Home Maoni Kila Mtanzania anahusika katika masilahi ya taifa

Kila Mtanzania anahusika katika masilahi ya taifa

1231
0
SHARE

Na DEO MBASA

MASILAHI ya Taifa ni suala lenye utata mkubwa, hasa katika nchi kama zetu ambazo bado zina taasisi changa. Lakini pia Tanzania haijabahatika kuongozwa na chama kingine cha siasa, hivyo ni rahisi kuhusisha masilahi ya taifa na ya chama tawala – CCM.

Nchi ambazo walau zimepata kuongozwa na vyama mbalimbali vya siasa, zinaweza kwa wepesi kufahamu ni mambo yapi yaliendelea kusimamiwa na Serikali zote, hata pale ambapo mabadiliko ya itikadi za vyama yalitokea.

Lakini nataka nijitahidi kuelezea kwa lugha na mifano rahisi ili tusaidiane kutoka huko kwenye fikra za kuhusisha CCM peke yake na masilahi ya taifa, kwenda kwenye fikra za kuhusisha sio tu vyama vyote vya siasa, bali pia wananchi wote wa Tanzania.

Taifa lolote huwa lina mipango ya siku za usoni, aidha ya muda mfupi, wa kati na mrefu. Bahati mbaya walimu wangu wa falsafa, akina Dk. Adolf Mihanjo (Sifahamu kama bado Dokta au Profesa sasa) pale UDSM walinifundisha kwamba falsafa ya Mwafrika huwa haina ‘future’ (haiangalii siku za mbeleni) bali hujikita na mambo yaliyopita na yaliyopo (Ingawa sina hakika). Sisi tunayo dira yetu ya maendeleo 2025, imebeba matamanio yetu na naweza kusema ni masilahi yetu ya taifa.

Lakini ni nadra kwa viongozi wa kiafrika wanaotokea kuwa na ‘vision’ kubwa kueleweka kwa wengi. Usipoeleweka kwa wengi na hasa kwenye siasa unaweza kujua madhara yake.

Kwa msingi huo, hata viongozi wetu wanalazimika kufanya mambo yanayoweza kuonekana au kuzaa matunda ndani ya miaka miwili (Ingawa Rais Dk. John Magufuli amejipambanua kidogo) la sivyo hawatafaa kwenye uchaguzi unaofuata.

Kwa lugha nyingine katika mazingira haya, akija kiongozi mwenye ‘vision’ kubwa kwa taifa, lazima ataanguka ndani ya miaka mitano ya mwanzo kwa vile atakuwa bado hana la kuoneshea.

Naamini hata Mwalimu Nyerere angeongoza miaka mitano au kumi tu ya mwanzo, yawezekana tusingekuwa na mengi sana ya kusimulia juu yake.

Tabia hii imetufanya tuwe watu tusiowekeza kwenye mambo yanayochukua muda mrefu kufikia malengo au matunda.

Wakulima wanafikiria walime mazao ya chap chap (tikiti maji zimekuwa mwarobaini wa haraka yetu). Wafanyakazi wanafikiria wafanye nini watajirike chap chap, wafanyabiashara wanawaza wafanye vipi watajirike chap chap, hata kama ni kwa kuchuuza vitu vya ajabu toka ng’ambo au kukwepa kodi.

Falsafa ya chap chap inatawala. Na huu ndio umekuwa msingi wa uharibifu kwa taifa letu. Kama mkoloni aliweza kupanda mazao au miti ya kuvuna miaka 10, 15 au hata 20, sisi kwenye nchi yetu wenyewe tunaona mbali saaana na hatuko tayari!

Ona ilivyomchukua Mwalimu Nyerere muda kujenga amani, upendo na mshikamano tulionao. Hata mipango mikubwa ya kiuchumi pia lazima itugharimu kazi na muda.

Kinyume chake masilahi ya taifa ni yale mambo muhimu kwa ustawi wa taifa sasa na baadaye. Na kwamba mambo hayo yakifanyiwa mzaha, baadaye yetu kama taifa inakuwa njia panda bila kujali ni watu wa aina gani wapo uongozini katika taifa.

Swali ni je, haya masilahi ya taifa letu ni yapi? Je, kila Mtanzania anayafahamu? Serikali zote zilizotangulia zilifanya jitihada gani kujenga utamaduni wa kuyatukuza masilahi ya taifa letu? Watoto wanapata mafunzo yapi ya kuwaelekeza kuyapenda na kuyalinda masilahi ya taifa letu? Je, tuko tayari kuyatetea hata kama yanadai kupoteza maisha yetu? Tuko tayari kuyatetea masilahi ya taifa letu hata kama kwa kufanya hivyo tunapingana na sera za vyama na imani za dini zetu?

Ninaweza kuyarahisisha masilahi yote ya taifa hili na hata ya taifa lolote lile na kuyaita ulinzi na usalama.

Hakuna jambo jema lolote linalofanywa katika taifa hili lisilohusiana na suala la ulinzi na usalama wa nchi yetu. Nasisitiza hakuna ‘end production’ ya jambo lolote jema lisilolenga kwenye ulinzi na usalama wa taifa letu.

Ndiyo maana inapotokea Mtanzania yeyote anafanya jambo linalohatarisha ulinzi na usalama anatukosea sana. (Najua hapo mawazo yameshakimbilia wanasiasa na polisi). Yumkini katika mijadala itakayofuata ukajikuta ni wewe ndiye unatukosea sana na kwamba suala la ulinzi na usalama sio la hao unaowafikiria peke yake, bali ndiyo shughuli yenyewe tunayofanya sisi wote kila kunapoitwa leo.

Ukitaka kujua kuna shida. Muulize mtu yeyote swali hili; “Usalama wa taifa ni nini?” Pamoja na majibu mengi utakayopata, halitakosa la kufikiri kwamba ni watu wanaokaa mahala fulani fulani wakihangaika kujua wengine wanazungumza, kufikiri na kutenda nini. Au kwamba ni majeshi ya Ulinzi na Usalama na mambo yanayoendana na hayo.

Tujiulize maswali yafuatayo kama sehemu ya kutafakari wajibu wetu katika ulinzi na usalama wa nchi yetu;

Kwanini tunalima? Kwanini tunaenda shule? Kwanini tunaanzisha na kufanya biashara? Kwanini tunafanya kazi au kutengeneza ajira mpya? Kwanini tunachagua viongozi na kuteua viongozi wa ngazi mbalimbali za utawala? Kwanini tunaanzisha taasisi mbalimbali kama vile mahakama, TBS, TFDA, NEMC n.k?

Shughuli zote hizi pamoja na kukunufaisha kama mtu binafsi, zinahusu ulinzi na usalama wa taifa na kwa maana hiyo zina masilahi makubwa kwa taifa. Taifa likiwa halina chakula, hakuna aina ya bunduki inayoweza kuleta amani na utulivu.

Taifa likiwa halina wasomi wa fani mbalimbali na haliendani na teknolojia na mabadiliko ya dunia, liko hatarini kupotea. Mfano mzuri ni mazungumzo yaliyofanyika kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick Gold. Hebu fikiria endapo taifa lisingekuwa na watu wanaoweza kuliwakilisha kwenye jambo nyeti kama hilo, tupo salama kweli? Masilahi yetu yangesimamiwa na nani? Kutokuwa na madaktari je? Walimu je? Kwa hiyo hata shule na vyuo vipo kwa ajili ya ulinzi na usalama.

Tunafanya biashara kulinda usalama wa nchi yetu kiuchumi na kijamii. Biashara inasambaza huduma kwa namna rahisi ambayo hata Serikali haiwezi (Kumbuka enzi za kupanga foleni ya sabuni au sukari).

Fikiria mfano wa Jiji la Dar es Salaam kukosa petroli au dizeli kwa muda wiki moja tu. Kuna usalama kweli? Tuache petrol, vipi habari ya sukari au chumvi kutoweka ghafla?

Tunapambana kushughulikia uwepo wa nafasi za kazi kwa sababu ni suala la ulinzi na usalama. Watu wasipokuwa na kazi hakuna usalama, lakini pia bila kazi wengi hawatashiriki kujenga uchumi wa nchi. Ikitumika nguvu kazi ya wachache kulisha wengi, masilahi ya taifa yatakuwa shakani.

Tunachagua viongozi kwa ajili ya ulinzi na usalama. Ndiyo maana taifa hili halijawahi kuacha kuwa na uongozi (Leadership Vacuum) hata kwa dakika 10. Ikitokea taifa lisiwe na uongozi kwa nusu saa tu, ndipo utaelewa ninachokiandika hapa. Hii ni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama.

Kwa ajili ya ulinzi na usalama wa biashara, mazingira, chakula na dawa na kila aina ya shughuli, zimeanzishwa taasisi ikiwemo mahakama ili kulinda haki, wajibu, mikataba na mali.

Hakuna mwekezaji anaweza kuja kuwekeza bila kujiuliza swala la ulinzi na usalama wa mali zake. Au hata jirani yako anaweza kukunyang’anya chochote kwa ubabe tu kusipokuwepo na ‘framework’ ya ulinzi na usalama.

Ukitafakari kwa makini kuhusu ni nini watu wanafuata makanisani na misikitini, utagundua ni ulinzi na usalama.

Siwezi kutaja yote kwa nafasi hii, lakini jambo la muhimu kutoka nalo hapa ni kwamba kila Mtanzania katika nafasi yake anahusika katika kutekeleza na kulinda masilahi ya taifa ambayo nimeyaita ulinzi na usalama. Najua tumekuwa tukifanya hivyo siku zote. Lakini tukiifahamu misingi, itatusaidia kujipima kama tupo sawa au tunasuasua.