Home Latest News KAMA MWISHO NI HIVI, MNGESUSA MWANZO!

KAMA MWISHO NI HIVI, MNGESUSA MWANZO!

792
0
SHARE

NA ABRAHAM GWANDU, ARUSHA

UCHAGUZI wa marudio uliofanyika Novemba 26, mwaka huu, kwenye kata 43 zilizoko katika mikoa 19 kote Tanzania bara, umeonesha namna Chama Cha Mapinduzi kilivyopata ushindi mkubwa bila kutarajiwa.

Chama hicho kimenyakua viti 42 kati ya hivyo, awali nusu vilikuwa mikononi mwa Chadema, viwili Cuf na kata moja ilikuwa ya Chama cha ACT Wazalendo.

Kutokana na ushindi huo wa kimbunga, mengi yamesemwa na yanaendelea kusemwa hata leo, kesho na siku zijazo kuhusu mbinu iliyotumiwa na CCM kujihakikishia ushindi. Swali kuu linaloulizwa ni je, ushindi huo ni halali kwa kuzingatia vigezo vyote vya uhuru na haki?

Binafsi mpaka sasa sijaelewa kilichotokea kama ni uchaguzi wa kidemokrasia au ni uchafuzi wa demokrasia katika nchi hii tangu mfumo wa vyama vingi vya kisiasa uliporejeshwa kwa hisani ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Sote tunajua ni yeye aliyeufuta mfumo wa siasa za vyama vingi mwanzoni kabisa nchi ilipojitawala kutoka kwa mkoloni na baadaye alipozidiwa na upepo mkali wa mabadiliko ya kisiasa ulimwenguni miaka ya 80 mwishoni, hatimaye aliurejesha rasmi mfumo huo mwaka 1992.

Kwa tafsiri yoyote, uwepo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini si kosa kisheria kwa mujibu wa sheria za Tanzania. Vyama vingi vilianzishwa kwa sheria namba 4 ya mwaka 1992, sheria ambayo ilifuta ibara ya 10 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ambayo ilikuwa ikielezea mamlaka ya chama enzi za mfumo wa chama kimoja cha siasa.

Sasa kama ni hivyo basi, kila mwananchi wa Taifa hili anao uhuru unaolindwa na sheria wa kuchagua au kuchaguliwa kuwa kiongozi ilimradi havunji sheria. Kwa msingi huo, nirejee kile nilichoona siku hiyo na hatimaye malalamiko ya vyama vilivyoshindwa uchaguzi na hatima ya mfumo wa siasa za vyama vingi hapa nchini.

Mosi, nikiwa mkazi wa mtaa mmoja jijini Arusha, mapema asubuhi ya Jumapili ya uchaguzi huo, kama ilivyo ada mimi kama Mkristo nilikuwa na ratiba ya kwenda kusali kanisani, lakini kutokana na uchaguzi wa marudio kufanyika siku hiyo sikuweza hata kwenda kumuabudu Mungu wangu, badala yake nilienda kutimiza wajibu wangu wa kukusanya, kuchakata na kuandika habari za uchaguzi huo kwa kutembelea vituo kadhaa kadiri nilivyoweza.

Yapo mambo kadhaa ambayo ni kawaida kabisa kuwepo katika shughuli za upigaji kura, mathalani uwepo wa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi, mawakala wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi, vyombo vya ulinzi na usalama kama Polisi na vinginevyo.

Tofauti na chaguzi zingine, katika uchaguzi ule kulikuwa na idadi kubwa ya askari polisi kiasi cha kuzua minong’ono na hofu kwa wapigakura na hata wapita njia katika kata ambazo zilikuwa zinafanya uchaguzi wa marudio katika Mkoa wa Arusha hususani katika wilaya za Arusha Mjini, Monduli na Arumeru.

Labda ni kwa sababu kata ni chache ikilinganishwa na idadi ya askari waliopo mkoa mzima na kwa hivyo sidhani kama Kamanda wa Polisi Mkoa, Charles Mkumbo, aliomba kuongezewa askari wengine, nasema hivyo kwa sababu hakukuwa na dalili zozote za uwepo wa uvunjifu wa amani katika eneo lolote kati ya kata hizo.

Ushahidi wa hili ni kwa sababu hatujatangaziwa na ile intelijensia yao inayong’amua mapema kitakachotokea kabla hakijatokea. Kila kituo kilikuwa na idadi kubwa ya askari kuzidi hata wapigakura katika nyakati fulani na inawezekana kabisa kama utafanyika utafiti, ni kwanini idadi ya waliopigakura ilipungua ikilinganishwa na uchaguzi mkuu uliopita, hili la uwepo wa askari polisi wengi ni kati ya vitu vitakavyojitokeza.

Pili ni malalamiko ya Chadema kupitia Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe aliyetangaza chama chao kujitoa katika kata zote za Arumeru. Sababu aliyotoa ni polisi kuwapiga wananchi ambao wao wanaamini ni wapiga kura wao, kutolewa nje ya vituo vya kupiga kura mawakala wa Chadema tena kwa nguvu iliyoambatana na vipigo, kukamatwa na kutishwa viongozi wao wakiwemo wabunge.

Ni kweli wapo watu waliojeruhiwa, wapo viongozi waliokamatwa na polisi na wengine walitimua mbio hasa wakikumbuka kilichotokea kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kule Dodoma. Kama binadamu hofu lazima iwepo hasa akikumbuka wahalifu wale bado wanasakwa na hawajakamatwa lazima ujiokoe kwa kutoka mbio.

Hapa kila upande kati ya vyama viwili, hasimu wa CCM na Chadema ananyoosha kidole kwa mwenzake. Chadema kinadai kilishindana na Serikali kwa maana ya mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, vyombo vya dola hasa polisi ikiongozwa na RPC hata vyombo vile vinavyofanya kazi chini ya busati.

CCM wao waliwatupia lawama Chadema kuwa ni chama cha vurugu ndio maana wananchi wameanza kuikataa, wakitumia matokeo ya uchaguzi huo kama kiashiria, lakini kubwa chama hicho kinajivunia matunda ya kazi zinazofanywa na Serikali ya awamu hii.

Ni kazi zipi, mimi na wewe msomaji tutafakari na huenda tunaziona katika maeneo tunayoishi.

Yote kwa yote uchaguzi umekwisha katika kata hizo na washindi walishatangazwa, kilichobaki ni walioshinda kuwatumikia wananchi waliowachagua. Sasa tunasubiri kata nyingine na majimbo ya Longido, Singida Kaskazini na hata Songea Mjini.

Hii ni iwapo hakutakuwa na sababu nyingine itakayofanya jimbo lingine nje ya majimbo hayo kuwa wazi, iwe ni kifo, kufukuzwa au kuhama chama kwa mbunge mwingine.

Kwa maoni yangu mazingira hayo na mapungufu mengine ambayo yalisababishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na hata ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kipindi cha kampeni, bado kama nchi hatuwezi kujivuna kabisa mbele ya mataifa mengine kuwa sisi ni Taifa linalofuata mfumo wa vyama vingi.

CCM ya sasa ni tofauti, sijui inapendwa au inatumia mbinu zingine halali na haramu katika siasa, lakini jukumu la vyama vingine si kulialia bali ni kubadili mbinu za kupambana kisiasa. Iwapo hamridhiki na namna siasa zinavyoendeshwa, zinavyosimamiwa, chaguzi zinavyoandaliwa na matokeo kutangazwa kwanini mnashiriki kuanzia hatua ya mwanzo?

Susieni chaguzi kama hamridhiki nao, wapeni wafuasi wenu sababu za msingi kwanini hamtaki kushiriki chaguzi zinazoandaliwa, ikiwa sababu ni tume ya Taifa ya uchaguzi kwa mfano, au msajili wa vyama au Serikali kwa ujumla na vyombo vya dola.

Mmechagua kuwa wanasiasa tena wa vyama shindani, si kazi rahisi hasa kwa nchi za Kiafrika, la sivyo kuweni ng’ombe waliorudi zizini bila mikia hakuna namna nyingine.