Home Habari KAMPENI ZA USAFI ZISIATHIRI MAPATO YA SERIKALI

KAMPENI ZA USAFI ZISIATHIRI MAPATO YA SERIKALI

4616
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Iwapo mtu atatembelea maeneo ya Ilala jijini Dar es Salaam, hawezi kukosa vielelezo vya ushahidi wa shughuli zilizokuwa zikifanywa na watendaji wa mamlaka za mkoa ikiwemo iliyokuwa Halmashauri ya Jiji katika enzi zile.

Na ninaposema “enzi zile” nazungumzia miaka ya 60 na kuendelea hadi katikati mwa miaka ya 70 hivi. Barabara nyingi katika maeneo hayo zina ushahidi unaowasuta watendaji wa sasa – zilikuwa za wa lami aina ya asphalt, na kingo zake za zege zilizotenga maeneo ya kuegesha magari kwa kila barabara. Hali hii pia ilikuwapo kwa baadhi ya maeneo mengine ya Kinondoni, Magomeni na Temeke.

Narudia, ni ushahidi unaowasuta sana watendaji wa sasa kwani enzi zile mamlaka zilikuwa zinawajibika vilivyo katika utoaji wa huduma za jamii na namna kodi za wananchi zilivyokuwa zikifanya kazi kwa viwango vya kuridhisha.

Katika kipindi cha muongo mmoja hivi uliopita barabara chache za maeneo ya Ilala kwa mfano zilifanyiwa ukarabati kwa kuziwekea lami mpya, lakini kwa viwango duni kama inavyodhihirika kila baada ya vipindi vya mvua.

Lakini tukiacha uchakavu wa miundombinu katika maeneo mengi ya Jiji hili, kuna hili suala la usafi – suala ambalo tangu Mkuu wa mkoa wa sasa, Paul Makonda aingie madarakani, limekuwa linatiliwa mkazo sana kupitia kampeni mbali mbali – lakini kwa namna isiyokuwa na mantiki. Nitaeleza hapo mbele.

Kwanza tukubaliane mambo mawili: Mosi – usafi katika mandhari ya miundombinu chakavu mara nyingi huwa haujitokezi sana mbele ya macho ya watu wengi. Pili sipingi juhudi zozote za wananchi za kuweka mazingira yao katika hali ya usafi lakini juhudi hizi hazipaswi kuathiri shughuli za sekta nyingine binafsi na za umma au hata kuathiri mapato ya serikali.

Tusisahau kwamba Dar es Salaam ni kitovu cha uchumi na biashara nchini pamoja na kuwa na bandari kubwa. Jiji hili linahodhi sehemu kubwa ya biashara, uzalishaji na huduma nyingine muhimu. Na ingawa ni makazi ya asilimia kumi tu ya wananchi wote, lakini zaidi ya theluthi mbili yawafanyakazi wote nchini katika sekta ya uzalishaji hukaa Dar es Salaam.

Inakadiriwa karibu asilimia 80 ya mapato ya serikali yanatokana na shuguli zinazofanyika jijini Dar es Salaam, hivyo kuwa sahihi kuitwa mji mkuu wa kibiashara nchini (Tanzania’s commercial capital) sifa ambayo Mkuu wa Mkoa anaitambua na kuitaja mara kwa mara.

Sasa kama ni roho ya mapato ya serikali, kwa nini ‘roho’ hii inaathiriwa na suala la usafi? Kuna agizo la serikali la takriban miaka miwili na nusu sasa kwamba kila Jumamosi ya mwisho ya kila mwezi shughuli zote za kibiashara zisifunguliwe nchini kote hadi ifikapo saa nne asubuhi.

Lakini mkuu wa Mkoa wa Dar alitoa agizo pekee kuhusu mkoa wake kwamba shughuli zote za kibiashara na uzalishaji zitafungwa kila Jumamosi. Hayo ni masaa manne ya shughuli za biashara (isipokuwa shughuli za kibenki nk), au zaidi ya masaa 16 kila mwezi, au zaidi ya masaa 200 kwa mwaka.

Kwanza tuache athari za kipato kwa wafanyabiashara wadogo wadogo ambao wengi wao wanafanya hivyo katika kutafuta riziki zao na familia zao, lakini pia kuna suala la athari kwa mapato kwa serikali na taasisi zake. Serikali inakosa mapato yake ya kodi ya ongezeko la thamani – VAT na kodi nyingine zitokanazo na shughuli za kibiashara na uzalishaji kutokana shughuli hizo kufungwa katika masaa hayo.

Taasisi kama Tanesco nayo inaathirika sana kimapato kutokana hali hii – kupungua kwa umeme unaotumika katika maeneo ya biashara, bila kuacha kutaja VAT inayotozwa katika mauzo ya umeme. Hapa naweza pia kutaja Dawasco, kwa kiwango fulani.

Swali hapa ni je, hivi msisitizo kuhusu usafi hauwezi kufanywa bila ya ulazima wa kufungwa kwa biashara kama vile ilivyo kwa miji mingine duniani? Inawezekana kabisa kwani kama kila mtu analazimika aweke usafi katika eneo lake basi na iwe hivyo, siku zote, na siyo mara moja tu kila wiki – na kila mtu awajibike vilivyo asipofanya hivyo.

Utaratibu mzuri unaweza kuwekwa kuhakikisha kila mtu anatekeleza hilo la sivyo adhabu zilizopo kama vile faini n.k. zimuandame. Lakini bila shaka kutokana na uzembe wa wafuatiliaji unaopaswa kufanywa na watendaji katika maeneo mbali mbali, au uchache wa idadi yao kusimamia maeneo ya makazi mengi jijini, hivyo mamlaka zimeonelea usafi ufanywe kupitia kampeni maalum, za mara kwa mara pamoja na za kudumu – hata kama zitaathiri mapato ya serikali.

Halafu kuna hili pia: Mara kadha utakutana na magari ya matangazo yakitangaza eneo lolote la makazi likukutwa chafu basi mmiliki wa nyumba husika atatozwa faini ya shilingi laki mbili papo hapo. Faini hii hata kama ipo kisheria au la, ni kubwa sana kwa wamiliki wengi wa makazi ambao hata kula yao na familia zao ya kila siku wanahangaika sana kuipata.

Na inaonekana kuna undumila kuwili katika kusimamia suala zima la usafi hapa jijini. Kama faini ya makazi yanayokutwa machafu ni shilingi laki mbili, je maeneo ya masoko kama vile soko la Ilala ambalo mazingira yake ya usafi daima hayaridhishi itakuwa kiasi gani?

Inakadiriwa soko la Ilala ndilo linaloiingiza mapato mengi zaidi kuliko masoko yote katika manispaa ya Ilala lakini suala la usafi linaonekana ni kizungumkuti kikubwa.

Lakini kama nilivyotaja hapo juu huenda miundombinu yake chakavu ndiyo inalifanya mazingira ya soko hilo kuonekana machafu, hivyo kuna umuhimu sana kwa mamlaka husika kulifanyia ukarabati mkubwa au kujenga soko jipya la kisasa.

Inasikitisha kuona si mbali sana na soko hilo kumejengwa majengo mawili makubwa ambayo tangu yakamilishwe miaka mitano hivi iliyopita yamekuwa hayana tija kabisa ikizingatiwa kusudio zima la kuyajengwa.

Haya ni majengo yanayojulikana kama ‘Machinga Complex’ – na pamoja na jina lenyewe (lisilo rasmi) lililenga ‘wamachinga’ (wafanyabiashara ndogo ndogo wa barabarani) kufanya biashara zao mle. Lakini hadi sasa ni kama hakuna watu wa jamii hiyo wanaofanya shughuli mle – labda wachache sana.

Sasa hivi mazingira ya usafi ya majengo hayo hayaridhishi na hali hii inachangiwa zaidi na mandhari ya majengo yenyewe ambayo hayavutii machoni. Hadi sasa mamlaka husika zinashindwa kuyafanya majengo hayo yatumike kwa tija.

Mara elfu fedha zilizojenga majengo hayo zingetumika kujenga soko jipya la Ilala ambalo lingekuwa linaiingizia serikali fedha nyingi kimapato.