Home Latest News Kauli za Masele, Ndugai na umuhimu wa diplomasia

Kauli za Masele, Ndugai na umuhimu wa diplomasia

3512
0
SHARE

NA ABBAS MWALIMU

“Lakini tumelazimika kumtafuta Mheshimiwa Masele kumrudisha nyumbani kuanzia Jumatatu, badala yake amekuwa akionyesha kugoma”

Hii ni sehemu ya maneno aliyozungumza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai aliyoitoa Bungeni Alhamisi 16/05/2019.

Kauli za baadhi ya viongozi mbalimbali nchini kwa wakati huu zimekuwa na changamoto kubwa sana.

Hali hii inaleta sintofahamu kubwa juu ya mwenendo wa siasa zetu na nafasi ya Tanzania katika jicho la kimataifa. 

Wengi tumekuwa tukijiuliza, tunaelekea wapi?

Swali hilo na mengine mengi tunayojiuliza watanzania ndiyo yaliyopelekea mimi kuona haja ya kuandika makala hii inayoelezea umuhimu wa diplomasia.

Kwa nini?

Sababu ni kauli zilizokuwa zikitolewa na viongozi wetu Mheshimiwa Stephen Masele ambaye ni Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP) na Mbunge wa Shinyanga Mjini na Spika Job Ndugai. 

Lengo la makala hii si kuwakosoa bali kueleza umuhimu wa diplomasia katika mahusiano ama ya ndani au ya nje.

Kwa sababu kauli zenye kuleta changamoto masikioni na vichwani mwa watanzania zimekuwa zikitolewa na viongozi wengi sana kwa siku za karibuni hali inayoashiria kwamba kuna kitu hakipo sawa na  nadhani inafaa kukumbushana. 

Ili tuweze kufahamu umuhimu wa diplomasia basi ni vema tuanzie kwenye chimbuko lenyewe la makala hii ambalo ni kauli za waheshimiwa wetu ambazo nitazinukuu kama ifuatavyo.

Katika maelezo ya msingi Spika alisema:

“Baada ya kumwandikia kwamba arudi nyumbani ili aje ahudhurie kwenye kamati ya maadili hapa amekuwa akuhutubia lile Bunge na kusema japo ameitwa na Spika lakini ameambiwa na Waziri Mkuu adisregard wito wa Spika na aendelee tu na mambo yake kule kitu ambacho ni uongo na kutudhalilisha kama nchi. Ni kiongozi ambaye amekuwa akifanya mambo ya hovyo hovyo na ndiyo maana tumemuita kidogo kwenye kamati ya maadili ili atufafanulie huenda labda yuko sahihi.”

Katika hali isiyo ya kawaida baada ya maelezo hayo ya Spika, inaelezwa kuwa Mheshimiwa Masele nae akajibu kwa kutumia akaunti inayodaiwa kuwa ni yake ya mtandao wa Twitter ingawa hakueleza moja kwa moja amemlenga nani. Masele aliandika:

*”I’m not going to deal with pretty stuff like that…I am professional,  coming from the disciplined, highly process-oriented Banking and Telecom, well raised by parents, upholding social values and respect.”* Mwisho wa kunukuu. 

Kwa tafsiri yangu ni kuwa ameeleza kuwa:

‘Mimi siwezi kujishughulisha na mambo madogo kama hayo, ni mweledi, natoka kwenye taasisi ya fedha na mawasiliano yenye utaratibu wa kinidhamu, nimelelewa vema na wazazi, ninasimamia misingi ya jamii na kuheshimiana.’

Jambo la kushukuru ni kwamba Mheshimiwa Masele amerejea nchini hali inayoonesha kuwa ameitika wito wa Spika na hivyo kuondoa dhana ya awali kuwa ‘amekuwa akionyesha kugoma.’

Lakini licha ya kurudi kwake, hapo kabla wakati akifanya mahojiano na DW mheshimiwa Masele alisema:

“Sijagonganisha mihimili na ninatimiza majukumu yangu kikamilifu na kwa weledi. Ni vema taarifa zinazosemw nafanya mambo ya hovyohovyo zingeeleza kinagaubaga ni kitu gani mi nafanya kuliko kusema mambo kwa mafumbo.  Mimi ni mtu ambaye nina heshima zangu, nina wananchi ninaowaongoza, nina familia, nastahili kuheshimiwa.”

Kwa mujibu wa kauli hizo ni wazi kwamba kuna haja ya kuifahamu tafsiri ya diplomasia na sifa za balozi (muwakilishi wa nchi). Nina imani inaweza kusaidia viongozi wetu wengi. 

Ili tuweze kuelewa umuhimu wa diplomasia na hasa sifa za mwanadiplomasia ni vema tuanze na tafsiri ya ‘diplomasia’ kama ilivyoelezwa na Sir Ernest Satow katika kitabu chake “A guide to Diplomatic practice”cha mwaka 1917 kilichoboreshwa baadae kuongoza wigo wa tafsiri. Satow ameandika ifuatavyo:

“Diplomacy is the application of intelligence and tact to the conduct of official business between the Governments of independent States and between Government and non-state actors.”

Kwa tafsiri yangu ni kuwa:

‘Diplomasia ni utumiaji wa maarifa na mbinu na ujuzi katika kufanya shughuli rasmi baina ya Serikali na washiriki wengine wa mahusiano ya kimataifa wasio dola.’

Hapa kuna maneno mawili ambayo yanabeba umuhimu wa diplomasia,  nayo ni intelligence na tact. 

Ili tuweze kuelewa maana iliyolengwa hasa kutokana na msuguano huu wa Spika na Mheshimiwa Masele nitaacha maneno haya katika lugha yake ili tupate msisitizo halisi!

*Intelligence* inaelezwa kama ability to acquire and apply knowledge and skills.

Kwa upana ni kwamba intelligence inahusisha ability to self awareness (kujitambua), cognitive (ufahamu), ability to plan (uwezo wa kupanga mambo), knowledge (maarifa) and understanding (uelewa). Lakini pia huhusisha ability to communicate effectively (uwezo wa kuwasiliana) researching before taking any action (kutafiti kabla ya kufanya maamuzi yoyote).

Neno *tact* limeelezwa kwa Kingereza kama *skill and sensitivity in dealing with others or with difficult issues.*

Kwa upana neno hili limeelezwa kwa lugha hiyo hiyo ya Kingereza kwamba ni *careful consideration of the values and feelings of another so as to avoid offence.*

Nilisema sitatafsiri kwa Kiswahili maneno haya (intelligence and tact) ili kama watanzania wasomi tuweze kupima changamoto halisi iliyopo. 

Tukitazama kile kilichojitokeza baina ya Spika na Masele tunaona kuna changamoto ya *Effective Communication* ambayo ni sehemu ya *Diplomatic Communication Skills* na kukosekana kwa tact hasa kwenye kupima na kutambua *values* kwa kila mmoja wao. 

Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa kuzijua (japo kwa uchache tu kwa sababu zipo nyingi mno) sifa za balozi au mwakilishi. 

Harold Nicolson aliyekuwa mwanadiplomasia wa Uingereza aliainisha sifa saba za mwanadiplomasia, nazo ni, ukweli (trustfulness), usahihi (precision), utulivu (calmness), uvumilivu (patience), kutokuwa na hasira (good-temper), kuwa na adabu (modesty) na uaminifu (loyalty).

De Callieres nae alisisitiza kwa kuandika; “mwanadiplomasia asiye mwaminifu hadumu.”

Kwa sifa hizi za balozi zilizoelezwa na Nicholson na kulinganisha malumbano yanayotokea baina ya viongozi wetu mbalimbali, hatuoni kuwa kuna haja thabiti kwa viongozi kusoma masuala ya diplomasia?

Baadhi ya viongizi wetu wanazungumza ukweli? Wana utulivu? Wana uvumilivu? Na je hawana hasira? Vipi kuhusu modesty?

Tukumbuke kuwa Mheshimiwa Spika alisema kuwa Mheshimiwa Masele alisema uongo kumtaja Waziri Mkuu. Je hatuoni umuhimu wa kujua kuwa viongozi wanatakiwa kuwa na trustfulness aliyosema Nicolson?

Kuna umuhimu wa kusoma diplomasia nadhani kwa mtazamo wangu. 

Katika kuongezea sifa za balozi Petric (2013:127) alitaja sifa zifuatazo:

Utumiaji wa maarifa na mbinu (intelligence),  maarifa (knowledge), ujuzi wa kuchambua mambo (analytical skills),  ukarimu (hospitality), mpole (charm), bidii (diligence), na mwerevu katika kupanga mambo (adroit planning).

Petric (2013) anaeleza kuwa mwanadiplomasia anatakiwa kusema ukweli kwa kiongozi/viongozi wake.

Lakini hatakiwi kusema ukweli wote (Telling the truth but not the whole truth) kwa wale wasio wa nchi yake. Alifafanua De Callieres. 

Pale anapoeleza ukweli kwa nchi yake anatakiwa awe na uthibitisho (facts) kama alivyoeleza tena Petric (2013:128).

“An experienced and intelligent head of mission, someone who is a personality both intellectually and in terms of characters, will report in accordance with the facts,  even though he/she knows that the message may cause displeasure among his superiors. A head of mission who lacks those personal qualities will omit or embellish the bad part of the news. This is the worst and the most damaging side of diplomats-work but sadly occurs time after time.”

Ukweli ni muhimu katika diplomasia na uongo hautakiwi lakini je unaeleza vipi huo ukweli?  Ndicho anachosisitiza Petric (2013), kutumia intelligence na tact ndiyo maana akasema, ‘someone who is a personality both intellectually and in terms of characters.’

Characters ni zile walizoeleza Nicolson na De Callieres. 

Kama viongozi wanakuwa na sifa hizo ndipo unapothibiti ule msemo maarufu wa Sir Winston Churchill aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza miaka ile ya Vita ya Dunia:

“Diplomacy is the art of telling people/someone go to hell in such a way that they ask for directions.”

Lakini zaidi pia mwanadiplomasia/mwakilishi anatakiwa kuwa na sifa za ziada za kiutendaji (functional qualities/duties) ambazo nitazitaja tu kwa ujumla wake nazo ni; duty of care, duty of loyalty,  dignity of risk, duty of commitment, duty of responsibility, duty of accountability and duty of silence.

Katika sifa hizi ningependa kugusia sifa ya ukimya (duty of silence).

Mwanadiplomasia hatakiwi kusema wakati wote, anatakiwa kujua muda gani wa kuzungumza, nini cha kuzungumza na kwa nini anazungumza. 

Hapa ndipo inapokuja ile sifa ya kufanya utafiti kabla ya kufanya uamuzi wowote (researching before taking any action).

Kwa nini kukaa kimya wakati fulani kunasisitizwa katika diplomasia? 

Abraham Lincoln anatujibu kwa nukuu yake kwamba:

“Better to remain silent and be thought a fool than to speak out and remove all doubt.”

Kwa kuwa na sifa hizi mwanadiplomasia humudu kufanya kile alichoeleza Mackay, Harvey yaani *”Swim with sharks without being eaten alive” (1988).

Ndugu zangu, tufahamu kuwa Tanzania ni nchi yenye heshima na nguvu kubwa za ushawishi katika Afrika. 

Heshima na nguvu hii inatokana mchango mkubwa iliotoa hasa katika kusaidia kupatikana kwa uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika ambapo Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi zilizo mstari wa mbele (Front line States).

Tanzania ilichangia pia kuanzishwa kwa OAU sasa AU na hata Kemisheni ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika ilikuwa Tanzania ikiongozwa na  Marehemu Jenerali Hashim Mbita akiwa Brigedia wakati ule. 

Ukitaka kuona ni namna gani Tanzania inaheshimika Afrika tazama picha aliyopiga Julius Malema kiongozi wa chama cha EFF kule Afrika ya Kusini. Tazama sura ya Julius Malema jinsi inavyoonesha bashasha kwa namna anavyotambua na kuiiheshimu nchi ya Tanzania.

Malema aliwahi kuwambia wananchi wa Afrika ya Kusini kwa kuhoji kwamba, “Nchi ambayo ilihatarisha usalama wake kwa ajili ya uhuru wa nchi yetu (Afrika ya Kusini) leo hii raia wake mnawaona maadui?”

Maneno haya yanadhihirisha namna gani wenzetu wanatutazama na kutuchukulia huko nje.

Je sisi tunajitazama hivyo? 

Nguvu ya ushawishi wa Tanzania inathibitishwa na Morgenthau (1973:105) alipoeleza sababu nane za nguvu ya taifa (elements of national power) akataja kuwa ni; geography (jiografia) national resources (rasilimali za taifa),  industrial capacity (uwezo wa kiviwanda), military preparedness (utayari wa jeshi) population (idadi ya watu), national character (uwepo wa kiongozi mahiri), national morale (morali ya wananchi) and quality of diplomacy (kiwango cha diplomasia).

Sifa hizi ziliwahi kuandikwa na Gross (1954:94) ambapo yeye alieleza sababu 7 wakati ule ambazo ni geographical (za kijiografia), economic (uchumi),  demographic (idadi ya watu kwa kutazama jinsia, rika, kiwango cha elimu n.k), military (jeshi) social-political (kijamii na kisiasa), cultural and social (kiutamaduni na kijamii katika muktadha wa saikolojia) na leadership/diplomacy (uongozi au diplomasia).

Katika sifa hizo nitakazia sifa ya quality of diplomacy au leadership/diplomacy.

Tanzania ni nchi ambayo tangu enzi imekuwa ikisifika kwa diplomasia ya kiwango cha juu na uongozi imara. 

Tukumbuke viongozi wengi wa nchi za Kusini mwa Afrika kama Joaquim Chissano, Samora Machel, Eduardo Dos Santos,  Eduardo Mondrane, Felipe Nyusi, Emerson Mnangagwa, kipindi kile walifundishwa diplomasia katika Chuo Cha Diplomasia Kurasini.

Je hatuoni haja kwa viongozi wetu wa sasa kutengenezewa utararibu wa kupitia Chuo cha Diplomasia ili kuondoa ombwe (vacuum) hili?

Tukumbuke kwamba wakati fulani kiongozi mmoja alizungumzia watu wanaofanya mahusiano kinyume na maumbile, nchi za magharibi na Ulaya zikatumia mwanya huo kujaribu kuiyumbisha Tanzania huku zikitambua kabisa kuwa si shehemu ya tamaduni za nchi hii kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 sambamba na sheria zake kama vile sheria ya Muendelezo wa Makosa ya jinai kifungu cha 154.

Hapa kulihitaji weledi wa diplomasia kwa kiongozi husika kwa bahati nzuri ni kuwa msemaji wa serikali alilifafanua lile suala vizuri na kueleza msimamo wa serikali kutokana na kuwa na weledi mkubwa wa diplomasia. 

Tutambue kuwa yapo mataifa duniani yanaitazama Tanzania kwa jicho la tamaa na husuda kutokana na na rasilimali (national resources) ilizo nazo. 

Hivyo basi kwa wakati huu ni muhimu sana kwa viongozi wetu kusoma diplomasia.