Home Makala JPM asiweke pamba masikioni  

JPM asiweke pamba masikioni  

924
0
SHARE

Baadhi ya wapiga kura wakiwa kwenye foleniNa Dk.Vera F. Muugittu, Scotland

JUNI 13, 2016 niliandika makala ambayo msingi wake ni kutoa rai kwa Watanzania nikieleza kuwa udikteta unahitajika kwa kiwango kikubwa katika kipindi hiki cha mpito cha kulikwamua taifa toka kwenye umasikini uliokithiri kwenda kwenye maendeleo ya kudumu nchini. Mradi tu dhamira ya kiongozi na taifa zima iwe safi…

Nikabainisha kuwa historia ya nchi zote zilizoendelea.. inadhihirisha kutumika kwa udikteta katika kiwango na vipindi tofauti vya mpito.

Vipindi vingine vilidumu kwa muda mfupi, na vingine kwa muda mrefu. Kufuatia andiko langu, wapo wachache walionipinga na wapo waliochukizwa sana na kunitumia ujumbe binafsi. Nawashukuru sana wote, na leo naomba nifafanue zaidi.

Dhana ya “udikteta mzuri” – yani ‘Benevolent Dictatorship’ – kwa lugha ya Kiingereza, ilianza kutumika kwa kiongozi, Lucius Quinctius Cincinnatus wa Roma wa mwaka 458 B.C.E. aliyerejea kuishi maisha  ya kawaida sana ya mkulima baada ya kustaafu uongozi. Taifa la Roma kila lilipokuwa na matatizo aliombwa kutwaa madaraka tena ili kulikwamua taifa lake.

Kila wakati Quinctius Cincinnatus alifanya hivyo na kuongoza kwa muda mfupi sana-pengine hata siku 16 tu mradi lengo la kuikwamua dola limetimia. Kamwe hakuzidisha hata siku moja zaidi. Alijivua madaraka na kurudi kwenye maisha yake ya utulivu kama mkulima.

Mtawala huyu, historia inamtambua kama kitovu cha udikteta mzuri kwani hakuwahi kutawala kwa maslahi binafsi, bali kwa faida ya wananchi wake.

Katika jarida lake, Shaun Randol anaandika.. “History has judged Cincinnatus to be the epitome of the benevolent dictator. That is, Cincinnatus ruled in order to serve the common good, rather than out of self-interest.”

Historia pia inawataja George Washington  aliyekuwa rais wa kwanza wa Marekani (1789–97) na Franklin Roosevelt aliyetawala Marekani wakati wa “Great Depression’ na Vita kuu ya Pili ya dunia (1933-1945) kuwa madikteta wazuri ambao waliongoza kidikteta ndani ya katiba ya kidemokrasia.

Viongozi hawa wanaheshimiwa kwa kufanya maamuzi ya haraka ya uthubutu bila kujali hofu ya wengi. Maamuzi yao yananukuliwa kulipatia taifa la Marekani heshima na ustawi baada ya kuwa katika hali ngumu kisiasa na kiuchumi. Matokeo ya utawala wao ni mafanikio ya kudumu kwa taifa la Marekani.

Wachambuzi wa kisiasa wanabainisha kuwa aina hii ya udikteta ilianza kuvurugwa na mataifa yaliyoendelea kwenye karne ya 19 yalipotaka kutwaa nguvu ya nchi zilizokuwa zinaendelea ili kuzitawala kiuchumi.

Mifano kadhaa inatolewa ambapo viongozi kama Muammar Gaddafi, Fidel Castro, Hugo Chavez, Paul Kagame na Lee Kuan Yew wa Singapore ambao licha ya mchango wao kuthaminiwa na wananchi wao, mataifa ya nje yanawalaumu kuwa madikteta wasioheshimu demokrasia.

Shaun Randol anasema, mtazamo huu wa nje umesababisha kuharibiwa na kuvuliwa thamani kwa dhana hii muhimu ya ‘Benevolent dictatorship”. Na hali hii imechangia kushamiri kwa uongozi dhaifu katika nchi nyingi zinazoendelea, ambapo tumekuwa na marais ‘wasioweza kuleta mageuzi ya kiuchumi”.

Historia iko wazi kuwa maendeleo makubwa hayaletwi na demokrasia pekee, bali na uongozi wenye dira na wenye kuthubutu kufanya maamuzi pale kila mmoja anaposita. Ila pia inawekwa bayana kuwa, udikteta wa aina hii ni lazima ujengwe ndani ya katiba sahihi yenye “Kulinda amslahi’ ya wengi.

Hapa naomba nisisitize kuwa kuna tofauti kati ya “kuhakikisha ustawi wa wote’… na ‘kuhakikisha ushiriki wa wote kwenye maamuzi’..  Katika kipindi cha mpito, taifa linahitaji katiba na taratibu za ‘Kulinda maslahi’ ya wote, hata kama maamuzi ya kutengeneza maslahi hayo yatafanywa na wachache. Mimi kwa mtazamo wangu, sasa hivi tunachohitaji kama taifa ni;

KWANZA: Kukifanya kipindi cha Rais John Magufuli kuwa cha mpito kikiwa na lengo maalumu la “Kulikwamua’ taifa kiuchumi. Nasema hivi kwa sababu simuoni Rais  Magufuli kama kiongozi anayefaa kuongoza kwa muda mrefu… hasa baada ya kumaliza kazi yake ya “utingatinga” – ambalo hutumika kutayarisha njia, na likishachimba barabara linarudishwa yadi kupaki.

Kisha vifaa vingine vinaendelea kuifikisha barabara katika kiwango cha lami..:) Katika kipindi hiki cha mpito, maamuzi ya haraka yanapaswa kufanywa ili kusimamia na kuhakikisha utekelezaji wa shughuli zenye kuleta maendeleo ya kweli. Ni lazima kufupisha ukiritimba wa maamuzi ili tuuvuke mto wa umasikini.

PILI: katika kipindi hiki, sambamba na kujikwamua toka kwenye umasikini na ufisadi, iwepo Katika sahihi yenye kulinda maslahi ya wote (Public interest). Na mikakati mahiri ya kujenga taasisi na uwezo wa kitaifa wa kusimamia na kuendeleza yatokanayo na kipindi cha mpito.

Uwezo wa kimfumo, kitaaluma na kisiasa wa kusimamia uchumi, siasa za nje, na ujenzi wa demokrasia ya kweli ni lazima ujengwe kuanzia sasa. Lengo ni hatimaye kuwawezesha wananchi wote kuwa na hamu, uwezo, sauti, na muda wa kufuatilia utendaji wa viongozi hao.

Kwa sasa, wananchi ni masikini na dhaifu mno, kiasi kwamba mfumo mzima wa uchaguzi na hivyo wa kufanya maamuzi haujajengwa kuhakikisha demokrasia ya kweli inapatikana. Tunachokiita demokrasia kwa sasa bado ni ulaghai tu.

Rushwa na ulaghai vimetawala kwasababu wananchi wana njaa, hawana elimu na wameghubikwa na shida nyingi hivyo kufuatilia utendaji wa serikali siyo kipaumbele kwao.

Rai yangu kwa Watanzania: hebu tuitazame awamu hii kama kipindi cha mpito. Kipindi cha kuondoa kashfa za umasikini zilizotuandama kwa miaka 55 sasa. Barabara mbovu, ukosefu wa madawati, vitanda mahospitalini, maji vijijini, walimu, vyoo mashuleni, n.k.. haya ni mambo ya aibu sana kujadiliwa katika karne hii.

Haya ni mambo ya kutekeleza haraka haraka kwani yanazuia majadiliano na utekelezaji wa mipango mingine mikubwa ya kiuchumi ya karne ya leo.

Mfano unashindwa kuzungumzia kuboresha elimu kupitia tehama kwakuwa hata vyoo tu mashuleni bado unashindwa kuimarisha mipango ya kujenga uwezo wa kupima afya za watu vijijini kuwa utaratibu wa kila siku kabla ya kuugua, kwa kuwa hata uwezo wa kupima wagonjwa wa malaria haupo.

Tukubaliane tu kuwa kwa hali ilivyo sasa hatuhitaji mlolongo wa ushirikishwaji kufanikisha mambo kama haya…!! Hebu tujiulize bila ushabiki, hivi mipango na majadiliano ya miaka 55 yametufikisha wapi? Sana sana gharama za uendeshaji wa majadiliano haya zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku.

Majimbo ya uwakilishi yameongezeka, gharama/posho za Bunge zimeongezeka ..lakini idadi ya madawati, vyoo, vitabu, darubini mahospitalini, ambulenzi, n.k bado haitoshi.

Hivi hatuoni aibu kuwa nchi yetu bado inakumbwa na milipuko ya kipindupindu? Hivi huu kweli ni ugonjwa wa kusumbua watu karne hii?… Eti shule hazina matundu ya vyoo? Hakuna madawati? Wajawazito wanalala chini? na mengine mengi ya aibu?

Ukweli hapa ni kuwa jamii yetu bado imeghubikwa na umasikini wa kizamani sana… Umasikini uliokwisahaulika! Uliokwishapitwa na wakati… Lingekuwa gari, tungesema hata spea zake zimeshafutika sokoni..Na ili kuuondoa umasikini huu wa kale hatuhitaji demokrasia ya ‘Wengi wape”.

Namuomba dereva wa tingatinga, ingawa tumemuachia apangue gear mwenyewe..maana yake tunauamini udereva wake, tunamsihi afuate ramani ya barabara iliyochorwa kitaalamu. Pia asikilize kelele za wahandisi kila zinapopigwa ili asijekukosea njia.

Maana yake asipofanya hivyo mwisho wa siku anaweza akawa amepoteza muda na mafuta yetu  kuchimba barabara isiyotufikisha tulikokusudia.. Huku yeye akiwa amechoka hoi taabani. Hapo wote tutakuwa tumepoteza miaka mingine mitano. Mungu ibariki Tanzania na watu wake.