Home Makala KASHFA YA UFISADI YAIYUMBISHA SERIKALI YA MSUMBIJI

KASHFA YA UFISADI YAIYUMBISHA SERIKALI YA MSUMBIJI

629
0
SHARE
Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji.

MAPUTO, MSUMBIJI


HATIMAYE ukaguzi wa kina wa mahesabu kuhusu kashfa ya mikopo iliyoikumba Serikali ya Msumbiji sasa umekamilika.

Mikopo hiyo ya Dola za Kimarekani bilioni 2, fedha ambazo Serikali ya Msumbiji ilikopa kwa usiri , ilisababisha Shirika la Fedha Duniani (IMF) kusitisha misaada yake kwa nchi hiyo.

Ilidaiwa kwamba, serikali ilichukua mikopo hiyo kwa matarajio ya kuirejesha kutokana na fedha ambazo zingepatikana kutokana na mauzo ya gesi asilia iliyopatikana kwa wingi nchini humo.

Wakaguzi wa mahesabu kutoka kampuni ya Kroll ya New York, Marekani wamekabidhi ripoti yao kwa serikali Ijumaa iliyopita.

Wakati huo huo, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa nchi hiyo amesema katika taarifa yake kwamba, ofisi yake itaendelea na kazi ya kutathmini hiyo ripoti na kwamba itatangaza yaliyomo katika ripoti hiyo haraka iwezekanavyo.

Kashfa hiyo iliibuka mwishoni mwa mwaka 2015, baada ya kubainika serikali ilikuwa imekopa fedha nyingi – ikiwamo mikopo mitatu ya jumla ya Dola 2 bilioni kati ya 2012 na 2014 ili kugharamia mradi wa kulinda mazingira katika maeneo ya pwani ya nchi hiyo.

Tume ya Uchunguzi ya Bunge mwezi Desemba ilisema serikali ilikuwa imekiuka sheria zake pale iliposhindwa kuomba kibali kutoka Bunge ili kupatiwa mikopo hiyo, na kuongeza kwamba serikali ilikuwa imevunja sheria za Bunge na Katiba ya nchi hiyo.

Baadaye serikali ilieleza kwamba, mikopo hiyo ilitumika kugharamia meli za jeshi na zana nyingine za kijeshi na kwamba (serikali) haikutangaza kwa sababu lilikuwa ni suala la usalama wa nchi.

Kashfa hii iliuathiri sana uchumi wa nchi hiyo, ambayo hadi hapo ilikuwa tayari imeathiriwa kutokana na kuanguka kwa bei ya bidhaa zake katika masoko ya dunia, hali ambayo nayo iliibua mgogoro mkubwa wa kifedha nchini humo tangu kumalizika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992.

Nchi fadhili kadha zilizokuwa zikiisaidia bajeti ya nchi hiyo pamoja na IMF na Beki ya Dunia zilisitisha misaada kwa nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika. Hivyo kufanya ukaguzi wa kina kuhusu mikopo hii ya siri iliyodaiwa kuwa na harufu ya ufisadi lilikuwa ni sharti kuu la kurejesha misaada hiyo.

Mwakilishi wa IMF nchini Msumbiji, Ari Aisen, alisema wiki iliyopita kwamba, IMF inatarajia kwamba ripoti hiyo ya ukaguzi kutoka kampuni ya kimataifa ya ukaguzi itawekwa hadharani na kukabidhiwa Mwendesha Mashitaka Mkuu.

Mikopo hiyo, ambayo serikali inashindwa kuirejesha ilichukuliwa kwa matumaini kwamba nchi ingepata faida kubwa kutokana na ugunduzi wa matrilioni ya futi mraba za gesi asilia nje ya pwani ya nchi hiyo, lakini hadi sasa mapato kutoka maliasili hiyo bado hayajaonekana.

“Serikali ilidhani ingelipa mikopo hiyo kutokana na mapato ya gesi asilia,” anasema Borges Nhamire, mtaalamu na mwanaharakti mmoja wa vita dhidi ya ufisadi kutoa taasisi ya CIP.

Vyama vya upinzani nchini humo vimetuhumu Rais wa zamani wa nchi hiyo, Armando Guebuza na wa sasa, Filipe Nyusi, kuwa wanahusika moja kwa moja kwa ufisadi katika kadhia hiyo.

Mwaka jana, Mkurugenzi Mkuu wa IMF Christine Lagarde alimtaka Rais Nyusi kuruhusu ukaguzi kutoka kampuni huru ya ukaguzi kutoka nje kuchunguza yaliyojiri katika sakata hilo hadi kupelekea IMF na Benki ya Dunia kusitisha ufadhili wao kwa Msumbiji.

Bosi huyo wa IMF alimwambia Rais Nyusi mjini Washington walipokutana mwishoni mwa mwaka jana kwamba, nchi yake inahitaji jitihada zaidi katika kuboresha uwazi baada ya serikali yake kudaiwa kulificha Bunge mikopo ya Dola za Kimarekani zaidi ya 1.4 bilioni.

Mwezi Aprili mwaka jana, IMF na Benki ya Dunia zilisitisha misaada kwa Msumbiji, baada ya kubainika kwamba ilitumia dola 40 milioni kununulia ndege mpya kwa matumizi ya rais.

Na mwezi uliofuatia kundi la nchi 14 wafadhili, zikiwamo Uingereza, Canada, Umoja wa Ulaya (EU), Ufaransa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nazo pia zilikata misaada yake kwa Msumbiji, nchi ambayo inategemea sana fedha za wafadhili katika kufanikisha bajeti yake.