Home Habari Karume amka uione Zanzibar uliyoiasisi

Karume amka uione Zanzibar uliyoiasisi

356
0
SHARE
Abeid Amani Karume

Na BAKARI KIMWANGA

AMEKWENDA, hakika hatutomuona tena na sasa ametimiza miaka 48 tangu alipouawa Aprili 7 mwaka 1972.

Tanzania inamkumbuka Abeid Amani Karume ambaye ni muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar aliyezaliwa Agosti 4 mwaka 1905 katika Kitongoji cha Pongwe katika Mudiria ya Mwera, ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia ya watoto watano wa bwana Amani Karume na Bibi Amina binti Kadir (Kadudu).

Mara tu baada ya kuzaliwa kwa Afro Shirazi Februari 5 mwaka 1957, Abeid Amani Karume alichaguliwa kuwa Rais wa chama hicho, mwaka 1947 kuliundwa Serikali za Mitaa na Baraza la Manispaa lilianzishwa 1954. 

Abeid Karume alichaguliwa kuwa Diwani  ambapo Juni mwaka 1954 alikwenda nchini Ghana kuhudhuria sherehe za Uhuru wa Taifa hilo, safari hiyo ilikuwa ni mwaliko wa kiongozi wa nchi hiyo, Kwameh Nkurumah kwa vyama vyote vya kupigania Uhuru barani Afrika.

Abeid Karume alipendekezwa na Chama cha ASP kuwa mgombea wa kiti cha Baraza la Kutunga Sheria wa Jimbo la Ng’ambo, katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa Zanzibar wa 1957 ambapo alishinda kiti hicho kwa kura 3,328 dhidi ya wapinzani wake Ali bin Muhsin Barwan wa ZNP aliyepata kura 918 na Ibuni Saleh mgombea binafsi aliyepata kura 55, baadaye uchaguzi wa mwaka wa Januari mwaka 1961 Karume alichaguliwa tena kuwa mjumbe wa baraza la kutunga sheria katika Jimbo la Jang’ombe katika uchaguzi huo wa pili.

Mara tu baada ya kumalizika uchaguzi huo wa mwaka 1961 uliokuwa na utatanishi Abeid Amani Karume alichaguliwa kuwa Waziri wa Afya na Mambo ya Kienyeji katika Serikali ya pamoja ya miezi sita.

Uchaguzi Mkuu wa tatu wa Zanzibar ulifanyika Juni 1 mwaka 1963. Karume alichaguliwa tena kuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria katika Jimbo la Kwahani na Jang’ombe, akiwa Waziri wa Afya.

Pia alishughulikia Afya, Ajira,Ujenzi wa Nyumba, Serikali za Mitaa na Serikali za Wilaya . Baada ya kuundwa Serikali ya Waziri Mkuu Muhammed Shamte kufuatia uchaguzi wa 1963, Abeid Karume aliteuliwa kuwa kiongozi wa upinzani katika baraza la kutunga sheria.

SABABU ZA MAPINDUZI

Kwa mujibu wa wanahistoria wa Zanzibar wanaeleza kwamba Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yalikuwa ni kilele cha mapambano ya Wananchi wa Zanzibar dhidi ya Usultan na ukoloni wa Waingereza. 

Mapambano hayo ya kujikomboa yalikuwa kama vuta nikuvute baina ya Mabwana watawala walio wachache na Watwana walio wengi, jambo muhimu lililojitokeza kwa wakati wote huo ni hamu ya wananchi wa tabaka la chini walio wengi kutaka kujikomboa na kujenga jamii iliyo huru kutoka minyororo ya ukoloni, ukabila na unyonyaji. 

Kwa upande mwingine harakati hizo zilipata mwako mpya na sahihi baada ya kujitokeza Abeid Karume aliyejitolea muhanga kuwaunganisha wananchi kwa rangi, dini na kabila zote katika mstari mmoja dhidi ya Ukoloni na Unyonyaji, vuta nikuvute hiyo ilikuwa ni kiini cha harakati za kisiasa zilozoishia kwa kukata minyororo ya matabaka na ubaguzi kwa misingi ya kipato, rangi na kabila katika jamii ya Zanzibar Januari 12, 1964.

JE MISINGI IMEIMARIKA

Naam kwa muda wa miaka 28 tangu alipoondoka Mzee Abeid Aman Karume hasa baada ya genge la wapinga Mapinduzi ya Zanzibar lililopanga njama hadi kumuua sasa bado nchi imekuwa ikishuhudia mabaki chuki, uhasama hasa yanayochangiwa na purukushani za kisiasa.

Hilo linakwenda kinyume na misingi ya Karume, ambaye aliasisi sera makini, uongozi bora, siasa safi na ustawi wa maisha ya watu ulioshamirisha maendeleo ya kisekta chini ya ASP.

Hata muasisi huyo wa Mapinduzi na Muungano wa Tanzania anabaki kama kielelezo muhimu kwa vizazi vyote kikiwemo kizazi cha sasa na vijavyo, vitaendelea kusoma, kuhifadhi na kufuatilia historia ya ASP pamoja na harakati zilizoleta ukombozi hadi kufanyika mapinduzi matukufu.

Ingawa miaka 48 imepita tangu rais huyo kuuawa, Watanzania bado wanaukumbuka msiba wa kumpoteza Mzee Karume ambaye maisha yake yalidhulumiwa kikatili.

Mzee Karume anakumbukwa na kuishi wakati wote kihisia kwa kuamini kilichokufa ni kiwiliwili chake, fikra, malengo na shabaha za Serikali ya ASP bado zingali zikidumishwa kwa lengo la kuleta ustawi wa maisha ya Watanzania wote.

Leo mzee Karume hayupo lakini Zanzibar aliyoiasisi ipo huku ikipita kwenye misusuko ya kiasiasa dhidi ya kundi moja likiona linadhulumiwa na lingine kwa kile tu kinachotajwa ni nani mwenye haki.

Ndio Zanzibar ni kisiwa cha wana Mapinduzi ambao sasa wamesaidia kukomaza fikra tunduizi kwa kuwa na kasi kubwa ya maendeleo katika nyanja zote muhimu hasa maji, elimu, miundombinu na hata mawasiliano.

Ninatamani Karume aamke aje aione Zanzibar aliyoiacha na majumba ya Michenzani aliyoyajenga pamoja na majongo la Mjerumani ya Kikwajuni, lakini sasa imependeza kwa kuwa na majengo makubwa ya kuvutia lakini pia ikiwa na namba kuwa na wananchi zaidi ya milioni moja wakiishi katika visiwa hivyo.

Si hilo tu sekta ya elimu, huduma za maji na hata mawasiliano imekuwa ni ajenda muhimu ya kuifanya Zanzibar izidi kujenga heshima yake kiasi kwamba inavutia kwa kila mgeni anayefika kwa kutamani kutembea au kuishi kabisa.

Karume amka umuone Dk. Shein akishirikiana na Rais Dk. John Magufuli wakiimarisha Muungano kwa kuhakikisha usawa unakuwapo pande zote mbili za nchi yetu na watu kuheshimiana kwa misingi ya kiudugu na umoja.

Wapo waliotamani miaka 48 ya kifo cha Mzee Karume itumike kama njia ya kielelezo cha kushudia malumbano yasiyo na tija eti kwa vile wanao ni wenye kuonewa dhidi ya wale wengine.

Lakini Watanzania nja Wazanzibari kwa ujumla leo wanamkumbuka Karume huku wakiishi na hata kuuona pasi na kuangalia huyo ni Mbara na yule ni Mzanzibari.

Ili nchi iweze kulinda tunu yake ni lazima iwadhimini na kumuenzi Karuma na Nyerere kama kielelezo cha umoja wetu ambao sasa umekomaa na kuwa na mfano wa kuigwa kwa mataifa mbalimbali duniani.

Wapo waliojaribu kuungana lakini wamejikuta wakiishia njiani ikiwamo kama nchi za Ulaya ambapo sasa Uingereza ipo pembeni iliyokuwa Urusi yenye nguvu sasa ipo vipandevipande lakini kwa Tanzania iko imara kuliko ilivyo kuwa jana.

Hakika Watanzania tunaadhimisha miaka 48 ya kifo cha Karume huku tukiwa na somo la kuimarisha umoja na mshikamano katika nchi yetu.