Home Habari JPM APIGA MARUFUKU FITINA CCM

JPM APIGA MARUFUKU FITINA CCM

824
0
SHARE

NA FLORENCE SANAWA, MTWARA


RAIS John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amewataka makada wa chama hicho kuacha kupigana vita na kufanyiana unafiki kwa kuwa mambo hayo ndiyo yaliyokisababishia chama hicho kupoteza majimbo kadhaa mkoani Mtwara.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo wakati akizungumzia hatua ya chama chake kupoteza jimbo la Mtwara Mjini ambalo  linashikiliwa na Chama cha Wananchi (CUF), ambapo alidai kuwa wamelipoteza jimbo hilo  kutokana na unafiki wa wanaCCM.

Rais Magufuli ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi  ya siku mbili mkoani hapa, pamoja na uzinduzi na uwekaji wa jiwe la msingi wa miradi mbalimbali pia alipata nafasi ya kufanya  mkutano wa hadhara katika viwanja vya mashujaa.

Alisema wanachama wa CCM wamekuwa wakipigana vita wao kwa wao hali inayokiathiri chama.

Alisema kitendo cha kuwapo kwa migogoro ya ndani ya kilisababisha jimbo hilo na majimbo mengine mengi kuchukuliwa na wagombea wa upinzani.

Alisema unafiki na vita vya wanaCCM ndani ya chama  ndio chanzo cha Mbunge huyo kupenya na kufikia nafasi aliyonayo kwa sasa hivyo kuwataka kukumbuka kuwa yaliyopita si ndwele bali washirikiane bila kubaguana vyama wala kabila kwa maendeleo ya mtwara.

“Huyu mbunge alipata bahati nzuri baada ya wana CCM  kuanza kugombana wao kwa wao wakapigana vita na kufanya unafiki wao kwa wao mbunge wa jimbo hili akapenya kwa kutumia unafiki wa wanaCCM, bila shaka sasa hivi kama kuna mahali pa kujifunza wamejifunza.

“WanaCCM walipigana vita wenyewe wengine nimekaa nao hapa mbele matokeo yake wakawachanganya wananchi ndio maana tulipoteza hili jimbo na huyu mbunge akapenya.

Tunashukuru kwakuwa mnae mbunge kijana anaetoa ushirikiano mzuri kwa serikali amejitahidi kufika katika miradi yote bila kubagua vyama kwakuwa maendeleo hayana vyama inaonekana ana moyo mwema anasura ya CUF lakini moyo wake ni CCM” alisema Magufuli

Aidha, Rais Magufuli aliwataka wananchi kushirikiana na serikali ili kuweza kupata maendeleo bila kujali vyama kama ambavyo Mbunge wa Mtwara mjini, Maftaa Nachumba anavyoshiriki kwenye shughuli za maendeleo bila kujali kuwa anatokea CUF.

Katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, CCM iligawanyika vipande vipande kutokana na kuwapo kwa makundi ya wagombea urais hali iliyosababisha kutishia uhai wa chama hicho.

Mgawanyiko huo uliochangia kuhama kwa makada wengi kuelekea upinzani, kulivinufaisha baadhi ya vyama hasa vile vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambavyo vilifanikiwa kupata majimbo na Kata nyingi huku mgombea Urais wa upinzani akifanikiwa kupata kura 6,072,848 ikiwa ni sawa na asilimia 39.97 ya kura zote, idadi ambayo haijawahi kufikiwa na mgombea yoyote wa upinzani tangu kurejea kwa chaguzi za mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.

CCM kinatarajiwa kufanya Mkutano wake Mkuu Maalum wa Taifa, mwishoni mwa wiki hii mjini Dodoma na kwamba Mkutano huo unafanyika kufuatia mageuzi makubwa yanayofanyika ndani ya chama ambayo yanahitaji kwenda sambamba na  marekebisho ya Kanuni na Katiba ya chama hicho.

Mbali na kufanya marekebisho ya Kanuni na Katiba ya chama hicho, pia Mkutano huo utakuwa na jukumu la kupokea taarifa ya ratiba ya uchaguzi mkuu wa chama na Jumuiya zake utakaofanyika nchini kote mwaka huu.

Marekebisho hayo ya Kanuni na Katiba ya chama hicho yanafanyika kufuatia maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM yaliyofikiwa mwezi Desemba mwaka jana, jijini Dar es Salaam.

Aidha, Mkutano huo utatanguliwa na mikutano ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa utakaoanza kesho na kufuatiwa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa utakaofanyika keshokutwa.