Home Latest News JUKWAA LA KATIBA SASA LATAKA MABADILIKO YA KATIBA

JUKWAA LA KATIBA SASA LATAKA MABADILIKO YA KATIBA

6282
0
SHARE

NA LEONARD MANG’OHA


Miongoni mwa mambo muhimu ambayo sasa hayazungumzwi na wengi, ni mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioanza mwaka 2012.

Mchakato huo ulianza baada ya Rais Dk. Jakaya Kikwete, kumteua Jaji Joseph Warioba, kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na na baadae kumwapisha pamoja na wajumbe wake, Aprili 13 mwaka 2012.

Kuundwa Tume hiyo kulitokana na matakwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011.
Makamu Mwenyekiti wa Tume alikuwa Jaji Mkuu Augustino Ramadhan (mstaafu), na ilikuwa na wajumbe 30, yaani 15 kutoka Tanzania Bara na 15 kutoka Zanzibar.

Baada ya kuapishwa kwa Tume hiyo, mchakato wa Katiba Mpya ulianza kwa hatua ya kukusanya maonia ya mwananchi. Rasimu ya kwamza ya Katiba Mpya ulitoka Juni 3, mwaka 2013, na ikazinduliwa jijini Dar es Salaam.

Licha ya mchakato huo kwenda vizuri katika hatua za awali, uliingiwa na ‘kidudu mtu’ baada ya kupelekwa katika Bunge Maalumu la Katiba lililoongozwa na Mwenyekiti Samwel Sitta.

Pamoja na mambo mengi muhimu yaliyikuwa ndani ya rasimu ya Jaji Warioba, Bunge likatawaliwa na hoja ya muundo wa Serikali. Baadhi ya wajumbe wakitaka kuwapo kwa Serikali mbili, yaani Serikali ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano, na upande mwingine ukitaka serikali tatu—Serikali ya Tanganyika, serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.

Kwa kuwa kila aliyejaribu kutetea alikuwa akiangalia maslahi binafsi, wajube wakashindwa kupata mwafaka. Mwisho wa siku, muda wa Bunge ukafikia tamati na mchakato ukaishia hapo. Hii ilitohana na kweli kwamba muda uliku mfupi kwa sababu 2015 kulikuwa na  Uchaguzi Mkuu, na isingewezekana Katiba hiyo itumike katika uchaguzi huo.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, Serikali ikajipambanua kuwa suala hilo sio kipaumbele chake, hivyo mchakato huo sasa umesimama kwa zaidi ya miaka miwili na nusu.

Hadi sasa hakuna amayefahamu kama mchakato huo utaendelea au la. Lakini wengi wanasema kuwa ji kama Tume ambayo ilifanya mikutano 1, 942 kwa ajili ya kukusanya maoni  ya wananchi zaidi ya milioni 1.365 na fedha nyingi iliyotumika, vyote ni kama bure!

Miaka miwili imesalia kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020, vilio kuhusu kasoro mbali mbali kuhusu mfumo wa siasa unaotumika sasa, vinaendelea kutamalaki miongoni mwa jamii—hususan

Kibaya zaidi, hata Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa Namba Tano ya mwaka 1992, nao umegonga mwambwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Je, tunakwendaje katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu mwaaka 2020?

Je, itatumika Katiba ya sasa ambayo wadau na vyama vya siasa wanailalamikia kuwa imekuwa na upungufu mengi katika kulinda haki za kisiasa na kiraia, Katiba inayodaiwa kuwa inakipendelea chama tawala—Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kutokana na kasoro kadhaa zinazotajwa kuwapo Katiba ya sasa, Jukwaa limeamua kutafuta mbinu mpya ya kukabiliana na baadhi ya kasoro hizo. Limeandaa mpango wa kupeleka bungeni mapendekezo ya mabadiliko ya baadhi ya ibara katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka , na katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, pamoja na Sheria ya Uchaguzi, baada ya kushindwa kukamilika mchakato wa Katiba Mpya.

Katika mkutano na vyombo vya habari hivi karibuni, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, anasema mapendekezo hayo yanalenga kuzishawishi mamlaka husika, kuona haja na ulazima wa kufanyika kwa mabadiliko ya haraka ya baadhi ya ibara za Katiba ya sasa, vifungu vya sheria na baadhi ya maneno ya kanuni, kuhusiana na mfumo, usimamizi na uratibu wa uchaguzi nchini.

Baadhi ya maeneo yanayopendekezwa kufanyiwa mabadiliko ni pamoja na kupatikana kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo muundo wake utaakisi majukumu yake kwa kuwapo Kamisheni yenye wajumbe tisa, itakayoongoza Tume hiyo katika utendaji kazi wake, ikiwa ni pamoja na kuwajibika kwa mambo yote ya kisera na kimaamuzi, pamoja na kuundwa kwa Sekretarieti ya Tume itakayokuwa chini ya Mkurugenzi wa Tume, kama mtendaji mkuu.

Kwa sababu mara nyingi Rais anayekuwa madarakani, anaweza kuwa miongoni mwa wagombea katika Uchaguzi, au anakuwa kiongozi wa chama kimoja wapo cha saisa ambacho kinasimamisha mgombea.

Jukwaa la Katiba linapendekeza kupunguzwa kwa mamlaka ya uteuzi kwa Rais kama ilivyo sasa, ambapo mamlaka yote ya uteuzi yako chini yake.

Badala yake inapendekezwa kuwa mchakato wa kuwapata makamishna wa Tume, utangazwe, ufanyike usaili na baada ya mchujo, majina 20 yapelekwe kwa Rais ambaye atapendekeza majina tisa yatakayopigiwa kura na Bunge.

Baada ya Bunge kufanya uchambuzi na kuyajadili, majina hayo yatayawasilishwa tena kwa Rais ili amteue Mwenyekiti. Rais atapeleka majina kwa Jaji Mkuu ambaye atayatangaza na kuwaapisha  makamishna wa Tume.

Pia Jukwaa linapendekeza kuwa, Rais atamteua Mkurugenzi wa Tume kutokana na majina mawili yaliyopelekwa kwake na Tume ya Uajiri wa Umma kutokana na mchakato huru na wa wazi wa uajiri.

Kwa mantiki hiyo, Mkurugenzi wa Tume ndiye atakuwa Mtendaji Mkuu wa Tume hiyo,  pia atakuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi na Katibu wa Kamisheni ya Tume (Bodi).

Katika mkutano wa Jukwaa, iliibuka hoja ya mgombea huru ambaye kimsingi alikwisha ruhusiwa katika hukumu mbali mbali katika Mahakama za ndani na ile ya Afrika, ambazo kwa nyakati tofauti, ziliitaka Tanzania kubadili Katiba yake ili kuruhusu haki mtu kuomba ridhaa ya kuchaguliwa pasipo kudhaminiwa na chama cha siasa.

Kuhusu usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi ambazo zimekuwa zikihubiriwa na wadau mbali mbali, yaani (50 kwa 50), Jukwa linapendekeza kupunguzwa majibo ya uchaguzi kuwa 75, kisha kila jimbo litoe wabunge wawili—mmoja wa kike na mwingine wa kiume.

Pia imependekezwa kuviruhusu vyama vya siasa kuungana katika chaguzi na kusimamisha mgombea mmoja, na kutumia ilani moja ya uchaguzi. Pia vyama viruhusiwe kujiua na kuunda chama kimoja, bila kulazimishwa kama ilivyo sasa.

Jukwaa linaamini kuwa matokeo ya urais yanapaswa kupingwa mahakamani, kama ilivyo matokeo udiwani na ubunge.

Hoja hii inaonekana kuwa na mashiko, kwa sababu Mahakama ndicho chombo cha juu cha kutoa uamuzi, na wananchi wanapaswa kupewa haki ya kuhoji, tofauti na sasa ambapo Tume ikishatangaza matokeo ya Urais, hayatakiwi kuhojiwa.

Kipengele hiki kinapaswa kuangaliwa upya, kwa sababu kinaweza kutoa mwanya kwa Tume kumtangaza mtu kwa sababu ya maslahi binafsi hata kama hakushinda na kupoteza haki ya waliyo wengi.

Mathalani kikundi cha watu wenye nia ovu, wakiamua kumpenyeza mtu katika mchakato wa kumpata Mwenyekiti wa Tume, kwa bahati mbaya mamlaka za uteuzi isiligundue hilo, ni wazi kuwa inaweza kulipatia taifa kiongozi asiye sahihi.

Inapendekezwa kwamba chaguzi zote, za serikali za mitaa, madiwani, wabunge na rais, zisimamiwe na chombo kimoja chenye taaluma na weledi wa kusimamia uchaguzi.

“Kuendelea kuuweka Uchaguzi wa Serikali za Mitaa chini ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ambayo iko chini ya Ofisi ya Rais, kunaleta hisia za unyonge kwa vyama ambavyo havijashika dola kwa sasa,” anabainisha Kibamba.

Jukwaa linashuri kuwa, ili kuleta hisia za haki, ipo haja ya kurejesha mfumo wa ushindi katika uchaguzi wa rais, kwa kigezo cha kupatikana kwa asilimia 50+1, ili kuhakikisha kuwa mgombea urais anayeshinda, anakuwa amechaguliwa na wananchi wengi, tofauti na sasa ambapo mshindi anaweza kupatikana kwa idadi yoyote—ilimdari tu amewashinda wenzake.

Athari ya kutozingatiwa jambo hili, ni kwamba ipo hatari ya rais kupatikana kutokana na kabila lake kuwa na idadi kubwa ya watu, jambo ambalo linaweza kuathiri hali ya kisiasa nchini.

Kudhibiti hama hama

Kutokana na kushamiri kwa vitendo vya Wabunge na Madiwani kuhama vyama vyao na kujiunga na vyama vingine, hali inayosababisha kurudiwa kwa uchaguzi katika majimbo na kata, Jukwaa linashauri kufanyika mabadiliko ya sheria yatakayoruhusu Wabunge kuhama bila kuhitajika uchaguzi wa marudio.

Pamoja na mambo mengine, Jukwa linataja gharama za  uchaguzi wa marudio kama moja ya mambo yanayolalamikiwa na wananchi kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kutokana na uzoefu, Jukwaa linashauri  kuwa ikiwa kiongozi aliyepo madarakani amefukuzwa uanachama na chama chake, basi aruhusiwe kuendelea na uongozi hadi hapo kipindi chake kitakapofikia ukomo.

Hili ni wazi kuwa litawezekana katika mfumo wa kuwa na mgombea binafsi. Lakini Jukwaa linaonya kuwa kwa mwanasiasa aliyejiengua mwenyewe uanachama, nafasi yake inapaswa kuchukuliwa na mtu aliyekuwa mshindi wa pili.

Ni maoni ya Jukwaa kuwa mwanasiasa aliyejiengua mwenyewe, awekewe kizuizi cha kisheria, ili asiweze kuomba tena kuchaguliwa katika eneo hilo, au jingine lolote katika kipindi cha angalau miaka kumi mfululizo.

Pamoja na kupendekeza jambo hilo, inashauri kuingizwa kwa kipengele cha sheria kinachoruhusu uchaguzi kurudiwa katika mazingira ambayo mwanasiasa/kiongozi amefariki dunia, ili kuepusha mazingira ya viongozi hao kuuana.