Home Makala KAMPUNI ZA KIZALENDO MKIAMINIWA MUAMINIKE!

KAMPUNI ZA KIZALENDO MKIAMINIWA MUAMINIKE!

4593
0
SHARE

Na BOLLEN NGETI


Kama lilivyo jina la safu hii, “Safari ya Kaanani” tunaendelea na safari yetu kuelekea nchi hiyo ya ahadi licha ya vikwazo lukuki njiani vinavyotufanya tusifike kwa haraka na mapema maana hata Rais John Magufuli hurudia kila mara kutuambia, “tumechelewa mno na tumechezewa vya kutosha” hivyo tunapaswa kukimbia kwa kasi na ari mpya ili kuyafikia maendeleo ya kweli yaliyokusudiwa na waasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume.

Katika mfululizo wa maandiko katika safu hii tumekuwa tukijadili vikwazo njiani kwa maana ya watu au masuala yanayokwamisha safari ya maendeleo ya kweli tuliyodhamiria kama Taifa iwe ni kisiasa, kiuchumi, kijamii hata kiutamaduni. Yeyote anayekwaza safari yetu ni adui yetu na hivyo hatunabudi kumpinga, kumkemea na hata kumnunia ili ajue hatufurahishwi na jitihada zake za kutukwamisha njiani.

Wiki iliyopita niliamua kufanya ziara mahsusi ya kimya-kimya jijini Dar es salaam “kukagua” maendeleo ya ujenzi wa barabara mbalimbali jijini humo nikiamini kuwa ili tuweze kuyafikia maendeleo ya kweli hasa ya biashara na viwanda hatunabudi kuwa na miundombinu ya barabara za uhakika kurahisisha usafiri ili kupunguza muda unaopotea barabarani katika foleni jijini.

Kwa hakika nilitamani kutumia usafiri wa anga yani chopa (elikopta) kujionea barabara hizo lakini kutokana na kukosa chombo hicho niliamua kutumia gari dogo, bajaji na baadhi ya maeneo nililazimika kutumia pikipiki al-maarufu “boda boda” na sehemu zingine pia nilienda kwa miguu ili kupata fursa ya kuongea na wananchi au wakazi wa maeneo husika kupata maoni na mitazamo yao katika zoezi zima la upanuaji wa barabara za pembezoni na mitaani ili kupunguza adha ya usafiri katika jiji la Dar es salaam.

Nimejiridhisha kwamba, kama kuna mtu anaweza kudhihaki kazi nzuri ya ujenzi wa barabara na miundombinu kwa ujumla inayoendelea kujengwa na Serikali hii ya Rais Pombe Magufuli basi ama mtu huyo ni kipofu, ni mnafiki au anajitoa tu ufahamu wa kutotaka kuona. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Kwa hakika muda si mrefu tatizo la barabara na madaraja litakuwa ni historia na hapo tutakuwa tumefika sehemu ya Kaanani (si Kaanani kamili) japo hata kwa karibu.

Katika ziara hiyo isiyo na wapambe ilinifikisha Manispaa ya Ilala katika barabara ya Kilomita 2.7 kutoka Vingunguti hadi Buguruni kwa Mnyamani inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Ikumbukwe kwamba unapozungumzia tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es salaam ni pamoja na magari kutoka Tabata-Relini hadi Tazara ili magari hayo yaende au yatoke Uwanja wa Ndege na Gongo la Mboto na ndio maana na sababu hasa ya kujenga “fly over” Tazara ili kupunguza foleni njia-panda hiyo. Kwa mantiki hiyo barabara ya kutoka Buguruni-Mataa kupitia Kwa Mnyamani hadi Vingunguti hadi Uwanja wa Ndege bila kupita Barabara ya Nyerere ni muhimu sana. Barabara hii sasa inajengwa ikiwa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Barabara Vijijini na Mijini, TARURA taasisi inayochukiwa upeo kwa sasa nchini na wapenda rushwa za 10%.

Ili kuweza kujionea ujenzi wa barabara hii muhimu kwa wakazi wa eneo hili niliamua kutembea kwa miguu kutoka Vingunguti hadi Buguruni kuona kazi kubwa inayofanywa na kampuni ya kizalendo ya Bharya Engineering & Construction Company Limited, BECCO. Nilichagua kukagua barabara hii kutokana na eneo hili kuwa korofi na lenye kujaa maji (water table) kwa miaka mingi na kila mara ilipojengwa ilichukua kipindi kifupi sana barabara kuanza kupasuka, kutoboka, kuchimbika na kuacha mashimo yaliyoharibu vyombo vya usafiri na hatimaye kukwaza kabisa watumiaji wa barabara hii muhimu.

Kwa sababu za wazi sitataja majina ya makampuni yaliyowahi kujenga barabara hii zaidi ya nne moja ikiwa ni ile iliyopigwa marufuku na uongozi wa mkoa kufanya shughuli za ujenzi katika jiji hilo. Ilikuwa ni ujenzi wa “wewe kandika tu udongo uje uchukue cheki yako.” Ni aina ya ujenzi uliolitia hasara kubwa Taifa hili katika maeneo mengi ya nchi na ndio maana nilipoambiwa barabara hii inajengwa na kampuni ya BECCO nilifarijika sana na kuamini kuwa ugonjwa umepata dawa sahihi na daktari sahihi.

Kwa wale wenye kumbukumbu maridhawa na bongo zisizo na vumbi watakumbuka majenzi mbalimbali ya barabara na madaraja yaliyofanywa na kampuni hii toka enzi za Mwalimu Nyerere lakini baada ya watawala wetu kushadadia soko huria na utandawazi tukafungua milango kwa wageni basi tukaanza kuonea kinyaa hata makampuni yetu ya kizalendo huku tukishangilia makampuni uchwara “ya kichina” ambayo hujenga kwa urembo na nakshi yakijua kabisa baada ya muda fulani barabara au daraja hiyo itaharibika ili iweze kuomba zabuni tena kuikarabati kwa gharama kubwa. JPM anaposema, “tumechezewa vya kutosha” tumwelewe, tuunge mkono visheni yake kwa Taifa.

Ieleweke kwamba siipigii debe kampuni ya BECCO maana mimi si mwanahisa wake, si msemaji wake, si wakili wake na hata sijui zilipo ofisi za kampuni hii na ninatambua kampuni kama BECCO za kizalendo ziko nyingi nchini isipokuwa ninasukumwa na kazi zilizowahi kufanywa na kampuni hii ambayo kwayo nimejiridhisha pasipo shaka kuwa ugonjwa wa barabara hii ya Vingunguti-Buguruni imepata dawa sahihi.

Ni kampuni hii ya BECCO iliyojenga barabara ya Pugu-Gongo la Mboto hadi njia-panda ya Chanika. Ni BECCO iliyojenga barabara ya Chang’ombe-Maduka Mawili pamoja na barabara ya kutoka Wazo inayopitiwa na malori yenye uzito mkubwa. Na kwa uzoefu wa zaidi ya nusu karne katika ujenzi wa barabara Serikali imeipa kampuni hii kujenga kipande cha reli cha SGR cha 35 Kilomita kutoka Pugu hadi Kisarawe. Katika ujenzi wa reli hii wataalamu wanaeleza kuwa hili eneo (Pugu-Kisarawe) ni eneo gumu sana kujenga kutokana na milima yenye miamba hivyo baada ya makampuni kadhaa kuomba TARURA ikaona kampuni “korofi” kwa maeneo korofi ni BECCO. Kampuni hii inajenga Mbeya, Songwe. Ina mradi huko Chita (Kilombero) mbali na Soni (Tanga) na maeneo mengine ya nchi.

Nimeamua kuyasema haya baada ya kukutana na baadhi ya wananchi katika maeneo haya ya Vingunguti na Buguruni wakitilia shaka ujenzi wa kampuni hii na kuona “ni wale wale” huku wengine wakienda mbali zaidi kutafuta hata namna ya kukwamisha ujenzi wa barabara hii.

“Kaka barabara hii ni sugu, imeshajengwa na makampuni kibao hata ya wazungu lakini wote ni wababaishaji tu baada ya mwaka mmoja utaona mashimo na kukatika lami ndio maana hatuna imani na hii kampuni,” anasema mkazi wa Vingunguti Ismaeli Kiondo (32) na kuongeza;

“Wewe angalia sasa ni zaidi ya wiki mbili njia imeziba kwa vifusi visivyo na idadi hatutumii barabara na watu wana biashara zao kwa nini wasifanye kazi usiku na mchana? Lakini pia ukiangalia kuna baadhi ya nyumba wanazifuata na kubomoa hata zilizo nje ya barabara kusema kweli tunateseka na ujenzi huu wa BECCO bora tukae kwa amani bila barabara.”

Naye Nathaniel Zahoro (65) wa Kwa Mnyamani anasema, “mimi nina miaka 40 hapa, nimeona kampuni nyingi zinajenga hii barabara lakini baada ya miaka miwili inarudia hali ile ile na pesa wanalipwa ndio maana tuna mashaka hata na hii BECCO itafanya tofauti?”

Ukweli ni kwamba kama kuna sekta inayotafuna hela za walipakodi katika nchi nyingi barani Afrika ni ujenzi. Mabilioni ya Dola za Kimarekani hutoroshwa nje ya nchi kupitia sekta ya ujenzi ambapo inaelezwa kuwa kila Dola 1 ya Kimarekani inayowekezwa katika ujenzi na makampuni ya kigeni huvuna Dola 3. Ni kwa kiburi tu cha kizalendo cha Rais Magufuli Tanzania itajenga SGR kwa Shilingi 7 Trilioni lakini kwa hakika reli hiyo ingejengwa kwa gharama pengine mara tatu ya kiasi hicho cha pesa tena kwa kukopa.

Hii ndio maana ninapoona miundombinu yetu kama barabara, madaraja, majengo, viwanja vya ndege, reli, ikijengwa kwa kampuni za kizalendo kwa maana kwamba hata fedha itakazolipwa sehemu kubwa hubaki hapa hapa nchini kupanua ajira ninapata matumaini ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 inayompasua kichwa Rais Magufuli.

Wakati wa “ziara” yangu hiyo nimekuta sehemu kubwa ya wafanyakazi kuanzia mainjinia, madereva wa mitambo na magari, wahasibu na washauri zaidi ya asilimia 80 ni Watanzania ambao hata mishahara yao haitofautiani sana na wageni.

Akitolea ufafanuzi na kuwatoa hofu wenyeji wa mradi unapojengwa barabara, Afisa Mwandamizi wa kampuni ya BECCO Joachim Sakoro anasema; “wakazi wa Vingunguti na Buguruni wameumizwa sana na kwa muda mrefu na ubovu wa barabara hii lakini niwahakikishie kuwa barabara hii ilikuwa haijapata kampuni ‘serious’ (makini) maana sisi BECCO kitu cha kwanza tunaangalia ‘money for value’ (thamani ya fedha) na ndio maana tunasimamiwa na Serikali yenyewe kupitia TARURA.”

Sakoro anaongeza; “tunafarijika sana Serikali ya Rais Magufuli kutuamini kampuni ya kizalendo na nitoe wito makampuni ya ujenzi ya kizalendo tujitahidi sana kutanguliza uzalendo katika majenzi yetu maana tunajenga chetu wenyewe tukiharibu tunajiharibia wenyewe na ninaamini tukijenga vizuri na gharama inayolingana na kazi hakika tutaweza kabisa kuleta ushindani mkubwa dhidi ya kampuni za kigeni ambazo kimsingi hawana jipya. Tumuunge mkono JPM kwa kuchapa kazi na ubora maana tunatumia kodi zetu wenyewe.”

Naye Injinia Mkuu wa BECCO Rashid Ramadhani anasema, “kampuni za kizalendo tunajitahidi sana tatizo ni kukosa uzoefu na mitaji ya kushindana na kampuni za kigeni jambo ambalo linatufanya tuendelee kuwa Sub-Contructors katika miradi mikubwa hata hivyo nashauri tu Serikali iendelee kutuamini kufanya kazi na makampuni makubwa haya ili kuongeza uzoefu wa kujenga miradi mikubwa maana kwa uzalendo wetu hata gharama za ujenzi zitapungua maana ni chetu.”

Akizungumza katika uzinduzi wa kitabu cha Reginald Mengi cha I can, I Must I will mwanzoni mwa wiki Rais Magufuli aliwaasa Watanzania kujiamini na kuacha kukatishwa tamaa. “Ninaomba Watanzania tuige mfano wa Mengi, tujiamini kuwa tunaweza haya makampuni yetu yanaweza tukiweka nia thabiti, tusikatishane tamaa, tuwaamini wenzetu mwisho tutaweza kujitegemea kwa vya kwetu.”

Kwa mfumo wa uendeshaji wa Serikali awamu ya tano chini ya Rais Magufuli na watendaji wake ni busara kutoa kipaumbele kwa makampuni ya kizalendo katika ujenzi wa miundombinu yetu na hata pale kampuni zetu zinaposhindwa utaalamu ni vizuri “kuazima” utaalamu huo kutoka nje huku tukiendelea kuwekeza kwa nguvu zote katika elimu ya sekta hii ya ujenzi.

Makala haya yameangazia eneo dogo la Vingunguti-Buguruni na kampuni ndogo na kongwe ya BECCO lakini ninaelezwa kuwa hali ni hiyo hiyo nchi nzima mikoani na wilayani. Makampuni ya kigeni yamekuwa yakipewa kipaumbele ilhali kazi zao ni zilezile zinazofanywa na kampuni za kizalendo tena wao (wageni) wakisukumwa zaidi na faida kuliko uzalendo unaozingatia umakini na ubora.

Aidha, nitoe wito kwa makampuni yetu ya kizalendo ya ujenzi na bidhaa nyingine kwamba “uzalendo” usitumike kama kichaka cha kuficha udhaifu na kufanya madudu hasa katika ujenzi wa barabara. Tunapowaamini basi fanyeni kazi kweli ili muaminike zaidi si hapa nchini tu lakini hatimaye nanyi mvuke mipaka mkajenge barabara ughaibuni. Kwa kufanya hivyo hatimaye tutafika Kaanani, nchi ya ahadi yaani maendeleo ya kweli. Mkiaminiwa, basi muaminike!