Home Habari Kampuni za simu zabebesha tozo wateja

Kampuni za simu zabebesha tozo wateja

293
0
SHARE

Mwandishi Wetu -Dar es salaam

KAMPUNI za simu za mkononi zinazofanya biashara ya miamala zimeendelea kuwabebesha wateja mzigo wa kodi ambazo zinatakiwa kulipa licha ya kutakiwa na Waziri wa Fedha na Mipango kutokufanya hivyo, uchunguzi wa Rai umegundua.

Tangu Juni 2016  wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Philipo Mpango, alipowasilisha bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2016/2017 alianisha vyanzo vipya vya kodi kwa serikali ikiwamo kodi ya kufanya miamala, na alizitaka kampuni za simu za mkononi kutokuhamishia mzigo huo kwa wateja wake.

Uchunguzi wa Rai uliofanywa kwa huduma za Tigo Pesa, M-PESA na AirTel Money, unaonyesha kuwa tangu wakati huo hadi sasa kumekuwa na ongezeko la malipo kwa watumiaji wa huduma hizo, hali inayoonyesha kuwa mzigo wa kodi uliobebeshwa kwao wameuhamishia kwa wateja wake.

Sheria ya Fedha iliyopitishwa wakati wa Bunge la Bajeti 2016/17 inaelekeza kutozwa kwa ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye ada zinazotozwa na watoa huduma katika kutuma na kupokea fedha badala ya ushuru huo kutozwa tu kwenye kutuma fedha pekee.

Tigo Pesa walikuwa wanatoza Sh. 300 kwa kutuma muamuala wa Sh. 10,000, huku wakitoza Sh. 1,300 kwa kutoa kiasi hicho.

Kwa sasa hivi, Tigo Pesa wanatoza Sh. 350 kutuma muamala wa Sh. 10,000, huku wakitoza Sh. 1,400 kutoa kiasi hicho.

Tigo Pesa wana viwango vya kutuma pesa 20, vikianzia Sh. 100 hadi Sh. milioni tatu. Katika viwango hivyo, ongezeko la kutuma na kutoa linaoneka kuegemea zaidi kwenye utumaji wa fedha chini ya milioni moja. Ongezeko hilo ni la kati ya Sh. 50 na 150 kwa muamala.

Airtel wana viwango 23 kuanzia Sh. 100 hadi Sh. milioni 10.

Ingawa viwango vya Tigo Pesa na Airtel Money vinakaribiana kwa karibu zaidi, M-PESA wanaonekana kuwa na viwango vikubwa zaidi.

M-PESA wana viwango 24 wakianzia na Sh. 100 mpaka zaidi ya Sh. milioni tatu. Kwa mfano mteja anayetuma Sh. 10,000 kwenda mitando mwingine atatakiwa kulipa Sh. 550, huku akitakiwa kulipa Sh. 1,450 kutoa kiwango hicho kwa wakala. Viwango hivi vipya vilianza kupanda kidogo kidogo tangu kuazishwa kwa kodi hizi zilizotarajiwa kubebwa na kampuni hizo.

Uchunguzi unaonyesha katika baadhi ya mitandao ada hizo zimepanda kati ya Sh. 50 hadi Sh. 200 kutegemeana na kiasi cha fedha kinachotumwa au kutolewa.

IDADI YA WATUMIAJI/MIAMALA

Ripoti ya takwimu za mawasiliano (Telecom Statistics) inayotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonyesha miamala ya fedha iliyofanywa kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka jana ilikuwa milioni 811.5 yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 27.7.

KAMPUNI ZA SIMU

Hata hivyo kampuni za simu hazikuwa tayari kueleza kwa undani sababu za kupanda kwa ada hizo kimya kimya.

TCRA-CCC

Hivi karibuni Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA- CCC), lilisema kuwa kuwa asilimia 90 ya malalamiko waliyoyapata, yanatokana na huduma za simu za mkononi ikiwamo wananchi kutuma fedha bila jina kuonekana.