Home Makala KILIMO: ATHARI ZA ‘KAULI MBIU’ BILA KUWEPO MSUKUMO WA DHATI

KILIMO: ATHARI ZA ‘KAULI MBIU’ BILA KUWEPO MSUKUMO WA DHATI

1247
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Hapa Tanzania kilimo ni miongoni mwa vitu viwili ambavyo vimekuwa vinaibua mijadala mizito kwa wanasiasa, wasomi na wananchi kwa ujumla – na hasa katika kuporomoka kwa viwango vyake. kingine ni elimu, lakini afya nayo imeingia katika kundi hili.

Tangu nchi hii ilipopata uhuru zaidi ya nusu karne iliyopita kumeibuliwa kauli mbiu kadha zenye lengo la kusukuma gurudumu la sekta ya kilimo – sekta ambayo daima hutajwa kama ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Kwa maneno mengine kumetokea majaribio kadha kupitia kauli mbiu ya kuleta ‘mapinduzi ya kilimo’.

Hizi ni kuanzia ile ya ‘Siasa ni Kilimo’ iliyotokana na Azimio la Iringa la mwaka 1972, wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza wa Mwalimu Julius Nyerere ikaja ‘Kilimo ni Uhai’ na sasa ‘Kilimo Kwanza’ iliyoibuliwa na utawala wa Awamu ya nne wa Jakaya Kikwete na ambayo inahusishwa sana na azimio lile la Iringa la wakati wa Mwalimu Nyerere.

Lakini mara zote kauli mbiu hizo huishia kama zilivyotajwa – kauli tu kwani serikali yenyewe ndiyo mbeba lawama mkuu. Na lawama kubwa inayotajwa, pamoja na mengine ni udogo wa bajeti inayotengwa katika sekta hiyo na kuwepo kwa asili kubwa ya ‘siasa’ ndani yake kuliko utaalamu.

Tunaambiwa kwamba hadi sasa sekta ya kilimo inayokua kwa asilimia nne, imeajiri asilimia 80 ya Watanzania, wengi wao wakiwa ni wakulima wadogo.

Hivyo awamu zote zilizopita za utawala zimekuwa zikijitahidi kuhamasisha kilimo kwa kuwaandaa wataalamu na kutumia wanasiasa katika majukwaa yao ili kuhimiza kilimo ambacho mpaka sasa hakina mafanikio ya kuridhisha. Hatujajua bado naye Rais John Magufuli atakuja kivipi katika harakati zake za kuinua kilimo nchini.

Hivyo dhana nzima ya “mapinduzi ya kilimo” ni ya kibepari na ilijengwa katika msingi wa chuki na mtazamo hasi dhidi ya wakulima wadogo wadogo. Wakulima wadogo wadogo huonekana kama chanzo cha umasikini wa nchi kwa kuwa uzalishaji wao haujikiti katika kulimbikiza faida. Ni uzalishaji wa kujilisha zaidi ambao ni duni kwa kuwa hutumia jembe la mkono, na mbinu za kale za uzalishaji.

Watetezi wa mapinduzi ya kilimo hutaka mkulima mdogo afanywe kuwa wa kisasa. Lakini kwa kuwa ni vigumu kumfanya mkulima mdogo kuwa wa kisasa na pia wao kuyagomea ‘mageuzi’ hayo basi watetezi wa mapinduzi ya kilimo huona kuwa njia pekee ni kumyang’anya ardhi ili akafanye kazi kama ‘manamba’ katika shamba la mkulima wa kibepari.

Hivyo dhana inayojitokeza ni kwamba katika mfumo huu injini kuu ya uzalishaji ni mkulima mkubwa ambaye uzalishaji wake

hutegemea sehemu kubwa la ardhi na mbinu za kisasa. Hizi ni pamoja na mashine kubwa kubwa za kulimia na kuvunia, mbolea za kemikali zinazozalishwa viwandani, dawa za kemikali za kuulia wadudu, na mbegu zilizobadilishwa vinasaba (genetically modified seeds).

Lengo la uzalishaji wa mkulima mkubwa ni kulimbikiza mtaji, na hulenga hasa kuzalisha mazao ya kibiashara ingawa kwa mfano atazalisha chakula, lengo basi ni kuuza sokoni ili pate faida zaidi, bila kujali kuwa chakula hicho huenda kumlisha nani. Soko linalolengwa hasa ni soko la kimataifa – soko la nje – hata kama ndani ya nchi husika kunaweza kuwa na watu wanaokumbwa na njaa.

Chukulia kwa mfano “Kilimo Kwanza” – mkakati ulioasisiwa 2009, ukiwa na lengo la kuongeza uzalishaji katika kilimo ili kukidhi mahitaji ya ndani, lakini pia ukilienga soko la kimataifa. Mzalishaji mkuu katika mkatati huo ni mkulima mkubwa, ambaye mbinu zake za uzalishaji zinapaswa kuigwa na wakulima wadogo na wa kati.

Kwanza kabisa wakulima wadogo wadogo  hawakushirikishwa mkakati wenyewe kwani ulikuwa ulikuwa ni makubaliano kati ya serikali na wafanyabiashara wakubwa nchini, makubaliano yaliyopelekea wafanyabiashara hao kupewa maelfu ya ekari za ardhi kwa ajili ya kilimo.

Lakini hata hivyo kulikuja wito wa kuwashirikisha wakulima wadogowadogo kwamba nao wakitaka kujikwamua kiuchumi waachane na jembe la mkono na wanunue vitrekta vya mkono yaani power tillers vilivyoagizwa na kuletwa nchini na wafanyabiashara wakubwa wakubwa.

Na tukitazama nyuma katika historia hapa Barani Afrika tunaona kwamba wakati wa ukoloni, wakulima wadogo wadogo walinyang’anywa ardhi yao ambayo iligawiwa kwa wakulima wakubwa wa Kizungu.

Unyang’anyi au tuseme uporaji huo wa ardhi ulitokea kwa kiwango kikubwa katika makoloni kama vile Kenya, Zimbabwe na Afrika Kusini – ingawa hapa Tanzania haikuwa kwa kiasi kikubwa. Hivyo kuirejesha ardhi iliyoporwa huwa ni mapambano ya muda mrefu na mara nyingine huibua vita baina ya wazalendo na mamlaka za kikoloni kama vile Vita ya Mau Mau nchini Kenya.

Huko Zimbabwe katika miaka ya karibuni wananchi kupitia serikali yao wamefanikiwa kurejesha ardhi yao baada ya mapambano ya muda mrefu, ingawa kwa Afrika ya Kusini

sehemu kubwa ya ardhi yenye rutuba bado inamilikiwa na kikundi cha weupe wachache.

Nako pia mapambano bado yanaendelea kwani kuna pengo kubwa kati ya wenye fedha na wasio na fedha. Wanyonge wa Afrika ya Kusini sasa wako katika harakati za kurejesha ardhi mikononi mwa watu weusi. Hivyo badala ya sisi kujifunza kutokana na kilichotokea kwa hao wenzetu watawala wetu sasa wanagawa ardhi bure kwa makampuni ya nje.

Aidha, mikakati hii ya mapinduzi ya kilimo huleta athari za kimazingira. Si siri tena kwamba kemikali zitokanazo na dawa za kuulia wadudu pamoja na mbolea za viwandani sio tu zimekuwa zikiharibu rutuba ya ardhi, bali pia zimeingia katika vyanzo vya maji na kusababisha madhara makubwa ya kiafya kwa binadamu, na viumbe hai wengine.

Inadaiwa kwamba kilimo cha kutumia mashine kubwa kubwa huchangia asilimia 30 ya gesi za ukaa, gesi ambazo huchafua anga, na kuna hatari ya kutoweka kwa uhai duniani siku za usoni kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yatokanayo.