Home Afrika Mashariki KENYATTA KUMKABA RAILA BUNGENI

KENYATTA KUMKABA RAILA BUNGENI

1375
0
SHARE

NAIROBI, KENYA

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema iwapo mpinzani wake katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu mpya utakaofanyika mwezi ujao, Raila Odinga akifanikiwa kushinda, chama chake kitamuondoa madarakani muda mfupi baadaye kupitia Bunge la nchi hiyo.

Uchaguzi mpya utafanyika tarehe Oktoba 17 mwaka huu, baada ya matokeo ya uchaguzi uliofanyika Agosti 8, mwaka huu kubatilishwa na Mahakama ya Juu ya nchi hiyo (Supreme Court).

Katika uchaguzi wa mwezi uliopita Kenyatta alikuwa ametangazwa mshindi kwa kupata zaidi ya kura 1.4 milioni dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga lakini kiongozi huyo wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) alikwenda mahakamani kupinga ushindi wake.

Katika maamuzi yake ambayo yalitikisa nchi na kwingineko Barani Afrika Mahakama ya juu iluitengua ushindi huo kwa kutaja kasoro kadha kwa upande wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zikiwemo ukiukwaji wa Katiba na kanuni katika uendeshaji uchaguzi na majumuisho na kusafirisha matokeo na hivyo kuagiza kurudiwa kwa uchaguzi.

Wakati uchaguzi mwingine umepangwa mwezi ujao (Oktoba 17) tayari kampeni baina ya wawili hao zimepamba moto na kuchukua mkondo wa kujibizana hususan kuhusu Tume ya Uchaguzi (IEBC) ambapo Nasa wanataka tume hiyo ifanyiwe mabadiliko kwanza kabla ya uchaguzi kufanyika.

“Hakuna cha kuogopa kama anavyosema William (Ruto). Hata Raila akichaguliwa, niambie atatawala nchi hii kwa njia gani hasa ikizingatiwa Jubilee tulivyo sasa,” alisema Kenyatta katika mkutano wake mmoja wa kampeni mapema wiki hii.

Aliongeza: “Katika seneti muhula uliopita tulipata tabu kwa sababu ya idadi ya wabunge, leo hii tukiwa na maseneta 41, tunaweza kuendesha shughuli la baraza hilo bila kuwa na mwanachama hata mmoja wa Nasa. Hatuwahitaji.”

Alisema sasa hivi Jubilee ina Wabunge zaidi ya 220, pungufu wabunge 13 tu kufikia theluthi mbili na hii ina maana kwamba chama chake kinaweza hata kubadilisha katiba bila kuwa na Mbunge wa Nasa.

Aliongeza: “Atafanya nini, hata mkimpatia kura zote, atafanya nini? Anaweza kufanya nini? Hata akichaguliwa, tuna uwezo wa ki-Bunge katika kipindi cha miezi miwili au mitatu tu kumtoa.”

Kwa mujibu wa katiba nchini Kenya, Rais anaweza kuondolewa madarakani iwapo tu atabainika kutokuwa na uwezo kimwili na kiakili kuongoza.

Anaweza pia kuondolewa madarakani iwapo atakiuka katiba au akitenda makosa ya jinai chini ya sheria za kitaifa au kimataifa.

Muungano wa upinzani Nasa umelishutumu vikali tamko la Bw Kenyatta na kusema halina busara.

Seneta wa Bungoma Moses Wetangula, na mmoja wa viongozi wakuu wa muungano wa Nasa alisema Uhuru Kenyata alijibu kwa kumwambia Kenyatta asiwadanganye Wakenya, kwani Jubilee, haina idadi ya kutosha ya wabunge kumuondoa Raila madarakani au rais yeyote Yule ma kumkumbusha asome kifungu 145 cha Katiba.

Kiongozi mwingine wa muungano huo Musalia Mudavadi ambaye ni makamu wa rais wa zamani pia amelishutumu tamko la Bw Kenyatta.

Mbali na kutishia kumuondoa madarakani Odinga iwapo atashinda, Rais Kenyatta alipokuwa anahutubu akiwa Ikulu ameushutumu upinzani kwa kutishia kususia kikao cha kufunguliwa rasmi kwa mabunge yote mawili.

Bw Kenyatta amesema mabunge yote mawili yanaweza kuendelea na shughuli zake bila kutegemea wabunge wa Nasa.