Home Latest News Kagere kuendeleza ubabe wafungaji wa kigeni TPL?

Kagere kuendeleza ubabe wafungaji wa kigeni TPL?

4148
0
SHARE

NA MAREGES NYAMAKA

ZIMEBAKI wiki chache kabla ya kumalizika kwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), huku vigogo Simba na Yanga, kila moja ikiwa ni nafasi ya kuutwaa ubingwa baada ya Azam kurudi nyuma.

Simba wenye pointi 83, wanaongoza ligi wakiwa wamekabiza michezo mitano, Yanga wakiwa na 80 kwa mechi tatu mkononi, huku Azam wanaoshika nafasi ya tatu wakiwa wamekusanya 69.

Hata hivyo, katika kila msimu, ukiacha hilo la ubingwa, huwa kuna mambo mengine mawili yenye mvuto mkubwa kwa mashabiki wa kandanda duniani kote.

Achana na uhondo wa timu za chini zinavyopigana vikumbo kulikwepa shimo la kushuka daraja, hasa kipindi kama hiki cha mechi zilizobaki.

Utamu zaidi ni ile vita ya kukifukuzia kiatu cha mfungaji bora, kama tulivyoshuhudia hivi Ligi Kuu ya England (EPL), ambapo wakali watatu; Mohamed Salah, Pierre-Emerick Aubameyang na Sadio Mane, walifungana, kila mmoja akiwa ameziona nyavu mara 22.

Kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, kinyang’anyiro hicho hunoga zaidi kwani huwa kuna ushindani mkali kati ya washambuliaji wa kigeni na wazawa.

Huenda hiyo inatokana na mvutano wa kisaikolojia, wakati wachezaji wazawa wakitaka kuthibitisha kuwa hakuna haja ya wageni kusajiliwa, ‘maproo’ nao hupania kuthibitisha uwezo wao, kwamba hawakuja nchini kushangaa maghorofa.

Ukitazama kinachoendelea hadi kufikia hatua hii ya msimu huu, ni kama ngoma imeonekana kuwa ngumu kwa wapachikaji mabao wa Tanzania kwani bado Meddie Kagere raia wa Rwanda amekaa kileleni kwa mabao yake 20.

Hakuna ubishi kuwa ni mmoja kati ya wapachikaji mabao hatari wa kigeni kufika nchini na huenda mchango wake wa mabao sita wakati Simba inatinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ukabaki kwenye kumbukumbu za muda mrefu klabuni hapo.

Tukirejea katika orodha ya wale wanaomkaba katika kinyang’anyiro hicho cha tuzo ya mfungaji bora TPL, bahati mbaya kwa washambuliaji wa Tanzania ni kwamba huenda hata wakaikosa nafasi ya pili kufikia mwishoni mwa msimu huu.

Wakati Kagere akiongoza, anayefuata ni ‘proo’ mwenzake raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Heritier Makambo, aliyepachika mabao 16, sawa na mshambuliaji mzawa, Salim Aye, anayeichezea Mwadui.

John Bocco, nahodha wa Wekundu wa Msimbazi, anafuata kwenye mbio hizo lakini idadi yake ya mabao 14 ndiyo aliyonayo staa wa timu ya taifa ya Uganda, Emmanuel Okwi, hivyo ni wazi ana kazi kubwa.

Kwa misimu 10 iliyopita, washambuliaji wa Tanzania wameibuka kidedea mara tano, kama ilivyo kwa wenzao wa kigeni.

Lakini, kwa misimu mitano iliyopita, ni mara mbili pekee imewashuhudia wazawa wakiipeleka nyumbani heshima hiyo (Simon Msuva na Abdulrahaman Musa).

Msuva, ambaye kwa sasa anaichezea Difaa Hassani El-Jadidi ya huko Morocco, alichukua kiatu msimu wa 2014-15 akiifungia Yanga mabao 17.

Msimu wa 2016-17 ulikuwa mzuri pia kwa wachezaji wa Tanzania kwani Msuva na Abdulrahaman wa Ruvu waligawana tuzo hiyo baada ya kila mmoja kufunga mabao 14.

Hivyo, misimu mitatu iliyobaki (2013-14, 2015/2016 na 2017-18) ilishuhudia Amiss Tambwe akiibeba mara mbili tuzo hiyo na ile moja ikitua mikononi mwa Okwi.

Akiwa na Simba msimu wa 2013-14, aliibuka mshindi kwa mabao 19, akiwaacha mbali Mrisho Ngassa na Elias Maguri waliokuwa na mabao 13 kila mmoja, kabla ya kufanya hivyo 2015-2016 kwa kuipachikia Yanga mabao 21.

Kwa upande wa Okwi, ni msimu uliopita, alipozifumania nyavu mara 20, nafasi ya pili ikishikwa na John Bocco (14), huku ile ya tatu ikiwa ya Obrey Chirwa (12).

Aidha, kwa kipindi chote hicho cha misimu 10 iliyopita, hakuna mshambuliaji wa Tanzania aliyemaliza msimu akiwa na mabao 20, wakati maproo wamefanya hivyo mara mbili, kwa maana ya Tambwe (21) na Okwi (20).

Bocco anabaki kuwa mshambuliaji pekee mzawa aliyeikaribia idadi hiyo lakini alipochukua kiatu msimu wa 2011-12 alikuwa amecheka na nyavu mara 19.

Hivyo basi, endapo kasi yake hii ya kuwatungua walinda mlango itaendelea, si tu Kagere atakuwa ameipiku rekodi ya Tambwe.

Pia atakuwa amewaongezea mlima mrefu washambuliaji wa Tanzania kutoka katika idadi yao hiyo ya mabao (19).

Faida kwa mpachikaji mabao huyo wa zamani wa Gor Mahia ni kwamba kati ya michezo mitano iliyobaki ni dhidi ya Mtibwa Sugar (miwili), Ndanda, Singida United na Biashara United.

Kati ya hiyo, mitatu itaikuta Simba ikiwa nyumbani katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ikianza na Mtibwa leo, kabla ya kumenyana na Ndanda mwishoni mwa wiki hii.