Home Makala KANALI KASHMIR, MAHFOUDH WALIVYOSAIDIA MSUMBIJI KUPATA UHURU -2 

KANALI KASHMIR, MAHFOUDH WALIVYOSAIDIA MSUMBIJI KUPATA UHURU -2 

1592
0
SHARE

NA SIMON NOEL


KATIKA sehemu ya kwanza tulizungumzia kidogo namna Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) lilivyoshiriki katika mapambano ya kuzikomboa nchi za Afrika.

Baadhi ya Watanzania ambao walijitoa kikamilifu kuhakikisha nchi za Kusini mwa Afrika zinakuwa huru kutoka kwenye makucha ya wakoloni wadhalimu ni marehemu Kanali Ali Mahfoudh na Kanali Ameen Kashmir.

Endelea na simulizi hii ambayo Kanali Ameen Kashmir anasimulia namna Watanzania walivyokuwa mstari wa mbele kuhakikisha Waafrika wenzao wanakombolewa.

Nakumbuka vizuri kabisa kuwa Ernesto Che Guevara aliwasili nchini mwaka 1965 mwanzoni. Na mara tuu baada ya kuwasili alifanya mkutano wa pamoja na viongozi wote wa wapigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika.

Nia ya mkutano huo ilikuwa ni kuwatia moyo na kuwaelekeza kwa ufasaha ni vipi wataweza kuyashinda majeshi makubwa yenye silaha kali  huku wakiwa na Majeshi ambayo sio imara sana. Che Guevara aliwaambia wanaharakati wale kuwa silaha kubwa sana ni umoja na wakiitumia vizuri watashinda mapambano kwa urahisi sana

Kwa kweli ilikuwa ziara yenye manufaa sana kwani wapigania uhuru walipata ari na moyo wa kupigana.

Vijana tuliowapeleka Algeria walirudi wakiwa na ari kubwa sana ya kupambana. Kwa bahati nzuri sana pia baadhi ya raia wa Msumbiji walikuwa wamesikia taarifa za FRELIMO kufanya mikakati ya kuanzisha vita na hivyo wakavuka mpaka na kuingia nchini kwetu na wote tuliwaweka katika kambi ya Nachingwea na mara moja tukaanza kuwapa mafunzo ya kijeshi.

 

KANALI MAHFOUDH UWANJA WA MAPAMBANO

Baada ya kuundwa kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kanali Mahfoudh aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa operesheni na mafunzo wa jeshi letu la JWTZ. Wakati huo mimi nikiwa ndie mnadhimu mkuu wa jeshi la wananchi wa Tanzania JWTZ. Kanali Mahfoudh ndie alisimamia mafunzo kwa vijana hao wapya pamoja na askari wetu wengine katika kambi ya Nachingwea.

Baada ya mafunzo hayo kukamilika tukaona hatuna sababu ya kuchelewa na hivyo tuanze vita mara moja. Kwa kipindi hicho jeshi la FRELIMO lilikuwa chini ya uongozi wa Fillipe Magaia kijana shupavu kabisa. Kwa hakika Fillipe Magaia alikuwa hodari sana na asiyevunjika moyo wakati wote wa mapambano.

Kabla ya kuanzisha mashambulizi kanali Mahfoudh aliomba kwanza kwenda kuzipeleleza kambi za kijeshi zilizoko huko Msumbiji pamoja na mazingira yote yalivyo huko Msumbiji.

Unajua Mahfoudh alikuwa ni mpelelezi hodari sana na vile alivyokuwa chotara wa kiarabu na Kiswahili ilikuwa ni vigumu kumtambua kuwa ni mtanzania. Aliingia Msumbiji kimya kimya na akazifanyia upelelezi wa kina kambi za kijeshi za Capo Delgado na Xai Xai baada ya hapo akarudi Nachingwea ili kuandaa mpango wa mashambulizi.

Balozi wa Cuba nchini Tanzania kipindi hicho Pablo Ribalta nae alikuwepo Nachingwea kipindi hicho.

Nilipofika Nachingwea nilikuta tayari Kanali Mahfoudh, Fillipe Magaia, Samora Machel na balozi Pablo Ribalta wameshaandaa mpango wa kivita. Kipindi hicho askari wa FRELIMO walikuwa wachache sana hawakuzidi hata 1000. Askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania JWTZ ndio walikuwa wengi kuzidi hata hao FRELIMO wenyewe.

Balozi Ribalta aliniambia kuwa vita hii ni lazima tutashinda kwani wao wenyewe wakati wanaanza vita huko Sierra Maestra walikuwa wachache sana kulinganisha na askari wa FRELIMO.

Vikosi vya FRELIMO pamoja na JWTZ vilivuka mpaka mwishoni mwaka 1964 na kuanzisha mashambulizi ya kasi sana katika kambi ya Xai Xai na kupata ushindi mkubwa sana. Nikiwa Nachingwea kazi yangu ilikuwa ni kupata taarifa zilivyo uwanja wa mapambano na kupeleka msaada wa haraka unaohitajika uwanja wa mapambano.

Kanali Mahfoudh, Fillipe Magaia, Samora Machel, Joachim Chisano, Raimundo Pachinuapa na Albert Chipande wao ndio walikuwa makamanda wa mstari wa mbele. Nilikuja kuambiwa baadae kuwa risasi ya kwanza kabisa ya kuikomboa Msumbiji ilipigwa na Albert Chipande na mpaka leo anaheshimika sana huko Msumbiji kwa hilo.

Vikosi vya FRELIMO pamoja na JWTZ walifanya mashambulizi ya kasi sana kiasi Kwamba askari wengi wa jeshi la wakoloni Wareno walisalimisha maisha yao kwa kukimbia na kurudi nyuma.

Baada ya kuteka kambi hizo za jeshi tulifanikiwa kuwakamata mateka ambao walikuwa ni waafrika raia wa Msumbiji waliokuwa wameamua kujiunga na jeshi la wakoloni wadhalimu Wareno na kuwatetea ili waendelee kutawaliwa. Mara baada ya kuwakamata mateka hao kanali Mahfoudh aliomba awashughulikie ili apate taarifa zaidi juu ya mienendo ya jeshi la Wareno.

Kanali Mahfoudh alikuwa anajua sana kufanya interrogation  (mahojiano ya nguvu ya kupata taarifa). Na kwa kweli alipata taarifa nyingi sana za kuhusu jeshi la Wareno na haswa mpango wao wa kivita dhidi ya FRELIMO.

Habari hizo za jeshi la FRELIMO pamoja na jeshi la wananchi wa Tanzania JWTZ kupata ushindi wa kishindo huko Xai Xai na Capo Delgado ziliwashtua sana wakoloni waonevu Wareno pamoja na marafiki zao wa South Africa na Rhodesia. Kwa kweli hawakuamini kama tungekuwa na uwezo wa kuwashinda kwa kiasi hicho.

Kwa upande mwingine zilikuwa ni taarifa za faraja kubwa sana kwa wananchi wa Msumbiji na dunia nzima ya wapenda haki.

Wananchi wa Msumbiji Sasa wakaanza kumiminika mamia kwa maelfu Kuja kujiunga na FRELIMO ili kuikomboa nchi yao.

Kufikia mwezi June mwaka 1965 kambi yetu ya Nachingwea ilikuwa Sasa imezidiwa na vijana kutoka Msumbiji na kwa kweli hatukuwa Sasa na uwezo wa kuwapatia mafunzo kwani kambi yetu ya Nachingwea ilikuwa ndogo kwa kipindi hicho.

Kwa haraka sana nilienda kumuomba Mwalimu Nyerere tuipanue kambi ya Nachingwea kwa haraka sana ili tuweze kuwapatia mafunzo vijana hawa wapya ili tuendelee kuwazidi nguvu na kuwatandika wakoloni waonevu Wareno.