Home Habari kuu JPM 2015-2020: Bajeti nne, bado moja

JPM 2015-2020: Bajeti nne, bado moja

1058
0
SHARE

*Ahadi kwa Watanzania na utekelezaji kwa vitendo

Na Mwandishi Wetu

JUMATATU wiki hii, mwaka mpya wa fedha 2019/2020 umeanza rasmi, baada ya Bunge kupitisha Bajeti ya Serikali.

Baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo ambayo ni ya nne kwa Serikali ya Awamu ya Tano, inabaki bajeti moja ili kukamilisha muhula wa kwanza chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli.

Bajeti kimsingi ndiyo dira kuu ya maendeleo, na pia ni kipimo cha uimara na umadhubuti wa Serikali kwa wananchi inaowaongoza.

Wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani 2015, Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ilikuwa Sh trilioni 22.4, ambapo fedha za maendeleo zilikuwa Sh trilioni 5.

Kutokana na kuimarika ukusanyaji wa mapato ya ndani, udhibiti wa matumizi ya fedha za umma, kuimarika kwa vita dhidi ya rushwa na usimamizi mzuri kwa upande wa Serikali, kumekuwapo ongezeko la bajeti katika mwaka huu wa fedha takribani Sh trilioni 11 tofauti na bajeti ya 2015/2016.

Kutokana na ongezeko hilo ambalo pia linaashiria ukuaji wa uchumi, Serikali imetenga Sh trilioni 12.2 kwa mpango wa maendeleo, fedha ambazo ni sawa na ongezeko la Sh trilioni 7.2, kulinganisha na bajeti ya 2015/2016 wakati Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani.

Akizindua Bunge la 11 jijini Dodoma Novemba 20, 2015, Rais Magufuli aliwaahidi Watanzania kuwa atatekeleza mambo yote aliyoahidi wakati akiomba ridhaa yao ili awe Rais.

“Niwahakikishie tu wananchi kuwa mambo tuliyowaahidi tutayatekeleza. Nataka niwatoe wasiwasi kabisa kwamba tuliyoahidi tumeahidi na ahadi ni deni. Nataka wananchi mniamini kuwa sikutoa ahadi ili tu mnipigie kura, niliahidi kuwatumikia na kuwafanyia kazi, na hicho ndicho nitakachofanya,” alisema Rais Magufuli katika hotuba yake.

Ahadi

Katika hotuba yake, Rais Dk. Magufuli aliyataja maeneo kadhaa ambayo yalikuwa kero na kulalamikiwa sana na wananchi katika kila kona ya Tanzania.

Baadhi ya maeneo aliyoyataja ni suala zima la rushwa, utendaji usioridhisha Tamisemi, sekta ya maji, reli, Tanesco, madini, huduma za afya, ajira, elimu, pamoja na ufufuaji wa Shirika la Ndege (ATCL).

Utekelezaji ahadi

Serikali chini ya Rais Magufuli imefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ndani ya muda mfupi wa kuwapo madarakani.

Miongoni mwao ni mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaogharimu takribani Sh trilioni 6.

Ujenzi wa reli hii ambayo itakuwa na vituo maalumu vya kusimama kupakua na kupakia abiria na mizigo maeneo mbalimbali kati ya Dar es Salaam na Kigoma, na Tabora na Mwanza, inajengwa kwa urefu wa kilometa 726 na imetoa ajira rasmi na zisizo rasmi zisizopongua 30,000.

SGR inajengwa kwa awamu tatu. Awamu ya kwanza ni Dar es Salaam-Morogoro (Km 300) kwa gharama ya Sh trilioni 2.8, awamu ya pili kutoka Morogoro hadi Makutupora –Dodoma (km 400) kwa gharama ya Sh trilioni 4.3.

Rushwa

Wakati akiingia madarakani, Rais Magufuli aliahidi kupambana na rushwa kwa nguvu zote, na katika jitihada hizo aliahidi kuanzisha mahakama maalumu itakayoshughulikia kesi za ufisadi.

Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, taifa limeshuhudia kesi kubwa zikihusisha wafanyabiashara wakubwa, maofisa waandamizi wa Serikali, ambazo baadhi zimeshatolewa hukumu, na nyingine bado zipo mahakamani.

 “Nataka niirejee ahadi yangu kwao (wananchi) mbele ya Bunge lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote. Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu, lakini bahati mbaya halina dawa nyingine,” alisema Rais Magufuli katika sehemu ya hotuba yake bungeni.

Pia kushika kasi kwa vita dhidi ya rushwa, kumechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma katika asasi za Serikali zikiwamo huduma za afya na zile zinazotolewa na Tamisemi.

Umeme

Mafanikio mengine ni mradi mkubwa wa umeme wa Stigler’s Gorge, ambao utakapokamilika, Tanzania itakuwa na umeme wa kutosha kwa shughuli za maendeleo kama viwanda, na hata kuwapo wa ziada ambao unaweza kuuzwa nchi jirani.

Madini

Katika sekta ya madini ambayo ni muhimu kwa uchumi, kumekuwa na mkazo katika kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za kuyaongezea thamani, ili kukuza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa.

Pia kumekuwapo mikakati mahsusi ambayo imewezesha kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi na biashara haramu nchini.

Soko la Tanzanite hapa nchini limeimarika zaidi na hivyo kuongeza mapato yatokanayo na madini hayo yanayopatikana Tanzania pekee.

Wachimbaji wadogo wamewezeshwa kwa kuwatambua, kuwarasimisha na kuwapatia maeneo ya uchimbaji madini pamoja na kuwapatia ruzuku, mafunzo, teknolojia na

maarifa ya kisasa kuendeleza shughuli za uchimbaji.

Miundombinu

Miradi mingine mikubwa inayoendelea ni pamoja na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Ziwa Albert (Hoima) nchini Uganda hadi Tanga, ambao utagharimu kiasi cha Dola za Marekani bilioni 3.55.

Ujenzi wa bomba hilo unapita katika wilaya 24 na jumla ya vijiji 184 katika mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Miradi mingine iliyopata mafanikio katika kipindi cha miaka minne ni ujenzi wa miundombinu ya bandari, viwanja vya ndege, viwanda vya madawa, na ununuzi wa ndege za abiria.

Kuimarishwa na kuanzishwa kwa miundombinu mipya ya barabara kunasaidia taifa letu kumaliza kero katika eneo hili.

Katika kushughulikia jambo hilo, juhudi zimeelekezwa katika kujenga barabara za juu (flyovers) ikiwamo ya Mfugale, Ubungo na upanuzi wa njia nane wa barabara ya Kimara, Dar es Salaam hadi Kibaha mkoani Pwani.

Miundombinu mingine ni pamoja na ujenzi wa daraja eneo Selander Bridge ambalo linapita juu ya Bahari ya Hindi hadi barabara ya kuekelea Hopitali ya Ocean Road na ujenzi wa daraja la juu ya Ziwa Victoria la Kigongo-Busisi, ambao usanifu wake unaendelea.

Usafiri wa anga

Ndege mpya za kisasa saba hadi sasa zimenunuliwa zikiwamo aina ya Bombardier Q400, Dreamliner Boeing 787-8 na Air Bus A 220-300.

Kunuliwa kwa ndege hizo kumelifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ambapo pamoja na kuboresha usafiri wa ndani, tayari ndege za Tanzania zimeanza kufanya safari kwenda nje katika nchi za Zimbabwe na Afrika Kusini.

Maji

Katika kutatua kero za maji, miradi mikubwa imezinduliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, ukiwemo mradi mkubwa wa maji wa Nyamazugo ulioko wilayani Sengerema-Mwanza, pia katika mikoa ya Arusha, Pwani, Kigoma na maeneo mengine nchini.

Hadi kufikia mwaka 2020, Serikali inakusudia kutekeleza miradi ya maji zaidi ya 1,800 kwa mujibu wa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa.

Afya

Kwa upande wa sekta ya afya, utekelezaji wa agizo la Rais kujenga vituo kila kata na baadaye kila kijiji umezinduliwa, na tayari unaendelea, ambapo vituo hivyo kwa sasa vina uwezo wa kufanya upasuaji na huduma ya mama na mtoto. Haya ni mafanikio makubwa ya kujivunia kama taifa.

Mafanikio mengine ni kuwepo kwa huduma za upasuaji wa moyo na upandikizwaji wa viungo kama figo na vinginevyo unaofanyika sasa nchini katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Mloganzila.

Hatua hii ya upandikizaji wa viungo na matibabu ya moyo imeokoa mabilioni ya fedha za kigeni zilizokuwa zikitumika kuwapeleka watu kutibiwa nje ya nchi.

Elimu

Kwa upande wa sekta ya elimu, ongezeko la fedha za Serikali kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia limeleta ahueni kubwa kwa wazazi pamoja na kuwapo kwa changamoto kwa kada ya ualimu, ambapo bajeti ya fedha za mikopo kwa wanafunzi imeboreshwa zaidi.

Pia ahadi ya elimu bure kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari imetekelezwa kwa asilimia 100, jambo ambalo limeongeza idadi ya wanafunzi tofauti na hali ilivyokuwa awali.