Home Habari JPM ATUMIKA KUSAKA KURA KENYA

JPM ATUMIKA KUSAKA KURA KENYA

1779
0
SHARE
Rais Dk. John Magufuli

NA MWANDISHI WETU

MWENENDO wa kiutendaji na kimaamuzi wa Rais Dk. John Magufuli sasa unatumika kama turufu ya kusaka kura za wananchi nchini Kenya.

Uchaguzi wa Kenya unatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi ujao, huku ushindani mkali ukitazamiwa zaidi kwa Rais wa sasa wa Taifa hilo, Uhuru Kenyatta na hasimu wake Raila Odinga.

Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto wanaungwa mkono na  vyama kadhaa vya upinzani vilivyounda muunganmo wa Jubilee.

Kwa upande wake Odinga na mgombea mwenza Kalonzo Musyoka kwa pamoja wanasimama kwenye uchaguzi huo kwa tiketi ya umoja wa vyama vya siasa wa NASA.

Katika kutafuta uungwaji mkono, tayari pande hizo zimeanza harakati za kutafuta namna ya kuwashawishi wapiga kura wao 19,611,423.

Odinga ambaye amewania nafasi hiyo mara kadhaa bila mafanikio, anatajwa kuutumia mwenedno wa kiutendaji wa Rais Magufuli wa Tanzania kuwashawishi Wakenya.

Akiwa kwenye mkutano wake wa kampeni katika mji wa Isebania katika kaunti ya Migori, iliyopo mpakani mwa Kenyas na Sirari, Tarime mkoani Mara nchini Tanzania, Odinga aliomba kura kwa wananchi wa eneo hili na kuahidi kushughulikia ufisadi, watumishi hewa na ulindaji wa rasilimali za Taifa kama anavyofanya Rais Magufuli.

Alisema Rais Magufuli ni mfano wa kuigwa barani Afrika kutokana na utendaji wake kuzingatia zaidi masilahi ya wananchi wake na nchi kwa ujumla.

“Nikifanikiwa kuwa Rais nitafuata nyayo zake, nitamwomba anipe ufagio wa mafisadi ili niwafagie hapa Kenya.

“Hapa kwetu wananchi wamekuwa masikini, hakuna chakula, sukari na vitendo vya ufisadi viko juu, wananchi wanafananishwa na punda aliyebeba mzigo mkubwa ambao hauwezi, lazima huu mzigo tuuteme na kuwapumzisha wananchi wetu.

“Mkinichagua, wanafunzi watasoma bure hadi kidato cha nne, miundombinu itatengenezwa na barabara za lami zitatengenezwa kwa sababu mimi ni Mhandisi, na hata hizi barabara mnazotumia sasa nilizilima mimi nilipokuwa Waziri wa Ujenzi  na hadi leo hazijakarabatiwa kwa sababu ya kukithiri kwa ufisadi,”alisema.

Mdahalo wa wagombea urais nchini humo unatarajiwa kuanza Julai 10 mwaka huu, na kushirikisha wagombea wa nafasi mbalimbali za urais na wawakilishi.

CCM SASA KUGUMU

Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mbali ya kuwa mfano kwenye utendaji wake Serikalini, lakini pia anatazamwa kuwa mwiba ndani ya chama chake.

Kwa sasa  mambo ndani ya CCM yamebadilika kwa kiasi kikubwa kutokana usimamizi mkali wa Mwenyekiti wake ambaye anapiga vita rushwa kwenye kila eneo.

Msimamo huo wa Rais Magufuli ndani ya chama umesababisha kupigwa marufuku suala la wagombea kutangaza nia kama ilivyokuwa awali.

Taarifa ya Katibu wa NEC-Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole imeweka wazi kuwa ni marufuku kutangaza nia au kufanya vitendo vyovyote ambavyo kwa namna moja ama nyingine vinaonekana vinataka kushwishi vikao ama vya maadili ama vya uteuzi ama vya maamuzi.