliokuwa nao wapigania ukombozi. Historia ya Afrika na hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara, kamwe haitamsahau Jonas Savimbi.

Jonas Savimbi ni nani?
Huyu alikuwa kiongozi mkuu wa  kikundi cha wapiganaji wa msituni—United Front for the Total Independence of Angola (UNITA). Aliongoza vita vya msituni vya muda mrefu kuliko vyote Kusini mwa Afrika.

Jonas Savimbi akiongoza vuguvugu la UNITA lilipelekea vifo vya zaidi ya watu milioni moja na maelfu ya wakimbizi nchini Angola. Kipindi chote cha takribani miaka 27, alikuwa akisaidiwa na Serikali ya Marekani na serikali ya kidhalimu ya mabeberu wa Afrika Kusini. Hivyo kwa mataifa ya Magharibi aliitwa Mpigania Ukombozi wa Angola Mpya!

Savimbi alizaliwa Agosti 3, 1934 na, kufariki Februari 22, 2002 kutoka na shambulio la kushtukiza lililofanywa na jeshi la Angola! Alikuwa ni wa kabila kubwa zaidi Angola la Ovimbundu na alikulia Jimbo la Kusini lililoitwa Moxico.

Savimbi alikuwa ana uwezo wa kuongea lugha sita kwa ufasaha kabisa—Kiingereza, Kifaransa na Kireno. Baada ya masomo yake huko Ulaya kati ya miaka ya sitini, alirudi na kujiunga na Vijana wa MPLA kupigana vita vya msituni dhidi ya Wareno!

Kutokana na mgogoro ndani ya MPLA, alijiunga na kundi la National Liberation Front of Angola (FNLA), mwaka 1964. Savimbi alikuwa mwenye uelewa mkubwa wa mbinu za kupigana vita. Mara kadhaa alikwaruzana na viongozi wa FNLA na hatimaye akaamua kuanzisha kundi lake lililoitwa UNITA mara baada ya kupata mafunzo maalumu nchini China.

Kulingana na taarifa za siri, Savimbi aliamua kufungua mazungumzo na wakoloni wa Kireno, ili waweze kumwachia nchi. Alikubali kupigana dhidi ya MPLA na FNLA katika operesheni maalumu ya kijeshi iliyopewa jina la Operation Timber (Maelezo yake yapo ndani ya kitabu cha Prof. Gerald Bender ).

Kufikia mwaka 1974, Wareno walishindwa kuhimili vita vikali vilivyoongozwa na MPLA, hivyo waliiacha Angola bila kuikbidhi kwa mtu au kundi.

Vikundi vyote vilikubaliana kuingia katika uchaguzi mkuu wa Novemba, 1975, ili Angola iongozwe kidemokrasia. Savimbi hakukubali hilo, alitaka waongoze nchi kwa zamu! Haikuwezekana, akarudi msituni na kuongoza vita vikali kwa zaidi ya miongo miwili. Savimbi alipata usaidizi wa karibu wa Holden Roberto wa Shirika la CIA la Marekani.

Serikali ya Ubaguzi wa rangi ya makaburu wa Afrika Kusini, iliingiza vifaa vya kivita na fedha kwa ajili ya kumsaidia Savimbi na UNITA.

Angola iligeuka uwanja wa vita baridi kati ya Marekani na Umoja wa Nchi ya Kisovieti chini ya Urusi. MPLA ambacho ni Movimento Popular de Libertação de Angola, kiliomba usaidizi wa Urusi ili kupambana na Savimbi. Haikusaidia kitu. Savimbi alitumia fedha na vifaa vya mabepari upande mmoja na kwingine akitumia mbinu za kisoshalisti alizopata Uchina! 
UNITA ilishambulia maeneo ya migodi, vituo vya afya na vyakula vya misaada. Kati ya mwaka 1980 mpaka 1988, Serikali ya Angola ilitumia Dola bilioni 30 za Kimarekani katika vita dhidi ya UNITA( Hii ni mara sita zaidi ya Pato la Taifa la Angola kwa wakati huo).

Pamoja na vita hivyo, Angola ilifanya uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1992. Kabla ya uchaguzi huo, mmoja kati ya waanzilishi wa UNITA Antonio da Costa Fernandes alijitoa! Alilaumu kuwa Savimbi amekuwa akiendesha vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na mauaji mabaya! Wakati malengo ya UNITA yalikuwa ni kuleta ukombozi wa pili kwa nchi ya Angola.

Athari za vita zilikuwa kubwa mno, kwa miaka 10 ya mwanzo, watoto 330,000 walifariki. Savimbi aliongoza ukatwaji wa viungo kama mikono na miguu kwa watu waliosaliti, au kuunga mkono serikali ya Angola.

Serikali mpya ya Marekani (Chini ya Bill Clinton), iliitambua MPLA kama chama tawala cha Angola, hivyo waliita UNITA katika meza ya makubaliano. Savimbi hakukubaliana na masharti ya kugawana madaraka! Akarudi tena msituni.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, likamtambua Rais Jose Eduardo dos Santos mwaka 1993, na Marekani ikafunga misaada kwa UNITA. Savimbi alikuwa ameshikilia migodi ya Almasi, hivyo aliendelea na mapambano!

Mwaka 1998, Umoja wa Mataifa ulipiga marufuku biashara ya almasi kati ya mataifa wanachama wake na UNITA.

UNITA ilikosa nguvu zaidi. Hivyo wapiganaji wake wakawa wanavamia vijiji na miji kupora vitu! Walisababisha njaa kwani walishambulia maghala ya chakula. Angola ambayo ilikuwa mzalishaji wa pili wa mafuta ghafi katika bara ya Afika, ikawa nchi isiyo na usalama kama Syria na Iraq ya sasa!

Kulifanyika majaribio karibu 15 ya kumuua Savimbi, na yalishindikana. Lakini Februari22,  2002, alishambuliwa na Jeshi la Angola na kufariki dunia. Nafasi yake ilichukuliwa na Antonio Dembo! Jonas Savimbi aliacha wake angalau 25 na mpaka sasa idadi ya watoto wake haifahamiki.

Hakuna aliyeamini Savimbi amefariki mpaka mwili wake ulipooneshwa kwenye televisheni ya Taifa la Angola. UNITA ilikubali kujigeuza kuwa chama cha siasa, na kuangushwa vibaya na MPLA katika uchaguzi wa mwak 2008. Wakati fulani vijana wa MPLA, ambacho ni chama Tawala walibomoa kaburi la Jonas Savimbi. Wote waliohusika walishtakiwa!

Bado swali linabaki, Je Savimbi anapaswa kuitwa muasi au mpigania ukombozi?