Home Habari Kanisa Katoliki lilivyoaninisha hitilafu za uchaguzi Burudi

Kanisa Katoliki lilivyoaninisha hitilafu za uchaguzi Burudi

582
0
SHARE
Kiongozi wa Upinzani Burundi, Agathon Rwasa

MWANDISHI WETU na MASHIRIKA

MATOKEO ya Uchaguzi Mkuu wa Burundi uliofanyika Mei 20 mwaka huu yametangazwa rasmi. Mgombea wa chama tawala cha CNDD-FDD, Jenerali Evariste Ndayishimiye ameibuka mshindi dhidi ya mpinzani wake mkuu, Agathon Rwasa wa chama cha CNL.

Ndayishimiye ambaye amekuwa mshirika na misaidizi wa muda mrefu wa rais aliyemaliza muda wake, Pierre Nkurunziza ametangazwa rasmi kuwa mshindi Mei 25, mwaka huu na hivyo hakuna shaka kwamba tayari ndiye Rais wa Burundi kuanzia sasa.

Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba aina ya uhuru wa mahakama zitakazopokea malalamiko ya wapinzani dhidi ya matokeo hayo, hauwezi kuvuka mamlaka ya chama tawala ambacho kilishaweka mizizi yake katika taasisi za utendaji na mihimili mingine inayoendesha nchi hiyo.

Ushindi huo wa Ndayizeye unahitimisha utawala wa miaka 15 ya Rais Nkurunziza ambaye alipata wakati mgumu sana alipojaribu kuwania nafasi hiyo kwa kipindi cha tatu na hatimaye aliamua kutowania tena kwa kipindi kingine, hivyo kutoa nafasi kwa mshirika wake wa karibu kushika kiti hicho.

MTAZAMO WA KANISA KATOLIKI

Jana, Mei 27, ikiwa ni siku mbili tangu kutangazwa kwa matokeo yaliyompa ushindi Ndayishimye, Kanisa Katoliki nchini Burundi limesema hitilafu kadhaa wakati wa uchaguzi wa rais uliofanyika wiki iliyopita nchini humo, zinasababisha mashaka juu ya matokeo yaliyokipa ushindi chama tawala. 

Katika waraka wake kuhusu matokeo hayo, Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki linasema waangalizi wake waliowekwa kwenye vituo vya kupigia kura nchini kote waliweza kushuhudia jinsi visanduku vya kura vilivyofanyiwa mizengwe na jinsi maofisa wa serikali walivyowabughudhi na kuwatisha wapiga kura. 

Baraza hilo pia linaeleza kuwa majina ya wakimbizi na ya watu waliokufa yaliwekwa katika daftari la wapiga kura.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, Mwenyekiti wa Baraza hilo la Maaskofu, Joachim Ntahondereye anatoa tamko kwamba kura zilihesabiwa kwa siri na kwamba watu ambao hawakuhusika na masuala ya uchaguzi wailingia na kutoka ndani ya vyumba vya kuhesabia kura.

Askofu huyo anaeleza kusikitishwa juu ya hitilafu kadhaa zilizojitokeza kuhusu uhuru na kutokuwapo uwazi katika mchakato wa upigaji kura. 

Pia anaeleza kwamba baadhi ya wagombea na wapiga kura hawakutendewa haki. Kutokana na mazingira hayo, mwenyekiti huyo wa baraza la maaskofu nchini Burundi anauliza iwapo matokeo ya uchaguzi hayakuwa na kasoro.

Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi iliyomtangaza mgombea wa chama tawala, Evariste Ndayishimiye kuwa mshindi wa uchaguzi kwa kupata asilimia 68.72 ya kura wakati mpinzani wake kiongozi wa chama cha upinzani, Agathon Rwasa aliambulia asilimia 24.19  ya kura imeendelea kukaa kimya juu ya tuhuma hizo.

Chama cha upinzani pia kimeyapinga matokeo hayo kwa madai kwamba udanganyifu ulifanyika na kinapanga kwenda mahakamani.

Baadhi ya madai yaliyotolewa na Kanisa Katoliki yameshabihiana na yale yaliyotolewa na chama cha upinzani cha CNL. 

Chama hicho kinadai kwamba maofisa wake walitimuliwa kutoka kwenye vituo vya kupigia kura katika siku ya uchaguzi.

Katika madai yao, CNL wanaeleza kuwa siku ya uchaguzi hawakuwapo waangalizi wa kimataifa kwa sababu hawakuruhusiwa kuingia nchini Burundi. 

Ofisa mmoja wa Kanisa ambaye hakutaka kutajwa jina anasema maombi ya Kanisa ya kupeleka waangalizi wao kwenye kila kituo cha kupigia kura nchini kote yalikataliwa, lakini Kanisa liliweza kuwapeleka waangalizi wake karibu 3000 kwenye manispaa zipatazo 119 kwenye uchaguzi ulioendelea bila ya kuzingatia athari za janga la Corona.

Uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na Serikali iliyomaliza muda wake ya Rais Nkurunziza ulimalizika baada ya Kanisa hilo kuupinga muhula wake wa tatu mnamo mwaka 2015. 

Watu wapatao 1200 walikufa kutokana na ghasia zilizosababishwa na uamuzi wa Nkurunziza wa kuendelea kubakia madarakani. Watu wengine zaidi ya 400,000 waliripotiwa kuikimbia nchi.

AHADI ZA RAIS MPYA

Wakati pande mbalimbali zikiendelea kukosoa uchaguzi huo wa Burundi na matokeo yake, mgombea aliyetangazwa mshindi wa kiti cha urais, Ndayishimiye anasema ushindi wake ni wa raia wote waliomchagua na wale ambao hawakumchagua.

Hiyo inaonekana kuwa ngao yake mpya ya kuonesha nia yake ya kuwaunganisha Warundi bila kujali waliomchagua wala wasiomchagua, ikiwa ni hatua ya kuonyesha uongozi usio wa kibaguzi.

Akihutubia baada ya kutangazwa mshindi Ndayishimiye anasema ushindi wake ni wa raia wote waliomchagua na wale ambao hawakumchagua.

Hivyo hakuna sababu ya wafuasi wa chama kimoja kuwabugudhi wengine. Pia anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuunga mkono hatua iliyofikiwa nchini humo.

Kiongozi hiyo wa chama cha CNDD-FDD aliyeibuka mshindi uchaguzi wa Mei 20 anaongeza kusema kuwa uchaguzi huo umedhihirisha kukuwa kwa umahiri wa kisiasa wa Burundi huku akiahidi kuwasikiliza raia wote Burundi bila ubaguzi.

”Tumejipa hadhi mbele ya Warundi na dunia, kwa kuionesha kuwa tulipofikia hatufundishwi tena demokrasia bali tunaweza kuwafundisha wengine. Hivyo ninaahidi kuwa nitawasikiliza wananchi wote bila ubaguzi ili maoni yao yaweze kulijenga taifa. Hivyo naitaka jumuia ya kimataifa kuiunga mkono hatua hii ya kupendeza tuliyoifikia,” anasema Ndayishimiye.

Pia Ndayishimiye anamshukuru mtangulizi wake, Rais Nkurunziza kwa hatua yake ya kuridhia alivyoridhia kuanzisha mchakato huu wa uchaguzi. Ndayishimiye anawataka wakimbizi kurudi nyumbani kuchagina katika ujenzi wa taifa.

KAULI YA RWASA

Naye Agathon Rwasa ambaye ni mgombea wa upinzani aliyechukua nafasi ya pili, kwa kupata asilimia 24 ya kura, anasema hatokubaliana na matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Burundi.

Rwasa anaahidi kuyafikisha malalamiko yake kwenye mahakama ya kikatiba na endapo hatotendewa haki basi ataelekea kwenye mahakama ya Jumuia ya Afrika Mashariki.

Tayari Tume ya Uchaguzi inakutana na wawakilishi wa vyama vya siasa ili kuwateuwa wabunge 21 kutoka katika jamii ya Watutsi na Watwa 3 watakaojumuishwa katika bunge la taifa ili kuleta usawa wa kikabila. 

NDAYISHIMIYE NI NANI?

Ndayishimiye aliyehudumu kama Jenerali katika jeshi, amekuwa Katibu wa chama tawala cha CNDD-FDD tangu mwaka 2016. 

Kabla ya kuchaguliwa kuwa rais, alikuwa mkuu wa Idara ya Masuala ya Kijeshi chini ya Ofisi ya Rais Nkurunzinza.  Pia alihudumu kama waziri wa Masuala ya Ndani katika kipindi cha mwaka 2006-2007.

Ndayishimiye anayefahamika kwa jina la utani kama ”Neva” alihudumu katika jeshi kwa muda mrefu kabla ya kujiunga katika siasa. 

Alikuwa mwanafunzi mdogo katika Chuo Kikuu cha Burundi mwanzoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwaka 1993.

Marafiki wa Ndayishimiye, wanamtaja kuwa mtu mwenye fikra huru lakini wakati huo huo mwenye hasira za haraka. 

Mmoja wa marafiki zake anasema Ndayishimiye ni mtu wa matani mengi na hupenda sana kucheka.

Mjumbe mmoja naye anasema kuwa rais huyo mpya ameonesha uwazi na uaminifu tofauti na majenerali wengine lakini atakabiliwa na wakati mgumu atakapoanza kutekeleza majukumu yake.

Tofauti na Nkurunziza ambaye wengi wamemtaja kuwa mtu katili, Ndayishimiye hajahusishwa na dhuluma za hivi karibuni zilizofanywa na chama cha CNDD-FDD dhidi ya wale wanaoonekana kuwa wakosoaji. 

Hata hivyo hakuingilia kati kutuliza ghasia zilizolikumba taifa hilo kufuatia uchaguzi uliokumbwa na utata wa mwaka 2015.