Home Latest News KAULI YA NDUGAI INATIBU UNAFIKI

KAULI YA NDUGAI INATIBU UNAFIKI

1122
0
SHARE

NA VICTOR MAKINDA 

KUNA wasomaji mlinitaka kuandika uchambuzi juu ya kile kinachotokea nchini Zimbabwe. Sitafanya hivyo leo, panapo majaaliwa nitafanya hivyo wakati ujao. Kwanini? Hii ni kwa sababu Tanzania kama Taifa tuna mengi sana ya kuyashikia bango yanayotusibu, kuhamasika kuandika na kuzungumza siasa za Zimbabwe na mahali pengine duniani kutatufanya tuache na kusahau masaibu yanayotusibu kama Taifa.  Tuendelee..

Unafiki ni ugonjwa mbaya sana. Unafiki maana yake ni kutenda jambo usilolisema na kuliamini au kutotenda na kutosema jambo unaloliamini. Mnafiki daima anakwenda kinyume na ukweli. Hii ni tabia ya binadamu walio wengi. Ugonjwa  huu     wa unafiki wanaugua watu wote mahali pengi duniani, Tanzania tumo kwenye nafasi nzuri kwa kuwa na wagonjwa wengi  wanaoumwa unafiki.

Tabia hii ya unafiki ina madhara makubwa katika jamii, kwani siku zote unafiki hukinzana na ukweli. Kutarajia matokeo chanya wakati upo kinyume na ukweli ni sawa na kutarajia kuvuna mchicha kwenye shamba ulilopanda bangi.

Ndiyo, zipo sababu nyingi za mtu kuwa mnafiki. Moja ya sababu hizo ni woga. Woga huo unaweza kuhofu    kupoteza madaraka au mali. Pia woga huo unaweza kuwa kuhofu kupoteza fursa au kutengwa na kikundi au chama, au taasisi fulani. Wanafiki wapo makazini, nyumbani, mitaani, bungeni na hata kwenye mabaraza ya mawaziri. Wanasiasa walio wengi wanaangukia hapa. Wanasiasa walio wengi wanaugua ugonjwa wa unafiki.

Sijasema wanasiasa wote la hasha. Wapo wanasiasa safi ambao wanauishi ukweli. Lakini walio wengi wao ni wanafiki. Naam, wanasema wasichokitenda na kukiamini na wanaamini na kutenda wasichokisema. Hii huenda ni kwa ajili ya hofu kuu iliyotamalaki miongoni mwao,     wanahofu kuwa watawaudhi watawala na wenye mamlaka ambao kimsingi ndio waamuzi wa kesho yao kisiasa.

Wanahofu watatengwa na kubaguliwa na hata kufukuzwa katika mifumo inayowapa kura na kula. Wanafiki wote huangalia kwanza matumbo yao. Ukweli ulivyo wanasiasa wanafiki kamwe hawafikirii kundi kubwa la wahitaji.     Hawawathamini waliowapa dhamana.     Hawathubutu kuwaudhi mabwana wao. Kwao ndiyoooo ni jibu sahihi hata kama kuna jibu la hapana ambalo ndilo linalostahili.

Tabia ya unafiki ni mbaya na inafifisha maendeleo. Maendeleo yanataka ukweli na uwazi. Maendeleo yanataka kuiita rangi kwa jina halisi ya rangi hiyo na si vinginevyo. Wanafiki nyekundu huiita nyeupe na nyeupe huiita nyekundu. Wanakfi ni wapika majungu na wafitini wakubwa. Wanafiki hawaishi kujikomba. Wao kesho yao ni salama pale wanapojikomba na kujisogeza karibu na mifumo kwa kuongea wasichokiamini.    Wanafanya hivyo wakijua wazi kuwa rangi hizo si halisi. Wanahofu wakiita nyeusi kwa kuwa ni nyeusi watawaudhi wanaowawezesha. Wanaihofu mifumo itawatema.

Mjini Dodoma hivi karibuni katika Bunge lililoisha, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muunganio, Job Ndugai, amewataka wabunge kufunguka na kuchangia kwa uwazi katika mijadala yenye tija kwa    Taifa. Ndugai akionesha kufurahishwa na mchango wa Mbunge Peter Serukamba (CCM), aliwataka wabunge wa CCM wafunguke kujadili hoja na si kujielekeza kupongeza zaidi. Ndugai alinukuliwa akisema katika mambo ya msingi, wabunge wasijifunge funge kwa kuwa ni wana CCM. Aliongeza kusema kuwa CCM haitaki mipango mibovu, aliwaambia wabunge wanatakiwa kusema kwa lengo la kusaidia wizara na Serikali kwa ujumla wake ili tusonge mbele kimaendeleo. Spika Ndugai aliwataka wabunge wanapomba kuchangia, kujiandaa kwa hoja na si kuunga tu mkono kwa kusema ndiyo.

Msomaji unajifunza nini hapa kutokana na maelezo, makanyo na mwongozo huo wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya wabunge wenzake hususan wa Chama tawala (CCM). Ukweli ulivyo ninampa kongole Spika Ndugai. Amekata mzizi wa fitina na kuusema ukweli ulivyo.    Katika hili Ndugai hakuonesha chembe ya unafiki. Amesema ukweli.

Ndiyo, baadhi ya wabunge wa chama tawala, CCM, wamekuwa wakiwakera na kuwashangaza  mno wananchi wanaowawakilisha. Wananchi walio wengi hawaridhishwi na namna wabunge hao wanavyochangia, kukosoa na kupinga hoja za Serikali. Wengi wa wabunge hao kazi yao kubwa ni kupongeza tu na kusema ndiyo kwa chochote kinacholetwa na Serikali bungeni. Ni nadra sana kusikia wabunge hao wakijenga hoja kinzani dhidi ya ama iwe miswada au hoja mbalimbali za Serikali. Na tujiulize sasa kazi ya mbunge ni ipi? Ni kusema Ndiyoooo?

Kwa mujibu wa katiba mbunge ana kazi kuu tatu. Ya kwanza kuwawakilisha wananchi wake anaowaongoza na kuyasemea matatizo yao serikalini.  Kutunga sheria na kuisimamia serikali.    Swali  ni je, utaisimamiaje serikali pasipo kuieleza ukweli? Usimamizi ni pamoja na kukosoa na kusema hili hapana. Hili sawa. Hapana kwa sababu a,b c. Na ndiyo kwa sababu hii na hii. Lakini hatuoni hili likifanywa na wabunge wetu hususan wa CCM. Wapo wabunge wachache wa CCM wenye uthubutu. Moja ya wabunge hao ni Hussein Bashe, Mbunge wa Nzega Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi     (CCM). Pia Peter Serukamba na Nape Nnauye wanaonesha tofauti sana ukilinganisha na wabunge wengine wa chama tawala.

Wabunge hawa wamejipambanua kwa hoja zao ambaZo hazina uchama. Wao wawapo bungeni wakaitwa kuchangia huchangia kwa sura na nmna iliyo kweli. Hawana chembe ya woga na wamekuwa ni wenye msimamo juu ya kile wanachokiamini. Aina hii ya wabunge ndiyo Tanzania inayoitaka na ndiyo Spika Ndugai anayoitaka, sina shaka ndio hata Rais wetu kipenzi cha Watanzania, Dk John Magufuli anaitaka.  Kwa bahati mbaya, wapo wanaowatazama kwa sura tofauti wabunge hawa. Wengine wameanza kuwaita wasaliti.     Swali, wanasaliti nini?

Rais wetu Magufuli anayo dhamira safi ya kuijenga nchi hii kisiasa na kiuchumi, mihimili mingine ya dola ikiwa ni pamoja na mhimili muhimu kabisa wa Bunge, una kila sababu ya kumsaidia Rais wetu kutimiza malengo yake hayo mazuri. Kama wabunge hawatakuwa wakweli na wakabaki kupongeza kila kitu watamkwamisha Rais wetu kutimiza ndoto yake ya kuipeleka Tanzania kwenye neema. Wabunge ambao wanadhani ukiwa CCM basi mdomo wako na ufahamu wako unafungwa wataikwamisha Serikali. Wanaodhani kuwa kupongeza ndiyo kuonekana mzalendo na mfia chama ni wabunge wanaozorotesha maendeleo yetu.

Kwanza nilidhani ni wananchi tu kuwa ndio wanaokerwa na hatu hii. Kumbe hata Spika wa Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, ambaye ni mbunge mkongwe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, anakerwa na tabia hii ya wabunge wa CCM ya kuitikia ndiyo pasipo kuwa na hoja zenye kujenga.

Kwanini wabunge wa CCM hawafunguki?

Yeyote asiyefunguka lazima atakuwa amefungwa?     Hii ndiyo sababu anahofu au anashindwa kufunguka/kujifungua. Tujiulize swali, nani kawafunga wabunge wa CCM? Nini kimewafunga wabunge wa CCM mpaka wanashindwa kufunguka kuchangia hoja za msingi kabisa kwa kujenga hoja zenye tija na matokeo yake wamebaki kuwa ni wenye kupongeza na kuunga mkono hoja?

Huenda CCM imewafunda wabunge wake wasiikosoe Serikali wala kukosoa hoja za serikalini wawapo bungeni. Nimesema huenda, kwa kuwa sina hakika kama CCM inaweza kufanya hivyo. Ikiwa CCM inafanya hivyo basi itakuwa inajiua bila kujua.     Kama Chama CCM kinafanya hivyo, kinawakataza wabunge wake kutoa hoja kinzani dhidi ya hoja za Serikali bungeni, basi chama hicho kinafanya makosa makubwa mno.

Matokeo ya makosa hayo ni chama kutofanikiwa kutimiza ilani yake. Ili ilani hiyo nzuri ya CCM  itekelezwe vizuri, inahitaji sana michango na hoja za wabunge kwa kuwa hawa ndio wawakilishi wa wananchi na ndio wanazifahamu kwa ukaribu changamoto za wananchi.

Ukweli ulivyo wabunge wetu wanatakiwa kuwa huru kuchangia kwa staha na heshima huku wakibaki na nguvu za hoja zenye tija kwa maendeleo.  Woga na hofu ya kuitwa msaliti au kufukuzwa chamani ni mauti kwa maendeleo ya nchi yetu. Ni vema wabunge wakafanya kazi iliyowapeleka bungeni. Kuchangia kwa mtindo wa kunyemelea uteuzi na uoga uoga ni aina ya unafki.     Unafki ni kikwazo cha maendeleo.