Home Habari Kampuni za simu zinavyowinda wateja

Kampuni za simu zinavyowinda wateja

961
0
SHARE

MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

TAKWIMU za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa robo ya pili ya mwaka inayoanzia Mei hadi Juni mwaka huu, zinaonyesha kuwa kumekuwa na kushuka kwa idadi ya watu wanaotumia mitandao ya simu, hivyo kusababisha kuyumba kwa hisa za soko kwa baadhi ya kampuni za simu za mikononi miezi hiyo mitatu.

Katika takwimu hizo za TCRA, kwa ujumla, upigaji wa simu na hisa katika soko kwa kampuni saba zilizoorodheshwa, kwa mwezi Aprili ilikuwa 43,874,333, Mei 43,553,260 na Juni 43,749,086.

Hii inamaanisha kutoka Aprili kwenda Mei kulikuwa na upungufu wa wateja 321,073, kutoka Mei kwenda Juni kulikuwa na ongezeko la wateja 195,826 hivyo kufanya wateja wasiojulikana waliko katika robo ya pili ya mwaka huu kuwa 125,247.

Tigo

Katika takwimu hizo, kwenye suala la upigaji simu na hisa katika soko kwa kampuni hizo za simu, kampuni iliyopoteza wateja wengi ni Tigo, ambayo Aprili hadi Mei ilipoteza wateja 284,292 na kati ya Mei hadi Juni ilipoteza 172,680 hivyo kufanya wateja 111,612 wasijulikane walipo.

Katika mtiririko huo, Kampuni ya Tigo, Aprili ilikuwa na wateja 12,132,781 waliopiga simu, Mei wateja 11,848,489 na Juni 11,675,809.

Vodacom

Katika kipindi hicho, Kampuni ya Vodacom ilionekana kuongeza wateja waliopiga simu. Kwa Aprili ilikuwa na wateja 14,187,223, Mei 14,204,622 na Juni 14,392,174.

Hii inamaanisha kutoka Aprili hadi Mei, kampuni hiyo iliongeza wateja 17,399 na kutoka Mei hadi Juni, iliongeza wateja 187,552, ikimaanisha katika robo hiyo ya pili ya mwaka iliongeza wateja 170,153 waliopiga simu hivyo kuongeza wigo wa hisa katika soko.

Airtel

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Kampuni ya Aitrel ilikuwa na wateja 11,505,012 waliotumia mtandao huo kupiga simu kwa mwezi Aprili, kwa Mei walikuwa 11,558,381 na Juni 11,538,358.

Hii inamaanisha kuwa kutoka Aprili hadi Mei, kulikuwa na ongezeko la wateja 53,369 na kutoka Mei hadi Juni kulikuwa na upungufu wa wateja 20,023, ikimaanisha kuwa katika kipindi hicho, kampuni hiyo iliongeza wateja halisi 33,346.

Halotel

Kwa Kampuni ya Halotel, Aprili ilikuwa na wateja 3,979,680 waliopiga simu na Mei 4,054,789 huku Juni ilikuwa na wateja 4,218,656.

Hii inamaanisha kuwa kutoka Aprili hadi Mei, Halotel ilikuwa na ongezeko la wateja 75,109 na kutoka Mei kwenda Juni kulikuwa na ongezeko la wateja 163,867 hivyo kufanya ongezeko halisi la wateja katika kipindi hicho kuwa 88,758.

TTCL

Kwa Kampuni ya TTCL, katika kipindi hicho cha robo mwaka ya pili, takwimu hizo zinaonyesha kuwa kwa Aprili ilipata wateja 837,024, Mei 673,363 na Juni ilipata wateja  716,206 waliopiga simu kupitia mtandao huo.

Hii inamaanisha kuwa TTCL ilipoteza wateja 163,661 kutoka Aprili kwenda Mei na kuongeza 42,843 kutoka Mei kwenda Juni, lakini hiyo haikuweza kuifanya isipoteze wateja 120,818 waliopotea kati ya Aprili na Mei na hawakuweza kuwarudisha hadi robo hiyo ya pili inamalizika.

Zantel

Kwa mujibu wa takwimu hizo zilizotolewa na TCRA, Kampuni ya Zantel, kwa Aprili ilipata wateja 1,231,643 waliopiga simu, Mei 1,212,646 na Juni 1,206,913.

Kwa hiyo, kutoka Aprili hadi Mei kulikuwa na upungufu wa wateja 18,997 na kutoka Mei hadi Juni kulikuwa na upungufu wa 5,733, hivyo kuifanya ipoteze wateja 24,730 katika kipindi hicho cha miezi mitatu.

Smile

Kwa Kampuni ya Smile, yenyewe takwimu zinaonyesha kuwa kwa Aprili ilikuwa na wateja 970, Mei 970 na Juni pia ilikuwa na wateja 970 waliopiga simu.

Hii inamaanisha kampuni hii haikupoteza wala kuongeza mteja katika kipindi chote cha miezi mitatu na iliendelea kubaki na wateja wale wale wale 970.

Katika uchambuzi uliofanywa na gazeti hili katika takwimu hizo, katika eneo la upigaji wa simu Kampuni ya Tigo ilipoteza wateja 111,612, TTCL ilipoteza wateja 120,818 na Zantel ilipoteza wateja 24,730 na kufanya wateja waliopotea katika kipindi hicho kwenye kampuni hizi tatu kufikia 257,160.

Katika eneo hilo, Kampuni ya Vodacom iliongeza wateja 170,153, Airtel iliongeza 33,346, Halotel iliongeza 88,758 na hivyo kufanya kampuni hizo tatu kwa pamoja kuongeza wateja 292,257

Kwa ongezeko hilo la wateja 292,257 walioongezeka miongoni mwa waliopiga simu katika kampuni hizi tatu za Vodacom, Airtel na Halotel, ikilinganishwa na wateja 257,160 waliopotea Tigo, TTCL na Zantel, inaonyesha kuwa kuna uwezekano wateja wapya ni 35,097 ambao hawakuwapo kwenye mtandao wowote wa simu.

Matokeo ya jumla

Katika taarifa ya jumla ya TCRA, ongezeko la jumla la wateja wa Kampuni ya Tigo kwa Mei ni pungufu ya wateja 284,292 na kwa Juni ni pungufu ya wateja 172,680 hivyo kuifanya kampuni hiyo kukosa wateja 456,972 katika eneo la upigaji simu.

Kwa Vodacom, TCRA ilieleza kuwa ongezeko la jumla kwa Mei lilikuwa wateja 17,399 na kwa Juni wateja 187,552 hivyo kuifanya kuvuna wateja 204,951 katika eneo hilo.

Kwa Halotel, TCRA ilieleza kuwa kulikuwa na ongezeko la wateja 75,109 kwa Mei na Juni ilikuwa wateja 163,867 hivyo kuifanya kampuni hiyo kuwa na ongezeko la jumla la wateja 238,976.

TCRA ilieleza katika taarifa hiyo kuwa ongezeko la jumla kwa wateja wa Airtel kwa Mei ilikuwa ni 53,369 na kwa Juni kulikuwa na upungufu wa wateja 20,023, hivyo kufanya idadi ya wateja walioongezeka katika robo hiyo ya pili ya mwaka kuwa 33,346.

Taarifa hiyo ya takwimu ya TCRA ilieleza kuwa kwa Mei Kampuni ya TTCL ilipoteza wateja 163,661 lakini Juni iliongeza wateja 42,843 hivyo kupoteza wateja 120,818 katika kipindi hicho.

Ilieleza kuwa kwa Zantel, ongezeko la jumla lilikuwa ni pungufu kwa wateja 18,997 kwa Mei na pungufu kwa wateja 5,733 Juni, hivyo kuifanya ipoteze wateja 24,730.

Kwa kampuni ya Smile iliendelea kubaki na wateja wake.

Kwa maana hiyo, kwa mujibu wa takwimu hizo za TCRA, kwa jumla ya simu zilizopigwa na wateja kupitia kampuni hizo saba, kwa zilizopoteza wateja kwa Mei ni pungufu ya wateja 321,073, kwa Juni zilizoongeza wateja walifikia 195,826 hivyo kuwa na upungufu wa jumla wa wateja 125,247.