Home Habari kuu JPM awapa nguvu wawekezaji

JPM awapa nguvu wawekezaji

425
0
SHARE

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

KATIKA kile kinachoonekana kuimarisha mkakati wa Serikali wa kuwa na uchumi wa kati kuelekea Tanzania ya viwanda, Rais Dk. John Magufuli amezidi kuwapa nguvu wawekezaji wazawa na wa nje.

Hatua hiyo inatokana na msimamo wake wa kuitaka sekta binafsi kuhakikisha wanatumia fursa zinatolewa na Serikali ikiwamo kuwekeza nchini.

Akizindua ghala na mitambo ya kuchakata gesi ya Kampuni ya Taifa Gas iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam, Rais Magufuli aliwataka wawekezaji kuwekeza ikiwamo ujenzi wa viwanda na utoaji ajira kwa Watanzania.

Alisema anapongeza  uwezo wa gesi ya mitungi nchini kutoka tani 8,050 mwaka 2016 hadi kufikia tani 15, 600 hivi sasa.

Aprili 9, 2019 akiwa mkoani Njombe, mkuu huyo wa nchi aliwashukia baadhi ya watendaji wa Serikali kwa kuwa vichwa ngumu na hata kugeuka vikwazo kwa wawekezaji nchini.

Alisema baadhi ya watendaji hawataki kuelewa na wamekuwa wakimuona mwekezaji kama adui badala ya kumwona rafiki na kuwataka kubadilika haraka

“Kuna matatizo ya uwekezaji katika nchi yetu, saa nyingine inakuwa inakatisha tamaa kuja kuwekeza, mtu anapotaka kuja kuwekeza saa nyingine anapata shida, masharti ni ya ajabu ajabu, baadhi ya watendaji wetu wamekuwa ni matatizo katika uwekezaji.

“Ninawaomba watendaji ndani ya Serikali wabadilike, mtu anataka kuja kujenga kiwanda unamzungusha mpaka mwaka mzima.

“Yeye ana pesa zake anataka kujenga kiwanda hata mabati na ajira zitapatikana hapa, lakini watu wamekuwa na vichwa vigumu sana, nafuu vichwa vya kamongo.

“Hawataki kuelewa, wapo wawekezaji wamekuja hapa wamewekewa mikwara mpaka wakaamua kwenda nchi za jirani,” alisema.

Hata hivyo wiki hii katika uzinduzi wa mitambo ya Kampuni ya Taifa Gas inayomilikiwa na mfanyabiashara Rostam Azizi, Rais Magufuli alisema hivi sasa matumizi ya gesi yameongezeka kutoka tani 17,000 mwaka 2010 hadi kufikia tani 92,500 mwaka jana.

Kutokana na hali hiyo, alisema matumizi hayo yamesaidia kutunza mazingira na misitu kwa kupunguza matumzi ya mkaa na kuni.

“Miongoni mwa kampuni za gesi zinazofanya biashara ya gesi ya mitungi hapa nchini ni Taifa Gas iliyokuwa inaitwa Mihan Gas, kampuni hii kama mlivyosikia imewekeza Sh bilioni 150 ikihusisha ujenzi wa maghala na mitambo ya kuhifadhi kwenye mikoa 20.

“Na mojawapo ni hili ghala kubwa nililolizindua leo (juzi), limeifanya Kampuni ya Taifa Gas kuongeza uwezo wa nchi yetu kuhifadhi gesi tani 7,650, pia kampuni hii imeongeza uwezo wa nchi yetu kuongeza gesi ya mitungi kutoka tani 8,050 mwaka 2016 hadi kufikia tani 15, 600 hivi sasa.

“Nimefurahi kumwona mmiliki wa kampuni hii ni Mtanzania, kwa utekelezaji huu mkubwa mmenipa moyo kwamba Watanzania wanaweza hasa tunapoamua, hivyo Rostam ninakupongeza kwa uwekezaji huu na kuwezesha ajira za hapa nchini kufikia 260, lakini zingine kutokana na gesi hii kufikia hadi 3,000.

“Pia nimesikia mmelipia kodi na tozo mbalimbali Sh bilioni moja kwa mwaka, ni matumaini yangu haya malipo yatakuwa yanaongezeka kadiri gesi itakavyokuwa inaongezeka.

“Vilevile kama mlivyosikia sio gesi yote wanayoagiza inatumika hapa nchini bali inatumika hadi nchi za jirani kama Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Rwanda, Burundi na Zambia, hii maana yake ni kwamba nchi yetu inapata fedha za kigeni,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli aliwataka wawekezaji wengine kuiga mfano wa Rostam kwa kufanya uwekezaji kwa vitendo.

“Nakushukuru Rostam, nimefurahi sana na hiki ndicho ambacho nataka mimi, huwa sitaki wawekezaji wa maneno maneno tu, umeonyesha mfano, hii imenipa nguvu sana.

“Tafuta wawekezaji wengi hata 10 au 20 wenye moyo wa namna hii wa kuwekeza, tuje tuwape ‘support’, tunahitaji wawekezaji wa kweli waje, wasisikilize maneno ya wale ambao hawatutakii mema.

“Tukiwa na wawekezaji wa namna hii tutawasaidia na wanapowekeza tunataka wananchi nao wapate, ndio maana ya ‘win win situation’, naendelea kuwashukuru wawekezaji wa aina hii ambao watakuja kwa moyo wa namna hiyo.

“Pia Rostam umeniambia kuhusu kiwanda cha ngozi cha Morogoro ndani ya miezi mitatu, ahadi ni deni, nitakuja, nitahakikisha kukifungua kwa sababu sisi tuna mifugo mingi na Tanzania sisi wa pili au tatu Afrika, lakini hatuna kiwanda cha ngozi wakati tuna ng’ombe zaidi ya milioni 30, lakini ngozi tunaagiza nje ile ni ‘poor planning’,” alisema Rais Magufuli.

Kutokana na hilo, alisema kama kuna mwekezaji ambaye anaweza kuja nchini kuwekeza anakaribishwa.

“Akija aje awekeze kwenye ngozi na afanye mpaka kwenye ‘final product’, hapo tutavaa nguo, viatu vizuri kutokana na ngozi na wanyama wetu, kwa hiyo ‘opportunity’ ziko nyingi,” alisema.

Rais Magufuli alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wamiliki hao wa Taifa Gas pamoja na kampuni nyingine ambazo zinajishughulisha na biashara hiyo ya gesi na mitungi.

“Kuhusu mkurugenzi kueleza changamoto mliyonayo ya eneo, ni matumaini yangu kwamba mamlaka husika imesikia kwa sababu Tanzania hatujawahi kupungukiwa na ardhi.

“Miradi hii huwa inanufaisha wananchi, hivyo kama utaendelea na wananchi watakuuzia ardhi hii itakuwa faida pia kwa watani wangu Wazaramo,” alisema.

Aliwataka wawekezaji hao wa gesi, kupanua huduma zao na kwamba wasiishie mijini, bali waende hadi vijijini kwa kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi huko na ndio wanaotumia kuni na mkaa.

MILANGO KWA WAWEKEZAJI

Aidha, alisema Tanzania ni mahali salama kwa uwekezaji, hivyo wawekezaji wajiamini kwa kuja kuwekeza nchini na kwamba Serikali itawasaidia na kuwaunga mkono.

“Sekta binafsi endeleeni kujiamini, hapa ni mahali salama kwa uwekezaji, tutaendelea kuwahitaji, kuwasaidia na kuwaunga mkono, kikubwa ni kwa sababu Serikali itakusanya kodi,” alisema.

Aidha, Rais Magufuli alizipongeza sekta binafsi nchini kwa kuamua kuungana na Serikali katika kuwekeza katika gesi asilia.

Vilevile aliwataka Watanzania wanaotumia mkaa kuanza kutumia gesi ili kupunguza gharama na kulinda afya zao.

“Kwa namna ya pekee naipongeza sekta binafsi kwa kuitikia wito na kuungana na Serikali katika uimarishaji wa nishati nchini kama mlivyomsikia waziri (Waziri wa Nishati, Medard Kalemani) ameeleza nchi yetu inayo kampuni nane zilizopewa leseni ya kuagiza na kusambaza gesi ya mitungi nje ya nchi.

Rais Magufuli alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana wamiliki hao wa Taifa Gas pamoja kampuni zingine ambazo zinajishughulisha na biashara hiyo ya gesi na mitungi.

“Kuhusu mkurugenzi kueleza changamoto mliyonayo ya eneo ni matumaini yangu kwamba mamlaka husika imesikia kwa sababu Tanzania hatujawahi kupungukiwa na ardhi.

“Miradi hii huwa inanufaisha wananchi hivyo kama utaendelea na wananchi watakuuzia ardhi hii itakuwa faida pia kwa watani wangu wazaramo,” alisema.

Aliwataka wawekezaji hao wa gesi kupanua huduma zao na kwamba wasiishie mijini bali waende hadi vijijini kwa kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi huko na ndio wanatumia kuni na mkaa.

MATUMIZI YA MKAA

Akizungumzia matumizi ya mkaa, Rais Magufuli alisema Dar es Salaam kwa siku wanatumia magunia 40,000 ya mkaa, hivyo aliwataka Watanzania kubadilika kwa kuanza kutumia gesi.

Kuhusu gharama za gesi, aliwataka wasambazaji kupunguza gharama za kuuza bidhaa hiyo.

Rais Magufuli pia aliipongeza Wizara ya Nishati kwa kuimarisha huduma ya nishati, huku wananchi wengi ikiwemo vijijini wakiunganishiwa umeme.

Alisema Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia miradi mikubwa.

ROSTAM NA UWEKEZAJI

Akizungumza mbele ya Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Gesi ya Taifa, Rostam Azizi, alisema wamevutiwa zaidi kuwekeza kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya kufanya biashara nchini.

Alisema kampuni hiyo inatarajia kuwekeza miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 500 ili kuongeza fursa za ajira na mapato serikalini.

Kampuni hiyo ambayo awali ilijulikana kama Mihan Gas, inayomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100 iliandikishwa mwaka 2005 na kuanza kufanya biashara mwaka 2008.

“Tuna kila sababu ya kukushukuru mheshimiwa rais na Serikali kwa kujenga misingi imara na uwanja sawa wa kibiashara kwa wafanyabiashara na wawekezaji nchini.

“Mafanikio tuliyoanza kuyaona ni matokeo ya kazi uliyofanya kwa weledi mkubwa tangu ulipoingia Ikulu mwaka 2015, wewe siyo tu mtetezi wa kweli wa Watanzania wanyonge, bali pia ni rafiki mkubwa wa sekta binafsi.

“Umetambua vema uhusiano wa sekta binafsi utatekelezwa katika uwanja ulio sawa na kuzaa kodi na ajira zitakazosaidia kuimarisha huduma za jamii na miundombinu,” alisema Rostam.

Alisema hatua zilizochukuliwa na Serikali zimesaidia kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini na kuwavutia wawekezaji wengi, wakiwemo Watanzania waliokuwa wamewekeza nje na kuamua kurudi nchini.

 “Historia itakukumbuka katika hili, msimamo wako thabiti dhidi ya matendo ya ujanja ujanja katika biashara na uwekezaji umetufanya kupata moyo wa kurejesha mitaji yetu nchini na kuwekeza,” alisema.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara wa ndani na nje kuja kuwekeza nchini kwani milango ya uwekezaji iko wazi, lakini akasisitiza wafanye biashara kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.

MKURUGENZI TAIFA GAS

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Hamis Ramadhani, alisema uwekezaji huo umegharimu Sh bilioni 150 na umetoa ajira kwa vijana 260 wakiwemo wahitimu 130 wa elimu ya juu na ajira zisizo za moja kwa moja 3,500.

Alisema gesi hiyo ya LPG ambayo inatokana na usafishaji wa mafuta ghafi, ni rahisi kusambazwa katika mitungi na kwamba hadi sasa wameshasambaza mitungi milioni moja ya ujazo kati ya kilo tatu hadi 38.

“Tunaunga mkono azma ya kujenga Tanzania mpya ili kulinda rasilimali za nchi, mazingira na kuongeza ajira. Faida ya hatua ulizochukua ndani ya uongozi wako ni huu uwekezaji mkubwa tuliofanya na tunatarajia tutakuza soko kwa asilimia 50,” alisema Ramadhani.

Hata hivyo, alisema matumizi ya gesi nchini bado yako chini kulinganisha na nchi nyingine, hivyo kunahitajika uwekezaji mkubwa sambamba na elimu kwa wananchi kuhusu nishati hiyo.

Alisema wananchi wengi bado wanatumia mkaa ambapo kwa wastani familia moja hutumia zaidi ya gunia moja kwa mwezi na kugharimu Sh 90,000 wakati gesi inagharimu kati ya Sh 45,000 hadi 50,000 na wengi wana uwezo wa kumudu.

 “Tunafanya biashara zaidi nje ya nchi, kama Kenya tunawauzia tani 2,000 kwa mwezi, pia tunauza Sudan, Burundi na Congo na hivi sasa tunakamilisha usajili Zambia na Afrika Kusini,” alisema.

DK. KALEMANI

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani alisema kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali, sekta ya nishati imepata mafanikio makubwa.

Dk. Kalemani alisema idadi ya Watanzania wanaotumia gesi ya kupikia imeongezeka kutoka milioni 1 hadi milioni 2.5.

Alisema kampuni nane za gesi ya kupikia zimeajiri Watanzania 12,000 na uzalishaji wa umeme kuongezeka kutoka megawati 1,280 hadi kufikia 1,601.