Home Makala KARIBU DK. BASHIRU ALLY, YAFANYIE KAZI HAYA…

KARIBU DK. BASHIRU ALLY, YAFANYIE KAZI HAYA…

5721
0
SHARE

MUDHIHIR MUDHIHIR


Tulizoea kukuona na kukusikia kupitia vyombo vya habari ukichambua kwa kina na weledi mkubwa tata na songosongo zenye kutamalaki siasa za ndani na za nje ya nchi yetu. Leo na pengine bila hata chembe ya matarajio umejikuta ndani ya kitovu cha chama kikongwe cha siasa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni zao la muungano wa vyama vilivyotuletea uhuru na ukombozi wa jirani zetu. Naam! Ukitaka kuujua uhondo wa ngoma ingia ucheze.

Karibu Dakta. Ninawapa kongole aliyekupendekeza na waliyokuidhinisha kuhudumu katika nafasi uliyonayo. Samaki wamempeleka baharini. Sikusudii kusema kuwa waliyokutangulia walipwaya katika nafasi hiyo. Hata kidogo! Bali nisilo na mhali nalo kulisema  ni kwamba mabadiliko haya yataleta uhaulishaji chanya ndani ya utendaji katika CCM. Watakaopenda kunishangaa kwa kauli au kwa kunitumbulia macho ruksa. Utendaji ndani ya CCM unahitaji mageuzi.

Hapana ubishi kuwa mabadiliko ndani ya CCM si jambo geni. Kila baada ya miaka mitano huwa na chaguzi zinazobadilisha uongozi. Kila muongo mmoja anakuwepo Mwenyekiti  wa Taifa mpya. Tumeshuhudia mabadiliko ya katiba, miongozo na sera. Tumeshuhudia pia mabadiliko ya watendaji katika ngazi mbalimbali. Dakta Bashiru umekuja na kitu kipya ambacho ni mabadiliko ya utendaji.

Tumekusikia uliposema tena kwa sauti na si kwa kunong’ona kwamba watendaji waache kuwa wasemaji kwenye majukwaa na mbele ya vyombo vya habari. Umeianza safari yako kwa mguu sahihi na kwa hakika iso shaka utenzi wa watendaji wengi ndani ya CCM umetokana na vigezo vya ustadi wa kushambulia jukwaa kwa kupanga vina na mizani, matumizi ya tamathali, nahau, misemo, mafumbo na vitendawili. Na baadhi yao ni zawadi.

Mabadiliko ya kiutendaji unayoyatamani Dakta ni muhimu bali yanahitaji mikakati na usimamizi. Yanahitaji nidhamu ya mabadiliko kifikra na nidhamu ya mabadiliko ya mazoea. Mabadiliko ya kiutendaji unayoyatamani Dakta yanahitaji udhibiti wa miungu watu miongoni mwa baadhi ya wenyeviti wa mikoa na wilaya, na miongoni mwa baadhi ya wabunge na madiwani. Ukiketi na watendaji wako utalifahamu tatizo hili kwa undani.

CCM ni chama kikongwe na kikubwa. Ni chama chenye wanachama na wapenzi wengi. Ni chama kilichosambaza mizizi yake katika kila pembe ya nchi yetu. CCM inamiliki rasilimali nyingi kuliko chama kingine chochote cha siasa nchini mwetu. CCM ni kama kinoo cha dhahabu ambacho thamani yake na manufaa yake hujionyesha pale dhahabu inapotumika vizuri. Basi ikiwa CCM ni dhahabu matarajio ya waliyokuteua ni kwamba wewe ni sonara.

Karibu sana Dakta Bashiru Ally. Ninaishabihisha CCM na dhahabu kwa sababu naifahamu fika thamani ya CCM. Lakini dhahabu ili iwe safi hupitia misukosuko mingi chambilecho ingekuwa ina kinywa vingesikika vilio vyake. Dhahadu huchenjuliwa kwa kemikali ikatoswa kwenye tanuru lenye moto mkali ili kupata miche yake kwa umbo na uzito unaotakiwa. Hii ndiyo dhahabu inayovutia kwenye mapambo ya vidani, vikuba, mikufu, bangili, herini, vishaufu na kadhalika.

Lipo tatizo la kufanya kazi kwa mazoea. Katibu hana ratiba ya kazi za siku, juma, mwezi wala robo mwaka. Yupo yupo tu kusubiri labda ratiba ya ziara ya Mbunge au yakiteremshwa maagizo kutoka ngazi za juu. Mkoa haujui ratiba ya wilaya, kinachotendeka katika kata hakifahamiki wilayani, na kata haina habari na kinachoendelea matawini. CCM oyee na Iyena Iyena hadi nyakati za kampeni.

Sikufundishi kazi Dakta. Bali ichague siku moja yoyote uitakayo uishukiye wilaya yoyote utakayoiteua. Uliza mpangokazi walau wa mwezi mmoja tu uone na usikie mambo. Teremka katani ukitazame kitabu cha wageni. Dakta nisikuchoche, huna sababu ya kuteremka hadi matawini. Tunachokiona hapa ni kuwa usimamizi katika utendaji ndani ya chama haupo.

Dakta unasikia kwenye vyombo vya habari wanakijiji wakilalamika dhidi ya serikali ya kijiji chao. Basi malalamiko haya hayajawahi kuwa ajenda katika Kamati za Siasa matawini wala katika Halmashauri Kuu zao. Hali ipo hivyo hivyo kwa Kamati za Siasa wilayani na katika Halmashauri Kuu za wilaya. Chama hakihoji wala hakisimamii miradi ndani ya wilaya zao. Kamati ya Chama ya Madiwani inafanya nini?

Chini ya utendaji wako Dakta Bashiru Ally, waliyokuteua na wapenzi wako wanataraji kuiona CCM imara na uongozi madhubuti. CCM ipambane na vyama vingine bila kupigana. Karibu Dakta katika kuicheza ngoma unayoijua.