Home Habari kuu JPM aacha ujumbe mzito Afrika

JPM aacha ujumbe mzito Afrika

372
0
SHARE

Na ANDREW MSECHU

-DAR ES SALAAM

ZIARA ya Rais Dk. John Magufuli katika nchi za Kusini mwa Afrika, iliyofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita, imeacha kishindo katika nchi za Afrika, akitumia fursa hiyo kuinadi lugha ya Kiswahili.

Rais Magufuli ambaye alianza kuinadi lugha hiyo inayoonekana kukua kwa kasi duniani mara alipoingia madarakani, ameendelea kupita katikati ya Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, ambao tayari wameshaona fursa zilizopo kupitia lugha hiyo, hivyo kuirasimisha katika nchi zao.

Februari 8, 2017 Bunge la Rwanda lilipitisha sheria ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kiofisi nchini humo sambamba na lugha za Kinyarwanda, Kingereza na Kifaransa.

Tangu wakati huo Kiswahii kilianza kutumika katika shughuli za utawala nchini Rwanda, huku kikiingizwa rasmi katika mitaala ya shule na vyuo kuanzia mwaka 2018.

Kenya ilishapitisha Kiswahili na kukifanya kuwa lugha rasmi ya kiofisi tangu Agosti 2010, na kupitia katiba yake mpya, kifungu cha 7, tayari ilishakitambua kuwa lugha rasmi baada ya Kiingereza.

Hiyo ni sehemu ya Kiswahili kuendelea kuwa lugha muhimu katika nchi za Afrika na dunia.

Rais Magufuli alichukua hatua madhubuti za kukinadi Kiswahili alipoamua kukitumia alipohutubia Mkutano wa Umoja wa Afrika Januari 29, 2017 mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Mkutano huo ulikuwa wa kwanza kwake kuhudhuria, huku alipewa pia heshima ya kuzindua rasmi jengo la ofisi la AU lililopewa jina la Kituo cha Amani cha Mwalimu Julius Nyerere.

Katika mwendelezo huo, kwenye ziara hiyo iliyoanzia Afrika Kusini, kisha Namibia na kumalizikia Zimbabwe, Rais Magufuli ameendelea kutumia fursa hiyo kukinadi Kiswahili na kutengeneza fursa mpya katika sekta ya wanataaluma wa elimu hasa waliobobea katika lugha hiyo.

Ziara hiyo ya kwanza kwa Rais Magufuli kusafiri kwa masafa marefu mfululizo nje ya nchi tangu alipoingia madarakani Oktoba 2015, imeacha kishindo hasa kwa namna alivyotumia fursa hiyo kukinadi Kiswahili.

Nchini Afrika Kusini, Rais Magufuli ambaye alikutana na Rais Syril Ramaphosa, alitumia fursa hiyo pamoja na mambo mengine kukitafutia soko Kiswahili na kukisimika katika mataifa ya Kusini, hasa yale yaliyo katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Ni katika ziara hiyo Rais Magufuli alifanikiwa kuishawishi Serikali ya Afrika Kusini kuona umuhimu wa kutilia mkazo ufundishaji wa lugha ya Kiswahili na kutangaza wazi uhitaji wa wataalamu wa lugha hiyo kwa ajili ya shule na vyuo nchini humo.

Hata hivyo, kwa Afrika Kusini huo ulikuwa ni mwendelezo wa juhudi zilizokuwa tayari zimeshaanza wakati wa utawala wa Jacob Zuma ambaye tayari alishafikia makubaliano na Serikali ya Tanzania kuhusu ufundishwaji wa Kiswahili nchini humo mwaka 2017 na kutangaza fursa za walimu wa lugha hiyo.

Afrika kusini iliidhinisha lugha ya Kiswahili kufundishwa katika shule za nchi hiyo Septemba 2018 na kufungua fursa kwa walimu kutoka ukanda wa Afrika Mashariki ambako lugha hiyo imechimbukia na kuzungumzwa.

Wakati wa ziara hiyo, taarifa rasmi ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Gerson Msigwa ilieleza kuwa: “Rais Ramaphosa amesema kufuatia uamuzi wa Afirka Kusini kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili, nchi yake itachukua walimu wa Kiswahili kutoka Tanzania ili watumike kufundisha somo hilo katika shule za msingi na sekondari.”

Akiwa nchini Zimbabwe, Rais Magufuli alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwa rafiki wa kweli wa Zimbabwe na ameahidi kuwa tayari kuwapeleka walimu watakaofundisha lugha ya Kiswahili katika shule na vyuo.

Wakati marais hao wakifikia makubaliano hayo, tayari mawaziri wa elimu wa Kenya, Profesa George Magoha na Afrika Kusini, Angelina Matsie Motshekga wametia saini makubaliano ya Kenya kupeleka walimu wa somo hilo. Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Nairobi Mei 16, mwaka huu.

Profesa Magoha alinukuliwa na gazeti la The Standard la nchini humo akisema makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa nchi hizo.

Waziri Motshekga alinukuliwa akisema kuwa asilimia 40 ya wanafunzi nchini Afrika Kusini tayari wanajifunza Kiswahili kwa namna moja ama nyengine.

Katika ziara ya Rais Magufuli, juhudi zake hazikuishia Afrika Kusini na Zimbabwe tu, bali pia Namibia ambazo kwa pamoja zilionesha kutilia mkazo ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi kwa ajili ya kuziunganisha nchi za Kusini mwa Afrika.

Kwa sasa, tayari lugha hiyo inatambuliwa kama kiunganishi cha mawasiliano kwa nchi za Afrika Mashariki na tayari ilishatambuliwa kama lugha rasmi kwa Afrika chini ya Umoja wa Afrika.

Akizungumzia ziara hiyo, Msemaji wa Serikali, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk. Hassan Abbasi,  alisema ililenga zaidi kuhamasisha diplomasia ya kiuchumi ambayo ndiyo inayosimamiwa na Serikali kwa sasa.

Alisema katika ziara hiyo ambayo imekuwa ya utangulizi kama sehemu ya maandalizi ya kuchukua uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Julai mwaka huu, Rais Magufuli amefanikiwa kufanya mazungumzo ya awali kwenye kuinadi lugha adhimu ya Kiswahili nchini Afrika Kusini na Namibia ambao wamefikia makubaliano ya kuanza  kufundisha rasmi lugha hiyo.

“Hatua hiyo ni kubwa na mikataba itasainiwa siku chache zijazo. Kwa hiyo tunahitaji kujiandaa kupitia mifumo ya ithibati ambayo inathibitisha utaalamu katika Kiswahili. Tayari Baraza la Taifa la Kiswahili (Bakita) wameanzisha kanzidata ya kitaifa ya Kiswahili na imeshawekwa kwenye tovuti yao,” alisema.

Alisema katika kanzidata hiyo, Watanzania 708 tayari wameshajisajili na wako tayari kupokea fursa hizo na kuwataka wote wanaodhani wana utaalamu wa Kiswahili kwa kufasiri na kufundisha wajitokeze kujisajili.

Dk. Abbas alisema katika ziara yake kwa nchi za Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe, Rais Magufuli alifanya kazi ya kuhamasisha diplomasia ya uchumi kwa mafanikio makubwa.

Alisema tayari Rais Magufuli ameshawaalika wawekezaji kutoka katika nchi hizo kuja kuwekeza nchini, hatua ambayo ilipokewa vyema.

MAENEO MENGINE

Awali katika taarifa yake akiwa Namibia – nchi ambayo Tanzania ilishiriki kwa kiasi kikubwa kuikomboa kutoka mikononi mwa wakoloni, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Msigwa alisema Rais Magufuli alitembelea kiwanda cha nyama cha kampuni ya Meatco kilichopo jijini Windhoek na kujionea utendaji wake.

Alisema katika ziara ya Rais kiwandani hapo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho, Jannie Breytenbach alieleza kuwa kiwanda kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 630 kwa siku, kikiwa kimeajiri wafanyakazi 650 na kwamba kampuni hiyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania kuanzisha viwanda vya nyama. 

Msigwa alieleza kuwa Rais Magufuli alisema Tanzania ni nchi ya pili kwa idadi kubwa ya mifugo barani Afrika na alitumia nafasi hiyo kuikaribisha kampuni ya Meatco kuja kuwekeza nchini. 

Akiwa nchini Zimbabwe,  Rais Magufuli alisema Tanzania itaiuzia Zimbabwe tani 700,000 za mahindi kufuatia nchi hiyo kukabiliwa na upungufu wa chakula.

Rais Magufuli alitoa ahadi hiyo muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo rasmi kati yake na Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa yaliyofanyika Ikulu jijini Harare.

SHAKA ANENA

Akizungumzia ziara hiyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, alisema imetoa mwanga utakaodumisha umoja, ushirikiano na mwendelezo wa historia kabla ya uhuru na mapambano ya Bara la Afrika ambalo hatimaye lilijikomboa kutoka kwa wakoloni.

Akizungumzia na wazee waasisi wa CCM, Shaka alisema kuwa kuna mambo kadhaa watendaji wa chama wamejifunza kupitia ziara hiyo, hasa kuhusu masuala ya uongozi.

Alisema ziara hiyo ni ya aina yake kwa mustakabali wa nchi zote zikiwamo za Maziwa Makuu na kusini mwa Afrika kudumisha siasa, uchumi na historia ya bara la Afrika.

Shaka alisema ziara hiyo licha ya kuendeleza dira ya umoja, ushirikiano, udugu, ujirani mwema kwa maendeleo ya kisiasa, kidiplomasia na kiuchumi, itaendeleza misingi kwa mataifa hayo kushikamana zaidi.