Home Habari Kaisari anapoteka Kanisa Altare ya Mungu huchafuka

Kaisari anapoteka Kanisa Altare ya Mungu huchafuka

926
0
SHARE

Joseph Mihangwa

WIKI kadhaa zilizopita, tukio moja lisilo la kawaida lilitokea mkoani Mbeya kwa Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila kuonekana akifuatilia mgogoro wa kiutawala wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kanda hiyo kudhibiti jambo la ndani ya kanisa hilo.

Siku ya kwanza, mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vilimwonesha mkuu huyo wa mkoa akikemea msigano miongoni mwa watendaji wa kanisa hilo kati ya makasisi na waumini na kutishia kuchukua hatua kali za Kiserikali dhidi ya wote watakaodharau maagizo yake.

Aliizodoa ofisi ya kanisa hilo kwa kujibu barua zake alizoliandikia Kanisa, kwa kutoa maelezo ya rojorojo akisema na kuonya wasimchukulie yeye kama mtoto mdogo au mtu wa kuchezewa hata kidogo; akatishia kufunga baadhi ya miradi ya kanisa yenye migogoro ikiwamo huduma za tiba, kwa maana ya hospitali za Kanisa.

Migogoro iliyoibuliwa kikaoni hapo ni pamoja na uhamisho wa kiholela na usiozingatia haki wa watumishi na Makasisi wa Kanisa; matumizi mabaya ya ofisi, rasilimali watu na rasilimali fedha na unyanyasaji wa kiroho na kiimani wa Makasisi kwa kutishiwa na utawala kufutiwa Ukristo wao. Mkuu huyo wa Mkoa alitoa siku kadhaa kwa Kanisa kuchukua hatua dhidi ya tuhuma hizi na kupelekewa taarifa.

Hatua ya pili ilihusu Mkuu wa Mkoa huyo kuitisha kikao kwa lengo la kupewa taarifa ya utekelezaji wa maagizo yake, ikiwamo kusomewa taarifa ya ukaguzi wa rasilimali fedha, miradi na uendeshaj wa shughuli. Wakati taarifa ikisomwa, aliinuka kitini na kuchukua kipaza sauti kutoa ufafanuzi mwenyewe juu ya mambo ya kikanisa na kuzidi kuelekeza kwa mengi.

Haya yakitendeka, mfumo wa Kikanisa [KKT] ulikuwa kimya (kwa hofu?) huku ikijulikana kwamba taasisi za kiroho zina Viongozi wake kwa mfumo na kwa maadili ya Kikanisa kwa Waajiriwa wake, Makasisi na waumini pia katika vikao na safari zote mbili, Mkuu aliandamana na vyombo vya Usalama, na wakati taarifa ya ukaguzi ikisomwa na yeye kusimama kufafanua mara kwa mara, pembeni mwake alikaa na Askari Polisi wenye sare za “Kikombati”.

Mtu anaweza kujiuliza: hivi uhamisho wa Makasisi; utawala/usimamizi wa kiroho na kiimani na mali za Kanisa ulimhusu nini Mkuu wa Mkoa wakati kuna Uongozi wa juu wa Kanisa, kama vile Askofu Mkuu, Baraza la Kitawala na  vikao vingine vyenye mamlaka ya kichungaji na utawala wa Kanisa?.

Pamoja na ukweli kwamba Serikali yoyote madarakani ina jukumu la kulinda amani pamoja na kuratibu kwa wema shughuli za taasisi za kijamii nchini, lakini mambo na shughuli za kiroho zina unyeti na upekee wake, na mara nyingi, mambo kama hayo, kama hayana viashiria vya uvunjifu wa amani; huachiwa watawala wa kiroho. Ni tukio lenye kuvuka mipaka ya Kikatiba inayotaka kwamba, mambo ya imani na uendeshaji wa shughuli za kidini ni jambo la mtu binafsi. Je, huku tukuite ni kulewa madaraka au kutojua wajibu?.

Duniani kote na si hapa kwetu pekee, pengine huwa si busara kwa Serikali kuingia malumbano na taasisi za kidini, hasa zinapotekeleza shughuli zake za “Kitume” kwa nia njema na kwa manufaa ya jamii pana; kinyume chake, mara nyingi Serikali kama hizo huweza kujipalia moto wa makaa na adha zinazoepukika.

Wala si busara sana kwa Serikali/Watawala kuonesha chuki au hasira pale wanapokosolewa na Viongozi wa dini kama ambavyo tu wao wanaweza kutoa ushauri [rudia: ushauri] kwa Viongozi wa Kikanisa kuwaimarisha “kondoo” wao kiroho na kijamii kwa kuwa lengo la siasa na dini ni moja: “Ukombozi” wa Mwanadamu kutoka kwenye minyororo, uonevu na ukandamizaji wa ki-Goliati.

Itoshe kwa utangulizi huu, kabla ya kudadavua juu ya mahusiano yanayopaswa kuwa, kati ya siasa [watawala] na dini, kutamka kwamba, picha hasi aliyoonesha Mkuu huyo wa Mkoa haikuashiria “usawa” kati ya taasisi hizi mbili muhimu katika jamii – utawala na dini kwa maendeleo ya watu, na pia kwa taasisi mbili hizi kutegemeana.

Zaidi ya miaka 100 iliyopita, mwanaharakati wa siasa za mapambano, Karl Marx, alidai kwamba, “dini” ni bangi inayolevya na kupumbaza watu, wasiweze kujua adui wao wala kupigania haki zao.  Kwa mtizamo huo, Marx aliona dini kama taasisi inayopinga mapinduzi ya wanyonge, wenye kuonewa na kunyanyaswa, akatangaza vita dhidi yake. Ni kwa sababu hii mpaka leo dini katika ujumla wake havikai meza moja na itikadi za Ki-Karl Marx, kwa maana ya Ukomunisti na dhana zingine za kimapinduzi za mwanadamu duniani.

Kabla ya hapo, Yesu Kristo [Nabii Issa], wakati akijibu mashtaka dhidi yake kwenye kesi ya uhaini, kwa tuhuma za kutaka kupindua Serikali ya Kaisari, alipewa mtego, aeleze ni kwa mamlaka yapi alielekeza utii wake; naye akajibu, “Cha Kaisari apewe Kaisari, na cha Mungu apewe Mungu”.  Hapo ndipo ikazaliwa dhana ya kutochanganya dini na siasa, tafsiri ambayo imewasilishwa kwa kupotoshwa katika jamii mara nyingi, kwamba Viongozi wa dini hawapaswi kukemea maovu katika jamii.

Katika makala haya nitatumia neno “kanisa” kumaanisha jumuiya za waumini wa dini mbali mbali katika jamii pana inayotawaliwa, bila ubaguzi wa ki-madhehebu.  Kwa kifupi, kanisa ni waumini wa dini chini ya madhehebu mbali mbali, na si majengo ya kuabudia pekee.

Kwa Karl Marx, hapo kale, dini na kanisa vilikuwa vyombo vya watawala na wenye elimu, vilivyotumika kuwakandamiza na kuwaogofya [juu ya moto wa milele], kuwadhibiti na kuwapumbaza wanyonge kwa ahadi ya “ufalme wa mbingu”, kwa kujikana wenyewe ili  wasielewe chanzo cha matatizo yao yenye kusababishwa na binadamu wenzao.

Kilicho wazi hapa ni kwamba, upofu wa Karl Marx haukuwa juu ya dini, bali ugomvi wake ulikuwa juu ya watawala na mwenendo wa Kanisa la wakati wake lililotekwa na ubinafsi wa watawala, wakachanganya dini na utawala kuzaa kinachoweza kuitwa utawala wa Kiotheokrasia, kwa maana ya Taifa kuongozwa kwa misingi ya kidini au Serikali ya Makasisi [Theocracy].

Wapo waliomtangulia Karl Marx waliogundua udhaifu huo wa Kanisa pekee la Roma la wakati huo [lililotekwa nyara na watawala tangu enzi za Mfalme Constantine wa I], lakini hawakushambulia dini, badala yake walishinikiza kufanyika marekebisho katika mfumo na mwenendo wa Kanisa bila kuathiri imani na nafasi ya dini katika jamii.  Hawa walikuwa ni pamoja na Mchungaji Martin Luther [1483 – 1534] aliyeanzisha Tawi la Kilutheri la Kanisa la Roma; Mfalme Henry wa VIII wa Uingereza aliyejiengua na kutangaza Kanisa lake la Anglikana; na John Calvin [1509 – 1547] aliyebuni mapokeo ya Ki-Kalvin, kwa kutaja matukio machache tu.

Wakati wa enzi za Karl Marx, kulikuwa na dini kuu mbili za Kimataifa yaani, Ukristo na Uislamu.  Misahafu ya dini hizi ni Biblia [Ukristo] na Kurani kwa Uislamu.  Kinyume na fikra za Karl Marx, misahafu yote miwili inatetea wanyonge na kupiga vita uonevu, ukandamizaji na unyonyaji, na kutoa wito kwa wanaoonewa kuasi dhidi ya vyanzo vya uovu na maovu. 

Kama Marx angeisoma vyema misahafu hiyo miwili bila kuyumbishwa na matendo ya watawala walioliteka Kanisa, wakaitumia dini kwa manufaa yao, bila shaka asingejenga uhasama na ukinzani kati ya falsafa yake na dini; badala yake angekuwa mtetezi mkubwa wa dini na Kanisa, kama itikadi inayomjenga na kumwendeleza binadamu dhidi ya ghiliba za Watawala.

Tuchukue mfano wa uanaharakati na uanamapinduzi wa Kristo:  Kuna wakati alizua ukinzani na watawala kwa kuwataka wajisafishe kwa maovu, uonevu na dhuluma kwa wanyonge, kitendo kilichosababisha akamatwe na kusulubiwa kwa tuhuma za kuchochea maasi dhidi ya utawala wa nchi.  Kati ya wanafunzi wake 12, wawili kati yao, Simon na Yuda, kabla ya kumfuata, walikuwa wanaharakati, wakereketwa [zealots] wa haki za binadamu na wapiganaji dhidi ya utawala wa kikoloni wa Kirumi nchini Uyahudi. Uanamapinduzi wa Kristo unathibitishwa pia na maneno kama: “Nimekuja kutupa moto duniani”; au, “Sikuleta amani, bali upanga” [Luka 12: 49 – 53], kwa maana ya  mapambano ya ana kwa ana dhidi ya udhalimu wa aina zote katika jamii.

Na kwa sababu jamii ya wakati huo ilikuwa imejaa maovu, kama ambavyo Taifa lolote linaweza kugubikwa na rushwa kubwa na ufisadi, pakatakiwa wachache kujitoa mhanga kwa manufaa ya walio wengi kama Krisrto alivyojitoa. Na ili kufanya hivyo alisema, “Mtu ajikane mwenyewe na anifuate”. Hata siku ya kusulubiwa kwake msalabani, hakujutia vita aliyoianzisha; akawaagiza wafuasi wake wauze kanzu [nguo] zao, ili wanunue mapanga kuendeleza harakati za kuwakomboa wanyonge.

Kuhusu utajiri wa kinyonyaji, aliwaonya watawala wenye uchu wa kujitayarisha, kwamba hawawezi kutumikia mabwana wawili, Mungu [watu] na mali [utajiri] bila kuteteresha ukweli na haki; akasema, ni rahisi ngamia [kamba nene, sio mnyama] kupita kwenye tundu ya sindano, kuliko tajiri [uchu wa mali] kuuona ufalme wa mbingu, ila kwa njia ya kutenda haki na kweli.

Aliwanyuka mijeledi wezi na wafanyabiashara, walioweka mbele maslahi yao binafsi kuliko utu, alipowakuta wakiuza bidhaa kwa ulanguzi hekaluni.  Ikulu, kama lilivyo hekalu na msikiti ni mahali patakatifu; kwa sababu ndipo maamuzi makuu hutokea.  Ni dhambi kubwa kwa wanasiasa, kama ilivyo kwa waumini, kupageuza mahali patakatifu kuwa pango la walanguzi, kama alivyobaini Mwalimu Nyerere na kupiga kelele mwaka 1990, alipoona wafanyabiashara matapeli kuizoea Ikulu, Rais na familia yake, kufikia kumwita “First lady” kikejeli – “shemeji”.

Usawa wa binadamu katika jamii umesisitizwa vizuri pia katika Kurani tukufu kwa kuhusishwa na zaka [zakat] na sala kuwawezesha “masikini” kuendesha maisha mazuri kama binadamu wengine [LXX: 24 – 25]. Kurani tukufu inasisitiza juu ya utu na wajibu wa kila mtu kwa jamii

[jamaa]

, mshikamano katika usawa, na ushirikiano kwa jamii nzima [XVII: 70]. Uislamu, kama ulivyo Ukristo, unasisitiza HAKI, wema, usawa na ukweli kwa watu wote, hata kama hayo hayatamfurahisha muumini mwenyewe, wazazi au ndugu zake [IV: 135]. Kuna ubaya gani kwa Viongozi wa dini kuitahadharisha jamii na watawala wanapokengeuka ubinadamu huu hata kujenga mzio dhidi ya Viongozi hao?.

Karl Marx hakuweza kuzitekeleza kwa vitendo nadharia zake, kwani alifia uhamishoni Uingereza kama mkimbizi na kuacha mabunda lukuki ya vitabu vya fikra zake. Katika zama zetu hizi, je, dini ina nafasi yoyote katika maendeleo ya jamii au bado ni yale yale ya mtazamo wa Karl Marx?  Nini chanzo na sababu za watawala kutaka viongozi wa dini wasichanganye siasa na dini?  Ni kipi hicho kinachoitwa kuchanganya siasa na dini?

Ukichunguza kwa makini, utaona kuwa mambo yanayopigiwa kelele na viongozi wa dini, na ambayo watawala wanadai ni kuchanganya siasa na dini, ni pamoja na mambo kama:  Tofauti kubwa ya umilikaji mali na utajiri wa nchi kati ya wageni wahamiaji wachache na wazawa; ufukara unaoendelea kukithiri, hasa kwa wananchi waishio vijijini; ubaguzi kwa misingi ya itikadi za vyama, maeneo, umri, kijinsia na aina zinginezo.

Mengine ni kukosa kazi kwa vijana mijini; kuongezeka kwa maovu kama vile rushwa, madawa ya kulevya na ufisadi; kuongezeka kwa siasa za kujuana kwa namna ya mshikamano kati ya matajiri wakubwa na kada ya watawala, na uwekezaji usiojali au usio na mguso chanya kwa wananchi walio wengi.

Kanisa kama sehemu ya jamii, linaguswa na yote yanayotokea katika jamii.  Na kama ambavyo tumekwishaeleza hapo mwanzo,  wajibu wa dini na Kanisa ni kutetea haki katika jamii kwa maendeleo ya wote, na hasa kwa wale wanaoathirika kimaisha kutokana na matendo ya wengine

[wachache]

wasiojali.  Kwa sababu hii Kanisa, na mtu  [binadamu] yeyote mwenye kujali ubinadamu na utu, hawawezi kunyamazia maovu  haya.

Vivyo hivyo, Kanisa makini haliwezi kuhubiri Injili ya amani na upendo, wakati waumini wake na jamii kwa ujumla, ni wenye njaa, wenye kuandamwa na magonjwa na umasikini uliokithiri ndani ya nchi yenye utajiri mkubwa wa rasilimali; wanaonewa na kunyanyaswa. Kunyanyaswa ni pamoja na kunyimwa haki ya kuishi maisha bora, na nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kutoa maamuzi ya nchi yanayogusa jamii pana, au fursa ya kupaza sauti wakasikika na kusikilizwa.

Kanisa [waumini] ni sehemu ya jamii, na hivyo jamii ni sehemu ya kanisa.  Waumini wa dini wanashiriki kulipa kodi, wanashiriki katika chaguzi za kuweka viongozi madarakani, wanashirki pia katika kazi mbali mbali za maendeleo ya nchi kwa jasho na damu.  Kwa nini wasitumie haki yao, kama wananchi wengine, kuonya, kukemea na kupigia kelele maovu yanayoisakama nchi yao?.  Kwa vipi huko kuitwe ni “kuchanganya dini na siasa”?.

Nchi yoyote inapodidimia katika maisha ya rushwa, umasikini wa kulazimishwa, kuvunjika kwa maadili mema, ufisadi na uporaji wa rasilimali za Taifa na kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi, Kanisa haliwezi kukaa kimya. Likifanya hivyo, litakuwa linakwepa wajibu wake wa kinabii [Prophetic ministry], na hivyo litapashwa kulaumiwa. Maovu ni chanzo cha kuvunjika kwa amani: Ni Mungu yupi anayetaka maovu na vurugu zitawale miongoni mwa watu wake?. Wala si sahihi kwa enzi zetu kudai kwamba watawala huwekwa madarakani na Mungu, eti kwamba kuwahoji kwa matendo yao ni kupingana na Mungu, au kuchanganya siasa na dini.

Mtazamo huu, unaoitwa kwa Kiingereza “The Positivistic view” au “mtizamo wa maoni chanya”, unawakweza watawala waovu waonekane kuwa karibu na Mungu ili waogopwe na kutetemekewa. 

Ni dhana ya kale iliyoasisiwa na Mfalme Constantine wa I wa Rumi ya kale, alipoingiza dini kuwa sehemu ya mfumo wa Serikali [Theocratic state] kuwalinda watawala wasiguswe wala kuhojiwa na jamii kwa kuwalinganisha na “Watakatifu” hata wakapata kuitwa “Watukufu”.

Mtizamo huo ulianza kupoteza nguvu karne ya 20 wakati wa utawala wa fashisti Adolf Hitler [Ujerumani] na swahiba wake Benito Mussolini wa Italia, pale watu walipoanza kuhoji, kama kweli wao waliwekwa madarakani na Mungu.  Na katika enzi zetu tunaendelea kuhoji, kama kweli madikteta Idi Amin [Uganda], Jean Badel Bokassa [Afrika ya Kati], Marcias Nguema [Equatorial Guinea], Mobutu Seseseko [Zaire/DRC], nao waliwekwa madarakani na Mungu.

Mtazamo wa “Positivistic view” na dhana nzima ya watawala kuwekwa madarakani na Mungu kwa mujibu wa “Warumi 13”, unapingwa vikali na waumini wa mapokeo ya Ki-Kalvin [Calvinistic view] kwa maelezo kwamba, anachoagiza Mungu na kuweka madarakani sio Serikali yenyewe, bali Mungu anaamuru mfumo wa Serikali inayofaa.

Ni kwamba, Serikali inayotimiza matakwa ya demokrasia na utawala bora na kukubalika na wengi, hiyo ndiyo Serikali inayostahili kuitwa imewekwa na Mungu, kwani sauti ya wengi ni sauti ya Mungu na Serikali inayokwenda kinyume cha hayo hupoteza mamlaka na haki ya kutawala, hivyo haiwezi kudai kuwa imewekwa na Mungu. Na hapa ndipo utume wa kinabii wa viongozi wa dini unapojitokeza zaidi kwa kuyaonya mataifa.

Kwa sababu hiyo, Kanisa haliwezi kukaa kimya kueleza ukweli, kwani jukumu lake ni kusimamia mfumo wa aina bora ya Serikali itakiwayo na Mungu kwa watu wake na kwa kufanya hivyo si kuchanganya dini na siasa, bali ni wajibu wake wa kiunabii usioepukika.

Kuna pande mbili za siasa za uzuri na ubaya; kwamba uzuri wa siasa bora ni ile shauku ya mwanasiasa ya kutaka kuona kuwapo kwa haki na utaratibu mzuri wa utawala unaojali. 

Na kwa upande wa ubaya, ni ile tamaa mbaya ya madaraka, utukufu na utajiri.  Hili la mwisho lazima lipigwe vita na waumini wa dini zote, kwa maana haliwakilishi mapenzi ya Mungu kwa watu wake.

Kwa hili, Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius K. Nyerere, analiweka wazi katika kitabu chake “Binadamu na Maendeleo”, akisema:  Ikiwa [waumini] hatutashiriki kwa vitendo katika kuondoa utaratibu wa maisha na uchumi unaowadidimiza watu kwenye umasikini, uonevu na unyonge, basi, Kanisa [dini] litakuwa halina uhusiano na maisha ya binadamu, na dini itakuwa kama ni mkusanyiko wa imani za ushirikina zinazokubaliwa na wenye hofu tu……….Na ikiwa hivyo, Kanisa litakufa, maana litakuwa halina maana inayoeleweka kwa mtu wa [leo] kisasa”.

Mwalimu anaelezea jinsi watawala walivyojigeuza miungu watu: “Tunasema kwamba binadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu.  Mimi nakataa kumfikiria Mungu aliye fukara, mjinga, mshirikina, mwoga, dhalili, ambayo ndiyo hali ya walio wengi [ambao eti ndio] aliowaumba kwa “mfano” wake mwenyewe. Binadamu wenyewe ni waumbaji, hujitengenezea hali zao za maisha; lakini tulivyo sasa tu viumbe, tena si viumbe wa Mungu, bali wa binadamu wenzetu”.

Hoja ya Mwalimu hapa ni kwamba, binadamu anapotawaliwa na tamaa mbaya ya madaraka, utukufu na utajiri, hujitengenezea hali ya maisha kwa kuwageuza wengine kuwa viumbe vyake, waonekane duni ili aweze kuwatawala vizuri; wamtukuze yeye na wawe tegemezi kwake wa maisha.

Anasema: …..lazima idhihirike kwamba, Kanisa linashambulia wazi wazi mtu au kikundi chochote kinachosaidia kudumisha unyonge huo wa mwili na roho, bila kujali misukosuko inayoweza kutokea, kwa kanisa na wafuasi wake…. Maana ikiwa kanisa halipingi maonevu yaliyoko, basi kuendelea kuwapo kwake, na dini yoyote ya Kikristo, kutaambatanishwa na kuendelea kwa dhuluma”.

“Kanisa lazima liwaongoze watu kumcha Mungu kwa kuungana nao katika kuzishambulia dhuluma na unyonge unaowasumbua…. maendeleo ya watu maana yake ni maasi. Inalibidi kanisa, likitumia wafuasi wake, kuwa mbele katika kulishambulia shirika lolote au utaratibu wowote wa uchumi wa maisha ya watu au wa siasa, unaowakandamiza watu na unaowanyima haki na uwezo wa kuishi kwa uhuru kama wana wa Mungu mwenye upendo”, anaonya Mwalimu.

Kanisa linapoingilia kati na kusimama upande wa wanaoonewa na kunyanyaswa na kwa kulaani dhuluma na uonevu huo, hapo suala la kuchanganya siasa na dini linatoka wapi?. 

Tukio la juzi, kwa namna Mkuu wa Mkoa alivyojiwasilisha kimwili, nahau na vitendo kwa taasisi hiyo ya kidini, kana kwamba alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara katikati ya “wapinzani” linatukumbusha historia ya kanisa kutekwa nyara na Kaisari zama za karne ya nne baada ya Kristo. Ikifikia hapo uhuru wa kuabudu na wajibu wa kinabii wa Kanisa vitatoka wapi?.