Home Habari JPM AWAPA ONYO LA MWISHO VIONGOZI JEURI

JPM AWAPA ONYO LA MWISHO VIONGOZI JEURI

5070
0
SHARE
NA JOHANES RESPICHIUS    |   

RAIS Dk. John Magufuli ametoa onyo la mwisho kwa viongozi wote jeuri, wanaoendelea kuwahamisha watumishi na wafanyakazi bila kuwalipa fedha zao.

Alitoa onyo hilo wakati wa maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani, ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Iringa.

Rais alisema mtu yoyote anayehamisha hamisha bila kulipa pesa ni jeuri na dawa ya mtu wa namna hiyo ni kumtoa na kwamba hakuna sababu ya kuwahamisha wafanyakazi ama watumishi bila kuwalipa stahiki zao.

“Na leo nimeona bango lingine hapa lililokuwa likipita, nafikiri ni chama cha waalimu, wanasema wao wanaendelea kuhamishwa bila kulipwa pesa, sasa najua viongozi wanaosimamia hizo wizara znazohamisha hamisha wapo hapa.

“Kama kutokuwepo na Mkurugenzi ama mtu yeyote anaweza akawahamisha watu, anampeleka kule na hajamlipa posho yake ya uhamisho na awe bado anaendelea kufanya kazi, Waziri Mkuu lisimamie hilo wao wahame moja kwa moja katika maeneo yao ya kazi.

Rais alisema haiwezekeni wao watoe maagizo kisha mtu mwingine aendelee kufanya anavyotaka yeye!

“Kwa sababu hatuwezi kutoa maagizo halafu mtu mwingtine anaendelea kufanya hivyo hivyo, tulishasema kwamba ukishamuhamisha awe mwalimu au mtumishi yoyote, mlipe pesa yake kabla ya kuhama, hayo ndio maagizo tuliyoyatoa full stop.

“Sasa kama yupo mtu anamuhamisha mfanyakazi au mtumishi hamlipi pesa yake, maana yule ni jeuri na jeuri majibu yake ni kumtoa.

“Naagiza tena viongozi ndani ya Serikali na maeneo mengine wasiwahamishe watu bila kulipa pesa zao, watu wamekuwa wakihamishwa hamishwa bila sababu za msingi, sasa kama wanawahamisha na pesa za kuwalipa wawe nazo.

“Kama ni mkurugenzi wa wilaya anahamisha na pesa za kulipa awe nazo. Ni matumaini yangu sitarudia tena kulizungumzia hili katika maisha yangu.”alihitimisha Rais.

Akihutubia maelfu ya wafanyakazi waliojitokeza kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika mwanzoni mwa wiki hii, Rais alisema hiyo imekuwa ni mara yake ya kwanza kwenda Iringa tangu achaguliwe kuwa Rais wa Tanzania mwaka 2015.

Aidha aliwapongeza wafanyakazi kwa kuiletea maendelea nchi yetu na kwamba wanastahili pongezi.

“Nitumie fursa hii kuwahakikishia wafanyakazi wote nchini kuwa Serikali ya awamu ya Tano inatambua mchango wenu, na kuthamnini sana, tunawapenda sana, tuko pamoja nanyi, tutaendelea kushughulikia kero zenu zinazowakabili na kuboresha mazingira yenu ya kazi, naomba muamini hivyo.”

Pamoja na mambo mengine Rais alisisitiza nidhamu kwa wafanyakazi na kunukuu moja ya kauli zilizowahi kutolewa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Mei 1, 1974.

Alimnukuu kwa kusema: Mkulima asiyefanya juhudi katika shamba lake wakati wa kilimo, anapunguza mapato ya nchi, lakini angalau yeye anapata adhabu yake, hatapokea malipo yoyote mazao yakikosekana au kuharibika kwa sababu ya uvivu wake.

“Kwa mfanyakazi ipo tofauti kubwa, yeye hapati adhabu anayoipata mkulima, anaweza kuharibu kazi, lakini mwisho wa mwezi anaendelea kupata mshahara wake kamili kama kawaida.”

Rais alisema maana ya kauli hiyo ni umuhimu wa nidhamu kwa mtumishi na kwamba mtumishi mzembe na mvivu anakosa kutoa mchango kwa maendeleo ya taifa, zaidi ya hapo anakuwa mnyonyaji kwa kupata mashahara wa bure.

MISHAHARA

Rais aliesema kwa sasa Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo hawezi kupandesha mishahara ya wafanyakazi kama lilivyo pendekezo la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA).

Alisema alitamani kupandisha mshahara mwaka huu, lakini aliamua kwanza amalize changamoto ambazo zipo ili kuweza kupata fedha ya kutosha itakayowezesha kuupandisha kwa kiwango cha juu.

Alisema kuwa baada ya kukamilisha zoezi la kuhakiki na kuanza kuajiri watumishi wapya, jambo kubwa ambalo atalipa kipaumbele ni kuboresha mishahara na maslahi mengine ya wafanyakazi.

AJIRA

Katika upande wa ajira, Rais Magufuli alisema kuwa mpaka serikali yake imeajiri watumishi wapya 18,101 wakiwamo Walimu zaidi ya 6,500, sekta ya Afya zaidi ya 3,752, mafundi Sanifu wa maabara 386, watumishi wa Mambo ya Ndani zaidi ya 6,164, watumushi wa Mahakama 200 na 4132 katika kada nyingine.

Alisema kuwa serikali inatarajia kuajiri watumishi wengine 22,150 kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha.

MIUNDOMBINU

Rais Magufuli alisema serikali inaendelea na ujenzi wa viwanja vya ndege 11 kikiwamo cha mkoani humo ambacho kitagharimu Sh bilioni 90 kwa lengo la kuongeza watalii nchini.

“Nimejenga reli, nimenunua ndege, kujenga barabara na vyote vinategemea chungu kimoja, naamini ukijenga reli utabeba mizigo mingi, ambazo baadae utazitumia kuongezea mishahara, sasa hivi tunajenga viwanja vya ndege 11, ikiwemo cha hapa Iringa kitagharimu zaidi ya bilioni 90.

“Hatupati watalii wengi kwa kuwa sekta ya usafiri wa anga kwa muda mrefu ilikuwa ‘hoi bin taaban’, kwa kuwa asilimia 70 ya watalii wanatumia usafiri wa anga,” alisema.

MFUMUKO WA BEI

Alisema wakati serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani mfumko wa bei za bidhaa muhimu ulikuwa ni asilimia 6.6 kwamba hadi kufikia Machi mwaka huu ulishuka hadi kufikia asilimia 3.9 hali ambayo inaleta unafuu wa maisha kwa mfanyakazi.

“Serikali itaendelea kuubana mfumko wa bei za bidhaa kuhakikisha bei za bidhaa zainashuka, hicho ndicho tunakifanya ili tuendelee kuwapa unafuu ndugu zetu wafanyakazi,” alisema.

VIWANDA

Alisema mpaka sasa kuna viwanda vipya 3306 ambavyo vimejengwa vikiwamo viwanda vya kati na vikubwa na vingine vinaendelea kujengwa.

Alisema katika Mkoa wa Pwani pekee zaidi ya viwanda vipya 80 vimeshajengwa kwamba ujenzi wa viwanda hivyo ni kuongeza ajira mpya kwa Watanzania.