Home kitaifa JPM AMALIZA HOJA ZA WAPINZANI

JPM AMALIZA HOJA ZA WAPINZANI

665
0
SHARE

NA FARAJA MASINDE,

MWENENDO wa Rais Dk. John Magufuli wa kushughulikia masuala kadhaa yaliyokuwa yakipigiwa kelele na wanasiasa ndani na nje ya Bunge, yanatajwa kumaliza kabisa hoja za wapinzani. RAI lnachambua.

Matukio matatu ya hivi karibuni yaliyofanywa na Rais Magufuli na Serikali yake yanahalalisha kuzamisha hoja za wapinzani ambazo zilionekana kuwa turufu yao kisiasa.

Uamuzi wa Rais Magufuli kuteua makada wawili wa chama cha ACT-Wazalendo kuingia kwenye serikali, kuunda Kamati ya kuchunguza sakata la usafirishaji wa mchanga wa madini nje ya nchi pamoja na uamuzi mgumu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) kuwapandisha kizimbani wahusika wakuu wa sakata la IPTL kwa pamoja yanatajwa kuwa maamuzi yanayomaliza kabisa hoja za wapinzani ndani na nje ya Bunge.

Uteuzi wa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na ule wa aliyekuwa Mshauri Mkuu wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo, ulimaliza kabisa hoja ya Rais Magufuli kutovipenda vyama vya upinzani.

Hoja hiyo iliibuka siku chache baada ya serikali ya awamu ya Tano kupiga marufuku maandamano na mikutano ya kisiasa kwa madai kuwa hiki ni kipindi cha kufanya kazi tu na si kuendekeza siasa.

Baada ya hoja hiyo kufa kifo cha kawaida, Rais Magufuli aliamua kiufifisha hoja nyingine iliyowahi kupigiwa kelele kwa kiasi kikubwa na wapinzani, wakitaka kuwe na uwazi kwenye mikataba ya madini.

Rais aliimaliza hoja hiyo baada ya kukubali mapendekezo yote ya Kamati ya Profesa Nehemiah Osoro  iliyokuwa imepewa jukumu la kuchunguza masuala ya kisheria na hasara iliyopata nchi kwenye usafirishaji wa Makinikia.

Moja ya mapendekezo zaidi ya 20 ya Kamati hiyo ilikuwa ni kutaka mikataba yote ya madini ipitishwe bungeni na kupewa ridhaa na wabunge.

Uamuzi wa Rais wa kukubali uwazi kwenye mikataba ya madini, sit u uliwafurahisha wananchi, lakini pia ulionekana kuwagusa wabunge wa upinzani ambao baadhi yao walikuwa vinara wa kutaka kuwepo kwa uwazi kwenye mikataba.

Aidha hatua ya TAKUKURU kuwapandisha kizimbani Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya PAP, Habinder Sing Sethi na Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering , James Rugemalira, imeonekana kunyongonyeza kabisa hoja nzito zilizokuwa zikishikiliwa na upinzani.

Tuhuma dhidi ya IPTL na akaunti ya Tegeta Escrow zilikuwa mwiba mkali kwa serikali ya awamu ya nne na hata Serikali ya Magufuli ilipoingia madarakani, baadhi ya wabunge wa upinzani walimtaka Rais kuonesha uzalendo kwa kushughulika na sakata hilo ambalo limekuwa likiitafuna nchi kwa muda mrefu.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe na mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila ni miongoni mwa wanasiasa waliokuwa wakilishikilia bando sakata hilo.

Kitendo cha TAKUKURU kuwafikisha mahakamani wawili hao kilimuibua Zitto ambaye alimpongeza Rais kwa uamuzi wake huo na kudai kuwa amekuwa akimpinga Rais kwenye mambo mengi na ataendelea kumpinga, lakini kwenye hili la IPTL amempongeza kwa madai kuwa ameitendea nchi haki.

“Leo ninaona vita dhidi ya ufisadi ina maana kubwa. Kumkamata Harbinder Singh Seth na kumfikisha mahakamani ni hatua kubwa ya kupongezwa,”alisema Zitto.

Kauli hiyo ya Zitto ambaye alikuwa kinara wa kuliibua sakata hilo ndani na nje ya Bunge la 10 inadhihidirisha wazi kufungwa kwa mjadala wa sakata la IPTL.

Mwenendo huu wa kimaamuzi wa Rais Magufuli tayari umeonesha kushusha umaarufu wa upinzani kama ambavyo utafiti wa hivi karibuni wa taasisi ya kitafiti ya Twaweza ilivyoonesha.

Hivi karibuni Taasisi hiyo ilitoa ripoti inayoonyesha kushuka kwa upinzani nchini ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

Akiwasilisha utafiti huo, Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema kuwa kati ya watu waliowahoji asilimia 63 walisema wapo karibu zaidi na CCM kuliko vyama vingine huku Chadema kikiwa na asilimia 17  na vilivyosalia vikiwa na asilimia moja kila kimoja.

“Asilimia 17 wamedai hawako karibu na chama chochote, pia utafiti umeonyesha kuwa kukubalika kwa Chadema kumeshuka tangu 2013, ukilinganisha na asilimia 32 ya wananchi ambao walisema wapo karibu na Chadema mwaka 2013 ni asilimia 17 ya wanaosema hivyo mwaka huu huku uungwaji mkono wa chama cha CUF Bara ukishuka kutoka asilimia nne hadi moja,” alisema.

Hali hiyo ya kiutendaji ya Rais inawaacha wapinzani na hoja chache za kufanyia kazi, miongoni mwa hoja hizo ni sakata la Katiba Mpya, Lugumi, pamoja na kile kinachoitwa uenevu wa polisi, wakuu wa mikoa na wilaya dhidi ya wanasiasa wa upinzani.

Aidha eneo la kuzuia mikutano bado limekuwa turufu ya upinzani katika kuibua hoja za kuisakama serikali, hata hivyo kama Rais Magufuli ataamua kuyafanyia kazi maeneo haya na kutoa maamuzi chanya kabla ya mwaka 2019 upo uwezekano wa kumaliza kabisa hoja za upinzani.

Hata hivyo upinzani unayo nafasi ya kuendelea kuisumbua Serikali na Chama Cha Mapinduzi kama itaamua kubadili mwenendo wake wa kisiasa kwa kuachana na siasa za majibizano na kuelekeza nguvu zao kwenye siasa za kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Siasa zenye tija ya moja kwa moja kwa wananchi ndio turufu pekee ambayo upinzani wanaweza kuitumia kuiangusha CCM kwenye chaguzi zijazo hasa ukizingatia kuwa kwa sasa ni Rais na Mwenyekiti pekee wa chama hicho ndie mwenye mvuto kutokana na kufanya mambo mengi yeye mwenyewe.

Hatua hiyo ya Rais kufanya mambo mengine kwa msukumo wake inahalalishwa na kauli yake aliyoitoa juzi kwenye ziara yake mkoani Pwani akiweka wazi kuwa amekuwa akipokea mialiko mingi ya kwenda nje ya nchi, lakini hawezi kwenda kwa sababu anahofia akiondoka aliowaacha watalala.

Kauli hii ya Rais inadhihirisha wazi kuwa kwa sasa anafanya kazi zaidi mwenyewe hatua inayotoa mwanya kwa upinzani kuwa na nafasi ya kukabiliana nae kama wataamua kubadili kabisa mwenendo wa siasa zao kutoka kwenye kusaka umaarufu wa vurugu nje na ndani ya Bunge na kuwa watendaji zaidi ya wasemaji.

Huenda sasa ndio wakati sahihi kwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na washirika wake ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na vyama vingine nje ya umoja huo kuanza kufanyia kazi kile alichowahi kukishauri Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Prof. Kitila alipokuwa ndani ya uongozi wa ACT-Wazalendo.

Julai 9, 2016, Lowassa akiwa kwenye kikao cha pamoja na Mameya wa Halmashauri wa Chadema alisema wakati umefika kwa chama hicho kuachana na uanaharakati na maandamano ili kiweze kujipanga kuchukua nchi 2020.

“Chama cha siasa kazi yake ni kukamata dola basi, hakuna kitu kingine duniani, vision ya chama cha siasa ni wanasiasa kukamata dola, mnapokaa hapa mjiandae kukamata dola na sio kitu kingine, acha habari ya maandamano, maandamano ni process.”

Kauli hiyo ya Lowassa inarandana kabisa na tahadhari aliyopata kuitoa Profesa Kitila kwa upinzani. Prof. Kitila aliutaka upinzani kujipanga upya ili kuweza kushindana na Serikali iliyopo madarakani.

Aidha aliutaka upinzani kukaa chini na kuchora ramani ya kukabiliana na Rais Magufuli kisiasa.

“Tuna tatizo katika pande zote za siasa, Serikali mpya ya Rais Magufuli inaonekana haijajua namna ya ‘kudeal’ na upinzani na upinzani nao unaonekana haujajua namna ya ‘kudeal’ na serikali mpya.

“Bado tunaendesha siasa zetu za upinzani kama tulivyofanya wakati wa JK, (Jakaya Kikwete)  ambaye ‘style’ yake ya uongozi ilikuwa tofauti mno na huyu, Rais wa sasa. Lazima kujipanga upya.

“Tunahitaji kukaa chini na kuchora ramani mpya ya namna ya kuendesha siasa za upinzani katika kipindi hiki. Kimsingi upinzani Tanzania ulitarajiwa kupanda ngazi kwa mwendo wa konokono (evolutionarily) lakini kuna uwezekano mkubwa katika kipindi hiki ukapanda ngazi kwa kasi ya kimapinduzi (revolutionarily).

“Hata hivyo ni lazima kujipanga upya-hili halitawezekana kwa kufanya siasa za aina ile ile na kwa mtindo ule ule,” alisema Profesa Kitila.

Kama ilivyokuwa kwa Lowassa na Prof. Kitila ndivyo pia Maalim Seif alivyonesha namna Rais Magufuli anavyoumaliza  upinzani na kwamba ipo haja ya kujipanga upya.

Maalim Seif aliutaka upinzani nchini kubuni mbinu mpya ya kujinasua na anguko la kisiasa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Alitoa tahadhari hiyo wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na wanachama wa CUF wa Temeke nyumbani kwa Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea.

Alisema kufuatia agizo la Serikali la kupiga marufuku shughuli za kisiasa hadi 2020 ikiwamo mikutano na maandamano wakati mtaji wa vyama vya siasa ni wananchi, ni bora wakatafuta njia mbadala ya kukutana nao kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Huku akisisitiza kuwa kitendo hicho si kizuri kwa kuwa kinaminya demokrasia na kinalenga kuwatenga wananchi na siasa.

“Viongozi wenzangu wa upinzani, hasa Ukawa, tuwe wabunifu ili tuwafikie wananchi popote walipo. Vinginevyo vyama hivi vya upinzani vitatolewa roho na njia moja ni kama hivi leo nilivyojumuika nanyi kwenye futari nasikia faraja,” alisema Seif.

Seif aliongeza kuwa ni jambo la ajabu kwamba vyama vya upinzani vimeridhia badala ya kubuni njia za kukutana na wananchi.

Maalim Seif alisema pamoja na kuzuia mikutano ya kisiasa, Rais Magufuli amekuwa akifanya ziara maeneo mbalimbali na kuzungumza anavyotaka, ikiwa ni pamoja na kuwaponda wapinzani.

“Rais anatushutumu wapinzani, lakini hataki kujibiwa. Tukisema demokrasia inapigwa vita nchini, tunaambiwa tumpe nafasi atekeleze ilani. Kwani miaka yote hakukuwa na ilani?.

“Hivi tukifanya shughuli zetu za kisiasa tunamzuia nani asitekeleze ilani? Usipotekeleza ni kwa sababu huna uwezo, si kwa sababu ya mikutano. Rais ajitathmini uamuzi wake wa kuzuia mikutano wakati Sheria ya Vyama vya Siasa hairuhusu,” alisema Maalim Seif.