Home Makala KIKUNDI CHA ‘MWAKENYA’ KILIITIKISA KENYA

KIKUNDI CHA ‘MWAKENYA’ KILIITIKISA KENYA

838
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Si mengi yaliyokuwa yanajulikana na wananchi wa Kenya kuhusu vuguvugu la Mwakenya, kikundi kilichokuwa kinaipinga serikali ya Rais Daniel arap Moi katika miaka ya 80 hadi hatimaye polisi na vyombo vya usalama vilipoingilia kukisambaratisha.

Lakini hatua hiyo iliambatana na nguvu kubwa dhidi ya wanachama na wafuasi wa kikundi hicho pamoja na yeyote yule aliyehisiwa kukiunga mkono – wengi walikamatwa na kuteswa na vyombo vya dola ili kuwafichua wafuasi wengine.
Baada ya Moi kuwa rais mwaka 1978 wanasiasa wengi mashuhuri na baadhi ya wasomi walimtuhumu kwa ufisadi, ukiukwaji wa haki za binadamu, kuminya demokrasia, ukabila na matumizi mabaya ya fedha za serikali.
JARIBIO LA MAPINDUZI 1982
Baada ya kushindwa kwa jaribio la mwaka 1982 la kutaka kuipindua serikali yake, Moi alichukulia tukio hilo kama sababu ya kuifanya nchi kuwa ya mfumo wa chama kimoja rasmi. Hata hivyo Kenya tayari ilikuwa na “mfumo wa chama kimoja” tangu 1979, ingawa si kikatiba.

Watu wengi walitiwa nguvuni kwa kosa la kuwa mfuasi/mwanachana wa Mwakenya (Muungano wa Wazalendo wa Kenya) kikundi ambacho kilipigwa mnarufuku na serikali kikidaiwa kupanga njama za kutaka kuipindua. Mamia walikamatwa na kuteswa na kushitakiwa mahakamani.

Hakuna mtu aliyesalimika – kama si yeye, basi mmoja miongoni mwa jamaa zake au rafiki zake. Msako uliwalenga walimu, na wahudumu ofisini kama vile makarani, makatibu muhtasi wa vigogo wa serikali na magazeti yalikuwa yanasheheni habari za kukamatwa kwa waliodaiwa kuhusika na Mwakenya.

Hata hivyo Mwakenya hakikuwa kikundi cha kigaidi wala hakikuhusika na mauaji kama vile kile vha Mungiki kilichoibuka miaka 30 baadaye.

KUHUSIKA KWA WAHADHIRI WA VYUO VIKUU

Hali ya namna hii ilipingwa vikali na jamii ya vyuo vikuu, hususan Chuo Kikuu cha Nairobi ambacho ndiyo kilikuwa kiini cha harakati za kudai kuondolewa Kifungu 2A cha Katiba ya Kenya kilichokuwa kimeifanya Kenya kuwa ya mfumo wa chama kimoja.
Awali kabisa Mwakenya hakikuwa kikundi cha siri. Wanachama wake walikuwa wakidai uhuru zaidi wa kidemokrasia kupitia mikutano ya ndani kama vile makongamano na semina na usambazaji wa vipeperushi na vijarida, vikiwemo “Mpatanishi” na “Mzalendo.”

Makongamano na vipeperushi vililenga tu kuelezea kile wanachama wa Mwakenya walivyokuwa wanakiona kuhusu mapungufu katika medani ya kisiasa nchini Kenya. Hivyo baada ya utawala kuanza kuwasaka wanachama wake, basi kikundi hichio kikageuka na kuwa cha kichinichini. Msomi mashuhuri, Profesa Ngugi wa Thiongo ndiyo alikuwa msemaji mkuu wa kikundi hicho.

Upinzani dhidi ya utawala wa Kenya, hata kabla ya Moi kushika madaraka, ulikuwapo na ulikuwa unajitokeza kupitia machapisho, na chapisho lake kuu lilikuwa “Independent Kenya” kijarida cha kikundi kilichoitwa “Chache.” Baada ya hapo kiliibuka kikundi cha “December 12 Movement” (Vuguvugu la Desemba 12) na jarida lake lililoitwa “Pambana.” Hivyo ni kutokana na “Vuguvugu la Desemba 12” ndiyo kikundi cha Mwakenya kiliibuka.

Aidha mara tu baada ya jaribio la kuipindua serikali la 1982, utawala wa Moi ukaanzisha kampeni kabambe ya kuwanasa wote waliosadikiwa kuwa wasaliti na kuwa na mkono katika jaribio hilo. Kasma nilivyotaja hapo mbele wengi wa hawa walikuwa wahadhiri wa vyuo vikuu. Miongoni mwa waliokamatwa awali kabisa walikuwa Maina wa Kinyatti, Prof Katama Mkangi, Wanyiri Kihoro na Paddy Onyango.

Maafisa wa usalama wasio katika sare na hata baadhi ya wanafunzi walisajiliwa na utawala kufuatilia nyendo za wahadhiri hasa kile walichokuwa wanafundisha madarasani. Lengo kuu lilikuwa ni wale wahadhiri waliokuwa wakifundisha nadharia za Kimarxist – somo ambalo lilikuwa linasanbazwa na wafuasi wa Mwakenya.

MOI ATHIBITISHA UTESAJI KWA WASHUKIWA

Waliokamatwa walikuwa wanateswa na kufanyiwa vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu hadi walipokubali kukiri kwamba walikuwa wafuasi wa Mwakenya na kufichua habari za wengine.

Haya yalithibitishwa na si mwingine bali Moi mwenyewe katika mkusanyiko wa wanafunzi mjini London mwaka 1989 aliposema “Tulikuwa tunawatesa wale tu wafuasi wa Mwakenya tuliokuwa tunawashikilia. Vinginevyo tungezipataje habari muhimu kutoka kwao? Hawa walikuwa na lengo la kuharibu kila chenye thamani katika jamii.” Utesaji mwingi ulikuwa ukifanyika Nyayo haose na Nyati House jijini Nairobi.

MWENDESHA MASHITAKA BERNARD CHUNGA

Aliyekuwa naibu Mwendesha Mashitaka Mkuu (Deputy Public Prosecutor), Bernard Chunga ndiye alikuwa mwendesha mashitaka wa kesi nyingi za kikundi cha Mwakenya. Kuna baadhi ya washukiwa walikamatwa, wakafunguliwa mashitaka na kuhukumiwa ndani ya siku moja tu.

Wengi wa washitakiwa hawakuruhusiwa kuweka mawakili. Chunga alikuwa akiwaambia mahakimu kwamba washukiwa walikuwa wamebuni njia mbali mbali za kupindua serikali kupitia kikundi cha siri kilichojulikana kwa jina la Mwakenya. Hakimu Mkuu wa Nairobi wakati huo, H. H. Buch ndiye alisikiliza kesi nyingi za watuhumiwa wa kikundi hicho.

Aidha Moi aliwahi kuwaambia Wakenya kwamba wanachama wa Mwakenywa hawakuwa watu wa kawaida, bali “wasomi wenye kufuga ndevu ambao walikuwa na lengo la kuwatumikia mabwana zao wa nje.”

Alisema wote walikuwa na hati za kusafiria na walikuwa tayari kuikimbia nchi iwapo kutaibuka vita ya wenyewe kwa wenyewe. Baadhi ya watu mashuhuri waliokamatwa ni Wanyiri Kihoro, Kiongo Maina, Mwandawiro Mghanga, Katama Mkangi, Wahome Mutahi, Lumumba Odenda na Oduor Ong’wen (aliyewahi kuwa mwenyekiti wa kikundi hicho).

MAANDAMANO YA WANAWAKE

Mwaka 1992 akina mama kutoka maeneo ya kati kati ya Kenya ambao watoto wao walikamatwa na kuhukumiwa kuhusiana na kikundi cha Mwakenya walijikusanya uwanja wa Uhuru Park jijini Nairobi baada ya jitihada zao za kumtaka Mwanasheria Mkuu Amos Wako kuwaachia ziliposhindikana.

Wakina mama hawa waliungwa mkono na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Wangari Maathai (marehemu sasa) na Monica Wangu Wamwere, mama wa Koigi wa Wamwere. Waliendesha mgomo wa kutokula chakula viwanjani hapo kwa miezi kadha kabla ya utawala wa Moi kutuma vikosi vya polisi kuwatimua.

Wakina mama hao walijibu hatua hiyo kwa kuvua nguo zao zote, jambo ambalo liliwafanya askari polisi wengi kutimua mbio kuwakimbia kwani ilidaiwa ni laana katika baadhi za jamii za Kenya kumuona mama mzima akiwa uchi.

Hadi ilipofika Julai 1993, wafungwa wote waliachiwa na sehemu ya Viwanja vya Uhuru Park ambako akina mama wale walisimika tenti lao sasa inaitwa Kona ya Uhuru (Freedom Corner).
Yule Naibu Mwendesha Mashitaka Mkuu Bernard Chunga, aliandamwa hadi akaachishwa wadhifa wake baada ya Umoja wa NARC, chini ya Rais Mwai Kibaki ulipouondoa madarakani utawala wa KANU mapema 2003.

Utawala wa Moi ulikuwa umemteua Chunga kuwa jaji Mkuu na ilidaiwa ilikuwa kama ‘zawadi’ kwake kutokana na jinsi alivyokuwa akiendesha mashitaka dhidi ya wafuasi wa Mwakenya.

Na pamoja na kwamba hakuwahi kufanya kazi ya uhakimu Chunga aliwapita majaji waandamizi wa Mahakama ya Rufaa ambao ndiyo walistahili kufikiriwa katika wadhifa wa kuwa Jaji Mkuu. Aliondolewa kupitia mchakato wa Tume ya Uchunguzi (Judiciary Tribunal) iliyoteuliwa na Rais Kibaki na ilikuwa ni mara ya kwanza rais kuanzisha rasmi uchunguzi dhidi ya Jaji.

Hata hivyo vuguvugu la Mwakenya likaanza kuyeyuka, lakini hasira za wananchi wengi kama walivyzionyesha kwenye ufuatiliaji wao wa kung’olewa kwa Chunga ilikuwa ishara jinsi Wakenya walivyokuwa wanachukizwa na namna dola ilivyolisimamia sakata zima la Mwakenya.