Home Habari JPM AWAPA MTIHANI WABUNGE

JPM AWAPA MTIHANI WABUNGE

5030
0
SHARE
NA JOHANES RESPICHIUS    |

RAIS Dk John Magufuli amewapa mtihani mzito Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) wa kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja ili kuleta maendeleo katika jumuiya hiyo.

Dk Magufuli alitoa mtihani huo Aprili 24, mwaka huu wakati akihutubia wabunge hao katika ukumbi wa Bunge Mjini Dodoma, ambapo alisema kuwa umoja huo unapaswa kuwa kama walivyo Marais na Mawaziri wa nchi hizo wanavyoshirikiana.

Pamoja na kuwataka wabunge hao kushirikiana pia aliwataka kutumia nafasi waliyonayo kama wawakilishi kuwaunganisha wananchi wa Afrika Mashariki kwamba wana jukumu kubwa la kuwaelimisha watu juu ya umuhimu wa jumuiya hiyo.

“Umoja wetu unatakiwa uwe umoja kama tulivyo sisi Marais, Mawaziri, watendaji mpaka wananchi wote. Ifike mahali tupendane wote, sisi ni ndugu hivyo tukishirikiana vizuri ‘on a win win situation’ tutaweza kuijenga Afrika Mashariki yenye maendeleo.

“Jukumu lililopo mbele yenu ni kubwa sana kwani ninyi ni wawakilishi na pia ni sauti ya wana Afrika Mashariki wote,” alisema Dk Magufuli.

Kuhusu sera ya Tanzania ya kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025, Rais Dk Magufuli alitoa wito kwa wabunge hao kulipa kipaumbele suala ya maendeleo ya viwanda kwa kutunga sheria nzuri zinazowavutia wawekezaji.

Ambapo alisema kuwa katika kuhakikisha lengo la kuwa na uchumi wa viwanda linatimia Serikali imekuwa ikifanya jitihada ikiwamo kuboresha miundombinu ya barabra, reli pamoja na anga.

“Tafiti zinaonyesha kuwa, gharama za usafiri katika nchi zetu za Afrika Mashariki ni mara nne hadi sita zaidi, ukilinganisha na gharama za nchi za Asia, Marekani na Ulaya.

“ Lakini tukiamua tunaweza, sisi Tanzania tumejaribu tukaona tunafanikiwa, ndio maana tumeweza kujenga reli ya kilomita 700.26 kwa thamani ya trilioni 7, kwa fedha zetu wenyewe.

“Pia tumeweza kununua ndege sita, hatukuomba mkopo. Sasa hivi tunajenga meli kubwa katika Ziwa Victoria hatukuomba mkopo. Tukiamua kutoka moyoni tutafanikiwa kisawasawa… kuna changamoto ya vikwazo vya biashara, lakini hatupendi kuyasema sema, nyinyi wabunge mnatakiwa muanze kuzitoa mapema.

“Kwahiyo niwaombe wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki mlipe kipaumbele suala la maendeleo ya viwanda. Mnapotunga sheria zenu muhakikishe zinawavutia wawekezaji kuja katika nchi zetu,” alisema Dk Magufuli.

Aliwahakikisha kuwa Tanzania ipo pamoja nao kwamba yale maamuzi ambayo yamekuwa yakufanywa na Bunge hilo lakini utekelezaji wake umekuwa ukicheleweshwa atahakikisha yanapelekwa kwa spidi.

Alisema kabla ya kuanza kwa Umoja wa Forodha mwaka 2005, thamani ya biashara katika nchi za umoja huo ilikuwa ni sawa na dola za Marekani bilioni 1.8 lakini baada ya kuanzishwa thamani imeongezeka hadi kufikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 5.

Alisema nchi za Jumuiya zimekuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali. Lakini licha ya utajiri huo bado haujawanufaisha wananchi wetu vya kutosha jambo lilimfanya ahoji haja ya kununua samaki kutoka nje wakati nchi hizo zimezungukwa na bahari, ziwa na mito.

“Kwanini tununue samaki wakati ukitoka huku chini mpaka kwenye mpaka na Somalia ni bahari kubwa, Ziwa Victoria limezunguka humu, muda mwengine tunaletewa samaki wenye low quality. Haya maswali lazima tujiulize.

“Nchi ambazo tunaziuzia malighali tunawatengenezea wananchi wake ajira wakati tungekuwa na viwanda tungeweza kuchakata hapa na watu wetu wakapata ajira, tuna madini, mifugo mingi Tanzania ni ya pili katika nchi za Afrika, bidhaa za kilimo, uvuvi, misitu, lakini licha ya utajiri huo kila mmoja anafahamu kuwa bado haujatunufaisha,” alisema.

Alisema kuwa anasisitiza suala la ushirikiano na umoja katika jumuiya huyo kwasababu masikini waliyopo Tanzania hawana utofauti yeyote na masikini wa Burundi, Rwanda, Uganda, Sudan Kusini au Kenya.

SIKU NNE ZA NGUVU D’DOMA

Rais Magufuli ambaye leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakayofanyika katika uwanja wa Jamhuri, amekuwa katika mchakamchaka tangu afike mkoani humo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mara baada ya kuingia Dodoma ambako tayari sehemu kubwa ya Serikali imeshahamia huko, Rais alizindua jengo la Mfuko wa Pensheni wa PSPF na tawi la Benki ya NMB lililopo barabara ya Chimwaga.

Mara baada ya kukamilisha zoezi hilo, siku iliyofuata Rais alipata hadhi ya kuwa mgeni rasmi kwenye Bunge la EALA ambalo linafanyika mkoani Dodoma.

Katika kudhihirisha kuwa Rais anatumia muda wake mwingi kuwatumikia Watanzania kesho atazindua barabara ya Dodoma hadi Babati yenye urefu wa kilomita 231.8.

Sherehe za uzinduzi huo zitafanyika wilayani Kondoa kwenye eneo la Bisha. Rais atapumzika kidogo na kisha Aprili 29, mwaka huu ataelekea mkoani Iringa kushiriki kwenye sherehe za wafanyakazi Mei Mosi ambazo mwaka huu zitafanyika kitaifa mkoani humo.