Home Uncategorized JPM endelea kung’arisha nchi

JPM endelea kung’arisha nchi

1162
0
SHARE

Na Franklin Victor

Tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli aanze muhula wake wa miaka mitano ya huduma kwa Watanzania, mambo mengi yamebainika, mengi yanaendelea kushughulikiwa na kazi inaonekana ikifanyika.

Kasi ya rais Magufuli kutekeleza azma na mipango ya serikali anayoiongoza kwa Watanzania sambamba na kufanikisha malengo ya ilani ya chama anachokiongoza, Chama Cha Mapinduzi – CCM, inatia moyo na hamasa hadi sasa.

Ingawa bado kazi ipo lakini miale ya nuru inaonekana. Kwa juhudi zilizofanyika serikalini kama ingekuwa ni mgonjwa tungesema ameanza kunywa uji tena akiwa kalishika bakuli na kuongoza kijiko kinywani mwenyewe bila msaada. Nchi inapumua, hapa kazi tu inaonekana kwa vitendo.

Tangu mwaka uanze tumeona na kusikia habari nyingi za u-hewa hewa zikitawala na watu wengi hewa wakibainika kuanzia watumishi hewa, wastaafu hewa, walipa kodi hewa yaani wakwepa kodi, na sasa wanafunzi hewa waliotengenezwa mahsusi ili watu wanufaike na fedha za elimu bure.

Mambo haya na mengine yafananayo lazima yafike mwisho. Tamati ya ubadhirifu, u-hewa hewa, mazoea na kadhalika itafikiwa kwa nchi kusafishwa vilivyo, kuanikwa juani ikiwezekana na kung’arishwa hadi ing’ae na kuurejea mvuto wake maarufu uliofujwa na kufujika. Majipu na yaendelee kutumbuliwa.

Jukumu hili la kusafisha na kung’arisha kona zote za nchi analolitekeleza rais Magufuli ni zito kweli hivyo anahitaji ushirikiano wa dhati wa kila Mtanzania ili mafanikio yatakayopatikana yafaidishe Watanzania na Tanzania yao.

Wiki iliyopita Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Angela Kairuki amesema hadi sasa Tanzania kuna watumishi hewa wa umma 16,127 waliobainika ndani ya taasisi 201, ambao kama wasingegundulika wangeligharimu taifa takribani shilingi bilioni 16 kwa mwezi kama malipo yao ya mshahara.

Hapo hapo wanaendelea kubainika wanafunzi hewa ambapo waliowabuni na kuwezesha uwepo wao walikuwa na azma ya kupata mgawo mkubwa zaidi wa fedha za ruzuku ya elimu bure kwa shule za msingi na sekondari zinazotolewa na serikali kutoka kwenye kodi za Watanzania.

Mamlaka ya mapato Tanzania – TRA ambayo imeshuhudiwa ikifanya vizuri kwenye ukusanyaji wa kodi na mapato ya serikali imeanza uhakiki rasmi wa namba za utambulisho wa mlipa kodi – TIN ili iwe na rekodi sahihi za walipa kodi. Kwa jinsi uhewa hewa unavyobainika kwa kasi, haitashangaza ukigundulika pia katika zoezi hili la TRA.

Ubinafsi, urasimu na utendaji wa mazoea vilivyokuwa vikiendekezwa katika sekta ya umma ndivyo vimefanya baadhi ya watendaji wasiwe na hofu ya kujiamulia tu mambo watakavyo bila kujali kama yanaongeza ugumu wa maisha kwa wengi. Licha ya kuonywa, kutahadharishwa, kuaswa na kuombwa bado kuna watu wanathubutu kufanya ndivyo sivyo kimazoea mathalani juu ya kodi za wananchi na mali za umma.

Kwani taasisi kama ile yenye jukumu la kulipa fedha za kujikimu kwa kaya maskini inawezaje kuwalipa wasiohusika na kuwaacha wahusika wakishangaa shangaa! Au ni ushujaa gani anaokuwa nao mhusika anapoamua kutengeneza wanafunzi hewa ili kusudi tu apate fedha zaidi ya stahiki za ruzuku ya elimu bure!

Katika harakati hizi chanya za kusafisha na kung’arisha nchi suala la ulinzi na usalama nalipa umuhimu miongoni mwa mengi mengineyo yanayobeba maelewano, utawala wa sheria na utulivu. Vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi nzuri hivyo kustahili na kuhitaji kupata ushirikiano hususan juu ya intelijensia na taarifa za matukio mbalimbali.

Jambo moja ambalo nimewahi  kulizungumza na naendelea kulisisitiza ni umuhimu wa kuitazama upya na kwa makini dhana ya polisi jamii/ulinzi shirikishi; hasa juu ya uwepo wa vikundi vingi vinavyojipa mamlaka na majukumu ya vyombo vya dola kwa aidha, makusudi au bahati mbaya vikisingizia polisi jamii.

Mheshimiwa rais Magufuli, uwepo wa vikundi vya polisi jamii vinavyolalamikiwa na wananchi ni ‘jipu’ kwa usalama wa taifa siku zijazo. Uwepo wa vikundi vinavyoogopwa mitaani kutokana na wanaohusika navyo kujichukulia sheria mkononi si jambo la kuachwa tu wakati huu serikali yako ikiisafisha kisha kuing’arisha vilivyo Tanzania.

Binafsi naendelea kuamini suala la ulinzi na usalama ni kazi nyeti, jukumu zito na fani inayohitaji watu mahiri, weledi, makini na waliofuzu vilivyo kinidhamu na uelewa hasa wa sheria, kanuni na taratibu nchi. Wakati usafi ukiendelea ingeswihi kukusikia mheshimiwa rais ukitoa kauli moja fupi itakayosambaratisha vikundi vyote vinavyotumia kisingizio cha polisi jamii kuonea, kujinufaisha na kukosesha raha wananchi.

Mengi yanashuhudiwa wakati huu rais Magufuli akirekebisha nidhamu na heshima za watendaji wa umma ili wang’ae kwa usafi wa kimaadili. Ukikutana na watendaji walioajiriwa kwa kutumia sifa zisizo zao kwa maana ya vyeti hewa, vyeti bandia utawaonea huruma kwa jinsi wanavyohaha kuhakikisha uhakiki unaofanywa na serikali kwa sasa ‘hauwatumbui’.

Yaani mtu anajua kabisa mamlaka aliyonayo, kazi aliyonayo aliipata kwa njia hewa, vyeti hewa na sifa hewa lakini hakubali ‘kutumbuliwa’ kirahisi. Ndiyo maana wahenga walinena wazi kwamba mzoea vya kunyonga, vya kuchinja haviwezi; na bado watu wakabisha.

Serikali ya awamu ya tano inafanya mambo makubwa licha ya changamoto za hapa na pale. Nia ya rais Magufuli ni nzuri kwa Watanzania na Tanzania yao kuyaelekea maendeleo yanayotakwa na kila mtu. Kazi hii inayofanywa ya kusafisha sekta zote na kuhakikisha Tanzania inarejesha nuru yake bila mawaa ya uhewa hewa, wizi, urasimu, mazoea katika utendaji, uonevu na kadha wa kadha inastahili kuungwa mkono.

Yapo mengi yanayolazimu kubainishwa, yapo mengi zaidi yanayohitaji kushughulikiwa kwa ukamilifu. Itoshe kwa sasa kusema kazi nzuri sana unayofanya mheshimiwa rais Magufuli na serikali yako; angalau ule mng’aro wa Tanzania halisi unaanza kuonekana. Kazi ndiyo kwanza imeanza, mheshimiwa Rais JPM endelea kusafisha nchi, ing’ae zaidi. Hakuna lisilowezekana.