Home Habari kuu Juhudi za Serikali bado inahitajika kutokomeza ukeketaji

Juhudi za Serikali bado inahitajika kutokomeza ukeketaji

708
0
SHARE

Anna Henga

UKEKETAJI ni kitendo kinachohusisha kukata au kuharibu sehemu ya uke wa mwanamke hasa kinembe kwa sababu zisizo za kisayansi. Kitendo hiki pia hujulikana zaidi kama tohara kwa mwanamke ambayo hutekelezwa kwa sababu za kiutamaduni.

Shirika la Afya Duniani limeelezea aina nne za ukeketaji; ambazo ni kutoa sehemu nzima ya kinembe, kutoa sehemu nzima ya kinembe na mashavu ya uke, kutoa sehemu za ndani za uke, ukataji wa sehemu yoyote ya uke.

Aina hizi zote ni mbaya kwani zinamletea maumivu makali sana mwanamke anayekeketwa na kwa Tanzania aina ya kwanza na ya pili hutumika zaidi.

Sababu nyingi za ukeketaji ni mfumo dume na mila kandamizi kwa wanawake, sababu za mila na utamaduni ikiwemo kutambikia masharti ya mizimu, desturi za wazee wa mila au kuondoa mikosi katika familia.

Pia kuna sababu za kiuchumi kwani umasikini umekuwa chachu ya jamii nyingi kubaki katika kitanzi cha mila ya ukeketaji kwani wazazi wa mtoto husika hutegemea kupata kipato kwa kumwozesha binti baada ya kumkeketa. Pia ngariba/mkeketaji hutegemea kipato kutokana na shughuli za ukeketaji.

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuboresha sheria na sera kwa lengo la kukabiliana na ukeketaji na kuwajibisha wote wanaoendeleza mila hiyo kandamizi kwa watoto wa kike na wanawake.

Lakini sheria za ukeketaji bado hazijitoshelezi kwani adhabu ni ndogo sana lakini pia hakuna sheria inayomlinda mwanamke mwenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea.