Home Makala Kangi Lugola na kilemba cha ukoka!

Kangi Lugola na kilemba cha ukoka!

637
0
SHARE

Mwandishi Wetu


KUTOKUWAJIBIKA ipasavyo kwa baadhi ya mawaziri na watendaji katika wizara na mashirika mbalimbali ya Serikali na taasisi zake, hasa katika masuala yanayohusiana na matumizi ya fedha za Serikali kwa mara nyingine tena kumemlazimisha Rais Dk. John Magufuli kuingia katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi(ICU) wanaosubiri upasuaji mkubwa na kuwapasua bila ganzi Kamshina Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF), Thobias Andengenye na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, mbali na shughuli zake nyingine nyingi, inamiliki chombo kinachopambana na uhalifu mkubwa na mdogo ndani ya nchi yetu ukiwemo wizi wa kuku hadi uhujumu uchumi na vikorombwezo vyake kama utakatishaji wa fedha, makosa na wizi wa kutumia mitandao (Cyber Crime), ikiwa ni pamoja na makosa yote ya jinai yanayoweza kutokea na yanayotokea ndani ya nchi yetu sanjari na kulinda usalama wa raia na mali zao ikiwa ni sehemu ya jukumu lao muhimu.
Kilichomtokea Lugola ni sawa sawa na kisa cha mchungaji aliyekula kondoo wa bwana wake au kushindwa kuwahami kondoo hao dhidi ya mbwa mwitu na wanyama wengine wa aina yake, ambao kila kukicha udenda unawatoka kutokana na kunona kwa wanakondoo wanaochungwa na mchungaji.
Kwa uchungu mkubwa uliojieleza wazi katika kauli na uso wa Rais Magufuli hasa pale alipouliza ni kwa jinsi gani Lugola na Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye walivyokuwa wanaendelea kunufaika na starehe ya viti vilivyokuwa meza kuu sambamba na Rais aliyekuwa katika sherehe ya ufunguzi wa majengo 12 ya makazi ya familia 172 za maofisa na askari wa Magereza katika gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Kwenye hafla hiyo, Rais Magufuli alimpongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Kingu kwa uamuzi wake wa kuwajibika, hatua ambayo alisema imempa heshima kubwa na inawezekana ametambua kwamba mambo yaliyokea katika wizara hiyo hakuyafanya mwenyewe na kwa kuwa yeye ni Katibu Mkuu amewajibika katika hilo.
“Nitaendelea kumheshimu, Lakini Lugola, Kamishina Jenerali Andengenye , ninashangaa kuwaona mko hapa, Ninawapenda sana lakini huu ndio ukweli, sitaki kuwa mnafiki. Urafiki na upendo uko pale pale lakini katika suala zima la kazi hakuna namna,”alisema Rais Magufuli.
Maneno haya ya uchungu aliyoyatoa Rais Magufuli yanayoonyesha taswira ya chuki aliyonayo dhidi ya dhuluma ya rushwa, ubadhirifu na kutowajibika vyema kwa baadhi ya wateule wake.
Ukiwasikiliza baadhi ya wateule wa Rais, wakati wakila viapo vyao Ikulu mbele ya Rais Magufuli, huwezi kuamini kwamba muda mfupi baada ya kuteuliwa baadhi yao hukiuka viapo vyao na kuiaibisha mamlaka iliyowateua. Hii inathibitishwa na orodha za mawaziri zaidi ya 20 waliotumbuliwa hadi hivi sasa.
Tumeona wengi na kuwasikia wengi, lakini Lugola alibeba beramu na kuonekana kwamba yeye pengine angekuwa bora zaidi, kwani hakuiacha Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo aliifanya leso ya kufutia jasho lake, muda wote akiwa nayo iwe ni katika mkutano wa hadhara, vikao vya ndani vya kiutendaji na pengine hata harusini na misibani.
Wananchi walio wengi hakika hawakutarajia kumwona Lugola ndani ya zizi la viongozi ambao huenda kwa makusudi na kwa hila kubwa walikuwa wakimng’ong’a Rais Magufuli ambaye ndiye mwajiri wao, hii ni aibu kubwa kwa Lugola aliyekuwa akijiapiza kula sahani moja na majambazi na wabadhirifu wengine baada ya Rais kugundua kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha uliotokana na utiaji saini wa makubaliano ya zabuni ya kununua vifaa vya Jeshi la zimamoto na Uokoaji vyenye thamani ya Euro milioni 408.5 sawa na zaidi ya Sh trilioni moja kutoka kampuni moja ya nje bila ya kufuata sheria, jeshi ambalo liko chini ya wizara aliyokuwa anaiongoza.
Hii ni kashfa yenye uzito wa pili katika nchi ambayo uzito wake umepindukia. Kashfa nyingine za namna hiyo isipokuwa kashfa moja mbele yake katika historia ya kashfa mbaya za ubadhirifu nchini ya Richmond.
Kundi la viongozi wasiowajibika vyema mawaziri waliotumbuliwa sasa limefikia idadi kubwa zaidi ya i 20, hii sio aibu kwa Rais wetu bali ni aibu kubwa kwa wanaokutwa katika kashfa hizi.
Rais kwa nafasi yake ameonyesha uwajibikaji uliotukuka kwa kuwatumbua bila ganzi wahusika kabla hawajaleta madhara makubwa katika uchumi wa nchi na utendaji wa taifa letu, nia ya Rais wetu ni kuhakikisha kuwa lengo la kuendesha Serikali isiyo na ubadhirifu, yenye kuheshimu haki za watu na yenye kujenga misingi ya nidhamu katika utendaji wake inaelekea kukamilika.
Na pengine sio muda mrefu ujao lengo hili litakamilika katika utaratibu utakaolifanya taifa hili kuwa bustani ya amani, ni hivi karibuni tu tumeshuhudia Rais akishuhudia utiaji saini wa mikataba tisa ya uchimbaji wa madini inayohusu uendeshaji wa kampuni mpya ya Twiga ambayo Serikali itakuwa mbia na Kampuni kubwa ya Barick.
Mikataba hiyo ambayo imezindua ushirikiano usio wa kinyonyaji kati ya Barick na kampuni hiyo ya kizalendo ya Twiga, ni ushindi mkubwa kwa nchi yetu na kwamba wale wote waliokuwa wanabeza mazungumzo yaliyokuwepo baina ya Serikali na Barick nadhani wamejutia kauli zao walizokuwa wanazitoa mbele ya umma.
Mapambano yaliyopelekea makubaliano hayo, yalikuwa ni makubwa mno yalitishia usalama wa uwekezaji nchini hasa kwenye sekta ya madini. Serikali kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Kamalagamba Kabudi ilikuwa katika hatua ngumu kwenye mazungumzo hayo kiasi cha yeye binafsi kufikia uamuzi wa kuandika barua ya kujiuzulu nafasi hiyo na baadaye aliichana barua hiyo.
Lakini kwa umahiri mkubwa na uvumilivu uliobebwa na uthubutu na hisia kali za uzalendo katika kipindi cha miaka mitatu ya mazungumzo baina ya Barick na Serikali, umezalisha ushindi wa kihistoria kwa sekta ya madini nchini. Na ndugu zangu Watanzania mambo ya aina hii makubwa katika nchi yetu tuyaunge mkono kwa dhati.
Kama Rais Magufuli ameliweza hili fupa la ngamia bila shaka baadhi ya wateule wake wanaojaribu kucheza na mali za umma wataishia katika tanuru waliloliwasha wao wenyewe!
Inawezekana kabisa baadhi ya wateule hawa wa Rais Magufuli hawajamwelewa vizuri alipokuwa akizungumzia umuhimu wa kuwa na mitambo ya kuchenjua madini nchini, badala ya kupeleka makinikia kuchenjuliwa katika nchi za ng’ambo.
Akili yao, baadhi ya wateule hawa, haikuwafikirisha katika njia nyingine aliyokuwa anaifikiria Rais wetu nayo pengine ilikuwa ni mbali ya kuwa na mtambo wa kuchenjulia madini (Smelter) kulikuwa pia na mtambo mwingine wa kuchenjua viongozi wasiotimiza vyema majukumu yao, wabadhirifu na wasiowajibika katika utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayozihusu kazi na nyadhifa zao.
Mtambo ndio kwanza umewaka ukiwa na moto mkali na matarajio ya mwandishi wa makala haya na wananchi ni kwamba viongozi wanaoteuliwa na Rais watafanya kazi na kutimiza wajibu wao wa kuutumikia umma wa nchi yetu, wakitilia maanani uwepo wa Smelter dhidi ya viongozi wabadhirifu na wasiowajibika.
Hongera Rais Magufuli kwa kazi njema ya utumbuaji na upasuaji wa majipu, ongeza kasi ya kulijenga taifa, sisi tuko nyuma yako, Aluta Continua!.