Home KIMATAIFA Kiburi cha madaraka kinavyomuumbua Aung San Suu Kyi

Kiburi cha madaraka kinavyomuumbua Aung San Suu Kyi

2406
0
SHARE

NA ERICK SHIGONGO

Waswahili husema ukitaka kujua tabia ya mtu mpe madaraka au cheo. Pia huongeza kuwa, ngoma ikivuma sana yakaribia kupasuka. Hivyo ndivyo unavyoweza kumtafsiri Kiongozi Mkuu wa Chama National League for Democracy (NLD) na mwanaharakati wa haki za binadamu, Aung San Suu Kyi ambaye amepata kuvuma sana kama mmoja wanaharakati waliowahi kupigania demokrasia lakini sasa heshima hiyo imeanza kuporomoka kwa kasi.

Suu Kyi ambaye ni mtoto wa Jenerali Aung San, shujaa wa uhuru na ukombozi wa Taifa la Burma aliyeuawa mwaka 1947. Burma sasa inafahamika kwa jina la Myanmar.

Mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 73, amekumbana na kadhia mbalimbali za kisiasa katika Taifa hilo lililopo kusini mwa bara la Asia kwa kuwekwa kizuizini kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15 na utawala wa kijeshi ulioshika hatamu kuanzia mwaka 1989 hadi 2011.

Misukosuko hiyo ya Suu Kyi ilitokana na harakati zake za kudai demokrasia jambo ambalo lilimpa heshima kubwa katika mataifa mbalimbali duniani na kupata tuzo ya mshindi huyo wa Amani ya Nobel mwaka 1991.

Hata hivyo, ahueni ndani ya nchi hiyo ilianza kuonekana kuanzia mwaka 2012 baada ya Serikali ya kijeshi kuondoka madarakani na mwaka 2015 Chama Kikuu cha Upinzani (NLD) kinachaoongozwa na mwanamama huyo kikafanikiwa kushika hatamu na kumuondoa Rais Thein Sein aliyekuwa akiungwa mkono na jeshi.

 Kwa mujibu wa mfumo wa uchaguzi nchini humo Bunge la Myanmar lilimchagua Htin Kyaw kuwa rais mpya wa nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia, hivyo kuwa rais wa kwanza wa kiraia kwa zaidi ya miaka 50, hatua inayomaliza utawala wa muda mrefu wa kimabavu wa jeshi.

Hatua hiyo ilitokana na Suu Kyi kuzuiwa na katiba ya Myanmar iliyo chini ya jeshi, kugombea urais kwa sababu watoto wake wawili ni Waingereza

Htin Kyaw ni mpambe wa karibu na rafiki wa muda mrefu wa Aung San Suu Kyi, alichaguliwa katika tukio hilo la kihistoria kwa kupata kura 360 kati ya 652 zilizopigwa.

NLD kilimteua Kyaw kuwa mgombea wake na wagombea wengine wawili walikuwa ni Henry Van Thio. Ushindi wa Kyaw ambaye ni mshirika wa Suu Kyi ulidhihirisha kuidhinisha sera yake ya mabadiliko.

Madaraka ya kulevya

Licha ya kusikifika duniani pote kama mmoja wa wanaharakati maarufu waliopigania demokrasia, Kiongozi huyo wa Myanmar anakabiliwa na lawama za kushindwa kulisimamia suala la machafuko nchini humo.

Machafuko hayo yamelazimisha Waislamu wa kabila la Rohingya takriban 370,000 kukimbia kuvuka mpaka wa Bangladesh.

Hata hivyo, mwanamama huyo alikanusha kuwapo kwa taarifa za machafuko hayo na kudai kuwa ni taarifa za uongo ambazo zinalengo la kusaidia maslahi ya magaidi.

Kauli yake hiyo imemsababishia kupoteza heshima yake kwa serikali mbalimbali na wanaharakati wa haki za kibinadamu ulimwenguni, wakiwemo baadhi ya wale waliowahi kutunukiwa tuzo ya amani ya Nobel kama yake akiwamo Nelson Mandela na Dalai Lama.

Hata hivyo, umasikini, ukosefu wa miundombinu na mizozo katika maeneo ya mipakani dhidi ya jamii ya watu wachache imeendelea kulitafuna taifa hilo.

Pia Shirika la Human Rights Watch lilisema sheria nyingi kandamizi nchini humo hazijafutwa ikiwamo sheria ya mawasiliano ambayo inazuia matumizi ya mitandao ya mawasiliano kufanya mambo inayoyataja kuwa ni kutisha, kukashifu au kusababisha usumbufu na vitendo vingine vinavyofanana na hivyo.

Kutokana na hali hiyo hivi karibuni Bunge la Canada limepiga kura kumvua uraia wa heshima aliotunukiwa Aung San Suu Kyi kutokana na ukimya wake dhidi ya uhalifu wanaotendewa jamii ya wachache ya waislam wa Rohingya.

Hoja ya kumuondolea uraia huo wa heshima Aung Sang Suu Kyi ilitolewa na mbunge wa upinzani Gabriel Ste Marie, ambaye alisema uamuzi huo uliopitishwa na bunge ni ishara kubwa na ya maana.

Serikali ya Canada ilimtunuku mwanaharakati huyo wa demokrasia ambaye pia ni alitunukiwa tuzo ya Rafto na Tuzo ya Sakharov mwaka 1990, uraia huo wa heshima unaotolewa kwa nadra mwaka 2007.

Lakini heshima ya Suu kyi mbele ya jumuiya ya kimataifa imeporomoka katika siku za karibuni kutoka na kushindwa kukemea kile kinachofanywa na viongozi wa kijeshi dhidhi ya jamii ya wachache ya warohingya.

Kukamatwa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamiii ambao ujumbe wao katika mitandao hiyo unachukuliwa kuwa kinyume cha maadili na kisheria vimekuwa vikiendelea chini ya serikali ya Suu Kyi.

Aung San Suu Kyi pia ametwaa tuzo ya Jawaharlal Nehru kutoka India, Tuzo ya Kimataifa ya Simón Bolívar kutoka serikali ya Venezuela na mwaka 2011, alitunukiwa tuzo ya medali ya Wallenberg.