Home Latest News Juve mabingwa Uefa msimu ujao?

Juve mabingwa Uefa msimu ujao?

770
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

LICHA ya utemi wao Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’, Juventus wanaumaliza msimu huu wakiwa na majonzi makubwa, chanzo kikiwa ni kushindwa kulibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ikiwa ni mara yao ya nane mfululizo kulibeba taji la Serie A, Juventus waliishia hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa, tena safari yao ikikatishwa na vijana wa Kiholanzi, Ajax.

Ni kweli huenda Ajax wana kikosi kizuri msimu huu lakini ni ngumu kuipa nafasi mbele ya Juventus yenye Cristiano Ronaldo, Paulo Dybala, Miralem Pjanic na Douglas Costa.

Mbaya zaidi kwa mabosi wa klabu hiyo ya mjini Turin, usajili wa bei mbaya (Pauni milioni 100) wa Ronaldo ulilenga kuipa taji la Ligi ya Mabingwa na si Serie A.

Je, nini kinachoweza kuifanya Juventus kuwa tishio msimu ujao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na hata kulipeleka mjini Turin taji hilo lenye heshima kubwa barani humo?

Kwanza, lazima kocha Massimiliano Allegri afungashiwe virago. Ndiyo, licha ya kufanya kazi nzuri katika michuano ya ndani tangu alipomrithi Antonio Conte, Allegri hana cha kujivunia Ligi ya Mabingwa.

Wachambuzi wamekuwa wakizikosoa mbinu zake, hasa inapofika hatua ya mtoano, kama ilivyoonekana dhidi ya Ajax, ambapo vijana hao wa kocha Erik Ten Hag walitawala michezo yote miwili (nyumbani na ugenini).

Swali ni je, ikiwa Juventus ndiyo timu tishio zaidi kwa misimu nane mfululizo ya Serie A, kwanini hadi sasa isiwe na walau taji moja la Ulaya?

Pili, ili kutamba Ligi ya Mabingwa, lazima safu ya kiungo ya Juventus ifanyiwe marekebisho makubwa. Ikiwa haina kwa sasa, inahitaji viungo wenye uwezo mkubwa wa kusukuma mashambulizi, ikizingatiwa kuwa ni timu inayopenda mashambulizi ya kushitukiza.

Ukikitazama kikosi hicho, ni Pjanic pekee ndiye anayeonekana kuwa kiungo wa kiwango cha juu, tofauti na Sami Khedira, Blaise Matuidi, Emre Can na Rodrigo Bentacur.

Tatu, uongozi wa Juventus unahitaji kusajili zaidi, ukiacha Aaron Ramsey ambaye atatua klabuni hapo wakati wa majira ya kiangazi. Ukizingatia uwezo na uzoefu, beki wa Real Madrid, Marcelo, anaweza kuwa na faida kwao.

Ujio wa Marcelo utakuwa na msaada mkubwa kwa beki mwingine wa pembeni, Alex Sandro, kwani Mbrazil mwenzake huyo ametoa ‘asisti’ mbili pekee tangu kuanza kwa msimu huu.

Pia, endapo Juventus watafanikiwa kuinasa saini ya staa wa Benfica, Joao Felix, watakuwa wameiimarisha safu yao ya ushambuliaji inayoongozwa na Cristiano.

Kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali uwanjani, anaweza kuwaweka kando Manzukic na Dybala ambao ni kama makali yao yameshuka kwa kipindi cha hivi karibuni.

Pia, katika eneo la ulinzi, bado Juventus hawatakiwi kupuuza harakati zao za kuiwania saini ya beki wa Ajax, Matthijs De Ligt. Si tu uwezo mkubwa alionao katika kuwadhibiti washambuliaji, pia umri wa miaka 19 alionao mlinzi huyo wa kati unaweza kuwa faida ya muda mrefu kwa kikosi hicho.

Mwisho, ukweli ni kwamba Juventus wanatakiwa kuvumilia, wakikumbuka kuwa fedha nyingi au wachezaji wenye majina makubwa si kigezo cha kulinyakua taji la Ligi ya Mabingwa.

PSG na Manchester City zinaweza kuwa shuhuda mzuri katika hilo, kwamba licha ya kiasi kikubwa cha fedha zilizotumia katika usajili, bado hazijaweza ‘kuiteka’ michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Ulaya.

Kama zilivyo Barcelona, Madrid na Bayern Munich, timu zinazoweza kutwaa ubingwa wa mashindano hayo ni zile zenye vikosi imara, vilivyojengwa kwa misingi ya kimfumo na si uwezo wa mchezaji mmoja.