Home Makala Kilichotokea kwa Gaddafi kinaweza kutokea kwa rais yeyote afrika

Kilichotokea kwa Gaddafi kinaweza kutokea kwa rais yeyote afrika

3347
0
SHARE

NA ERICK SHIGONGO

Wiki hii nimeangalia kipande kidogo cha video kinachoonyesha siku ya mwisho ya maisha ya shujaa Muammar Gaddafi, aliyekuwa rais wa Libya kwa muda wa miaka 42.  Nimesikitika, kidogo tu machozi yanitoke; ametolewa kwenye kidaraja kidogo alimokuwa amejificha, kapigwa kupindukia, uso wote umejaa damu!  Muda wote akipigwa anawauliza wapigaji “Nimewakosea nini?”  Hakuna anayeonekana kumjibu, anaendelea kupokea kipigo kutoka kwa watu ambao moyoni mwake anaamini aliwafanyia kila kitu chema.

Nafumba macho yangu kidogo baada ya kuiangalia video hiyo, natafakari mambo ambayo Muammar Gaddafi aliifanyia nchi yake tangu alipochukua madaraka kwa kumpindua Mfalme Idris mwaka 1969; ni Gaddafi aliyeleta Mapinduzi ya Kijani nchini mwake na kuleta maji kwenye Jangwa watu wakaanza kulima jangwani, huyohuyo Gaddafi ndiye aliyeukuza uchumi wa nchi yake mpaka kuwa nchi ya tano katika Afrika kwa utajiri.

Akajenga barabara na miundombinu mbalimbali, huduma za afya, elimu zote zilikuwa bure, si hizo tu ni katika nchi ya Libya peke yake ambako huduma kama simu, umeme zilitolewa bure chini ya utawala wa rais huyo.  Zaidi ya hayo yote, wananchi walijengewa nyumba bure, kijana alipoona alipewa fedha za kuanzia maisha, hii si kwa mkoa mmoja bali nchi nzima.

Kwa vigezo na mambo haya ambayo Gaddafi aliyafanya, sioni uzito wa ulimi wangu kusema alikuwa rais mzuri pengine kuliko marais wengi duniani!  Lakini huyu ndiye watu wake wamemchomoa chini ya daraja alikokuwa amejificha, kumdhalilisha na kumpiga hadi kifo chake.

Bila shaka vijana hawa waliokuwa wakimpiga na kumdhalilisha Gaddafi ndiyo aliowasomesha bure, kuwatibu bure,  kuwajengea nyumba  na kuwapa mitaji ya biashara pale walipooa!  Nadhani ndiyo maana wakati akipigwa Gaddafi anaukumbuka wema wake na kuwauliza “Nimewakosea nini?” sababu halioni kosa lake kwao.

Watu aliowapenda na kujitoa kadiri awezavyo kuwaboreshea maisha ndiyo sasa walikuwa wakimuua, kibaya kabisa si kwa sababu amewatendea mabaya, bali wamejazwa chuki dhidi ya kiongozi wao na mataifa ya Magharibi ambayo hayakumpenda  Gaddafi, kiasi cha kuamua kumwondoa madarakani na kumuua kabisa.

Wakristo wanafahamu historia ya Yesu Kristo, alikuja kwa ajili ya kuwakomboa  Wayahudi, lakini Wayahudi haohao aliokuja kuwakomboa ndiyo waliomsulubisha msalabani wakidai eti alijiita Mfalme wa Wayahudi.

Hapa ninajifunza jambo moja kuwa si kuwatendea wanadamu mema peke yake kunakoweza kuwafanya wakupende; unaweza kuwajengea barabara nzuri, ukajenga reli ya kiwango cha juu kabisa, ukawasomesha na kuwatibu bure, ukawagawia misaada na fedha mitaani, lakini bado akatokea mtu mmoja kwa maslahi yake, akakuchonganisha na watu uliowatendea mema na wakakuchukia na hata kukutendea kama walivyotendewa Yesu Kristo na Gaddafi.

Nikiitazama Libya leo, ikiwa ni miaka zaidi ya saba baada ya kifo cha kiongozi huyo , ninachokishuhudia ni majuto, machozi machoni na mioyoni mwa wananchi wa Libya.  Nchi yao si ya amani na neema tena kama ilivyokuwa enzi ya utawala wa mtu waliyemuua; imegawanyika vipande vipande chini ya vikundi vya waasi, idadi kubwa ya watu wamepoteza maisha yao katika vita vya wao kwa wao, maelfu wanakufa katika Bahari ya Mediterranean wakijaribu kutoroka kwenda Ulaya kutafuta maisha bora.

Lakini watu hawa wanaokimbia na kulia leo waliwahi kuwa na nchi yao nzuri yenye utajiri mkubwa, wakipewa kila walichokitaka na kiongozi wao, lakini kwa ujinga na kutokuwa makini na propaganda za Magharibi,  zilizojengwa kwenye misingi ya chuki dhidi ya kiongozi wao, wakaingia katika machafuko na kuivuruga nchi iliyowahi kuwa na neema ikawa uwanja wa mapigano.

Tanzania na nchi nyingine za Afrika zinatakiwa kuchukulia tukio la Libya kama somo, kwani kilichotokea katika nchi hiyo kinaweza kutokea katika nchi yoyote ile kama tu kiongozi wake atakwenda kinyume na matakwa ya mabeberu wa Magharibi ambao lengo lao kubwa ni kuudhibiti ulimwengu mzima.

Viongozi wengi wa Afrika wanalichukulia tukio la Libya kama mfano, hofu imewajaa mioyoni mwao, kwamba wakienenda tofauti na Marekani au mataifa makubwa ya Magharibi wanaweza kuadhibiwa kama ilivyotokea kwa Muammar Gaddafi na familia yake, matokeo yake wanatii kila kitu kinacholetwa na mataifa hayo jambo ambalo si sahihi na mara nyingi limekuwa halina faida kwa mataifa yao.

Lakini wapo viongozi jasiri na mashujaa, ambao wameamua kwa nia moja kutetea maslahi ya wananchi wa nchi zao, wameukataa unyonyaji na ugandamizaji wa mataifa ya Magharibi, wanataka utajiri wa nchi zao  uwanufaishe wananchi wao maskini badala ya kunufaisha wezi wa mataifa ya Magharibi.

Mara tu baada ya kuingia madarakani waliitazama upya mikataba ambayo nchi zao ziliingia na mataifa ya Magharibi, katika uchimbaji wa madini, gesi au matumizi ya raslimali ambazo zimekuwa zikichotwa na makampuni ya Magharibi bila kuwanufaisha wazawa.

Pengine wameonekana kuenenda kinyume na sera  za kibepari za Magharibi na kuelekeza macho yao kwenye sera za Mashariki ambazo ni za Kikomunisti ambako wanapokea misaada mingi ya maendeleo isiyo na masharti na isiyoingilia mambo ya ndani ya kisiasa, pengine wamekwenda tofauti na sera za uzazi wa mpango tofauti na ambavyo nchi za Magharibi zinataka, wao wamewahimiza wananchi wao kuendelea kuzaa kwa wingi.

Mambo haya na mengine mengi hayawafurahishi mabeberu, ambao makampuni yao ya kinyonyaji yaliyowezeka katika bara la Afrika yamebanwa yasiendelee kuwaibia maskini wa bara hilo, maamuzi haya yanajenga chuki kila siku dhidi ya viongozi wenye msimamo ya kutetea maslahi ya wananchi maskini wa nchi zao.

Chuki hizi ndizo zilipelekea Muammar Gaddafi akachukiwa na mataifa ya Magharibi na hatimaye mikakati ya kumwondoa madarakani na kumuua ikaandaliwa kwa kuwatumia watu wake mwenyewe, walipaswa kusimama na kiongozi wao, kumtetea mpaka dakika ya mwisho, badala ya kufanya hivyo walizikubali njama za mataifa hayo na kusababisha vurugu katika nchi yao ambazo hatimaye zilimwondoa madarakani mtu aliyesaidia taifa hilo mpaka kufikia uwezo mkubwa kabisa kiuchumi.

Hili ndilo somo ambalo nataka Waafrika tujifunze kutokana na tukio la Libya, ambako leo hii wanajuta na kusaga meno, wanamtamani marehemu Gaddafi angekuwa hai na Libya yao ya zamani ikiendelea kuwepo jambo ambalo haliwezekani tena.  Waafrika tunatakiwa kuwa makini na propaganda za Magharibi, tusimame na viongozi wetu wakati wote, tusikubali kabisa kuvuruga nchi zetu zenye neema na utajiri mkubwa kwa faida ya mataifa hayo ambayo mwisho wa siku yatakuwa yamekaa pembeni yakitucheka.

Kama hatuwezi kusimama na viongozi wetu, hakika yaliyotokea Libya yanaweza kutokea mahali popote katika bara la Afrika, ikiwemo Tanzania, kwani makampuni makubwa ya kibeberu yanashindwa kuleta Shilingi bilioni 150 na kuwahonga wajumbe  150  wa kikao maalum cha kupitisha jina la mgombea wa urais na kumwondoa madarakani yule wanayemwona  ni kizuizi kati yao  na utajiri wa taifa? Jambo hili linawezekana tu kama hatutasimama na viongozi wetu na kukubaliana na njama za mabeberu.

Mungu ibariki Afrika,

Mungu ibariki Tanzania,

Mungu wabariki viongozi wetu.