Home Makala Kauli za chuki, ubaguzi zikemewe

Kauli za chuki, ubaguzi zikemewe

1087
0
SHARE

DK. HELLEN KIJO BISIMBA

BAADA ya kukaa kwa mwaka mzima nikiwa likizo baada ya kustaafu, leo nimeona nianze kuyaangazia masuala mbalimbali yanayoendelea nchini na hata nje ya nchi.

Nia kubwa niliyo nayo ni kuona ni kwa vipi sisi Watanzania tutaendelea kuwa vinara wa amani na upendo si kwa raia wa Tanzania tu bali hata kwa raia wa kigeni nchini mwetu na nje ya nchi.

Wakati naangaza nianzie wapi nilikutana na maneno haya katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram wa Shirika la  BBC Swahili wakimnukuu Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta aliyekuwa katika safari hapa nchini kumtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Joseph Magufuli napenda kunukuu:

“Nimekuja hapa Chato kama ndugu, jirani na rafiki. Na hii ndio Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sisi tunaitaka, sio jumuiya ya watu ambao wana fikra ndogo za zamani.

“Sisi tunataka Jumuiya ya watu wenye maono ya mbele ambao wanajua kwamba Kenya ikitajirika Tanzania imetajirika , Tanzania ikitajirika Kenya imetajirika. Watu ambao hawawagawi watu kwa mambo madogo madogo ambayo hayasaidii”.

Nilisoma maneno haya nikiyatafakari mambo yanayoendelea nchini kwetu na hata nchi za jirani hadi nchi za mbali hasa katika eneo la kuwagawa watu kwa mambo madogo madogo.

Ulimwegu tulio nao sasa ni ulimwengu wa utandawazi. Dunia imefupika na hivyo watu wako karibu zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Sasa hivi ni rahisi mtu kufika Afrika Kusini, Ulaya na hata China kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Wakati mwingine watu hufika si kimwili bali kwa njia ya mtandao na teknolojia.

Hivyo, ukisikia kauli za chuki na za kibaguzi kama ambazo tunazisikia dhidi ya watu wasio na mrengo mmoja wa kisiasa, ambapo naiona sana hapa nchini kwetu nashangaa sana kuwa tunataka kuijenga vipi nchi hii iwapo hatushikani mikono hata katika tofauti zilizopo za kiitikadi au hata za kidini na zinginezo.

Dunia ilivyo inahitaji tuyaangalie yajayo kwa pamoja ndio maana huko Ulaya walijiunga kuwa Jumuiya moja ya Ulaya pamoja na changamoto zake.

Yule Mbunge wa Kenya wa Jimbo la Starehe, Charles Njangua aliyetoa matamshi ya chuki dhidi ya wageni wanaoishi nchini mwao alilaumiwa na hata nchi yake ilitoa kauli kuyakana matamshi hayo na hata Bunge la nchi hiyo liliyakana matamshi hayo.

Huenda kutokana na kujiondoa katika matamshi hayo Rais wa nchi ya Kenya akaona afanye safari ya kindugu, kirafiki na kijirani. Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania nao hawakupendezewa kabisa na kauli ile kwani nao walilaani na wakataka Serikali yetu ipate ufafanuzi kutoka Serikali ya Kenya na pia kuwahakikishia usalama watanzania wanaoishi Kenya. Watanzania pia kupitia mitandao ya kijamii walizungumzia sana kauli ile.

Hili suala la chuki na ubaguzi halikubaliki kwa vile kama anavyosema Rais Kenyatta tuko katika kuijenga Jumuiya ya Afrika Mashiriki.

Hii Jumuiya inaanza na nchi zetu, iwapo katika kila nchi ya jumuiya tutaweza kupendana na kuheshimiana itakuwa rahisi sana kuendeleza hali kama hiyo hata kwa nchi jirani tunazojaribu kujijenga tuwe kitu kimoja.

Hapa nchini siku za karibuni tumesikia kauli za baadhi ya wakuu wa wilaya wakifukuza watu wakisema hawataki kumwona mtu fulani kwenye wilaya yake.

Kauli kama hizi nazo ni za chuki na za kibaguzi kwani Watanzania hapa ni kwao na kwa mujibu wa Katiba hawahitaji visa kuondoka wilaya moja kwenda wilaya nyingine.

Kauli niliyoisikia nyingine ni ya Mkuu wa Wilaya wa wilaya mojawapo huko Tanzania visiwani akimtaka raia aliyetokea Tanzania bara arudi bara mara moja. Nilipofuatilia nikaona kisa ni kuwa raia huyo anashutumiwa kufanya biashara haramu ya binadamu.

Hiyo shutuma kama ni ya kweli kinachotakiwa kama ambavyo wamefanya ni kuchukua hatua za kisheria kwani ipo sheria dhidi ya biashara ya uuzwaji wa binadamu.

Kwa mujibu wa sheria hiyo mtu yeyote atakayekutwa akifanya hivyo atapelekwa mahakamani kujibu mashtaka yake na akibainika kuwa amefanya hivyo basi atahukumiwa kwa mujibu wa hiyo sheria.

Katika sheria hiyo hakuna sehemu inapomtaka mkuu wa wilaya kumfukuza raia huyo. Hii imetokea kwa vile huyo mtuhumiwa ana asili ya bara iwapo angekuwa ana asili ya huko visiwani angefukuziwa wapi? 

Katika suala hili nimeona tayari katika mitandao ya kijamii watu wakianza kuzungumzia maneno ya kuligawa Taifa kama ilivyokuwa kwa kauli ya chuki ya yule mbunge wa Kenya, ambapo watu walianza kuonyesha kuwa wapo wa Kenya Tanzania na hali kama hizo.

Rais Kenyatta alisema tunataka watu wenye maono ya mbele yaani tunaweza kusema watu walio na mtazamo mpana wanaoangalia masilahi mapana zaidi si kuangalia mambo kwa ubinafsi na kwa nia ambayo haijengi bali inabomoa.

Huu ni ukweli mpana ndio maana tuliona waasisi wa hizi nchi zetu walijitahidi kuyaangalia masilahi makuu ya nchi. Na walijaribu hata kuona jinsi gani wataijenga Afrika na si nchi moja moja.

Tukianzia hapa ni makosa sana tunapoona viongozi wanainamia kuangalia pale alipo yeye haiangalii Tanzania anaona wilaya yake, mkoa wake badala ya kuiangalia Tanzania na hatimaye Afrika Mashariki na hata Afrika.

Tuliona jinsi Serikali ya Kenya ilivyochukua hatua za haraka kusafisha kauli iliyotolewa na mtu mmoja pamoja na kuwa ni kiongozi tena mbunge.

Tunapaswa kujifunza pale kiongozi mmoja anapotoa kauli za chuki katika sehemu alipo dhidi ya watu wengine au hata raia wenye kutoa kauli za chuki suala hilo likemewe na ikibidi hatua kali za kisheria zichukuliwe mara moja. Wanapofanya hivyo mara nyingi wanaachiwa tu kiasi kwamba inaanza kuonekana kuwa ndivyo ilivyo. 

Sikuwahi kusikia wakati nakua hapa nchini kauli za watu wakiweka mitazamo na hoja za kikabila. Sasa hivi kauli kama hizo zimeshamiri na hazijakemewa ipasavyo.

Mwalimu Nyerere alitahadharisha masuala ya ukabila kuwa hayako mbali kama yasipokemewa. Ukianza kusikia kauli za kutaja mtu kwa kabila lake, kuwaangalia watu waliopo sehemu fulani kwa kabila lao ni hatari kwa watu tunaodhani tunatakiwa kuwa na mtazamo mpana.

Tanzania ni yetu na ukianza kuingalia kwa undani unaweza kukuta kila mmoja wetu kuna alipotokea tukajikuta hapo tulipo. Kama tumefika hapa tuijenge nchi kwa nia njema, mifumo tuliyojiwekea tuiheshimu. Tuliamua kujenga mfumo wa demokrasia ya vyama vingi tukauweka katika Katiba kabisa. 

Tulikubali kuwa haki za binadamu zitaheshimiwa kwa mujibu wa Katiba hivyo kila mtu ana uhuru wa kuabudu dini aitakayo n.k.

Haipendezi kabisa pale ambapo zipo sheria lakini misingi yake haifuatwi kabisa. Wapo watu wengine wanaoonekana ama wako juu ya sheria au nje ya sheria kiasi kwamba wanatoa matamshi ya chuki ya kibaguzi lakini hatua stahiki hazichukuliwi.

Hizo fikra ndogo alizozisema Rais Kenyatta ni pamoja na kutojali hisia na haki walizonazo watu wengine. Ukosefu wa utu ni janga baya nchini.

Kujenga vidonda ndani ya mioyo ya watu ni hatari ndio maana mjadala ulioendelea katika Bunge la Kenya baada ya mbunge mwenzao kukamatwa kwa matamshi yale, walisema ni vyema masuala kama hayo yazungumzwe ili kuona hali halisi ni ipi na irekebishwe vipi.

Tunahitaji kujihoji kama watanzania kuwanini kimetokea hadi tumefika mahali tulipo ambapo mitazamo siyo ya kindugu, kirafiki au ya ujirani? Bado sijaweza kuelewa jinsi mbunge alivyopigwa risasi akanusurika na akiwa katika matibabu anafutwa kuwa mbunge na zaidi ukimya unaoendelea baada ya hayo.

Hali hii ni hatari kwa mustakabali wetu wote. Kama kuna wakati tulitakiwa kuwa wamoja ni wakati huu kwani dunia itatutazama kiuchumi na hata kijamii, Utu ni thamani ya kweli inayoweza kuzuia  athari ya maneno na matendo ya chuki kati yetu.