Home Makala Kila mmoja ameisoma namba kwa nafasi yake

Kila mmoja ameisoma namba kwa nafasi yake

747
0
SHARE

NA FARAJA MASINDE

LEO ni takribani siku 363 tangu Rais Dk. John Magufuli aingie kwenye Ikulu ya Magogoni kama kiongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano  katika histori ya Tanzania.

Dk. Magufuli amebakiza siku mbili ambayo ni keshokutwa ili aweze kutimiza mwaka mmoja akiwa madarakani kati ya ile mitano ya kuliongoza taifa la watanzania wanaokaribia milioni 50-.

Licha ya kwamba imesalia siku moja kutimiza mwaka mmoja madarakani lakini mpaka sasa, JPM amejiwekea rekodi ya aina yake ikilinganishwa na mtangulizi wake, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete(JK).

Upekee huo unatokana kwamba tangu ateue  Baraza lake la Mawaziri hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanywa ndani ya baraza hilo tofauti na JK ambaye itakumbukwa kuwa Katika Baraza lake la kwanza aliteua Mawaziri na Manaibu Mawaziri 60, Januari 2006 na ilipofika Oktoba 2006, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya kwanza makubwa ya baraza lake la Mawaziri kwa kuwahamisha vituo vya kazi Mawaziri 10 na Naibu Mawaziri wanane licha ya kwamba hakuna aliyejeruhiwa na mabadiliko hayo.

Aina hiyo ya kipekee ndiyo inayomchora, JPM kwenye picha ya kipekee mpaka jambo linaloelezwa kuchangiwa na utendaji kazi wa, Mawaziri aliowateua.

Hata hivyo tangu kuwapo madarakani kwa kiongozi huyo ambaye mpaka sasa hajatoka nje ya mipaka ya Afrika Mashariki, kumeendelea kuibua taswira tofauti tofauti kutoka miongoni mwa watanzania anaowaongoza.

Hali hiyo inachangizwa na kile kinachoonekana kama hali ngumu ya uchumi inayowakabili watanzania kwasasa kwenye nyanja mbalimbali.

Ugumu wa maisha kwa sasa umeonekana kuwa mwiba mkali kwa watanzania ikilinganishwa na miaka ya nyuma jambo ambalo limefanya wengi kwa sasa kuishi kwa mtindo wa kubana matumizi.

Mdororo huu umeonekana kuzikumba mpaka biashara mbalimbali jambo ambalo limepelekea baadhi yao kufunga au kuhamisha kabisa biashara zao kutokana na kukosekana kwa wateja wa bidhaa zao.

Mbali ya wafanyabiashara hao kuondoa biashara zao bado adha kubwa inaonekana kuwakumba watanzania wa kawaida ambao kufuatia kutokumudu gharama za maisha.

Hali hiyo inatokana na watanzania hao kutokuwa na fedha mfukoni za kuwezesha kuendesha maisha ya kila siku ambapo hali inadhihirisha kuwa wengi wa watanzania kwa sasa wanaishi kwa kukopa hali inayowafanya waandamwe na madeni.

Kwani hata wale ambao hawakuwa na ujasiri wa kukopa kipindi cha nyuma nao wamejikuta wakilazimika kufanya hivyo ili kuzinusuru familia zao.

Ni wazi kuwa mzunguko wa fedha umepungua kwa kiwango kikubwa, jambo ambalo linaelezwa na wataalamu wa masuala ya uchumi kuwa litasaidia sana katika mfumko wa bei, kwani fedha haitakuwa holela na hivyo itakuwa hadimu jambo na hivyo kuifanya iwe na thamani kubwa.

Wataalamu hao wanaongeza kuwa kutokana na kupotea huko kwa fedha  kutasababisha kushuka kwa bei za bidhaa jambo ambalo litawaathiri wafanyabiashara huku likiwa na faida kwa walaji ambao ndio wanufaika wa mwisho.

Mbinu hii inayotumiwa na Serikali ya Awamu ya Tano inatajwa kuwa bora jambo litalopelekea hata watu wa chini kuweza kumudu gharama za vitu mbavyo awali vilikuwa vikiuzwa ghari.

Hata hivyo wananchi kwenye maeneo mbalimbali ambao ndiyo wanufaika wakubwa wa mkakati huu wameonekana kuwa njia panda na hatima ya maisha yao kufuatia kuanza kupoteza imani yao kwa JPM kutokana na namna mambo yanavyoenda mpaka hivi sasa.

Wengi wanaamini kuwa, nia hii ni rafiki kwa vijana na watanzania wenye nguvu za kufanyakazi tu ambao wanaweza kumudu kuishi kwenye usemi wa ‘Utakuwa kwa jasho lako’ lakini siyo kwa wazee, walemavu na hata watoto.

Maamuzi ya JPM licha ya kwamba yamekuwa na dhamira ya kurejesha nidhamu ya kazi kwa watanzania, lakini sasa yanaonekana dhahiri kugeuka mwiba na hata kwa wasiohusika na mkakati huu, jambo ambalo linaongeza idadi ya watu wasiojiweza ambao wanaishi chini ya dola moja hali inayowasukuma kuwa ombaomba ili maisha yaweze kusonga.

Licha ya kurejesha nidhamu bora ya matumizi ya fedha kwa Watanzania ambao baadhi yao walizoea kuishi kama ‘Malaika’ kwa kufanya manunuzi nje ya nchi na vitu vingine visivyokuwa vya msingi.

Lakini kwa sasa hali imekuwa ngumu kwa pande zote na sasa unafananishwa na msumeno ambao unakata pande zote mbili. Hauangalii itikadi za vyama wala nafasi za watu, jambo ambalo linafanya baadhi ya watanzania  kutamani maisha wanayoishi sasa hivi yasalie kuwa ndoto.

Ombwe la kati ya wenye nacho na wasio nacho kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja ambao, Rais Magufuli amekuwa madarakani limeonekana kupungua kwa kiwango cha juu kama siyo kuondoka.

Wananchi wengi wenye kipato cha chini wameonekana kufarijika zaidi na hali hii kutokana na kubaini kuwa hali ngumu ya maisha haiko kwao tu isipokuwa pande zote huku wakimsisitiza kiongozi huyo kujaribu kuregeza kamba.

Kipindi cha mwaka mmoja cha rais Magufuli kinachambuliwa na wataalamu wa masuala ya uchumi kama kipindi ambacho kilikuwa kikisubiriwa kwa miaka mingi na idadi kubwa ya  watanzania kwa lengo moja la kutaka kuitengeneza Tanzania ambayo ilionekana kupoteza mwelekeo.

Katika mtazamo mwingine iwapo kasi hii itasalia kuwa ile ile basi ni wazi kuwa watu wengi watapoteza ajira kutokana na sekta nyingi za uzalishaji kufungwa.

Kwani tayari dalili zimenza kuonekana mapema kuanzia kwenye kufungwa kwa mahoteli ambayo yamewaacha waliokuwa wafanyakazi wasijue cha kufanya kwani wafanyakazi hawana pakwenda badala yake wanageuka kuwa tegemezi mtaani.

Mbali na mahoteli kuna maeneo kama  viwanda, makampuni na mashirika ambayo yamekuwa yakitangaza kupunguza wafanyakazi kila kukicha kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kupanda kwa gharama za uendeshaji.

Tayari kumekuwapo na minong’ono ya taasisi nyingi za fedha ambazo zinaelezwa kuanguka katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa uongozi wa rais Magufuli kutokana na kufilisika.

Benki zilizozoea kutoa mikopo kwa  wafanyabiashara kwa riba kubwa sasa hivi zinaelekea kukosa wateja jambo linalopelekea kuwa katika hali ngumu kimtaji. Wajasiliamali wengi kwa sasa wanalitazama suala la kukopa kama jambo haramu jambo linalofanya kufa kwa taasisi hizi za fedha.

Ni mwaka huu mmoja tu wa rais Magufuli madarakani ndiyo unaotazamwa kama chanzo cha ongezeko la vitendo vya uhalifu kwenye maeneo mengi nchini.

Kwani ‘dili’ nyingi kwasasa zimekwenda na maji ukiwamo wengi kupoteza vibarua vyao na hivyo kujikuta wakilazimika kutafuta njia nyingine ya kuishi.

Hali inayowasukumia wengi kwa sasa kujitumbukiza kwenye vitendo vya kihalifu, Ujambazi, Ukahaba, Utapeli na hata Wizi.

Kwa hali ya kawaida hakutakuwa na uvumilivu wa kumshuhudia mtu anatoa milioni mbili benki au ATM, ilihali kuwa yeye hata maji ya kunywa hajayaona siku mbili.

Hivyo kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja natambua fika kuwa rais Magufuli ataipima kasi yake kwa watanzania ambao wengi wanaonekana kuelewa kile ambacho amekuwa akikimaanisha kupitia hali hii iliyopo kwa sasa.

Japo kila mmoja anatambua kuwa kuna hali mbili kwa sasa ambazo ni hasara zaidi na faida kwenye maamuzi haya ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. Kwa namna nyingine hali hii huenda ikawa na msaada  mkubwa kwa watanzania wa kawaida kwani watapata kipaumbelea katika suala zima la kumiliki ardhi.

Ardhi ilikuwa imepandishwa kwa kiwango kikubwa kutokana na wengi waliokuwa wakinunua kwa bei kubwa kudhibitiwa kiuchumi.

Hivyo kwa sasa hakuna mwenye nafuu kwani kila mmoja analia chozi lake, mpaka nyumba sasa hivi wapangaji wamekuwa ni wakutafuta siyo wao kuzitafuta nyumba na hii inatokana na ukosefu wa pesa mifukoni.

Matarajio ya watanzania wengi ni juu ya rais Magufuli kusikia na kufanyia kazi minong’ono hii ya kuwapo kwa hali ngumu ya maisha jambo ambalo linafanya kila mmoja kuisoma namba kwa nafasi yake.