Home Habari Kazimbaya adaiwa kufanya kazi vibaya

Kazimbaya adaiwa kufanya kazi vibaya

1929
0
SHARE

NA IBRAHIM YASSIN, MBOZI

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe, Kazimbaya Makwega anahusishwa na upotevu wa mali za umma, hatua inayochangia kufanya kazi vibaya. RAI linaripoti.

Hatua hiyo imekuja baada Baraza la Madiwani kumbana Kazimbaya likitaka kujua sababu ya matumizi mabaya ya fedha na mali za umma.

Madiwani hao wanadai kuwa baadhi ya mali za umma zilizopotea ni gari aina ya Toyota V8, lenye namba za usajili SM 5240 aliyokuwa akiitumia.

Gari hilo linadaiwa kuwa haijulikani lilipo, ingawa na majibu yanayotolea ni kwamba limepelekwa gereji kwa matengenezo na madiwani walipokuja juu, inadaiwa gari hilo lilirudishwa likiwa halina baadhi ya vifaa.

Diwani Kata ya Idiwili (CCM ), Christopher Ntandale alisema anashangaa kuona fedha za matengenezo ya gari zikitolewa pasipo kikao na ridhaa ya madiwani na kwamba licha ya kutoa fedha hizo, pia gari halionekani liliko.

Alishangaa kuona utendaji mbovu wa Mkurugenzi huyo, na kwamba amekuwa akilidharau Baraza na kutoa majibu ya hovyo.

Aliomba kiitishwe kikao maalum cha kumjadili Mkurugenzi huyo kwa kuwa ana mapungufu mengi ya kiutendaji.

Diwani wa Kata ya Ilolo (Chadema), Richard Kibona kwa upande wake alisema mkurugenzi huyo ni mgeni, lakini anakowapeleka siko.

“Tunataka kujua gari na mali zingine za halmashauri zilikoenda, hatuwezi kuendelea kufanya kazi na mkurugenzi wa aina hii,” alisisitiza.

Diwani Viti Maalumu (CCM), Messiah Swella, alisema mkurugenzi ameacha kujadili masuala muhimu,badala yake  anaeleza mambo mengine. Alihoji lilipo gari ambalo lina thamani kubwa na kwamba kiasi cha shilingi bilioni 45 hazijatumika vizuri.

“Halmashauri inaidaiwa milioni 600 na kampuni moja, lakini katika kabrasha fedha, hazijaandikwa. Pia halmashauri inadaiwa zaidi ya bilioni 1.5  ikiwa ni malimbikizo ya madai mbalimbali ya watumishi.”

Mbali na gari, pia yapo madai kwamba kwa kipindi kifupi cha siku 38 za uongozi wake, amewapangua madereva walioajiriwa na kumtumia kibarua kumuendesha.

Inadaiwa pia ameuza eneo lililotengwa kwa ajili ya ukumbi wa kisasa wa Halmashauri na eneo la machinjio la Vwawa na Mlowo ambayo yalifidiwa bila vikao halali kupitisha.

Aidha, Diwani Kata ya Itumpi (CCM), Richard Mahaya alisema kumekuwa na mchezo mchafu unaohusisha uchimbaji wa mchanga unaosomba pasipo kupimwa na kwamba huenda wataalamu wamekula njama ya kuiibia halmashauri.

“Sasa hivi ukienda Mlowo, hupati chumba, kwani nyumba za wageni zimejaa baada ya watu hao kupanga na kufanya kazi ya kusafirisha mchanga nyakati za usiku, sisi kama madiwani tunataka Mkurugenzi pamoja na meza kuu, mtupe majibu sababu ya kushindwa kukusanya fedha, wakati serikali inasisitiza ukusanyaji mapato’’ anasema Mahaya.

Naye Diwani wa Harungu, (Chadema), Maarifa Mwashitete alisema kwa mfumo huo, itakuwa vigumu kwa wilaya hiyo kufikia lengo la makusanyo ya ndani,

“Kwa nini Mbeya Cement iwalipe milioni 20 wakati tunaidai sh milioni 80? Alihoji diwani huyo.

MKURUGENZI AJIBU

Akijibu tuhuma hizo, Mkurugenzi Kazimbaya alisema Halmashauri inadaiwa zaidi ya bilioni tatu, kutokana na madai ya malimbikizo ya mishahara, uhamisho wa watumishi pamoja na kushindwa kesi mahakamani.

“Halmashauri ilikusanya mapato zaidi ya bilioni 43 mwaka 2017, mwaka 2018 imekusanya shilingi bilioni 42, lakini pia Serikali inapata asilimia ya mapato kutoka kwenye kiwanda cha saruji, hivyo tunalazimika kuacha kudai hadi kibali kitakapokuja kutoka kwa Waziri Mkuu, magari ya mchanga yanapimwa mizani, hatuna kibali cha kudai, tuwe watulivu,” alisema.

Mkuu wa Wilaya, John Palingonaye alimuunga mkono Mkurugenzi huyo kwa kuweka wazi kuwa Wilaya haina kibali cha kukusanya ushuru wa mchanga, hadi hapo watakaporuhusiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kuhusu gari, Kazimbaya alisema lipo ujenzi kwenye karakana  ya serikali na kuwa mafundi wanafanya tathimini kujua ukubwa wa tatizo, ili kujua kiasi cha fedha inayotakiwa kwa ajili ya matengenezo.

Alisema mapato yanapungua kutokana na faini kuwa ndogo, wananchi wanazingatia sheria, hivyo suala la kuwatoza faini limepungua na hata mapato yamepungua, na baadhi ya vyanzo vya mapato vimekuwa vikikusanywa na Serikali Kuu.

Awali alisema kitendo cha gari la serikali kupelekwa gereji za mafichoni, badala ya karakana zilizoidhinishwa na serikali kupitia TEMESA hakikubaliki, na kuwa fedha za matengenezo hutolewa pasipo kufuata taratibu za manunuzi ni wizi.