Home Habari kuu Kamwelwe: Mafisadi hawana nafasi Bandari

Kamwelwe: Mafisadi hawana nafasi Bandari

451
0
SHARE

Mwandishi Wetu

UFUFUAJI wa bandari katika Ziwa Victoria umeshika kasi ambapo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imekamilisha maboresho ya bandari za Kemondo Bay na Bukoba ambazo zipo tayari kuanza kuhudumia meli kubwa za mizigo na abiria.

Kutokana na hali hiyo serikali imesema kuwa hatua ya kusuasua kwa bandari hizo kwa miaka 15 iliyopita ikiwamo kusimama kwa huduma kulichangia kwa kiasi kubwa kuibuka kwa bandari bubu katika eneo hilo.

Hali hiyo inakwenda sambamba na maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, ambapo imechagiza kuongezeka shehena za mizigo na mapato kwa kiasi kikubwa.

Hatua hiyo inamfanya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe, akiwa mkoani Kagera kuonya kuwa uendeshaji wa bandari nchini hautarudishwa nyuma kama ilivyokuwa imefanywa na mafisadi.

Akikagua maboresho ya Bandari za Bukoba na Kemondo, anasema baada ya bandari nyingi kusitisha shughuli zake kwa kipindi kirefu kulisababishwa na matatizo mbalimbali, wakiwamo mafisadi waliokuwa wakipenda kujinufaisha wenyewe, Serikali imeanza mkakati wa kuzifufua na kuboresha zaidi zinazofanya kazi.

“Tunafanya maboresho katika bandari zetu zote, tunataka turudishe huduma kwa kasi kubwa hata kwa zile ambazo zilikuwa zimesitisha huduma zake, ulifanyika uzembe, waliturudisha nyuma mafisadi, lakini tumefanikiwa kunyanyuka, hatutakubali kurudishwa nyuma tena walikokuwa wametufikisha.

“Juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli za kukarabati bandari na meli, meli zinabadilika zinakuwa mpya, hususani meli ya Mv Victoria na Mv Butiama ambazo mpaka Aprili mwakani zitaanza kufanya kazi.

“Nimekuja kukagua maboresho haya yanayofanyika, kazi inaendelea vizuri na ninaipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kwa kazi kubwa wanayofanya katika uboreshaji huu wa bandari.

“Usafiri wetu wa raha uliopotea kwa miaka mingi, sasa unarudi, Mv Victoria sasa itatoa huduma zake katika ziwa hili na itafika Uganda mpaka Kenya, tunatarajia wananchi wataondokana na shida ya usafiri ambayo imekuwapo kwa muda mrefu,”anasema.

Akizungumzia maboresho yanayofanyika katika reli, Kamwelwe anasema kwa sasa serikali imepanga kufufua usafiri huo kuwa kama wa barabara.

UGAWAJI MABEHEWA

Pamoja na hali hiyo anasea kwa sasa Serikali ipo tayari kugawa mabehewa kwa wafanyabiashara ili waweze kusafirisha mizigo yao kwa kwa usafiri wa treni na meli kama njia ya kuimarisha sekta ya uchukuzi kupitia usafiri huo.

Anasema katika mkakati huo watagawa mabehewa hayo zaidi ya 1,000  yanayomilikiwa na Shirika la Reli Tanzania(TRC) kwa wafanyabiashara wakubwa ambao watayahitaji kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao kutoka bandarini kwenda sehemu mbalimbali nchini.

Mhandisi Kamwelwe anasema kuwa mchakato huo wa kutoa mabehewa hayo utaanza baada ya kufanyika kikao kati yake na wadau mbalimbali wakiwamo wafanyabishara wanaotumia usafiri wa meli na reli kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao.

Hata hivyo anasema kuwa mabehewa hayo watakayopewa wafanyabishara hao wanaohitaji pamoja na kuyafanyia matengenezo kwa fedha zao bado yatabaki kuwa mali ya Shirika la Reli Tanzania (TRC).

“Mabehewa ambayo tunayo pale TRC tutawapa wafanamyabiashara na sisi tutawaruhsu kutumia miundombinu ya reli lakini tutakuwa tukipata ushuru unaotokana na kutumia reli.

“Hivyo kati ya siku mbili hizi nitakuwa na kikao na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania(TRC) Mhandisi Masanja Kadogosa ili kujadili kwa kina suala hilo ambalo sasa litatufanya turahisishe utoaji wa huduma za usafiri, tunaka tukimbie badala ya kuendelea kwani imetuchelewesha sana,” anasema Kamwelwe.

HALI KATIKA BANDARI YA BUKOBA
Akiwa katika Bandari ya Bukoba, Waziri Kamwelwe, anasema kuwa ilianza kujengwa mwaka 1943 na kukamilika mwaka 1945 ambapo wakati huo ilianza kutumia kwa vyombo mbalimbali vya majini lakini baadaye serikali ikawa na meli zake ikiwamo za Mv Bukoba, MV Victoria na MV Butiama.

“Mv Victoria kwa bahati mbaya ilizama lakini pia tulikuwa na meli nyingine Mv Clarias iliharibika. Lakini baada ya kuanza Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk.John Magufuli,  ambaye amekuwa na dhamira thabiti ya kusubutu na ametoa maelekezo ndio mnaona haya maendeleo sasa Bandari hii inakarabatiwa ili iwe mpya.

“Kinachofanyika ni pamoja na kukarabati magati kwa ajili ya meli ili ziweze kufika sehemu na kupaki lakini pia maghala kwa ajili ya mizigo, chumba cha abiria ambao wa nasubiri kusafiri, ofisi za wafanyakazi wa TPA, Kampuni ya Meli Tanzania pamoja na TASAC ambaye ni dhibiti ili sasa bandari hii ianze kufanyakazi rasmi,” alisema

Anasema kwa sasa meli ya MV Umoja imeanza kazi ya kubeba mizigo na ina uwezo kubeba mabehewa 19 kwa wakati mmoja pindi yanapowasili kwa treni na hakuna haja ya kushundwa kwani ndani ya meli hiyo kuna reli.

BANDARI YA KEMONDO

Kwa upande wake Meneja wa Ziwa Victoria, Morris Mchindiuza, anasema Bandari ya Kemondo Bay,  ipo wilayani Bukoba mkoani Kagera, hii ilijengwa kuanzia mwaka 1971 na kukamilika mwaka 1974.

Anasema lengo kuu la Bandari hii kwa wakati huo lilikuwa zaidi kusafirisha shehena za mizigo mbalimbali na hasa zao kuu lilikuwa kahawa lakini pia ilikuwa inahudumia abiria kilikuwa kituo kikubwa cha kuibeba mizigo ikiwamo mihogo na ndizi na maparachichi ambayo yalikuwa yakisafirishwa kwa wingi kutoka katika eneo hili. 

“Lakini pia mizigo yote iliyokuwa ikitolewa mkoani Mwanza kama vifaa vya ujenzi ikiwamo saruji pamoja na nondo Ilikuwa ikifikishwa hapa na baadaye kutawanywa katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kagera pamoja na vitongoji vyake. 

“Kwa takribani miaka 15 iliyopita hapa katika Bandari ya Kemondo Bay ilikuwa I nakwenda kwa kusimama na kusuasua na baadaye kabisa tukajikuta hatuna oparesheni zozote zinazofanyika kwenye hili eneo kubwa la Bandariya Kemondo Bay. 

“Niseme pia Bandari ya Kemondo inasemu mbili kuna sehemu ya mwalo ambayo ipo pale pembeni na sehemu hii ambayo ni Bandari kuu, hapa zilikuwa zinafunga meli kubwa kabisa lakini baada ya mdororo uliotokea hapa katikati ambapo meli kubwa zikawa hazifiki katika eneo hili bado kukawa na mahitaji ya watu wanapokwenda visiwani na hivyo kukawa na boti ndogondogo ambazo zilikuwa pembeni mwa bandari,” anasema Mchindiuza

Anasema TPA kwa kuona uhitaji na pia ya hizi boti ndogondogo tukajenga eneo la uwezeshaji katika eneo hilo la pembeni ambapo tumejenga gari dogo ambalo linaweza kuhimili boti ndogo kutia nanga. 

“Katika kipindi ambacho huduma imesimama kwenye eneo hili Bandari ya Kemondo kule upande wa mwalo huduma zikawa zinaendelea kwa tuna boti ambazo zinatoka huduma katika visiwa kwenye eneo hili. 

“Kwa kifupi baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania kuona kwamba hali hii inaendelea tukasema hapana Mamlaka ikajaribu kuwekeza na kuhuisha miundombinu iliyopo hivyo tukaanza kufanya ukarabati kwenye jengo la abiria lakini pia tukaja kwenye hili eneo la daraja la reli. 

“Reli zilizopo hapa kama mnazoziona zilikuwa zimefukiwa kabisa kwa hiyo kulikuwa hakuna uwezekano wa kuingiza behewa zikawesha kufanya kazi,” anasema

UFUFUJI KWA MILIONI 800

Tokana na umuhimu wa bandari hiyo katika kukuza usafirishaji na uchumi wa nchi TPA iliamua kuwekeza kiasi cha Sh milioni 815 kwa ajili ya kufufua bandari hiyo ambayo ilikuwa mkombozi kwa wananchi na wafanyabiashara wa mazao na bidhaa mbalimbali wa nchini na nchi za jirani za Uganda na Kenya.

“Tukasema tuwekeze fedha hapa kiasi cha cha zaidi ya milioni 815 kwa ajili ya kufanya kazi hiyo na kazi hii tumeianza wiki tatu zilizopita na sasa tupo mwisho kabisa kuikamilisha ili kazi zianze za kuingiza mizigo katika bandari hii. 

“Tuna amini bandari hii itakuwa ni kichocheo cha ajira katika eneo letu hili lakini pia kumuwezesha mwananchi wa kipato cha chini mkulima mtanzania ambaye yeye analima ndizi na maparachichi. 

“Tunaambiwa hapo zamani walikuwa wakibeba ndizi na maparachichi wakiingiza katika meli zinapelekwa Mwanza wanapata fedha kwa ajili ya kujikimu ndicho hicho kilio cha wana Kemondo na sasa tunahakikisha tunawarejeshea miundombinu na kuweza kuwafanya sasa waanze kuona faida ya moja kwa moja ambayo imefanywa na Mamlaka ya Bandari,” anasema Mchindiuza

Meneja huyo anasema kupitia Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, wanatarajia itaanza kuanza kazi kabla ya Desemba mwaka huu

WATEJA NA MATUMAINI

Mchindiuza anasema kuwa tayari kuna mteja ambaye wamekuwa wakifanya naye naye kazi toka awali. 

“Toka tumekubali kuwekeza fedha tulikuwa tayari tuna mawasiliano na mteja ambaye ni Simba Cement ambaye atakuwa anatoa saruji kutoka Tanga akisafirisha kwa reli kuja mpaka Mwanza South Port ambapo pale itaingia itaingia moja kwa moja kwenye meli ya mizigo kuleta hapa Kemondo Bay. 

“Kwa hiyo tumekuwa tukiambatana naye na kuangalia maendeleo ya kazi iliyokuwa tunayofanya TPA na bahati nzuri mteja huyo alikuja hapa akiwa amekusanya mawakala wake wakiwamo pia wateja wakubwa wanaozunguka eneo hili na watakuwa wanasambaza kwao saruji nao wameona kazi kubwa nayofanywa na sasa wameshaanza kutoa oda za mahitaji ya saruji wanasubiri kupata mabehewa ili tuanze kuleta mzigo katika bandari hii,” anasema

UJUMBE KWA WAFANYABIASHARA 

“Ujumbe wetu kwa wafanyabishara wengine ni kwamba tunawakaribisha kutumia bandari hii ya Kemondo ambayo awali tuna imani walikuwa wanajua havifanyi kazi lakini tunawaammbia sasa Bandari ya Kemondo Bay iko tayari kufanyakazi kwa namna ile ile iliyokuwa iliyokuwapo miaka ya nyuma. 

“Wito wetu ni kwamba waendelea na kujaribu kuangalia fursa zilizopo katika Mkoa wa Kagera pamoja na nchi jirani zinazotunguka katika eneo hili kwa namna gani wanaweza kutumia na tuna wahakikisha kwamba usafiri wa kutumia reli na bandari uko chini zaidi ukilinganisha na njia zingine za usafirishaji,” anasema Mchindiuza