Home Latest News KAMA HAWA NI MADIKTETA BOKASA, MOBUTU WATAITWAJE?

KAMA HAWA NI MADIKTETA BOKASA, MOBUTU WATAITWAJE?

5870
0
SHARE
Na Joseph Mihangwa     |

KAMUSI ya Kiingereza – Kiswahili iliyotolewa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili [TUKI] ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, inatafsiri neno “dictator” au “dikteta” kuwa ni “Mtawala wa mabavu”; na hivyo kwamba utawala anaoendesha kuwa wa kidikteta. Kwa mantiki hii, utawala wa kidikteta ni ule unaoendeshwa kwa amri ya mtu mmoja mwenye hatimiliki ya mawazo na kazi ya wengine wote ni kuitikia tu, wapende wasipende. Ni utawala usiojua demokrasia, utawala bora, utawala wa Sheria wala umuhimu wa Katiba na maridhiano katika jamii.

Wachambuzi wa mambo ya siasa, Sosholojia na Wanasheria wa Katiba, Afrika inaongoza kwa kuzalisha, sio idadi kubwa tu ya Viongozi madikteta, bali pia kwa ukatili wa kinyama wa madikteta hao. Kuna ukweli gani juu ya tuhuma hizi?.

Wakati hatukatai wala kukubali tuhuma hizi kwa misingi ya swali: “Nani hasa dikteta na kwa mazingira yapi?”. Tupende awali ya yote, kujinasibu kwa kutoa aina mbili za udikteta na madikteta: Udikteta mwema na udikteta kichaa, na hivyo dikteta mwema na dikteta kichaa.

Kwa mfano, Rais John Pombe Magufuli [JPM] anapokataa kusikiliza sauti za pembeni [ushauri] akisema aachwe huru ainyooshe [sio “wainyooshe” au “tuinyooshe”] nchi kwanza, huo ni udikteta; lakini kwa malengo yapi?.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere aliwahi kukiri kwamba, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilimpa madaraka makubwa mno kutosha kumfanya awe dikteta lakini hakuwa. Zaidi ya hayo, chini ya Sheria ya Kuweka Kizuizini Mtu [The Detention Act] alikuwa na mamlaka ya kumtia kizuizni bila kikomo mtu yeyote aliyeonekana hatarishi kwa usalama wa Taifa lakini alifanya hivyo kwa nadra na baadaye kutelekeza kabisa Sheria hiyo licha ya kuendelea kuwapo.

Lakini ilipokuwa kujadili na kutekeleza mambo yenye manufaa kwa Taifa, Mwalimu ilikuwa humwambii kitu, akapachikwa jina “Haambiliki”. Bila jeuri ya Mwalimu hali ya amani na utulivu tunayojivunia leo [kama zao la Azimio la arusha/Ujamaa] isingekuwapo. Alikuwa dikteta mwema.

Udikteta mwema na hivyo “dikteta mwema” ni mtawala mwenye kujitoa mhanga kutekeleza mambo mema kwa manufaa ya jamii pana kwa kusukuma mambo hayo kwa amri ndani ya jamii yenye uelewa duni kuhusu agenda ya “uhuru na maendeleo” kwa jamii hiyo.

Kundi la Viongozi hawa linaundwa na watu mashuhuri kama kina Napoleon Bonaparte [Ufaransa ya karne ya 18]; Mao Tse Tung [China]; Joseph Bronz Tito [Yugoslavia]; Dakta Kwame Nkrumah [Ghana], Julius Kambarage Nyerere [Tanzania], John Pombe Magufuli, Samora Machel na wengine walioanzisha harakati za kuponya nchi zao kwa maono dhidi ya maovu ya kijamii kwa raia wengi bila kujua.

Nabii Mussa alikuwa dikteta mwema katika safari ya kuwatoa Wanaisraeli kutoka utumwani Misri kwenda nchi ya “ahadi” – Kanaani; akakabiliwa na maasi jangwani, pale Watumwa hao walipodai eti ilikuwa “heri wangebakia utumwani kwa Farao, kuliko kukabili mateso ya kuvuka jangwa la Sinai”.

Ni udikteta mwema pia kumshurutisha mgonjwa wa malaria kunywa dawa chungu ili apone, hata kama ni kwa mjeledi. Lakini si udikteta mwema kumshikia mjeledi mgonjwa kumlazimisha anywe dawa usiyoijua lakini yeye [mgonjwa] akijua kwa uhakika kwamba si dawa ya malaria bali “sumu ya panya”; ukamcharaza mijeledi bila kumsikiliza kwa sababu tu wewe ni mtawala, akafa.

Udikteta kichaa ni uongozi wa kiimla usio na dira au malengo mema na thabiti kwa jamii ila kwa maslahi binafsi kwa kujua au bila kujua, huku ukijinasibu kwa mbwembwe za ukuu kwa kutukuzwa na kuabudiwa.

Kundi la Viongozi wa aina hii, linajumuisha watawala kama kina Mfalme Louis wa XV [Ufaransa ya 1700]; Adolf Hitler [Ujerumani]; Ferdinand Marcos [Ufilipino]; Joseph Stalin [Urussi]; Mobutu Seseseko [Zaire/DRC]; Jean Bedel Bokassa [Jamhuri ya Afrika ya Kati – CAR]; Macias Nguema [Guinea ya Ikweta – IG] na Idi Amin Dadah [Uganda], Dakta Hastings Kamuzu Banda [Malawi], kwa kutaja wachache. wachache.

Kama ni kweli Afrika inaongoza kwa kuzalisha idadi kubwa ya Madikteta, basi itakuwa ni kwa mitizamo ya aina mbili hizi za udikteta, kwa kuwa zinajumuisha pia kipindi cha enzi za utawala kwa mfumo wa Chama kimoja na utawala wa kijeshi pia barani Afrika, kwani kwa tafsiri ya nchi za Magharibi zenye kujinasibu kwa demokrasia komavu, mfumo wa utawala wa Chama kimoja ni udikteta.

Lakini yafaa pia tuwe waungwana kukubali sehemu ya tuhuma hizi kwamba, Afrika imetokea kuzalisha baadhi ya madikteta wabaya, wezi na makatili kuliko Adolf Hitler wa Ujerumani anayesemekana kuongoza duniani kwa sifa mbaya. Wapo wengi, lakini majina yanayotujia haraka akilini ni ya pamoja na Jean Bedel Bokassa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati [CAR], Joseph Desire Mobutu [baadaye kuitwa Mobutu Sese Seko Ngbendu Kuku wa Zabanga] wa Congo Leopoldville iliyoitwa Zaire na ambayo sasa inaitwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo [DRC], na wengine.

Dikteta mwema au dikteta nguli? 

Kama kuna udikteta halisia na wa ovyo uliowahi kutokea barani Afrika na ambao Viongozi wa Kiafrika wanapaswa kujipima walipo, wasiige wala kufananishwa nao, kwa muonekano au kwa matendo waweze kusalimika madarakani, basi ni ule wa madikteta nguli Jean Bedel Bokassa na Mobutu Seseseko kama tutakavyoona katika makala haya. Kila kitendo tu cha kufanana nao, ni kuashiria udikteta uliokomaa kwa Kiongozi wa watu kujiepusha kuharibikiwa kama ambavyo Viongozi hao walivyoharibikiwa na kuishia pabaya, lakini wakiwa wamechakaza Mataifa yao.

Jean Bedel Bokassa alizaliwa Februari 12, 1921 nchini CAR; akapata elimu katika shule za Kimisionari hadi elimu ya Sekondari kabla ya kujiunga na Jeshi la Kifaransa kama Askari mpiganaji wa Jeshi hilo.

Alitumikia Jeshi hilo kwa miaka 17 kufikia cheo cha Luteni, lakini mwaka 1961 aliporejea CAR na kupewa jukumu la kusaidia kuunda Jeshi la Kitaifa la CAR huru, alipandishwa cheo kuwa Kapteni, ambapo mwaka 1964, akiwa na umri wa miaka 43 aliteuliwa na Rais wa kwanza wa nchi hiyo, David Dacko [ambaye pia alikuwa mjomba wake], kuwa Mkuu wa Jeshi hilo lenye wapiganaji 500 tu wakati huo. CAR ilipata uhuru na kuwa Jamhuri Agosti 13, 1960.

Wakati akitumikia Jeshi la Kifaransa, Bokassa alipigana vita ya Pili ya dunia [WW II] katika nchi mbali mbali za Mashariki ya Mbali [Indo – China] na kutunukiwa medali 12 za ushujaa, zikiwamo mbili za heshima, “The Croix de Guerre” na “the Legion d’Honneur”.

Hata hivyo, katika kipindi cha mwaka mmoja tu, Rais Dacko alianza kubaini mapungufu ya Kapteni Bokassa kama Mkuu wa Jeshi; akapanga kumwondoa kwa wakati mwafaka; lakini Bokassa akabaini mapema na kumpindua hima mjomba wake kwa kunyakua madaraka Desemba 31, 1965 akimtuhumu [Dacko] kuongoza nchi kizembe na kwa kutoshaurika. Kuanzia hapo demokrasia [Bokassa akiita siasa na uzembe] nchini CAR ikatoweka, ukatili wa dola ukachukua kiti cha mbele; ufisadi na ubaguzi kutamalaki.

Licha ya kudai kwamba yeye hakuwa Mwanasiasa na kwamba siasa isingeleta shibe kwa Wa-CAR, lakini licha ya kuiweka kando Katiba ya nchi, hakukifuta Chama cha Siasa cha “Social Evolution Movement of Black Africa” [MESAN] kilichoasisiwa na Bartholomey Boganda [mpwa wa David Dacko] na kuleta uhuru wa nchi hiyo; badala yake akajiteua kuwa Katibu Mkuu wake akisema Chama kilikuwa yeye na yeye alikuwa ndiye yeye na hakuruhusu vyama vingine.

Hatua ya kwanza ya Bokassa baada ya kunyakua madaraka, ilikuwa ni kuwaua hadharani Mawaziri wanne wa zamani kwa kupigwa marungu kwa tuhuma za kutoonesha heshima kwa Jeshi wakati Bokassa akiwa Mkuu wake kabla ya Mapinduzi; naye Mkuu wa Usalama wa Ndani akanyongwa kikatili hadharani. David Dacko, kwa upande wa pili, aliwekwa kizuizini kwa miaka mitatu.

Haya yakitokea nchini CAR, mwaka huo huo dikteta wa aina ya Bokassa alikuwa ameibuka nchini Congo Leopoldville kwa jina la Kanali Joseph Desire Mobutu, kwa kupindua Serikali ya Rais Joseph Kassavubu wa nchi hiyo kwa madai ya kutaka “kuiokoa Congo kutoka kwenye machafuko, ufisadi na rushwa na kujenga Congo mpya”.

Mobutu, kama swahiba yake Bokassa kufuatia Mapinduzi, aliua Mawaziri wanne kwa kupigwa risasi hadharani mbele ya umati wa watu 50,000 kutisha wananchi waiogope Serikali. Kwa madai ya kutaka kunyoosha nchi kwanza, alisema, “Mtawala lazima atoe mfano wa aina yake na kujenga mazingira ya nidhamu kwa Serikali”. Akaongeza kusema, “Mtemi [Chief] anapotoa maamuzi, anakuwa ameamua, kwisha!”.

Hapo tena, demokrasia nchini Congo, kama ilivyokuwa nchini CAR, ilikuwa imetekwa nyara na Mtawala dikteta; Congo ikaingia kwenye machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe viliyohusisha Mataifa ya nje yenye kugombea na kupora rasilimali za Congo.

Bokassa alipenda kujipambanua kama “Mfalme Mkuu asiyehojika” [absolute monarch] na alipiga marufuku watu kutaja maneno “demokrasia” na “uchaguzi”. Alijipandisha vyeo vya kijeshi, kwanza kwa kujipa cheo cha “Jenerali” na baadaye “Jemedari” [Marshal]. Na kuwa Mwafrika wa kwanza kushika cheo hicho. Hadharani, alipenda kujinasibu kwa medali nyingi za kijeshi na tunu kiasi kwamba ilibidi sare maalum itengenezwe kwa ajili yake, mahsusi kubeba medali hizo zikining’inia.

Alipenda miundombinu mbali mbali ipewe jina lake kwa heshima yake, kama vile Shule, hospitali, Kliniki, vyuo na miradi ya maendeleo. Kurasa za mbele za kila daftari la mwanafunzi wa shule nchini zilibeba picha ya Bokassa.

Alipozuru nchi za nje, kila mara aliandamana na idadi kubwa ya wajumbe na alibeba viroba lukuki vya almasi kutoa zawadi kwa wenyeji wake. Nchini, kila agizo lake la mdomo liligeuka kuwa sera ya Serikali bila kujali misingi ya uongozi au uhalisia wake kwa maendeleo.

Kwenye Serikali, Bokassa alishikilia Wizara 12 na aliingilia atakavyo Wizara zingine. Alidhibiti utoaji maamuzi, upandishaji au ushushaji vyeo watumishi na utoaji tunu [zawadi] au adhabu. Mawaziri walibadilishwa kila mara kwa wastani wa mara sita kwa mwaka, au kila baada ya miezi miwili kuhakikisha hawawi tishio kwake.

Maofisa wa Serikali walitakiwa kuwa “masikio wazi” saa zote kusikia nini Bwana Mkubwa angetamka siku hiyo, mara nyingi, bila kutarajiwa na pengine kwa kisichotarajiwa. Na kwa sababu mawasiliano ya simu nchini hayakuwa madhubuti, walitakiwa kutozima Redio zao kutarajia maagizo kutolewa moja kwa moja kutoka Ofisi ya Rais.

Wakati Bokassa akiendelea kutesa kwa udikteta nchini CAR, nchini Zaire [Congo], Mobutu naye alikuwa akitesa kivyake lakini karibu kwa staili pacha: Bokassa alitumia nguvu ya dola hadharani; Mobutu alijificha nyuma ya Chama kimoja na pekee alichojiundia – Chama “Mouvement Populaine de la Revolution [MPR] au “Chama cha Mapinduzi” ambamo alijiteua mwenyewe kuwa Kiongozi, mwelekezi Mkuu na Msemaji. Na ndiye pia aliyetoa itikadi ya Chama kwa kila mtu kufuata iliyofahamika kama “authenticite/authenticity” au “Uhalisia”, japo jina lilibadilika kuitwa kifupi “Umobutu” [Mobutism] yenye nguvu za Kisheria; kwamba kutozingatia lilikuwa kosa la kikatiba na dhidi ya Mobutu pia kama “Mtemi” asiye na mshindani.

Kuhakikisha anabakia madarakani, alitegemea sana vikosi vya Kijeshi na vya Polisi vya kisomi, vyenye kama vile kikosi maalum cha Rais “Division – Speciale Presidentielle” vyenye Makamanda wateule wa kabila lake la Ngbendi waliolipwa vizuri na marupurupu tele. Kama alivyofanya Bokassa, Mobutu naye alibadili Baraza la Mawaziri na Watendaji Wakuu Serikalini kila baada ya miezi mitatu; au kuwafukuza kazi au kuwafunga kuhakikisha hawakuwa tishio kwake. Alisema, katika kutenda kazi hakuwa na rafiki wala ndugu, bali “Kazi tu”.

Walitaka kuwa miunguwatu 

Taratibu, Mobutu alianza kujilimbikizia madaraka, akitawala kwa maagizo [decrees]; alidhibiti ajira zote na michakato ya kupandisha vyeo watumishi; akajipachika madaraka ya kuamua matumizi ya mapato ya Serikali. Akajipachika majina ya sifa kubwa kubwa kama vile “Baba wa Taifa”, “Mkombozi wa Watu”, “Mpiganaji Mkuu, “Mwanamikakati Mkuu”. Matendo yake yalitungiwa nyimbo za kumsifu na kumtukuza kama mungu wa Taifa.

Taarifa za luninga [TV] zilitanguliwa na sura ya Mobutu amevalia kofia ya ngozi ya Chui, akishuka kutoka mawinguni [mbinguni] kama “Masiya”. Sehemu na mahali alipofanya kazi na kuishi zilitukuzwa kama “sehemu za kitaifa za kuhiji” na taamuli au tafakuri. Kwa udikteta huo, aligeuka Mungu-mtu kama anavyoelezea Waziri wake wa Mambo ya Ndani, Engulu Baanga Mpongo: “Mungu kailetea Zaire Mtume Mkuu, Kiongozi Mkuu adhimu, Mobutu. Yeye ni mkombozi wetu, Masiya wetu; Kanisa letu ni Chama MPR; Mkuu wake [Kanisa hilo] Mobutu. Tunamheshimu mno kama ambavyo mtu anavyomheshimu Papa. Injili yetu ni Umobutu”.

Bokassa: Akiongoza Wizara 12 chini yake na kuingilia zingine alivyotaka, Bokassa, kama alivyokuwa Mobutu, alikuwa Mkuu wa miradi yote ya ujenzi na uwekezaji nchini. Kwa kujitafutia sifa, miradi ya Maendeleo iliweza kuanzishwa kwa mbwembwe na shauku ya vipindi, kisha ikatelekezwa mara utashi wake [Bokassa] ulipofifia na fedha kuhamishwa kukidhi wazo jipya.

Hundi zote za Serikali na Mashirika/taasisi za umma zilitakiwa kutiwa sahihi ya nyongeza [counter signature] na Bokassa mwenyewe kuthibitisha uhalali wa kutolewa kwake vinginevyo zilikuwa batili kutoweza kulipika Benki. Kwa kifupi, Bokassa hakujali Bajeti ya Serikali, badala yake alipendelea matumizi kwa maagizo ya papo kwa papo huku watumishi wakienda bila mishahara hadi miezi tisa. Matumizi mengi na makubwa yalikosa nyaraka wala maelezo juu ya uhalali wake na “wahojaji” kufungwa midomo.

Mfano, lilianzishwa vyema Shirika la Ndege la Taifa – “Air Centrafrique” [ACAL], lakini kwa mtindo huu huu likatelekezwa ghafla na kuachwa kuvunjika baada ya ndege zake kuruka kwa mwaka mmoja tu.

… Itaendelea…..

jmihangwa@yahoo.com/0713-526972